UTAWALA WA KIFIKRA. - Msamaa.
Headlines News :
Home » » UTAWALA WA KIFIKRA.

UTAWALA WA KIFIKRA.

Written By Unknown on Wednesday, December 5, 2012 | 6:16 AM

USIOMBE KUTAWALIWA KIFIKRA.

Fikra ni zao la akili ya mwanadamu na kila papambazukapo hujichomoza hizi na zile ima njema au mbaya.Fikra mbaya huzaliwa ni akili iliyokosa tafakuri safi na mara nyingi humfanya mwenye nazo kuchanganyikiwa au kufanya jambo bila kujitambua, hatma yake maamuzi mabaya hujipa mamlaka na kusababisha huzuni tena zilizosheheni majuto.

Akili ni jambo linalotawalika sawa na kiwiliwili ingawa utawala huu wa mwanzo huwa ni mbaya kupitiliza kwani ndio mashine ya kuzalishia mawazo au kwa jina jengine fikra za ujenzi wa maisha ya mtu binafsi na jamii iliyomzunguka.
Kwa maana ya jumla,utawala wa kifikra ni kitendo cha kuishinda akili ya mtu fulani kwa ghilba na kuidunisha kimawazo ili uweze kuitumia kwa maslahi yako binafsi huku mtawaliwa akishangilia.Utawala huu humfanya mtawaliwa akubali tu azimio au mpango wowote wa mtawala bila kuuingiza katika mizani, kupima usahihi,faida na hasara katika utekelezaji wake.

Mtawaliwa hujikuta katika dimbwi lenye kina kirefu la dhiki baadae, huku mtawala akila kiyoyozi(sawa na Waislamu leo hii Tanzania kama wataliwa).Itakumbukwa kuwa, utawala huu hufanywa kwa njia za propaganda ambapo kitu hupambwa kwa kupewa sifa kinyume na kilivyo na ghilba hutumika kama usafiri wa kumfikisha Mtawala atakako.Propaganda hizi chini ya mwevuli wa ghilba,huendeshwa kwa ustadi mkubwa wakumfanya mtawaliwa asizinduke kwa urahisi bali kuitikia “Ndio” kwa lolote atakaloambiwa hata kama ni kitanzi cha kutaifisha maisha yake na jamii yake.Kinyume chake ni mtu aliye huru kifikra.

Mtu aliyehuru kifikra huishibisha akili yake tafakuri safi na kulipitisha kila aambiwalo katika chujio lipimalo usahihi wa matendo na maelekezo ili atamke “Ndio” au “Hapana” kulingana na sehemu na muda muafaka.Aliye huru kifikra huujua ukweli na kuukubali,jema na baya, pia uongo kwake huutambua kufumba na kufumbua.

Itoshe kwa maelezo hayo yachambuayo angalau kwa ufupi maana ya utawala wa kifikra ili sasa nipate nafasi mwanana kuonesha ubaya wake na faida ya kuwa huru kiakili na kimwili.Katika uchambuzi wangu nitamgusa Nyerere kama mtu aliyejivika joho hili la ghilba na akawafisidi Waislamu-Tanzania- kupitia propaganda mbali mbali na utapeli.Nyerere alijifunza utawala huu na kuwaghilibu Waislamu ambapo wale waliokuwa huru kifikra,waliishia gerezani au kuwa wakimbizi na wengine wakawa marehemu kabisa kwa kukataa kwao kudhalilishwa na kutapeliwa kwa ulaghai wa maneno.

Pia nitaigusa Zanzibar ili wale walio lala mpaka leo huku wakiwa wanafunzi watiifu wa kueendeleza azma ya mwalimu wao licha ya kuondoka kwa mda sasa tangu 1999, waamke.Lau kama unga wa ndere umeharibu bongo zao na kunajisi fikra zao kiasi cha kushindwa kuamka na kuuona ukweli wakaukubali na wakaufuata,basi wasubiri kubatizwa na kusulubiwa msalabani huku wengine wakiwazomea kwa aibu walizozichuma kwa mikono yao.

Naelewa fika kwamba ukweli unauuma na kuukubali kunahitaji ujasiri mkubwa lakini watu wa kale walisema “lisilobudi hutendwa”.Mtu anaweza akawa ni mzee chambilecho vijana “Dingi” lakini akaukana ukweli akasema yeye si mzee bali ni “kijana wa mda mrefu”.Sawa na ukweli huu leo utakavyokanwa na wengi hususan wale waliotawaliwa kifikra na kuzama katika dimbwi la fikra finyu.

Nianze na Zanzibar kama mkoa tu kwa sasa, maana hata mtandao wa Tigo wanaujua ukweli huu.Uthibitisho niliupata nilipotoka Dar-es-salaam kwenda Unguja,kwani mara tu nilipowasili bandari ya Malindi nilitumiwa ujumbe usemao “Ukiwa mkoa huu,pata MARA MBILI ya Salio SIKU NZIMA,KILA SIKU uongezapo salio na TIGO.Salio kutumika kupiga simu mtandao wowote TZ” (Ujumbe huu nilitumiwa tarehe 03-08-2011 saa 02:39:35pm).Ujumbe kama huu nilitumiwa nikiwa Moshi mwezi wa kumi mwaka 2011 na hapo ndipo akili ikakamilisha kiu ya kutaka kujua hadhi ya Zanzibar sambamba na yale yanayojiri siku hadi siku.

Wanajipa moyo sana kwamba sasa wanaelekea kupata nchi yao mana katiba ya Zanzibar , inatamka wazi kwamba Zanzibar ni nchi kwa marekebisho yaliyofanywa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa,lakini mambo sivyo yalivyo.Katiba mpya ijayo ni dudu lakuwaeneza sumu wakafa na wao wenyewe ikiwa haya niyasemayo watayadharau, achilia mbali nchi yao.Muswaada wa katiba mpya una mapungufu kadha wa kadha wakuimaliza Zanzibar kupitia muungano lakini Wawakilishi na Wabunge wa Zanzibar wamekaa kama waliopigwa na bumbuwazi vile.Mbunge mmoja aliishia kusema “kwa hali hii Wazanzibari hamututaki…lakini muungano huu hatukuja na sahani kuomba chakula bali mlitoa kilo mbili na sisi kilo mbili….” na akaishia hapo kuitetea Zanzibar hatimae kitanzi kikapita cha kuinyonga Zanzibar wakati nae anashuhudia.Wazanzibari wanapaswa ukweli huu waujue kwasababu ni matunda ya Wahafidhina wao.

Ni ukweli usiopingika kuwa Watanzania walio wengi wametawaliwa kifikra,hasa wale ndugu zetu kule Zanzibar.Wengi watalikataa hili kwa sababu kipimo cha uhuru wao ni mambo mawili.
Moja ni kule kutembea bila minyororo miguuni na mikononi au watu wakuwasimamia eti sasa wako huru mda wote kwenda watakako.Kwa mimi nitauita Uhuru wa kiwiliwili.La pili ni kule  kupeperusha bendera zao za kujitawala tangu tarehe 9 Disember 1961 kwa Tanzania bara na eti 12 January 1964 kule Zanzibar.Watanzania hawa wamesahau kwamba “jiko moja haliinjiki chungu”.Uhuru wa kiakili ambao huzaa fikra za maendeleo na utamaduni wa heshima tena wakupigiwa mfano,wameusahau na kuudharau wakatosheka na uhuru wa mawili yale.

Ukitaka kujua namna Wazanzibari walivyozama katika utumwa huu leo ,zungumzia utamaduni wao wa Kiislam,utamaduni uliowajengea heshima na utu wao ukadhihiri. Wanawake-vijana kwa wazee- ukiwagusia jambo la kujistiri, wengi wao watakwambia “nijitie maguo na joto hili? Babu samahani,acha nijipe raha.Raha mtu ajipa mwenyewe’’.
Kwake yeye kujitia kibandiko ndio sahihi na usasa, badala ya kulinda utu wake kwa kuvaa mavazi ya heshima.Hapa wenzetu Wamagharibi wamefanikiwa sana kuzitawala akili za vijana wengi wa Kitanzania hususan Wazanzibar mana ni Waislamu asilimia 99.Lengo kuu la wenzetu hawa ni kubadilisha akili na fikra (mind set) za vijana ili waone utamaduni wa magharibi ndio sahihi na mujarrabu kwa dunia ya leo kusudi utamaduni wao upate nguvu,kumbe utamaduni wao ni upotevu mkubwa ambao humtoa mtu katika uungwana akabaki kama mnyama pori tu.

Sheikh Abdul-aalaa Maududi katika moja ya hotuba alizopata kuwahutubia Wanafunzi wa vyuo vikuu anasema, “Imethibitika kwamba taifa lolote likikosa ustaarabu wake wa kitaifa na likajivika ustaarabu wa taifa jengine,hiyo inamaanisha kwamba taifa hilo limetoweka na kupotea”(soma Abdul-aalaa Maududi ‘Jukumu la Wanafunzi katika kuijenga hali ya baadae ya Ulimwengu wa Kiislamu uk:8”).Maana ya maneno haya ni kubwa mno lakini kwa ufupi katika kuakisi hali ya Zanzibar ,Wazanzibar kutokana na kutawaliwa kifikra na wakaona bora utamaduni wa Wamagharibi, wakaacha utamaduni wao wa heshima,tafsiri yake taifa lao limo mbioni kupotea na mda si mrefu wale wavuta unga wachache waliopo,makaka poa na madanguro,yataongezeka mithili ya mapovu ya bahari.


Huko nisiende sana, kwani azma yangu hasa ni kuonesha namna Nyerere pia alivyotumia propaganda na ghilba mbalimbali kutawala akili za Waislamu.Waislamu wa Tanganyika na Zanzibar walighilibika na maneno ya tapeli huyu yaliyo waasa na kuwataka wasichanganye dini na siasa huku yeye akikoroga hasa na sio kuchanganya tu kupitia mwevuli wa chama.Padri John C,Sivalon anasema “Nyerere ambaye mwenyewe ni mkatoliki,alikuwa na uhusiano wa karibu sana na viongozi fulani wa kanisa na hivyo alionekana kuwa ni kiungo kati ya Kanisa na Serikali…”Uk:11.

Nyerere aligundua ufaafu wa njia hii ya kuwatawala watu kifikra na kweli alifanikiwa maana alikuwa akinywa juisi kwa mrija na furaha tele pamoja na Wagalatia wenzake huku Waislamu wapigania uhuru wakionja joto la jiwe, wakiteswa ni uzalendo wa nchi yao.Waislamu wa Zanzibar waliokuwa wakijinata kipindi hicho kwa maadili mema na uchumi bora,leo maisha yao ni yakubahatisha-hohe hahe- lakini bado hawajasita kulinda chama na muungano badala ya Utu wao.

Nyerere alizitawala akili za Wazanzibari wahafidhina,akapandikiza chuki baina yao kwa misingi ya chama,wakasahau matakwa ya dini yao(Uislamu).Hatimae wakawa mawakala wazuri kuwatelekeza ndugu zao wakauwawa kinyama huku wengine wakinajisiwa kwa amri ya  mwanafunzi aliefunzika tena aheshimuye ukatoliki wake aliofunzwa na mwalimu wake,januari 26 na 27,2001 kule Unguja na Pemba, ndugu  Binjamin William Mkapa .Siku ile Maaskari walipandishwa vyeo si kwasababu ya elimu zao,bali kutokana na kukamilisha azma ya Watawala(Zanzibar na Tanganyika) ya kulinda chama na ushindi wa kishindo maana kama hayakutokea yale mauaji, kishindo ilikuwa hakijakamilika.

Kiongozi wa Zanzibar pia alishadidia na kusifu jitihada za Maaskari kuwaauwa wengi katika watetea haki zao, kwasababu akili yake ilikuwa haiwazi chochote ispokuwa matakwa ya watawala wake.Kibaya zaidi, Wahafidhina hawa waliendelea kuitikia “Daima” kwa sauti yakupendeza tena yenye kila ithbati ya kuridhika juu ya kila yaliyokuwa yanaendelea, kila panadiwapo “Mapinduuuuziiii!” Yote haya yalikuwa matokeo ya utawala aliouasisi Nyerere kupitia ile ile ghilba na kwa bahati mbaya sana Wazanzibari hawakujua kama wanatumiwa na mpaka leo kuna wengine hawajazinduka.Ndugu zangu hawa wa Zanzibar walisahau kua,Nyerere na wagalatia wote waliosalia wenye mamlaka na wasio mamlaka,kike kwa kiume azma yao kubwa ni kuhakikisha zile asilimia za Waislamu zinazotajwa kuwepo, zinabakia kama hadithi za kale.Ukiangalia waraka unaoelezea mafanikio ya wakatoliki Zanzibar utathibitisha hili.Kipengele kimoja kina sema “Sera zilizopo hivi sasa kwa upande wa uingiaji na utokaji Zanzibar imetusaidia sana katika uingizaji wetu(Wakristo) kutoka Bara na hivyo kusaidia kufuta ile imani kuwa Zanzibar ni kisiwa cha Waislamu eti Wazanzibari kwa zaidi ya asilimia 99 ni Waislam.Ujaji wa Wakristo kwa wingi kutoka Bara umewezesha kuongezeka kwa idadi ya mabaa na vilabu vya pombe.Hivi sasa ni jambo la kawaida kuona magari ya aina mbali mbali yanayomilikiwa na eti Waislamu yamebeba kreti za bia na pombe kali”

Sambamba na hilo,masheha wahafidhina huwakumbatia wagalatia wageni kwa kuwapa vitambulisho vya “Uzanzibari Ukaazi” kwa misingi ile ile ya chama ambapo Wazanzibari wazawa hawapewi,wanaitwa wageni kwa sababu tu ya itikadi tofauti za chama.Mambo yote haya ni matunda ya kutawaliwa kifikra.

Waraka unaendelea kuainisha mafanikio ya Makafiri Zanzibar kwa kusema “Hali ya kutoelewana kisiasa baina ya Wazanzibari imetoa mwanya kwetu kuingiza vijana wa Kikristo wenye asili ya Bara kwa wingi kwani wamekuwa wakiaminika zaidi kuliko vijana wa Zanzibar……Kwa upande wa mashamba(vijijini) tumepata wasaa mzuri wa kununua ardhi toka kwa Waislamu ambao hadi sasa bado hawajashtuka.Ardhi hizi zimetuwezesha kujenga makanisa kadhaa ambayo hapo awali hayakuwepo.Idadi ya skuli na vituo vyetu (ambavyo licha ya picha ya juu kuwa haviendeshwi kwa misingi ya Kikristo lakini kiukweli ni vituo vya kimisionari) vimeongezeka kwa hali ya kuridhisha”

Kwa upande wa Muungano nao, namna ulivyo asisiwa ulipokelewa kwa shangwe na Wahafidhina bila kung’amua utapeli uliopitishwa na fundi yule wa kuimeza Zanzibar .Mafanikio yote ya Wagalatia Zanzibar ni sababu ya muungano feki kupitia wahafidhina ambapo sasa hata utamaduni pia umevurugwa kiasi cha kutupwa.Muungano ni jambo jema sana lakini ukiangalia namna ulivyoletwa, ulikuwa sio ule wakuleta neema Zanzibar na Tanganyika kwa usawa bali kuinakamisha Zanzibar kupitia utapeli wa  Chama.

Jengine kubwa kupitia muungano,Wazanzibar walinyimwa na wanaendelea kunyimwa haki yakumchagua wamtakae,mwenye uzalendo na nchi yake ambapo raisi hawi raisi mpaka achaguliwe Dodoma kupitia misingi ile ile ya kudumisha chama kumbe yote yanatendeka kukiwa na koti la ghilba na malengo hasi dhidi ya Zanzibar.Mgombea na Raisi atakaechaguliwa Dodoma-kwa sababu hakuna kushindwa kwa CCM wakishapeleka vibaraka vyao siku ya matokeo ya uchaguzi-(Bwana Ali Hassan Mwinyi na Mkapa anaetiririka mate kutaka kuwafuta Wazanzibari katika ramani ya dunia kwa vile alipewa wasia na mwalimu wake)-WanaCCM wa Unguja na Pemba hawampingi tena eti ukimpasua atatoka rangi za bendera mgombea wao,hata kama utu na huruma ya kulinda wenzake haipo.

Pia Nyerere alipendekeza chama kiitwe CCM (Chama Cha Mapinduzi),kwa ushawishi huku akificha ajenda ya siri juu ya maana ya herufi hizi tatu.Baada ya hapo mahubiri yaliyofanywa kuelezea azma ya chama hichi yalijaa matumaini ya kuendeleza nchi bila ubaguzi halafu nyimbo mbalimbali zikaimbwa za chama kwa sauti nyororo moja ikiwemo “Chama Chetu Cha Mapanduzi chajenga nchi” huku watawaliwa wakiikariri kila uchao.Lakini kumbe lengo lake ilikuwa ni kuwaziba macho Waislamu hasa wale wa kule Zanzibar kwani wangejua kilichojificha nyuma ya pazia juu ya maana ya herufi hizi tatu,wasingekubali kamwe kupokea jina hili na kulishangilia.Ila kwa sababu walitawalia barabara kifikra waliitikia “Hewallah Bwana” bila kufikiria upande wa pili wa shilingi huku wakimuogopa Nyerere kama Mungu.

Nyerere alikitumia kifupi CCM kama kichaka cha kuwahujumu Waislamu Tanzania na kuwafanya omba omba Wazanzibari kama walivyo leo huku mapembe kikiwa chakula chao cha ajiwezae kwa sasa.
Ni dhahiri kwamba maana halisi ya Chama hichi, Wakereketwa wataipinga na watahisi kama ni hujuma lakini ukweli utabakia kuwa ukweli siku zote.Sina nia kabisa yakuhujumu chama chochote ila ukweli tu ndio ulionisukuma kuyasema haya kinaga ubaga kuwaamsha Waislamu Tanzania kwa ujumla wao na Wahafidhina kule Zanzibar.
Dhamira yangu ni kuwaweka huru kiakili na kimwili.Ukweli ndio ngao kwa wale waliotengwa na ulimwengu wa habari sahihi, maana yote hayo wakati yakitokea chini ya msimamizi wao(Nyerere) walidhani ndio sahihi kumbe sivyo kabisa.Nyerere alitumia ghilba na propaganda mbalimbali kuwazuzua Watanzania na Waislamu wakiwemo Wazanzibari kwasababu msingi hasa wa utawala wa kifikra hutokana na mawili hayo.

Kama tulivyosema awali kwamba Nyerere aliwaasa watu kutochanganya dini na siasa ilhali yeye alikuwa akikoroga badala ya kuchanganya tu,ndivyo vivyo hivyo alivyofanya katika uteuzi wa jina la chama.Alikiita Chama Cha Mapinduzi kumbe ni Christian Church Movement ,Sawa na CHADEMA leo(Soma kitabu “Nyerere Against Islam In Tanganyika and Zanzibar”.Ambacho unaweza kukipata pia kwenye mtandao).Azma ya Nyerere na wakatoliki wenzake ni kueneza ukristo Tanzania bara na visiwani lakini hasa Zanzibar na ndio maana leo hii makanisa na mabaa yanachipua kila siku kwa idadi ya kutisha kila uchao, wakati wenyewe wakikaa tu wakikhadithiana sehemu za kupata urojo mtamu.Nadhani utapata picha juu ya ubaya wa utawala wa fikra.

Ithbati ya jina lililofichwa kwa manufaa ya wachache inapatikana pale Padri,Dr.John C.Sivalon katika kitabu chake aliposema “katika kuelezea uhusiano maalum wa kanisa Katoliki na viongozi wa CHAMA na SERIKALI,tumeshagusia kidogo nia ya viongozi wa Kanisa katika kujenga uhusiano huo kwa njia ya utume wao wa kijamii.Kwa mfano,katika maneno ya yule Askofu aliyekaririwa katika sura ya pili,alisisitiza kuwa lengo moja la mafundisho ya uongozi kwa walei lilikuwa kuzuia Chama cha kupigania uhuru kisiangukie mikononi mwa mawakala wasiofaa.Katika barua iliyopelekwa Vatikano sababu mojawapo iliyotajwa ya kumuunga mkono Nyerere ilikuwa kwamba itakuwa kwa faida ya Kanisa siku zijazo…”uk:26.Maneno haya yanaweka wazi kile kinachojiri leo Tanzania,Waislamu kunyanyaswa na kunyimwa haki zao mchana kweupe na Zanzibar kupoteza hadhi yake na maadili mema yaliyokuwepo dahari kwa dahari.Baraza la mitihani pia kwa sababu lilipachikwa Wakatoliki safi,limekuwa likitumika kama chinjio la watoto wa Kiislamu kwa miaka yote.Nyerere wakati wa uhai wake alikuwa kiongozi wa dini,chama na serikali kwa wakati mmoja na kweli alitumia nyadhifa zake kupitia vitatu hivyo na kuwapeleka Waislamu hapa walipo leo huku Waislamu wenyewe wakiendelea kuimba msemo wa kizushi kwamba “hakuna kuchanganya dini na siasa” kwasababu tu Nyerere aliukariri msemo huu kwa maneno ya ghilba kwa kuficha akifanyacho yeye na wenzake.

Sambamba na hilo Padri Sivalon anasema hata maamuzi ya serikali yanafanana na Kanisa jambo ambalo linaakisi usahihi wa jina husika lililofichwa.Ukurasa wa 16 unaweka bayana kwa kusema “Muhimu zaidi ni kwamba shughuli na mazingira ya shule za bweni zimewezesha hadi sasa kukua kwa uhusiano kati ya viongozi wa kanisa na wa Serikali na Chama.Hali hii imefanya matendo, msimamo na uamuzi wa Serikali ufanane mara kwa mara kwa namna moja au nyengine na mafundisho na mwelekeo wa Kanisa”. Mfano mzuri ni yale maamuzi ya serikali kutokubaliana na  mapendekezo ya Waislamu juu ya kujiunga na OIC na lile shinikizo la Zanzibar kuitaka kujitoa OIC na ikajitoa,kuanzisha Mahkama ya kadhi kupitia serikali na kuvunjwa kwa makubaliano ya kanisa katoliki na Serikali juu ya kuchotewa mabilioni ya fedha ya walipa kodi  wakiwemo Waislamu kwa idadi yao kubwa,kunufaisha Kanisa na taasisi zake.Wakatoliki wanaendelea kujiimarisha kila jua lichomozapo kupitia fedha hizo ambapo sasa wameenda mbali zaidi kuwaritadisha Waislamu wa vijijini kutokana na umaskini wao,kununua ardhi na nyumba kule Zanzibar kwa bei kubwa na kujenga au kubadili kuwa makanisa na vituo vyao vya kigalatia.Wanaendelea kujenga hospitali zao kule Zanzibar na Tanzania Bara huku wakieneza Ukristo wao wakati Waislamu wameachwa hatua mia nyuma na serikali yao.

Pia vilabu vya pombe vimekuwa ni jambo la kawaida sasa, ambapo madanguro si kitu cha kushangaa tena Zanzibar.Wahafidhina walitawaliwa na wakashindwa kuona hujma hizi huku wakilinda chama cha watu, chenye malengo tofauti na yale yahubiriwayo majukwaani.Bwana mkubwa aliiandaa mbinu hii kwakushirikiana na wagalatia wenzake zilizojaa maneno ya kilaghai kuwahujumu Waislamu na Uislamu wao lakini kwa ubaya wa bahati wengi wao walishindindwa kung’amua haya na mapaka leo wengine wanaendelea kutumiwa na Makafiri.

Wahafidhina wa Zanzibar huwaambii kitu juu ya CCM hata kama uhuru wa nchi yao umepotea kwa njia za kutatanisha,mabinti zao wanafanywa kama biashara mahotelini kwa sababu ya umaskini,wazee,watoto na vijana wote wanaimba wimbo mmoja wa hali ngumu za maisha.Watoto wanavitumbo kama wajawazito-utasema wamebahatika kupata ujauzito kabla ya umri kumbe ni utapia mlo,hospitali zao kama majumba yaliyohamwa karne nyingi zilizopita,majumba mengi kama yaliyonyeshewa na mvua yenye kemikali ikababua rangi kama ilivyotokea kule Ujerumani ,bara bara haziridhishi,biashara hazifanyiki kiasi kwamba yatosha kusema ukame umetanda-dhiki,balaaa mtindo mmoja- lakini bado hata hiyo afadhali yao ya serekali ya umoja wa kitaifa waliyoipata kama mkongojo wao wanaihujumu.Haya yanathibitsha namna ambavyo kutawaliwa kifikra ni kubaya mno tena kiasi cha kutisha.

Harakati zote alizoziasisi Nyerere za hujma hizi zilikuwa na mafungamano ya moja kwa moja na chama husika na serikali.Waislamu Tanzania bara waliponzwa na uzalendo wa nchi yao kwa kuamini ghilba ya Nyerere wakati Wazanzibar walibakia kama watu wenye utindio wa ubongo.Walikubali maagizo yote yaliyokuwa yakitolewa na bosi wao bila kupima usahihi na mafanikio yao kwa dhana ya kulinda chama.Mfano mzuri ni mauaji ya tarehe 26 na 27,2001 na kunajiswa Waislamu Zanzibar yaliyofanywa na serikali ya rais mstaafu William Benjamin Mkapa kupitia migongo ya Waislamu waliotawaliwa kifikra wakashindwa kuona uadui wa Wagalatia na mauaji ya Mwembe chai mwaka 1998.

Kitabu cha Dr.John C.Civalon cha Kanisa Katoliki na Siasa Ya Tanzania Bara,1953 hadi 1985,uk:21 kinaeendelea kutoboa siri kwakusema “Hivyo kutokana na Nyerere kuwa Mkatoliki,na kuwa kiini cha kundi la watawala,alikuwa kiungo muhimu kati ya kanisa na serikali.Uhusiano huo uliimarishwa zaidi na shughuli za viongozi muhimu wa Kanisa ambao walimsaidia Nyerere katika mambo ya siasa na nafasi yake katika kuiongoza TANU..”
Kwa ushahidi huo ambao Wagalatia hawawezi kuupinga,ni wakati sasa Waislamu kufanya mambo yafuatayo hususan kule Zaznzibar:-

Moja,Kuangalia kwa umakini muswada wa utungaji wa katiba mpya.CHADEMA wanalalamika kwamba eti Zanzibar imepewa nafasi kubwa lakini inafaa ifahamike kuwa ajenda yao na wakatoliki wengine inafanana, ya kuimeza Zanzibar na kuifanya sehemu isiyo na maadili ya Uislamu hivyo hata kizazi kijacho kiishi kama wanyama tu kwa kukosa Utaifa wao.Nimesisitiza kuangaliwa vyema kwa muswada wa mabadiliko ya katiba kwasababu bado kipengele cha muungano kina utata.Muswaada haukutoa uhuru wa Muungano kujadiliwa kwa njia ya kukubalika au laa,bali kuimarishwa bila kuonesha uwezekano wa mapendekezo ya Wazanzibari kukubaliwa iwapo watahitaji ujadiliwe upya,hivyo hili ni dudu jeusi,katika jiwe jeusi kwenye kiza totoro.

Pili, Wazanzibari wanatakiwa wajue kwamba muungano uliopo ni wa ghilba na ndilo kaburi lao hivyo waangalie upya tena kwa umakini mkubwa.Vipengele vya muungano hasa majeshi ya ulinzi, uchumi na mapato, fedha na matokeo ya uingiaji hovyo hovyo wa wagalatia kumeifanya Zanzibar si chochotee si lolote na kuwa koloni la Tanganyika.Leo Wazanzibari hata ushuru wanalipa tena mara ya pili hata kama Zanzibar wameshalipa, jambo ambalo limewaangusha kiuchumi na bandari yao pia imedhoofishwa na muungano.

Tatu,Waislamu wote wanapaswa kufanya kazi kama Waislamu kuirejesha Zanzibar kwenye utu na uchumi bora badala ya mgawanyo wa vyama wakileweshwa na usemi wa mwalimu wao wa kutokuchanganya dini na siasa.Wajue kua dini ni mfumo mzima wa maisha kama alivyojua Nyerere akawafikisha kuwa wakatoliki watarajiwa kwa dhiki za maisha walizonazo leo ambapo aliwagawa ili awatawale.Zanzibar inapaswa kuendeshwa Kiislamu hata kimfumo wa mabenki na taratibu zote za uchumi.elimu,siasa,jamii na utamaduni.Itakuwa ni vichekesho na msiba mkubwa kuona watu wenye muongozo wao tena sahihi wakauwacha kwa kisingizio cha “u-secular” wa Nyerere .

Nne, Waislamu kwa ujumla wanapaswa waelewe kwamba jina la Chama wanalohubiriwa siku zote ni la kuwatawala kifikra na usahihi wa jina umefichwa kwa malengo binafsi ya Wakatoliki.Angalia idadi ya wakatoliki kwenye chama na serikali ambapo Waislamu wachache waliopandikizwa lengo kuu ni kuwaziba macho na wao waone mbona wamo.Pia maamuzi yanayofanywa na chama na serikali dhidi ya Waislamu ni uthibitisho tosha wa usahihi wa jina lililofichwa nyuma ya pazia.

Mwisho, Waislamu wa Tanzania Bara na Zanzibar wanapaswa washughulike kwa namna inayofaa.Katika Uislamu mtu haki yake anachukua hasubiri kupewa na imefika mda wa kusema sasa basi kutawaliwa kifikra na kupelekwa pelekwa kama punda. Waislamu wasikubali tena kutumiwa na kurubuniwa kwa utapeli wa maneno uliowafikisha kuwa watu wa daraja la tatu katika jamii.Wazanzibari wanapaswa waelewe kwamba CHADEMA kimejivika joho la ghilba la uzalendo na eti  kuguswa na dhiki za wananchi lakini ajenda yao siyo waihubiriyo.Kinachohuzunisha kuna waitwao Wazanzibari wauzao dini yao kwa dunia kwa vijisenti vichache lakini yafaa waelewe kuwa Chadema hawana nia njema nao.Wametekwa  kifikra na CHADEMA na wengine ni wanachama hasa, wakisahau kauli ya Wabunge wa Chadema bungeni ya kutaka Zanzibar ipunguzwe nguvu na wakadiriki kusema si nchi.Wazanzibari hili nalo neno lifikirieni na mkishindwa kutumia bongo zenu kwa manufaa yenu na nchi yenu na vizazi vyenu vilivyopo na vijavyo,msubiri kusulubiwa msalabani.


Share this article :

0 comments:

Speak up your mind

Tell us what you're thinking... !

ZILIZOSOMWA SANA.

Followers

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Proudly powered by Blogger
Copyright © 2011. Msamaa. - All Rights Reserved
Template Design by Creating Website Published by Mas Template