- Msamaa.
Headlines News :
Home » »

Written By Unknown on Thursday, March 21, 2013 | 11:10 AM


MAUAJI YA 2001-ZANZIBAR.


Mauaji ya Kutisha ya Elfu Mbili na Moja

DIBAJI YA WAANDISHI

Mwanzo wa kuandika kitabu cha kumbukumbu za mauaji hatukujua tuanzie wapi. Hii ni kwa sababu hata huko enzi ya siasa za ukoloni pia kulikuwa kukitokea rabsha, fujo na wakati mwengine mauaji. Hata hivyo, tulipoangalia huko tuliona mauaji yalikuwa yakichukua sura halisi ya mapambano ya kikabila ambayo yaliweka nchi yetu katika hali ya kitabaka. Katika fujo na mauaji ya wakati ule, dola ilikuwa na kazi moja tu. Sio kuukinga upande mmoja na kuuangamiza mwengiine, bali ni kuwa msuluhishi baina ya makundi na hata kubuni njia bora za kuleta amani baada ya kusikiliza pande zilizozozana.

Hapa tulipata funzo halisi la historia ya nchi zetu kuhusu migogoro ya kisiasa ambayo wengine wanajaribu kusema kwamba ni ya muda mrefu na inajirudia kama tabia ya mambo ya kihistoria. Funzo lenyewe ni kuwa, kumbe misuguano ya kijamii enzi hizo ilikuwa ni jambo la kawaida sio kwa Zanzibar tu bali kwa nchi nyengine katika Bara la Afrika na duniani kote. Ukweli unabakia kwamba katika mahusiano ya dola na pande zilizogombana, dola ilikuwa makini kuwa msuluhishi ili taathira ya mapambano isiendelee.

Kwa hivyo, tukapata majumuisho kwamba, kwa kuwa mapambano katika siasa za leo si ya makundi miongoni mwa watu katika jamii, basi hayawezi kamwe kulinganishwa na yale ya enzi ya kikoloni. Kwa maana hii, ni dhahiri basi siasa za zamani si sababu nzito za kuelezea mauaji ya Januari 26 na 27, 2001.

Vile vile, kwa sababu hii ya dola ya zamani kuwa msuluhishi wa matukio mbali mbali, tulichukua muda tukaiangalia dola katika siasa za leo na kugundua kwamba, sio tu kwamba dola ya leo inakuwa msuluhishi, lakini ndio muhusika mkuu wa kupanga na kuendesha vituko, fujo na hata mauaji katika jamii. Ndio maana, pamoja na kwamba maandamano ya Januari 27, 2001 yalikusudiwa kuwa ni ya amani lakini dola kwa kutumia vyombo vyke iliyasitisha kwa risasi za moto. Kuanzia hapo, dola iliendesha mauaji siku ya nyuma yake (26 Januari, 2001) dola ilifanya mauaji hata bila ya hata kuwepo kwa maandamano.

Kama tutavyoona katika sehemy ya historia, Zanzibar ilikuwa ikipita katika vuguvugu la matukio ya vurugu za kisiasa na mara nyengine mapambano ya kijamii, lakini wakati haya yakitokea mara zote dola iliingilia kuzima kuliko kuendeleza. Baada ya uhuru na muungano wa Tanganyika kuliko hata ilivyokuwa katika siasa za kupigania uhuru. Mwaka 1972, aliekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania Bwana Ali Hassan Mwinyi, alilazimika kujiuzulu wadhifa wake baada ya mauaji makubwa yaliyoendeshwa na Polisi dhidi ya raia. Mauaji mengine ni yale Mwembechai ya mwaka 1998 pamoja na mauaji yaliyohusisha mahabusu wa Gereza la Bulyankulu ya mwaka 2002 kwa kutaja machache.

Kwa upambanuzi huu, tumegundua kwamba historia ya Zanzibar sio tu inapooshwa na baadhi ya waandishi wa historia za kuunga, bali vile vile inatumiwa kuhalalisha maovu ya dola kwa jamii. Hili la mauaji ya Januari 26 na 27 lilifuatiwa na msululuu wa matukio ya unyanyasaji, ubaguzi, ukandamizaji na mateso ya kila aina. Yote haya yakifanywa na dola, na imejidhihirisha kwamba mauaji yameshamiri hasa baad ya kuja mfumo wa vyama vingi kuanzia mwaka 1992. mfumo huu haukupokewa vibaya bali uliletwa vibaya, kwani pamoja na kujigamba kwamba umekuja kwa ridhaa ya Chama tawala, ilikuwa ni dola ya chama tawala iliyohakikisha kwamba upinzani hauji juu Tanzania ili siku zote kuthibitisha ile dhihaka ya awali kwamba waliokubali ni asilimia ndogo.

Kwa kupata muhtasari huu, ni dhahiri basi chimbuko na chanzo cha mauaji ya tarehe 26 na 27 Januari, 2001 ni kutokana na dola ya Tanzania kuipiga teke demokrasia na kujizatiti kwa kuendesha vitendo vya kunyima uhuru na kuoheshimu haki za binaadamu kinyume na Katiba za Tanzania. Hali hiyo ilipelekea chaguzi za vyama vingi za 1995 na 2000 kufanyika katika mazingira mabaya kwa kila hali. Kufurukutakwa wananchi kukataa ubaya huu ndiko kuliko sababisha dola kufutuka, kuhamaki na kuvinjari kuua. Ndio maana hata Rais Mkapa akakiri kwamba Tanzania imeingia dowa, kwani si jambo la kawaida kwa nchi kama Tanzania ambayo hapo nyuma iliwatumia Watanzania kusaidia ukombozi wa nchi nyengine kwa hali na mali, leo vyombo vyake dola vigeuke na kuanza kuwahujumu wananchi.

Doa lilikuwa kubwa kwani kwa mara ya kwanza Tanzania ilitoa wakimbizi wa kisiasa badala ya ile tabia iliyojijengea ya kupokea kutoa nchi nyengine. Si hayo tu, dowa lilikuwa kubwa zaidi pale majeshi yetu yalipoacha matumizi ya busara na nidhamu ya muda mrefu na badala yake yakatumbukia kufanya unyama, jirani na uhalifu wa kivita kwa raia wasio silaha kwa kuwararua kwa risasi wanaume huku wakiwaingilia akina mama bila kisisi.

Tulijiuliza mengi iwapo Majeshi yaliyofanya vile ni ya kutoka nchi na waliouliwa na kudhalilishwa kiasi kila ni raia wan chi ipi? Basi hata Jeshi la Wananchi wa Tanzania! Kwa nini wauwaji wapongezwe na huku familia za waliouliwa wakebihiwe na badala ya kufarijiwa ? si kebehi ya maneno tu ya viongozi wakuu wan chi, bali hata “Ripoti ya Tume ya Mbita” iliyopewa jukumu la kuchunguza mauaji ilidhihaki? Lakini jiulize suala moja zaidi kabla ya kuendelea ambalo ni iwapo Tume ya Mbita ilichaguliwa na Rais wa Jamhuri ya Tanzania ambae ndiye Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi yaliyofanya mauaji, nini ungetaraji katika Ripoti ya Tume hiyo? Tanzania twaelekea wapi? Kwa masuala haya Watanzania wenyewe ndio wenye majibu.

Yalipotokea mauaji haya, Tanzania haikuwa ikipigana vita, ingawa hata kama tungekuwa katika vita basi bado Majeshi yetu sio tu yangepewa amri ya kuuwa, lakin baadae Jumuiya ya Kimataifa ingestahiki kuyaweka katika makundi ya majeshi yaliyoendesha uhalifu wa kivita na kuyafikisha mahkamani kama vile inavyofanywa kwa majeshi ya Burundi. Hata hivyo, baada ya mauaji na uhalifu huu wa kutisha kumalizika, baadae tulipata Muafaka. Utekelezaji wa Muafaka huo (hasa kwa mambo madogo ambayo yamo ndani ya uwezo wa Rais wa Zanzibar) bado unasuasua.

Suala sasa sio Watanzania tunaelekea wapi, suala ni jee Watanzania tunaelekezwa wapi? Ndio kweli tumeshaamua kuangalia mbele na kuacha tulikotoka? Ndio maana Mwenyekiti wetu Profes Lipumba akasema, “tunaweza kusamehe lakini ili tusirejeshwe tena tena tulikotoka, basi tusiyasahau yaliyotokea tarehe 26 na 27 Januari, 2001”.

Huku waandishi wa kitabu hiki wakiwatakia heri wasomaji, pia wanachukua nafasi ya mwanzo kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kumudu kazi hii pamoja na kuwapongeza wote waliochangia hoja na maarifa ili kazi hii ikamilike.

Kwa niaba ya The Civic United Front (CUF – Chama cha Wananchi)

Waandishi wa Kitabu

Julai 2003

 

 

 

 

 

 

 

 

SURA YA KWANZA

UTANGULIZI

Utangulizi wetu unahusu mambo ya kihistoria kwa ufupi.  Tunatanguliza historia kutokana na umuhimu wake wa kutukumbusha tunakotoka.  Tanganyika na Zanzibar zina uhusiano wa muda mrefu kutokana na sababu za kijiografia.  Ingawa kisiasa zinatafautiana, watu wa nchi hizi wamekuwa na mahusiano hata kuchanganya damu.  Wakati Tanganyika ikiwa chini ya utawala wa Kijerumani, Zanzibar ilitawaliwa na tawala za Kisultani za Oman na baadae kuwa katika himaya ya Uingereza.  Baada ya Uhuru wa 1963 na baadae Mapinduzi ya 1964, Zanzibar ilifanya Muungano na Tanganyika ambayo nayo ilikwishapata uhuru tokea mwaka 1961.  Madhumuni makubwa ya sehemu hii ya kihistoria ni kujikumbusha tutokako kisiasa na kiuchumi ili historia ituongoze kufahamu leo tulipo katika uhusiano wa kisiasa na kiuchumi baada ya miaka 40 ya Muungano wetu.

Sehemu ya 1: Tanganyika na Zanzibar – Historia fupi

1.1.1    Uhusiano wa Kihistoria

Kihistoria nchi za Tanganyika na Zanzibar zimekuwa na uhusiano wa muda mrefu hasa kutokana na ukaribu wake kijiografia.  Ukaribu huu umewafanya watu wa nchi hizi hasa katika sehemu za mwambao kuwa na mashirikiano na mahusiano hata ya damu kwa karne nyingi, hata kabla ya kuzaliwa Nabii Issa, (Othman, 1996).  Wavumbuzi na wafanyabiashara wa kigeni hasa kutoka Uajemi walizitembelea sehemu za pwani ya Afrika Mashariki mnamo karne ya 7AD na kupafanya Zanzibar kuwa kituo kikuu kwa serikali za miji hiyo ya mwambao.  Baadae, mwanzoni mwa karne ya 18 watawala wa Kiarabu walianza kuja katika sehemu hizi za mwambao ambapo, pamoja na kuitawala Zanzibar, pia waliifanya kuwa ni Makao Makuu ya tawala zao ambazo walizipanua kuelekea sehemu za Bara.  Vile vile, kwa mujibu wa (Gray,1962), katika karne ya 19 wavumbuzi wa Kizungu pamoja na Wamishionari, nao waliitumia Zanzibar kama kituo cha kujipenyeza katika Bara la Afrika.

1.1.2    Tawala za Kikoloni

Kisiasa, historia za Tanganyika na Zanzibar zinatafautiana.  Kufuatia Mkutano wa Berlin wa mwaka 1884/1885, Tangayika ilianza kuwa chini ya Utawala wa Kijerumani.  Wakati huo, tayari Zanzibar ilikuwa inatawaliwa na Seyyid Said, Sultani wa Oman aliehamisha makao makuu ya utawala wake kutoka Oman na kuanzisha utawala wa Al Busaidy katika visiwa vya Zanzibar.  Baada ya kumaliza utawala wa Seyyid Said, mtoto wake Seyyid Ali bin Said alitawala.  Wakati huo kulitokea mvutano wa mataifa ya Ulaya kuiwania Afrika ya Mashariki, na Seyyid Ali aliruhusu Zanzibar kuwa chini ya Himaya ya Waingereza [British Protectorate] kuanzia tarehe 4 Novemba, 1890, [Hollingswomth, 1953].  Halkadhalika, kufuatia kushindwa kwa Mjerumani katika vita vya kwanza vya Dunia, Umoja wa Madola (League of Nations) uliyagawa makoloni ya Mjerumani kwa nchi zilizomshinda.  Kutokana na hali hii, nayo, Tanganyika ikagawiwa na kuwa chini ya utawala wa Mwingereza kwa amri ya Umoja wa Madola na baadae chini ya utaratibu wa udhamini wa Umoja wa Mataifa [bates, 1957].

Jambo la msingi la kuzingatia katika tawala zile za Mwingereza kwa Tanganyika na Zanzibar ni kwamba, licha ya nchi hizi kuwa chini ya mtawala mmoja, lakini utaratibu wa kiutawala wa kila nchi ulitafautiana.  Gavana wa Kiingereza wa Tanganyika alikuwa anawajibika kwa Wizara ya Makoloni London; na kila baada ya muda, Serikali ya Uingereza ilitakiwa kuwasilisha taarifa Umoja wa Madola na baadae Umoja wa Mataifa, [Kaniki, 1979].  Kwa Zanzibar, pamoja na kwamba Mtawala wa Kiingereza aliwajibika moja kwa moja kwa Waziri wa Makoloni mjini London, hata hivyo, katika maamuzi yake ilimbidi kutilia maanani hisia za Sultani wa Zanzibar.  Aina hii ya uwili wa kiutawala hata hivyo, haukumaanisha kwamba Zanzibar ilikuwa ikitawaliwa na nchi mbili – yaani Oman na Uingereza.  [Shariff na Ferguson, 1991], wanaeleza kwamba, mtawala hasa alikuwa Mwingereza.

1.1.3    Uhusiano wa kisiasa

Kwa mujibu wa historia, Jumuiya ya African Association iliundwa Tanganyika katika mwaka 1929 na kufungua tawi lake Zanzibar mwaka 1934.  kwa sababu hii, wengi wa wafuasi wake hapa walikuwa Wazanzibari waliokuwa na asili ya Tanganyika [Othman H., 1996].  Madhumuni makuu ya chama hiki yalikuwa ya kijamii hasa kwa Waafrika wa Dar es salaam na sehemu nyengine za mijini.  Kwa Zanzibar, pamoja na Jumuiya hii ya Waafrika, pia kulikuwa na Jumuiya nyengine za makabila mbali mbali.  Hizi ni pamoja na Jumuiya ya Wahindi (Indian Association), chama cha Association), Chama cha Washirazi (Shiraz Association), Chama cha WaAssociation, Chama cha Washirazi (Shirazi Association) na Chama cha Waarabu (Arab Association).

Ingawa jumuiya hizi zilianzishwa kwa madhumuni ya kijamii, lakini katikati ya miaka ya 1940s, kulianza kujitokeza kwa madai mbali mbali ya haki za kijamii kutoka kwa Watawala na hii kuonesha kuwa, wakati huo Jumuiya hizi zilianza kuonesha hisia za kiitikadi.  Ifahamike vile vile kwamba, kabla ya kuanzishwa vyama hivi vya wananchi, kulikuwa pia na vyama vidogo vidogo vilivyokuwa na mwelekeo wa kisiasa na kutetea maslahi ya wafanyakazi.  Kwa mfano katika mwaka `1922, chama cha “Tanganyika Territory Civil Servants Association” kilianzishwa.  Kwa Zanzibar, Sheria ya kuhalalisha vyama vya wafanyakazi ilipitishwa mwaka 1931.  wafanyakazi wa Bandari ya Dar es salaam waligoma katika mwaka 1047 na kufuatiwa na Bandari ya Zanzibar katika mwaka 1948, [Clayton, 1976; Iliffe, 1970; Shivji 1986: 166 – 178].

Vugu vugu la kudai uhuru katika nchi za Bara la Afrika pia liliikumba Afrika ya Mashariki, ambapo hadi kufikia katikati ya miaka ya 1950s, vyama vya kisiasa vilianza kuanzishwa kwa madhumuni hayo.  Chama cha Tangayika National African Union (TANU) kilianzishwa Tanganyika mnamo tarehe 7 Julai, 1954 mwenyekiti wake akiwa Mwalimu Nyerere.  Pamoja na chama hiki pia kulikuwa na vyengine kama vile United Tanganyika Party (UTP) na African National Congress (ANC).  Vile vile, baada ya uhuru, kati ya mwaka 1962 na 1963, vyama vya Peoples Convention Party (PCM), African Independence Movement (AIM) na Peoples Democratic Party (PDP) viliundwa Tanganyika.

Kwa Zanzibar, Chama cha Zanzibar Nationalist Party, ZNP au kwa kifupi Hizbu kilianzishwa Disemba 1955 chini ya Rais wake Sheikh Ali Muhsin.  Nazo jumuiya za African Association na Shirazi Association ziliungana na kuzaa chama cha Afro Shirazi Party (ASP) tarehe 5 Februari, 1957.  Mnamo March 1960 chama cha Zanzibar and Pemba People’s Party, ZPPP chini ya Sheikh Muhammed Shamte nacho kiliundwa kufuatia mgawiko katika ASP.  Vile vile, chama chengine kilichoundwa ni Umma Party katikati ya mwaka 1962 chini ya mwenyekiti wake Sheikh Abrahman Babu kufuatia kumeguka kutoka ZNP.  Pia kulikuwa na Muslim Association ambayo iliwahi kushiriki katika uchaguzi wa mwanzo wa Zanzibar 1957 na kunyakua kiti kimoja kati ya 6 vilivyo vikigombaniwa.

1.1.4    Nguvu ya Umoja na Harakati za Uhuru

Katika jitihada za kudai uhuru, vyama vya kisiasa katika Bara la Afrika vilikuwa na Mkakati wa pamoja wa kuunganisha nguvu za vyama vya kupigania uhuru katika kila nchi.  Haja hii ya kuendeleza mapambano ya pamoja ya madai ya uhuru, ilipelekea kufanyika kwa mkutano wa Septemba 1958 huko Mwanza ulioitishwa na TANU kwa vyama vya kupigania uhuru vya nchi za Afrika Mashariki na Kati.  Vyama vya ZNP na ASP vilihudhuria mkutano huo ambao ulijadili kuunda chombo cha Umoja.  PAFMECA (Pan Afrika Freedom Movement for Eastern na Central Africa) yaani Umoja wa kupigania uhuru wa waafrika wa Afrika Mashariki na Kati, uliundwa katika mkutano huo.  Baadae vyama vya Kusini mwa Afrika viliongezeka na umoja huo ukaitwa PAFMECSA (Pan African Freedom Movement for Eastern, Central and Southern Africa).  Mkutano mwengine wenye madhumuni hayo hayo, ulifanyika Accra, Ghana Disemba 1958, chini ya Uenyekiti wa Kwame Mkrumah wa Chama cha Convention People’s Party.

Kushiriki kwa vyama vya ASP na ZNP kwa pamoja kulidhihirisha kwamba vyama hivyo vilikuwa na lengo moja tu la kupigania uhuru wa Zanzibar hata kama vilitafautiana kwa sera na mikakati.  Hata Mwalimu Nyerere wakati huo alikubali kwamba lengo la vyama hivyo lilikuwa ni kutafuta uhuru.  Kukubali kushiriki wa pamoja kunaonesha namna kulivyokuwa na mashirikiano ya aina Fulani kwa makusudi na vyama vya kisiasa Zanzibar japo sera za vyama hivyo zilitafautiana.

Hata hivyo, chengine kilichojidhihirisha ni kwamba mashirikiano ya vyama vya Kizanzibari yalififia kadiri chama cha TANU kilivyojikwekweneza na kuunga mkono upande mmoja huku ikihujumu mwengine.  Hapa ndipo palipoanzisha mtafaruku na kutoelewana kwa Wazanzibari.  Kwa hivyo, hatua zilizofuzta za kuzidisha kujipenyeza kwa vyombo na taasisi za Tanganyika katika Zanzibar kunazidi kuvichafua visiwa hivyo na kuvirudisha nyuma badala ya kuvijenga hata baada ya miaka 40 ya Muungano uliotandikwa kuhalalisha yote yatendwayo na CCM iliyoviuwa TANU na ASP.  Bila shaka nguvu za umoja zilizoleta uhuru sasa zinatumika kuimaliza Zanzibar kisiasa, kiutamaduni na kiuchumi, ingawa gharama ya kazi hii ni kuirudisha nyuma Tanzania kwa kila hali.

Sehemu ya 2: Uhuru

1.2.1    Uhuru wa Tangayika

Kwa nchi za Mashariki, Kusini na Kati mwa Afrika, Tanganyika ndio nchi ya kwanza kupata uhuru.  Tanganyika ilipata uhuru tarehe 9 Disemba, 1961.  baada ya uhuru, Tanganyika ilifanya jitihada za kusaidia kupatikana uhuru kwa nchi nyengine.  Kwa mfano, ilikubali ardhi yake kutumika katika kufungua kambi za kufundishia silaha wanachama wa vyama vya kupigania uhuru.  Vile vile ilifungua mipaka kwa wakimbizi wa nchi nyengine ambao walikimbia mateso katika nchi zao.  Iliruhusu pia vyama vya nchi nyengine kufungua ofisi zao ili ziweze kurahisisha mawasiliano na nchi nyengine pamoja na jumuiya za kimataifa.  Pia ilitoa misaada ya kisiasa na hata kidiplomasia kwa vyama hivyo vya kupigania uhuru.  Kwa ari yake hii ya Kiukombozi, ndio maana Tangayika ikapewa heshima ya kuwa Makao Makuu ya Kamati ya Ukombozi ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika mwaka 1963.  Kazi ya Kamati hiyo ilikuwa ni kuratibu misaada kutoka Afrika na duniani kote kwa vyama vya siasa vinavyopambana na ukoloni, ukabila, ubaguzi wa rangi na ubwana wa wahamiaji wa Kizungu katika Bara la Afrika [Othman, 1996].

Kwa uzoefu huu wa Tanganyika katika mambo ya kisiasa na kidiplomasia, hakuna ambae angetarajiwa kuwa leo, ingeweza kushindwa kuwa na Muungano usioisha migogoro ya kisiasa na nchi ndogo kama Zanzibar.  Aidha  haingetarajiwa pia, kuwa uzoefu na nidhamu ya muda mrefu ya majeshi yetu ya ulinzi na usalama wa nchi na raia ingechafuka kwa kukubali kutumika vibaya kiasi cha kuitia nchi yetu katika aibu kama ya mauji ya raia wasio hatia ya tarehe 26 na 27 Januari, 2001.  baada ya uhuru wa Tanganyika, kulikuwa na mtihani kwa chama cha TANU ambacho ndicho kilichokuwa kikiendesha Serikali.  Mtihani huu ulihusu nafasi ya chama hicho mbele ya vyama vya ukombozi vya Zanzibar.

Kama tulivyosema, awali Zanzibar ilikuwa na vyama vya ZNP na ASP ambavyo vyote vilikuwa na msimamo wa kupinga utawala wa kikoloni.  Kwa ASP, msimamo wa TANU ulikuwa wazi, lakini kwa ZNP kulikuwa na mushkeli.  Othman, [1996:7] anasema kwamba ZNP kilipinga ubaguzi wa kikabila wazi wazi katika sera na programu zake.  Hata hivyo, ilionekana kuwa, pamoja na Tanganyika kuwa kinara wa kupinga ubaguzi wa rangi kwa nchi yake na nchi nyengine za Afrika pamoja na kuunganisha vyama vya kupigania uhuru katika nchi hizo, haikuweza kufanya hayo kwa Zanzibar.  TANU iliamua kukiunga mkoni ASP moja kwa moja na kuiwacha mkono ZNP hali iliyoibakisha Zanzibar ikigawika kiitikadi pande mbili sawa sawa kama wafuasi wa vyama hivyo walivyo wakijitokeza kutoa maoni ya kuunga mkono vyama vyao.

TANU iliisaidia ASP katika mambo kadhaa kwa hali na mali.  Kwa mfano, viongozi wa ASP walikuwa wakitayarishiwa hati za kusafiria pamoja na kupitia Tanganyika.  Watoto wa viongozi wa ASP waliweza kupatiwa nafasi za masomo kupitia Tanganyika.  Wakati wa chaguzi za Zanzibar, wanasiasa mashuhuri na TANU, hasa Bi Titi Mohammed na Ali Mwinyi Tambwe walikuwa wakipelekwa Zanzibar kupigia ASP kampeni.  Uamuzi wa TANU kukiunga mkono chama cha ASP ulizua mzozo katika siasa za Zanzibar.  ASP ilikituhumu ZNP kuwa kisingeangalia maslahi ya Waafrika na kingerejesha utumwa pindipo kingekuwa katika madaraka.  Kwa upande wake ZNP, ilikituhumu ASP kwamba kingeiuza Zanzibar kwa Tanganyika kama kingeshika madaraka baada ya uhuru.

Hali hii ndiyo iliobakia katika historia hadi leo.  Hatutafautiani na wana historia kwa hayo, lakini tunatafautiana kwa wao kukubali sehemu tu ya historia na kuwacha nyengine iliyo muhimu kufahamisha matatizo yetu ya kisiasa.  Ukweli huu kwamba kilicholeta mtafaruku na mapambano Zanzibar ni kujipenyeza kwa taasisi za Bara na kuegemea kwa tabaka moja hautakiwi na wanahistoria wetu.  Kujizatiti kwa kila kundi katika visiwa vya Zanzibar sasa kunatoa uhalali kwa kufanya mauaji kwa mwengine.  Huku hili likitokea, matatizo yanaongezeka na Zanzibar yamalizika ikimaanisha kumbe CCM haipendi mtu Zanzibar, bali ina lengo la muda mrefu la kuwagombanisha Wazanzibari wavichukuwe visiwa chini ya himaya yao baada ya kuwa chini ya himaya ya Kiingereza kwa dahari.

1.2.2    Uhuru wa Zanzibar

Kwa Zanzibar, njia ya kuelekea kwenye uhuru ilikuwa na misukosuko kuliko Tangayika.  Wakati chama cha TANU kikiungwa mkono na wafuasi wengi sana Tanganyika, kwa Zanzibar vyama viwili vikuu vya siasa vya ZNP na ASP vilikuwa na nguvu sawa [Othman, 1996:8].  Katika safari ya kuelekea uhuru, palifanyika chaguzi nne.  Wa kwanza ni ule wa mwaka 1957 ambapo ASP ilishinda viti 5 kati ya 6 vilivyogombaniwa.  Kiti kimoja kilichukuliwa na Muslim Association iliyojizatiti katika Mji Mkongwe wa Zanzibar.  Huu ni uchaguzi wa kwanza kwa Afrika ya Mashariki uliokusudiwa kutoa uhuru.  Baada ya ushindi huu kwa ASP na hatimae kunyimwa nafasi ya kutawala, chama hicho kilianza kumeguka kwa baadhi ya viongozi kukiacha na kuunda Chama cha ZPPP chini ya uenyekiti wa Sheikh Muhammed Shamte.

Kufuatia kuundwa kwa ZPPP chaguzi zote zilizofuata, chama hicho kilikuwa na mashirikiano na ZNP.  Uchaguzi wa pili ulikuwa Januari 1961.  Matokeo yake ni kuwa muungano wa ZNP/ZPPP ulipata viti 12 (ZNP 9 na ZPPP 3) katika Baraza la Kutunga Sheria.  Hata hivyo, kiti kimoja kilikataa kuunga mkono umoja huo na hivyo kubakia na viti 11.  Kwa kuwa ASP ilishinda viti 10, kwa hivyo ilijikuta ikiwa na 11 kama ZNP/ZPPP kufuatia kiti kimoja cha ZPPP kukiunga mkono ASP.  Kwa hali hii, hapakuweza kupatikana ridhaa ya kuunda Serikali na hivyo uchaguzi mwengine wa tatu ukapangwa kufanyika Juni 1961, ambao baada ya kumalizika palitokea fujo na baadae umwajikaji wa damu ulioacha watu 68 wafu na mamia majeruhi.  Kati ya watu 68 waliokufa, 65 walikuwa ni Waarabu na 3 Waafrika [Okello, 1967].  Matokeo ya uchaguzi huo wa Juni 1961 ni kwamba ASP ilipata viti 10, ZNP viti 10 na ZPPP viti 3.  Kwa hivyo, umoja wa ZNP/ZPPP ndio uliokuwa na wingi wa viti 13 kwa 10 vya ASP, na hivyo kupewa uwezo kisheria wa kuunda Serikali ya pamoja na Sheikh Mohammed Shamte wa ZPPP kuwa Waziri Mkuu.

Baada ya uchaguzi wa Juni 1961, Serikali ya Muungano wa ZNP/ZPPP ilidumu kwa miaka miwili kabla ya uchaguzi mwengine ambao ndio ulikuwa uwe wa mwisho kabla ya kutolewa uhuru kamili.  Kwa hivyo, kipindi cha kuanzia Juni 1961 hadi Julai 1963 kilikuwa na umuhimu kwani ni kipindi cha mazungumzo ya Katiba mpya ya Zanzibar baada ya Uhuru.  Mkutuano wa kwanza wa kujadili Katiba ulifanyika London mwaka 1962 na vyama vya kupigania uhuru vilishiriki.  Ujumbe wa ZNP/ZPPP uliwakilishwa na Sheikh Ali Muhsin na Sheikh Shamte, wakati ule wa ASP uliongozwa na Mzee Karume na Othman Sharif.  Huko Lancaster House mazungumzo yalifanywa bila ya pande hizo kukubaliana juu ya mwelekeo wa Katiba mpya.

Kilifika kipindi cha uchaguzi wa mwisho wa kuelekea uhuru ulifanyika Julai 1963 na uchaguzi ukafanywa.  Matokeo ya uchaguzi huo ni kwamba ASP ilipata viti 13 (Unguja 11 na Pemba 2), ZNP ilipata viti 12 (Unguja  6 na Pemba 6) na ZPPP ilipata viti 6 (vyote kutoka Pemba).  Kwa hivyo, muungano wa ZNP/ZPPP ndio uliokuwa na viti 18 dhidi ya 13 vya ASP na hivyo muungano huo ulipewa uwezo wa kuunda Serikali, sasa ya kukabidhiwa Uhuru.  Ikumbukwe tu kwamba, kabla ya uhuru kamili, kwamba Zanzibar ilipata madaraka ya ndani tarehe 24 Januari, 1963, na Sheikh uhuru wa Zanzibar ulipatikana rasmi tarehe 10 Disemba, 1963, na Sheikh Muhammed Shamte Hamad akiwa Waziri Mkuu.  Kutokana na mizozo ya kisiasa kushangaza kwa uhuru huu, TANU na ASP kuuita ‘uhuru wa bandia’.  Upewe jina lolote, lakini inabakia katika historia ya Zanzibar kwamba tarehe hiyo ndio ya uhuru wa Zanzibar.

 

 

Sehemu ya 3: Mapinduzi ya Zanzibar

1.3.1    Mapambano ya Kikabila Na Athari za Utabaka

Wakati mazungumzo ya Uhuru yanaendelea, fikra za Kimapinduzi pia zilikwisha jengeka miongoni mwa viongozi wa ASP.  Chama hiki kilipata furaha zaidi ya moyo pale baada ya Sheikh Abdulrahman Babu aliekuwa Katibu Mkuu wa ZNP kuihama Hizbu na kuanzisha Umma Party mwanzoni mwa 1963. kwa fikra za kisoshalisti na kimapinduzi Babu alipokelewa haidhuru ‘shingo pegani’ baada ya kujitambulisha kwa Mzee Karume.  Baadhi ya waandishi wanatoa maoni kuwa wengi! James Cameron, akiandika kutoka Zanzibar mwaka 1960 alisema:  “Hivi sasa kisiwa hiki kilichodorora hakitaweza kusaidia vya kutosha jitihada zetu za kuendeleza mapinduzi ya Afrika”.  Maneno haya hayakudumu sana kwani miaka mine tu baadae, Mapinduzi yalifanyika.

Hata hivyo, pamoja na maoni haya, upo ushahidi kwamba Mapinduzi ya Zanzibar yalipangwa muda mrefu kabla ya kufanyika kwake.  [Okello, 1967:85], anaeleza; “I gave much thought to the political problems of the Africans of Zanzibar and by the end of 1962 I had decided that revolution was the only solution”.  Maana yake ni kwamba “ nilizingatia sana matatizo ya kisiasa yanayowakumba Waafrika weusi wa Zanzibar, na mwisho wa mwaka 1962, nilikwisha amua kwamba mapinduzi ndio dawa ya mwisho”.  Zanzibar kabla ya Mapinduzi ilikuwa na mgawiko wa wazi wa makabila uliosababisha matabaka.  Kwa mujibu wa Lenin, mapambano yoyote ni mapambano ya kikabila yaliyodhamiriwa kuondosha ukabila, kwa kweli Mapinduzi yaliondoa aina moja ya utabaka na kuanzisha aina nyengine.

1.3.2    Mfumo mpya wa siasa

Baada ya kuundwa Serikali ya Jamhuri iliyotokana na Mapinduzi ya 1964, kulitokea mabadiliko mengi na ya ghafla.  Inasemekana kwamba ukiacha nchi ya Guinea chini ya Ahmed Sekou Toure, hakuna nchi iliyobadilika kwa haraka sana katika Afrika, Kusini ya Sahara, kama Zanzibar baada ya Mapinduzi [Martin, 1978:60].  Badiliko la kwanza lilikuwa ni kufuta Katiba ya Uhuru ya mwaka 1963 na kutangaza ‘Katiba ya Kisheria’ ambayo ilijenga Serikali ya Kikatiba na Utawala wa Sheria (Sheria ya SMZ na.5 ya 1964).  Madaraka ya kutunga sheria  na Sheria za Kikatiba (Sheria Kuu za Jamhuri ya watu wa Zanzibar) yakawa chini ya Baraza la Mapinduzi.  Japokuwa mara tu baada ya Mapinduzi Serikali iliahidi kuitisha Mkutano wa Kikatiba baada ya mwaka mmoja (11 Januari, 1965) ili kuithibitisha Katiba, hili halikufanywa.  Na kwa hivyo, kwa mara ya kwanza Zanzibar ilipata Katiba yake baada ya miaka 15 (Mwaka 1979).  Pamoja na hili la Katiba, mara tu baada ya Mapinduzi, Rais wa Zanzibar Marehemu Karume alitangaza kwamba uchaguzi wa kwanza ungefanyika baada ya miaka sitini, [Othman, 1996:12].  Badiliko jengine kubwa la wakati ule ni kule kuufuta mfumo wa vyama vingi vya siasa na kuanzisha mwengine wa chama kimoja; na papo hapo kuingia katika muungano na Tanganyika.

Sehemu ya 4: Muungano wa Tanganyika na Zanzibar

1.4.1    Chanzo na sababu

Tangayika na Zanzibar ziliungana tarehe 26 April, 1964 miezi mitatu tu baada ya Mapinduzi ya Zanzibar.  Ingawa fikra za muungano zilikuwepo miongoni mwa vyama vya ukombozi Barani Afrika hata kabla ya Uhuru, lakini kwa Zanzibari Muungano uliharakishwa na khofu zile zile za msuguano wa kitabaka kama za kabla ya Mapinduzi.  Hivyo ilikuwa ni sababu ya ndani.  Ndio maana ikachukua siku nne tu (22 – 26, April 1964), tokea mazungumzo ya kufanya mungano kuanza na kumalizika, [Jumbe, 1995:8].  Jumbe akiwa katibu Mipango wa ASP na Mjumbe wa Baraza La Mapinduzi anasimulia kwamba alikuwa Pemba na hakua na tetesi juu ya jambo hilo hadi aliporudi tarehe 26 April 1964, na kuarifiwa na Mzee Karume kwamba Zanzibar imeungana na Tanganyika.  Baada ya kupewa habari hii yeye alijibu vyema, “Umoja ni nguvu.”

Kwa upande wa nje, pia baadhi ya Mataifa makubwa ya Magharibi yalikuwa na khofu juu ya Zanzbiar kugeuzwa Cuba ya Afrika.  Abdulrahman Babu ambae alikuwa Waziri wa mambo ya Nje wa Tanzania mara baada ya Muungano alikuwa ni mwanamapinduzi aliekuwa na fikra za kikomunisti.  Hili liliitia khofu Marekani ambayo ilihisi Zanzibar ingeweza kuwa Cuba ya Afrika.  Maoni mengi yanaonesha kwamba, ijapokuwa Karume alikuwa na pupa kuingia katika muungano kwa sababu za kiusalama, lakini kilichochangia zaidi ni nguvu za Washington.  [sheriff,1994:152]  anathibitisha kwamba, katika simu ya maandishi kwa Balozi wa Marekani katika Afrika Mashariki ya Machi 3, 1964, Katibu wa Marekani wa wakati ule Dean Rusk alipendekeza: “Would it be useful to raise with Nyerere, despite his previous objection the idea of a Zanzibar – Tanganyika Federation as a possible way to strengthening Karume and reducing Babu’s influence.”  Maana yake ni kwamba “pamoja na kukataa kwa Nyerere juu ya wazo la Shirikisho la Tanganyika na Zanzibar, ingekuwa vyema kulisisitiza ili kumpa nguvu Karume apunguze athari za mawazo ya Babu” [Wilson 1989:48].

1.4.2    Makubaliano ya Muungano

Katika Mkataba wa Muungano mambo tuliyotakiwa kukubaliana nayo hasa ni kumi na moja.  Kwa mujibu wa maelekezo ya kisheria, haya ndio yanayotufunga katika Muungano.  Mambo hayo ni:  Katiba na Serikali ya Muungano, Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.  Polisi, Kutangaza hali ya hatari, Uraia, Uhamiaji, Biashara ya Nje na Mikopo ya Kigeni, utumishi katika vyombo vya Muungano, Ushuru wa Forodha, kodi  za mapato na kodi za mashirika;  Bandari, anga, Posta na Simu.  Muungano huu si wa kihistoria tu lakini pia ni maalum.  Nchi kama Tanganyika, yenye watu wapatao milioni thelethini kung’ang’ania Muungano na Zanzibar yenye watu wasiozidi milioni moja ni jambo maalum na pengine lenye unyeti wake, hasa kwa vile halikujaribiwa na nchi nyingi za Afrika licha ya kuwa fikra za muungano ndizo zilikuwa msimamo wa nchi hizo wakati wa kupigania uhuru.  Aidha umaalum wa Muungano wetu katika misukosuko mizito ya migogoro.  ‘Kero za Muungano’ ndilo jina linalopendwa na baadhi ya Watanzania ingawa kwa kukosa nia njema ya kuziondosha kero hizo, hata haioneshi kwamba zinawakera viongozi kuliko raia.

Moja kati ya kasoro kubwa ni kule kuongezwa kwa vipengele ambavyo hapo awali havikuwa katika orodha ya mambo ya Muungano.  Hadi sasa, badala ya mambo 11 ya awali yaliyokubaliwa katika Mkataba wa Muungano, yameongezwa tena mambo mengine 11 ambayo ni :  Leseni za viwanda na takwimu, Elimu ya juu, Gesi na utafutaji wa Mafuta, Baraza la Mitihai, Usafiri wa Anga, Utafiti, Utabiri wa Hali ya Hewa, Takwimu, Mahkama ya Rufaa, Usajili wa vyama vya siasa.  Katiba ya Jamhuri ya Tanzania ambayo yenyewe ni sehemu moja kati ya kumi na moja, leo ndio imegeuzwa kuwa na mamlaka ya kubeba mengine.  Agenda ya uhalali wa Muungano wetu huwa si jambo linalosahaulika kwa baadhi ya Wazanzibar, lakini hoja sio tu uhalali wa namna Muungano ulivyozaliwa, lakini pia ni namna ya ulivyokuzwa.  Kuna maoni kwamba ridhaa ilihitajika katika kila hatua ya kudumisha na kuimarisha Muungano.  Sasa suala si ridhaa tu kwa mambo ya Muungano lakini imeongezeka haja ya kuwa na tathmini ya namna Muungano unavyosaidia maendeleo ya watu wake.  Wanafalsafa wa dunia nzima husisitiza juu ya haja ya kuwa na mapitio ya utekelezaji wa mipango na sera zao, na hata wale wa Tanzania, pia wanalikubali hili lakini si kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Kwa hivyo basi, huku Muungano ukizidishwa kasi na upande mmoja wenye nguvu, majibizano ambayo hayajesha kati ya jamii inayodhulumiwa na Muungano ni yale pia yanayohusu sura au muundo wa Muungano wetu.  Wakati wa kuchafuka kwa ile iliyoitwa ‘hali ya hewa ya kisiasa, Zanzibar’ (1983/84), malumbano juu ya muundo wa Muungano yalivungwa kwa jibu la kihesabu, pale Mwalimu aliposomesha kwamba 1+ 1 = 2 na sio 3;  Mwalimu akimaanisha kwamba, Tanganyika ni  1 na Zanzibar ni 1; na kwa hivyo ukijumlisha 1 na 1 unapata 2.  mwalimu alisahau kwamba vile vile moja, (kwa hali yoyote) ni sawa sawa na moja lakini Tanganyika kwa hali yoyote) si sawa sawa na Zanzibar.  Kwa hivyo, kama Mwalimu alikusudia Tanganyika ni “moja” basi alisahau kwamba Zanzibar lazima itakuwa ni “moja gawa kwa milioni moja.  Ama kama alikusudia Zanzibar ndio “moja” basi pia alisahau kwamba Tanganyika lazima itakuwa ni “moja zidisha milioni moja”

Hata hivyo, kwa upande mwengine katika maajabu ya hesabu za Mwalimu ni kuwa, zilipojumlishwa Tanganyika na Zanzibar, Zanzibar inabakia bila kubadilika lakini Tanganyika inabadilika jina na kuwa Tanzania.  Ni vyema wale wababaishaji wa siasa kama Mwalimu wafahamu kwamba iwapo moja na moja ni mbili, basi zitabakia mbili iwapo utazijumlisha au la.  Kwa nini Watanganyika na Wazanzibari wajitafutie matatizo kwa kujumlisha moja na moja wakati jibu ni mbili hata bila ya hesabu ya Mwalim, Zanzibar haionekani kuathiriwa kwa maajabu haya ya kihesabu, bila shaka, iwapo Tanganyika ni sawa na Zanzibar kama ilivyo 1 na 1 haya kupona au kumega Mamlaka ya Zanzibar na kuwa Tanzania.  Ama kweli; kilinge kikifichuka inayobaki ni dhulma tupu.

Hii ndio maana kila Tanzania inalolifukuzia katika dunia, inalifukuzia na kuinufaisha Tanganyika bila ya kuifikiria Zanzibar huku ikisahau kuwa nguvu hizi za Tanzania kufanya inavyotaka katika dunia hazikupatikana kama si kuingiza maajabu haya ya kihesabu katika siasa.  Sio tu kwamba Zanzibar hainufaiki lakini inadamirika kwa maajabu ya kihesabu kwani kwa kukosa mamlaka haiwezi kuvuka bahari wala anga.  Kwa vile maajabu haya ya kihesabu hayawezi kuzidi na kuwa muujiza, itakuwaje sasa moja na moja ielekee kuwa moja (kama vile ambavyo haiwezi kuwa tatu) kama sera ya CCM ya Serikali mbili kuelekea moja inavyoelezwa?

Haya ndio baadhi ya mambo ambayo yameiburuza Tanzania kwa muda mrefu sana na haionekani kwamba hata walioungana walikuwa wakitambuana kwa hili na ndio maana kuna kauli nyingi zinazopingana kuhusu sura ya Muungano.  Kwa mfano, [Msekwa, 1982] anasema, wengine wanaufananisha Muungano huo na uhusiano kati ya Uingereza na Ireland ya Kaskazini.  Hata hivyo, Frank Carlucci, akitoa taarifa yake kutoka Zanzibar siku ya pili tu ya Muungano, alisema kwamba, Karume bado anaamini kwamba alichokubali ni shirikisho kati ya nchi mbili zilizo huru na sio Muungano kamili kama ilivyo katika Makubaliano ya hivi sasa [Wilson, 1989:79].  Muungano umesimamishwa juu ya makubaliano ya Muungano ya mambo 11 tu yaliomo ndani ya Mkataba wa Muungano.  Makubaliano ya Muungano ndio sheria mama ya Jamhuri ya Muungano; na Katiba zote za Tanzania na Zanzibar na sheria nyengine zote zitokane na sheria hiyo mama iliyozipa sheria hizo uhalali  [Shivji, 1990:6].  Kama sheria mama yoyote ile, hakuna sheria nyengine au sheria inayotokana na Katiba inayoweza kupingana na makubaliano hayo.  Kuna Tume nyingi zimeundwa na Rais aliepita na huyo wa sasa kushughulikia matatizo ya Muungano lakini hazina jibu kwa sababu ya hila ya kihesabu ya Mwalimu ambayo wanafalsafa wa Tanzania wanaipa nguvu kuliko kukabili ukweli na kuondosha matatizo ya Muungano.  Hatuwa yoyote ambayo Tanzania inahisi inapiga kujiimarisha katika utandawazi wa kikanda na kimataifa inafanya kwa haraka zaidi ili kulififiliza suala la Muungano wetu. Hata hivyo, kila wakati katika maisha.  Tanzania itajikuta hatua moja nyuma ya wengine kwa kulazimika kulishughulikia suala la Muungano.

 

 

 

1.4.3    Matatizo ya Muungano.

Muungano, hata kama umekuja kwa hofu ambazo kwa sasa hazipo tena, lakini kuwa nao ni suala zuri hasa kwa sasa ambapo dunia yote inakaribiana na kuwa kisiwa.  Kwa hivyo, hoja yetu sio kuendelea na Muungano ili uwe na manufaa kwa pande zilizoungana.  Kwa ujumla basi, kumekuwa na kilio cha Zanzibar juu ya aina au muundo wa Muungano (structure), namna unavyoendeshwa (modus operendi) na fursa za kuweza kujadiliwa ili kuuboresha (modus vivendi).  Kukosekana kwa uwezo wa wananchi wa kuangalia upya viungo hivyo vitatu muhimu, kunaufanya Muungano wetu kufifia na kuzidi kuibua matatizo siku hadi siku.  Pamoja na kwamba kuliundwa Tume ya Jaji Nyalali na kupendekeza Mfumo wa Serikali tatu ili kuupunguzia matatizo Muungano wetu, lakini hili lilikataliwa  na CCM pamoja na Serikali zake.  Lengo kuu na la muda mrefu kwa CCM ni kuwa na Muungano wa Serikali moja kama inavyoeleza Ripoti ya Shelukindo juu ya kero za Muungano.

Hili lilithibitishwa katika Halmashauri Kuu ya CCM katika kikao chake cha mwezi wa Agosti, 1994 mjini Dodoma.  Hili licha ya kwamba ni sawa na kuimeza Zanzibar hasa kutokana na udogo wake, hata hivyo, haikuwa azma ya Muungano wakati wa kutiliana saini.  Kwa maneno ya Jumbe tena, dhana ya muungano wa shirikisho inathibitishwa zaidi na makala ambayo ilichapishwa na gazeti moja la Observer la Uingereza hapo April 20, 1968 karibu miaka 4 tokea Muungano wa Tanzania kuasisiwa pale ambapo Rais Nyerere alisema; “Iwapo umma wa Zanzibar bila ya ushawishi kutoka nje, na kwa sababu zao wenyewe, wataona kuwa Muungano una hasara kwa uhai wao, sitawapiga mabomu kuwalazimisha. ……., Muungano utakuwa hauna tena sababu ya kuendelea iwapo washiriki wake wataamua kutathmini na kuthibitisha jambo hasa tukio la kihistoria kama Muungano.  Mwalimu Nyerere alisahau alichosema na kuandikwa wakati huo, kwani ndie yeye tena aliesema kuhoji muungano ni dhambi.

Nguvu za kuulinda Muungano kwa hali yoyote haikuelekezwa kwenye Katiba badala yake imeelekezwa kwenye matumizi ya vyombo vya ukandamizaji vya dola.  Vyombo hivi havitatui ila huzidisha matatizo.  Kwa mfano, katika Kamati ya Jaji Kisanga iliyoundwa na Rais Mkapa July 1998 kupata mapendekezo ya wananchi juu ya mabadiliko ya Katiba ya Muungano ya mwaka 1977, udhaifu wa uendeshaji wa Muungano ulijitokeza wazi.  Serikali ilianza na maoni yake katika “White Paper” na baada ya kamati kupata mapendekezo ya wananchi, Mswada wa marekebisho ya katiba ulipelekwa katika Bunge la Tanzania.  Hata hivyo, kwa kuwa hili ni suala la Muungano lingehitaji kuungwa mkono kwa thuluthi mbili ya Wabunge wa Bara na thuluthi mbili za Wabunge wa Zanzibar kwa mujibu wa Katiba kifungu cha 98 (1)(b).

Kwakuwa, Bunge la Tanzania lilikuwa na wajumbe wa upinzani (CUF) wa kutosha kutoka Zanzibar, hali hii ilionekana wazi kwamba ile tabia ya kupata thulithi mbili kutoka Zanzibar ili kujaza mambo ya Muungano kwa mara hii isingefanya kazi bila ya wapinzani kuunga mkono.  Ili Wazanzibari waendelee kuburuzwa, Spika wa Bunge Mhe. Pius Msekwa aliamuru kuvunjwa Katiba bila ya aibu pale alipoamua kutumia kifungu cha 98 (1)(a) ambacho kinatoa maamuzi kwa thuluthi mbili za Wabunge wote.  Hata baada ya Serikali kutupilia mbali maoni ya Jaji Nyalali, iliamua kutumia mamilioni mengine na kuunda Kamati ya Shellukindo katika mwaka 1994 ili kufanya uchambuzi wa hizo zinazoitwa kero za Muungano.  Licha ya kwamba yaliyotafitiwa yamebaki kuwa ni ‘siri kali ya serikali’, hakuna la msingi lililorekebishwa hadi leo kati ya mambo yanayoleta kero katika Muungano wetu.

Uzoefu wetu katika Muungano umekuwa ukijenga hoja, iwapo ziada ya ‘nguvu za umoja’ wetu zina ishara ya kutupeleka tuliko kusudia au tunatimiza wajibu tu, wa kuogelea katika bahari iliyochafuka.  [Smith, 1971] anasema, miaka miwili kabla ya Uhuru wa Tanganyika, Mwalimu Nyerere alisema kwamba tatizo kubwa la Tanganyika kwa miaka ijayo litakuwa ni Zanzibar.  Mwalimu aliongeza ‘sifanyi mzaha, nina wasiwasi tatizo hilo litatuumiza vichwa”.  Kujitokeza waziwazi kwa matatizo aliyotabiri Mwalimu ndio zaidi kumeufanya Muungano wetu ni maalum kwani, kwa kipindi chote cha uhai wa Mwasisi huyo Muungano wetu umekuwa dhambi kuuhoji, kuutathmini na hata kuutolea fikra mpya juu ya namna ya kuuimarisha na kuufanya wenye maslahi kwa pande zilizoungana.  Tukifuatilia namna uharaka wa Muungano ulivyokuja na tukiangalia namna Zanzibar inavyoburuzwa katika Muungano, maswali yanayogonga namna Zanzibar inavyoburuzwa katika Muungano, maswali yanayogonga vichwani mwa Watanzania wengi ni jee, Muungano ni wa nani na kwa ajili ya nani?

SURA YA PILI

KISA CHA MAUAJI YA JANUARI 26 NA 27, 2001

Tunachokusudia kukieleza hapa ni kuwa, historia ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ya Zanzibar haiwezi kujengewa kisingizio cha hoja kuwa yana uhusiano wa moja kwa moja na mauaji ya Januari 26 na 27, 2001.  Ni kweli kwamba kulitokea mambo katika historia, yanayoshabihiana kwa namna fulani na yanayotokea leo, lakini si lazima kwamba leo yanatokea kwa kuwa tu na kale yalitokea.  Kuikataa hoja hii ya baadae ni kujenga dhana inayopelekea swali ‘ni kwa nini kwa yale mema yaliyotokea katika historia nayo pia yasijirudie?’ wakati historia yetu migogoro ya kisiasa ilichukua sura ya mapambano ya kitabaka, leo hakuna mapambano isipokuwa dhulma na unyanyasaji unaofanywa na dola (yenye silaha pekee) dhidi ya raia wasio hatia.  Ama kwa hapo zama za kale, hata pale makabila na matabaka yalipoamua kupambana, bado ushahidi wa kutosha wa kihistoria unaonesha kuwa dola haikuwa ikitumia silaha vibaya kuangamiza umma

 

 

Sehemu ya 1: Upotoshwaji wa Historia na Mauaji ya Januari 26 na 27, 2001

Katika hatua za kuchambua mkasa wa mauaji hayo, Tume ya Uchunguzi wa Mauaji chini ya Brigedia Hashim Mbita ilitaja kwamba chanzo kikubwa cha mauaji ya tarehe 26 na 27, Januari, 2001 kinatokana na athari za kihistoria za muda mrefu katika siasa za Zanzibar.  Maoni haya yapo katika kifungu cha 186 cha Taarifa ya Mbita aliyoiwasilisha kwa Rais baada ya kufanya uchunguzi aliosema ‘ni wa kina’.  Kwa mfano, kifungu hicho cha 186 kinasomeka kama hivi.

“Historia ya Zanzibar kama ilivyoelezwa katika sehemu ya pili ya Taarifa hii, inadhihirisha kuwepo kwa makundi na tabaka kadhaa wakati wa ukoloni na kudumu kwa kiasi Fulani hata baada ya Mapinduzi.  Makundi hayo yalijumuisha Waarabu, Wahindi na Waafrika.  Matabaka haya yaligawanyika kwa misingi ya ukabila, tafauti na kifikra na misimamo yao ya kisiasa.  Vyama vya siasa vilivyoanzishwa kabla ya uhuru vilichukua sura ya mgawanyiko huo”.

Na katika kifungu cha 189, taarifa inaendelea kuwa, “baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi wa 1992, na vyama vya siasa kuandikishwa, inadaiwa kwamba huko Zanzibar, chuki zilizokuwepo chini chini ziliibuka ghafla baina ya CCM na CUF.  Hali hii iliendelea hivyo na kuwa moja kati ya vyanzo vikubwa vilivyosababisha matukio ya tarehe 26 na 27 Januari, 2001 nchini hususan Zanzibar”.  Mwisho wa kunukuu.

Sehemu hii ya Taarifa ndio inayotupeleka kuangalia japo kwa kifupi mambo ya kihistoria ili tuone kuna ukweli kiasi gani katika kauli hii ya Mbita.  Kwa kuwa Mbita ameanza katika ile sehemu ya historia ya Zanzibar, wakati wa Jumuiya za Kikabila na ya wakati wa vyama vingi vya kabla ya uhuru, basi na sisi hatuna budi kupita humo humo japo kwa ufupi kuangalia hali halisi ilikuwaje.

Hata hivyo, kabla ya kuanza na uchambuzi huu wa kihistoria, ni vyema tumuulize Mbita swala moja la msingi kutokana na kauli yake ya hapo juu.  Swali hili ni : iwapo Mbita anasema kwamba matabaka ya hapo nyuma yaliyojengeka kwa misingi ya kikabila na sio kifikra na misimamo ya kisiasa, na kwa kuwa wakati huo pia ulikuwa ni wa vyama vingi kama leo jee, ni lipi lililozifanya jumuiya na tabaka hizo zisiwe na misimamo ya kisiasa wakati huo, hata leo jumuiya hizo ambazo zimekufa zijiibue wazi katika historia ya kisiasa?  Na kwa kuwa jumuiya hizo za kitabaka zilijionesha wazi wazi katika jumuiya za leo zinazotajwa na Mbita na ambazo zimejenga vyama vya leo ziko katika sehemu gani za Zanzibar?  Baada ya Mbita kujibu haya sasa tuendelee kujifunza ukweli halisi.

2.1.1    Jamii ya Zanzibar Kabla ya Vyama vya Uhuru

Wachunguzi wengi huiona historia ya Zanzibar ni maalum kwa vile ilipita chini ya tawala za Usultani wa Kiarabu tafauti na nchi nyingi katika Bara la Afrika.  Kutokana na tafauti hii ya kimfumo, huonekana kama kwamba uzoefu wa kiutawala pamoja na sura na hali ya migogoro ni wa kipekee na maalum katika dunia, hii ikimaanisha kwamba, hata namna ya kuyaeleza na kuyatafutia ufumbuzi matatizo ya kisiasa yanayoendelea kuikumba jamii ya Zanzibar ni ya kipekee.  Ifahamike tu kwamba, katika kipindi hicho cha vyama vingi vya kale (katikati ya miaka ya hamsini), athari za kimfumo wa kisultani ambao ulianza na biashara ya utumwa na kujikita katika mgawanyiko wa wazi wa kitabaka zilikwisha futika.  Utumwa ulipigwa marufuku Zanzibar katika mwaka 1873.  haroub Othman, katika makala yake ya Mei 31, 2001 ya Gazeti la Rai anasema kuwa, “ukweli ni kwamba ilipofika miaka ya 1930 hakukuwa tena na dalili za dola ya Sultani.  Ijapokuwa Waingireza walitilia maanani matakwa ya Mfalme na kulinda maslahi ya mabwanyenye, lakini nchi hiyo ilikuwa ikitawaliwa kama koloni jengine lolote”.  Vile vile wachunguzi wa historia ya Zanzibar  wanakubaliana kwamba, harakati za kisiasa zenye mwelekeo wa kutaka kuheshimiwa kwa maamuzi ya wengi katika Zanzibar, zilianza hata katika nyakati ambapo Zanzibar ilikuwa katika utawala na himaya za wakoloni.  [Anthony Clayton, 1976], anaelezea kwenye kitabu maarufu cha historia ya Zanzibar cha ‘The Genetral Strike in Zanzibar 1948’,  Kwamba mgomo wa makuli katika bandari ya Zanzibar wa mwaka 1948 ulikuwa na madhumuni ya kisiasa licha ya madai mengine.

Tunazidi kuwafahamisha akina Mbita kwamba katika mgomo huo wa makuli, madai ya wazi ya Waafrika wa mwaka huo wa 1948 yalikuwa ni kuongezwa mishahara ingawa wanahistoria hao wanasema, hisia za kisiasa zilikwisha kereketa.  Matokeo ya mgomo huo nikuwa Serikali ya Mkoloni ilipata hasara kubwa sana, kwani meli zilikuwa haziwezi kupakia wala kupakua mizigo.  Hata hivyo, pamoja na hasara na uchungu huo serikali ilioupata, iliunda Tume ya Uchunguzi; na madai ya makuli yakasikilizwa na hatimae kuongezwa mishahara.

Leo, baada ya miaka 40 ya uhuru, kwa Zanzibar watu wanaodai haki ya kupiga kura wanakandamizwa na kunyanyaswa na vyombo vya dola na hata wale wanaoamua kuchagua chama cha upinzani wanakoseshwa ajira, waliomo katika ajira hufukuzwa na wengine kufungwa magerezani bila hatia, ingawa wale waliotoa maoni kwamba uchaguzi si wa haki wanauliwa kinyama, wanawake kunajisiwa na wengine kulazimishwa kwenda ukimbizini nchi za nje.  Haya yote yakitendeka Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar zinatanguliza kauli za kupongeza wale waliofanya unyama wote huu.  Labda Tume ya Mbita wangekuwa wakweli na wawazi wakusema nini tatizo la historia hapa?

Kwa mfano kama huo, leo baada ya miaka 40 ya kujitawala, wenye mabasi ya madaladala wanafanya mgomo kama wa mwaka 1948, tena ni mgomo baada ya kupeleka madai yao Serikalini kwa zaidi ya miezi sita bila kusikilizwa.  Jee, hukumu ya Serikali ya Mapinduzi ya kuwazuia magari hayo yasiendeshwe tena maisha inatokana na historia gani ya kisiasa?  Kwa uamuzi kama huu, jee ni Serikali ipi jeuri na yenye ukatili kwa watu wake kati ya Mkoloni na hii ya Kimapinduzi inayotangazwa kwa juhudi zote ikubalike kuwa ni ya watu wote.

Ushahidi wa kihistoria unazidi kutufahamisha kwamba, wakati huo wa kabla ya siasa za kupigania uhuru, pamoja na mgawiko huo wa kitabaka uliokuwepo, hata hivyo, jamii ya watu wa Zanzibar haikuishi kwa chuki, uhasama na uhasidi mkubwa kama ilivyo leo.  Haroub Othman katika  makala tulioitaja juu, akimnukuuu Michael Lofchie (1965) katika kitabu chake cha “Zanzibar: Background to Revolution”; anaeleza, ‘hapakuwepo miongoni mwa jamii za kienyeji, kuwa na uhasama dhidi ya Waarabu, hasa miongoni mwa watu wa Pemba’, na John Gray katika kitabu chake “History of Zanzibar from the Middle Ages to 1856”, anaeleza mwaka haioneshi kulikuwa na upinzani wa wazi juu ya kuchukuliwa kwa ardhi na Waarabu.

Mohammed Bakar [1997], anaelezea kwamba siasa za Zanzibar kiuchumi zilijengeka katika misingi ya kitabaka, Waarabu wakiwa juu wakimiliki nguvu za uchumi hasa ardhi pamoja na maamuzi ya kisiasa, wakifuatiwa na Waashia ambao wakimiliki zaidi harakati za biashara na Waafrika wakiwa katika nafasi ya chini kama wakulima na vibarua.  Anaendelea kusema, “Lakini jambo moja la kufurahisha ni kwamba mahusiano kati ya waliomiliki ardhi na wakulima hao hayakuwa ya chuki na mara nyingi waliweza kushirikiana katika kudai mambo yenye faida kati na baina yao”.  Maoni ya Abdul Sheriff [1991], yanaeleza kwamba wakati wa harakati za kupigania uhuru waliomiliki nguvu za uchumi, wakulima wakiwa miongoni mwao, waliachana na siasa za kihasama na kitabaka na kuimarisha umoja.  Nae Shao, anakubaliana na maoni kama hayo kwa kusema “ingawa ukabila ulijengeka katika nafsi za wengi na kuathiri siasa za kila siku, kwa hakika ilikuwa ni mgawiko wa kitabaka na mashirikiano uliojenga nguvu ndani ya siasa za Zanzibar”.  Ushahidi huu unatafautiana kwa kiwango kikubwa sana na ripoti ya Mbita.

Kumbukumbu nyengine za karibuni zinazohusu misuguano ya kijamii katika historia ya Zanzibar kabla ya vyama vya kupigania uhuru ni zile za vita vya ng’ombe na ugomvi wa jamii ya Kihindi na Waarabu kuhusu zao la karafuu.  Kama tulivyokwishasema, katika awamu hii ya kabla ya siasa za wazi, ingawa madai ya wazi yalikuwa juu ya haki na maslahi mbalimbali ya kijamii, hata hivyo hisia za kiitikadi pia zilianza kuvukuta.

Katika vile vilivyoitwa ‘vita vya ng’ombe’ (Anthrax Revolts) vya 1951 wananchi hasa wa sehemu za Kiembesamaki Unguja, walivunja amri ya kupeleka ng’ombe zao kwa ajiili ya kuchanjwa ili kuzuia kile kilichoitwa kuenea kwa maradhi ya miguu na midomo.  Waliovunja amri hii ‘halali’ ya Serikali ya Mkoloni waliwekwa rumande na kuzuiliwa ng’ombe zao ili wasieneze maradhi.  Waliopelekwa rumande baadae walishitakiwa mahakamani.  Ile siku ya kesi wenzao wakiwa na marungu na mapanga walivamia gari la washitakiwa wakati wakiteremshwa kuelekea kwenye mashtaka.  Walifanikiwa kuwaokoa baadhi ya washitakiwa katika purukushani ile, na hakuna taarifa ya mauaji yaliofanywa na dola katika kadhia hiyo.

Ilikuwa ni baada tu ya kuona kwamba kwa vile wamefanikiwa pale nje ya Mahkama, sasa waende ndnai ya gereza kuwaokoa watuhumiwa wengine.  Hapa palitokea mapambano na watu 10 waliuliwa na Serikali.  Haya yalikuwa ni mapambano ya dhahiri kati ya raia waliojidhatiti dhidi ya chombo cha dola.  Haya hayakuwa maandamano ya amani ya madai barabarani kama yale maandamano ya tarehe 27 Januari, 2001.  hatumaanishi hata kidogo, kusifu mauaji ya watu 10 wakati wa historia, tunachoelezea ni kwamba mauaji haya yalitokea kwenye gereza ambako wananchi waliojidhatiti walikwenda kwa madhumuni ya kupambana ili kuwaokoa watu waliokuwa katika mikono ya sheria.  Haya ni tafauti na mauaji ya Januari 27 kwa raia waliokuwa barabarani na zaidi ni tafauti na mauaji ya tarehe 26 kwa waislamu waliokuwa msikitini baada ya sala ya Ijumaa.  Kwa mfano huu wa kihistoria, Mbita atueleze,iwapo kweli historia yetu ina ubaya kuliko dola ya Tanzania inayoangamiza raia kwa madai ya haki!

Hata hivyo, pamoja na kwamba mauaji ya mwaka 1951 na mengine yoyote hayawezi kuhalalishwa, lakini pia hayawezi kulinganishwa na yale yalioondosha takriban watu zaidi 70 waliokuwa katika maandamano ya amani ya 27 Januari 2001.  katiba zote mbili za Jamhuri ya Muungano na Zanzibar hazipingi maandamano.  Hizi kama ndio sheria mama, hizi sheria zinazozuia sheria mama zisifanye kazi  au kuheshimiwa zimepata uwezo kutoka wapi?  Iweje mtu au sheria (ambazo huwa chini ya Katiba kupata uwezo zaidi ya ule wa Katiba?  Leo, Tanzania kuna pendekezo la ‘Tume  ya Nyalali ya Mfumo wa Vyama’  la kufuta sheria zote kandamizi, lakini Serikali zinaendelea kulikataa pendekezo hili ili kutoa nafasi ya kutumia vyombo vya dola vibaya.  Kubakia kwa sheria hizi zinazopingana na ustawi wa mfumo wa vyama vingi ni chanzo kimoja kikubwa cha mauaji ya mwaka 2001.  kubakia sheria hizi bila kufutwa pia hakuondoshi uwezekano mwengine wa mauaji popote Tanzania.  Hili likiendelea, nchi hii yapongezwa na ulimwengu kwamba eti inatii utawala wa sheria na misingi ya haki za binadamu.

Tukirejea basi, baada ya mkasa huu wa mauaji ya 1951 hakuna taarifa iwapo askari wa Mkoloni  baada ya kuua watu wale 10 waliendelea kupiga watu nyumba hadi nyumba pamoja na kupora na kuingilia wanawake kwa nguvu kama ilivyokuwa kule Pemba, Januari 27, 2001.  huu ni ushuhuda mwengine wa ukatili wa Serikali ya CCM kinyume cha maoni ya Tume ya Mbita ya kusngizi historia.  Sisi tunazidi kukubaliana na Mbita na chama chake cha CCM kwamba ukoloni ni  mbaya, lakini kwa maovu haya yanayotokea leo wakati ukoloni hauko tena, hatuwezi kusingizia historia.  Ukatili mkubwa uko ndani ya “Amani na Utulivu” na ndio maana hata baada ya kuua bado kauli za kwanza za wakubwa zilikuwa ni kuwapongeza askari kwakufanya kazi vizuri.  Askari wote walioshiriki kuuwa wamehamishiwa Tanzania Bara pamoja na kupewa vyeo n amakaazi bora.  Nyumba za kisasa za askari polisi zimejengwa kwa mara ya kwanza huko Wawi, Pemba.  Haya si matunda ya Mapinduzi bali ni matunda ya mauaji ya tarehe 26 na 27 Januari, na iwapo haya ni matunda ya kuendelea Mapinduzi basi kimantiki kuendeleza Mapinduzi ni sawa na kuendeleza mauaji.

Mkasa mwengine wa kihistoria ni ule wa ugomvi wa Jumuiya ya Wahindi na Jumuiya ya Waarabu hapa Zanzibar.  Kisa ni kwamba Waarabu walishindwa kulipa deni la fedha walizokopeshwa na Wahindi kwa ajili ya kuendeleza kilimo cha karafuu.  Hali hii ilipelekea hata kufilisika kwa Waarabu kwani ilibidi walipe fedha na riba.  Waarabu ndio waliomiliki mashamba huku Wahindi wakiwa wanunuzi na wauzaji wa karafuu na bila shaka wengi wa Waafrika wakiwa vibarua kama ilivyo leo.  Katika hali ya kuwasaidia Waarabu ambao walikuwa ndio wakulima wa karafuu, Serikali ya Kiingereza ilitoa rai ya kuanzishwa kwa Jumuiya ya Wakulima wa Karafuu yaani Clove Growers Association (CGA).

Hii ilisaidia sana uchumi wa nchi kwani baada ya muda mfupi wakulima wa karafuu walimudu kulipa madeni na maslahi ya kijamii yakaimarika.  Rai ya CGA ndio iliomaliza ugomvi wa kijamii.  Haya yalitokea katika mwaka 1934 na ndio wakati maarufu ujulikanao kama “Batileti” kutokana na Mzungu alieletwa kutoka Uingereza kuwa Meneja wa CGA aitwae Barlett.  Leo baada ya miaka 40 ya uhuru, CCM ambachi kinajiita chama cha wakulima, wanyonge, wafanyakazi, wakwezi n.k…, ndio kwanza kinaamrisha dola kunyang’anya watu karafuu majumbani mwao, Zanzibar.  CCM inazuia watu kununua na kuuza karafuu ingawa ina ilani ina sera ya uchumi huria ulio muhimu kwa siasa ya vyama vingi.  Uchumi huria wa Tanzania hauwasaidii wakulima wa chai, tumbaku, korosho na kahawa ambao hukopwa mazao yao kila msimu ingawa yanapolipwa fedha hazitoshi hata kununulia pembejeo za msimu mwengine.  Uchumi huria lakini wakulima wa mwani wamepigwa mweleka na mazo yao hayana bei.  Haidhuru haya ni kiuchumi, lakini bado Mbita atueleze lipi ni janga kwa wakulima kati ya CGA na ZSTC?  Ni hostoria au ukatili wa dhola ndio tatizo la Zanzibar?

Tume ya Mbita inasema moja ya sababu za mauaji ya Zanzibar hasa kule Pemba (ambako yalikithiri) inatokana na kusahauliwa Pemba kiuchumi.  Nani anawajibika kwa hili, na ni kwa nini wanaodhulumiwa kiuchumi ndio wawe wakosa hadi kupelekea kuuliwa?  Kwa mujibu wa historia ya CGA, na katika kurekebisha tatizo hili la ugomvi wa Waarabu na Wahindi katika enzi ya madhila ya ukoloni, basi bei ya karafuu ilipandishwa kutoka rupia 3 hadi rupia 6 kwa farsila moja  na karafuu zilinunuliwa bila ya mpango wa leo wa CCM wa “ununuzi wa kubamburikiwa”.  Leo miaka 40 ya kujitawala bado wako watu wamefungwa jela (sasa hivi) kwa kuonekana na akiba ya karafuu katika nyumba zao.  Mmoja wa hawa ni mtu aitwae Majoka wa Msingini, Chake chake ambae anatumikia kifungo cha miaka 30 kwa kuonekana na akiba ya karafuu.  Akina Mbita waeleze, ipi mbaya hapa, ni historia au utawala wa CCM?

Ama kwa ushahidi huu, ni dhahiri kwamba Wazanzibari hawajaanza leo harakati za kudai kila waliloliona ni haki yao inayotawaliwa kwa nguvu au hila.  Inaonesha pia kwamba misuguano ambayo ni sehemu ya maisha ya jamii yoyote, ilipatiwa ufumbuzi kwa njia ya kistaarabu kila ilipokuwa ikitokea.  Tafauti na leo, Serikali ndio inayobuni mbuni za kuanzisha na kukuza migogoro ili kupata kisingizio cha kuangamiza watu kwa nguvu na zana za dola.  Migogoro  hiyo hasa ya kisa cha Ng’ombe, inaonesha tu kwamba pamoja na misuguano ya kijamii iliyotokea, vile vile kuna funzo la kihistoria ndani yake.  Hili ni kuwa Wazanzibari waliamka na kutanabahi mwanzo katika kudai kila walichoona si haki.  Pili, Wazanzibari waliweza kushirikiana pale ambapo palihitaji umoja bila woga na bila kujali athari za kitabaka.  Tatu, hakukuwa na mapambano kati ya hayo Mbita aliyoyaita matabaka ya kikabila isipo  mwaka 1961 ambapo mapambano yalitokea baad ya uchaguzi uliokosa haki na uhuru.  Kwa hivyo, basi migogoro ya kisiasa ambayo baadae kuzaa maafa na vifo yanatokana na chaguzi zisizo za haki na huru.  Bila shaka basi, hii ndio chanzo cha mauaji ya januari 27, 2001 na sio historia za kitabaka katika siasa za Zanzibar kama anavyodai Mbita na kwa hivyo ukabila Zanzibar si tatizo kama ambavyo si tatizo Tanzania bara kwenye makabila zaidi ya mia moja.  Nadharia hii yakubaliana na maneno ya [Bowles, 1991], anaesema, tambulisho za kikabila ni mawazo walionayo watu moyoni mwao na kwa wenzao na kuyategemea katika kufanya uchambuzi ni sawa na kuandika historia ya kuwazika (kusadikika)”.  Akina Mbita kwa kukosa kufahamu haya, ndio leo wanawadanganya Watanzania kuwa ‘historia ndio chanzo cha mauaji’

Historia pia inatueleza kwamba, kadri ya pima joto ya madai ilivyo ikipanda, madai yalianza kuchukua sura ya kiukombozi kuutaka utawala wa kikoloni kubadilisha mfumo mzima wa maisha ya watu.  Ukoloni ni mbaya kwnai unabagua, unanyanyasa na kudhalilisha na ndio maana tukauondoa.  Kosa kubwa la CCM ni kule kudhani kwamba “ijapokua ukoloni wa kihistoria umekomeshwa lakini wakoloni bado wapo miongoni mwa kizazi cha wananchi ambao aila zao zinanasibika na zile za zama za ukoloni”.

Imani hii ndio inaoendeleza ubaguzi katika jamii na kwa vile majukumu ya jamii baada ya  kujitawala ni kujiletea maendeleo, basi uduni wa maendeleo ya kijamii, kisiasaa na kiuchumi unatokana na Serikali kujishughulisha na siasa za kiubaguzi na unyanyasaji kuliko kuikusanya jamii kwa maendeleo ambayo kamwe hayapatikani katika jamii iliyogawika.  Ubaguzi ni hali ya tabaka moja kulitenga jengine na sio kamwe kwa mtu mweupe kumtenfa mweusi kama CCM wanavyo tufanya tuamini.  Ubaguzi ukifanywa hupunguza nguvu za kisiasa na kiuchumi kwa watu kwamba hata kiuchumi inarudi nyuma.  Ni bahati mbaya basi, ubaguzi ndio injini ya CCM hata baada ya miaka 40 ya uhuru.  Bahati mbaya, baadhi ya wachunguzi wa mambo ya kisiasa hutoa maoni ya kupalilia ubaguzi badala ya kuusafisha.  Kwa hivyo, sura ya migogoro ya kisiasa ni ya aina ya upinzani dhidi ya ubaguzi na unyanyasaji.  Kwa utawala kama wa Tanzania, haya yangeweza kutokea hata kama yasingejitokeza katika historia.

Tumeanza kwa kujaribu kuonesha namna angalau Serikali ya Mkoloni (ambao hatuisifu kwani ukolono mbaya) ilivyokuwa ikijaribu kusawazisha kila hali mbaya ya machafuko ya kijamii yalipojitokeza ili kujaribu kuepusha maafa na mauaji.  Tumeona kwamba, pale makundi ya makabila yalipotaka kukabiliana au hata pale wananchi wengine (Waafrika) walipojaribu kuleta madai kwa njia ile ya mgomo basi hii tu ya madai, lakini hata pale wananchi walipotokea kupigana na Serikali wazi wazi, basi taratibu ya kuingilia fujo zilikuwa za kistaarabu tofauti na sasa.

Uzoefu wa kushughulikia madai ya wananchi Tanzania unaonesha kwamba, matatizo yanapokuwa ya kisiasa yanasingiziwa historia na kwa kuwa hayapati ufumbuzi basi husukumiziwa sheria, lakini yanapokuwa ya kisheria huhukumiwa kisiasa.  Bila sha, tumejionea namna historia inavyotumiwa vibaya ili kujenga sababu na hoja za nguvu ili siasa za Zanzibar zionekane kama kwamba ni za kipekee na zenye udhia katika dunia.  Lengo la mkakati huu ni kuifarakanisha na kuigawa jamii ya Watu wa Zanzibar ili kutafuta uhalali wa kuendeleza mradi wa muda mrefu wa kuiondosha Zanzibar katika ramani ya Afrika Mashariki na dunia.  Ikumbukwe tu, kipindi tulichokizungumza ni kabla hata ya mfumo wa vyama vya siasa ambao kwa Zanzibar ndio jaa litumiwalo na baadhi ya wanahistoria na wanasiasa uchwara kupandikiza chuko na hasama ili kuongeza kasi ya kukamilisha mradi huo.

Ni dhahiri basi, katika kipindi tulichokieleza, iwapo athari za makabila zimewacha nyufa za kitabaka, basi kipindi cha siasa za wazi ndicho kingetarajiwa kuwa na athari kubwa za kuigawa jamii kwa mujibu wa mtazamo wa wanahistoria hao mashuhuri wa masuala ya Zanzibar pamoja na wanasiasa wao wanaowatumikia.  Kwa mantiki hiyo basi, madhumuni ya sehemu inayofuata ni kuendelea na udadisi wa mambo muhimu ya kihistoria yaliyotokea katika mfumo wa kwanza wa vyama vingi(ambao ni pia ni sehemu ya historia) ili kuchunguza uwapo siasa za wakati ule zilileta mgawiko, unyanyasaji na mauaji kwa jamii ya Wazanzibari kwama kujionea iwapo kuna ithibati kwamba historia yetu ya kisiasa ndio chanzo na sababu za madhila ya unyanyasaji wanayofanyiwa Wazanzibari na pia ndio sababu ya mauaji ya Januari 26 na 27, 2001.


2.1.2    Jamii ya Zanzibar katika Mfumo wa Zamani wa Vyama vingi

Uchambuzi wa sehemu hii ya kihistoria unaonesha tena kuwa, historia ya kisiasa ya Zanzibar imekuwa ikitumiwa vibaya na baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa ili kuleta tafsiri mbaya za harakati za kisiasa.  Mambo haya yanapelekea kuendeleza khofu, chuki, uhasama, malumbano na hatimae migogoro miaongoni mwa makundi yenye itikadi tafauti za kisiasa Zanzibar.  Matokeo ya mwisho ya uchambuzi huu mbaya si mapambano kati ya wanachama wanaotafautiana kiitikadi (kama ilivyokuwa zamani), bali ni unyanyasaji wa dola (ambayo hujizatiti kukilinda chama kilichopo madarakani, CCM) dhidi ya vyama vyenye msimamo tafauti na chama hicho tawala.  Mwisho wa misuguano hii hufikiwa kwa dola (yenye silaha) kuingilia na kukilinda chama tawala kwa kuangamiza jamii na kuleta maafa kuirudhisha Zanzibar nyuma kimaendeleo kwani jamii iliyo na khofu na iliyogawika kusimaia mfumo wa leo wa vyama vingi, sio tu kwamba zimeshindwa kuzuia hali hii mbaya, bali uzoefu umeonesha kuwa, huwa zenyewe ndio chanzo na kichocheo cha maafa na mauaji hayo kinyume na ilivyokuwa siku za nyuma.

Uchambuzi huu ni muhimu kwani unaelimisha juu ya mambo ya msingi ya kuzingatia katika uendeshaji na usimamizi wa harakati za kisiasa hasa ndani ya vipimo vya demokrasia, ambavyo hujionesha wakati wa zoezi la uchaguzi.  Zaidi ni kwamba tunapata fursa ya kujikumbusha namna mfumo wa vyama ulivyoendeshwa zamani na kulinganisha na hali ya mfumo tulionao hivi sasa pamoja na kuangalia mazingira ambayo vyama vimekuwa vikikulia na vile vile harakati na matukio mbali mbali katika kujenga na kuimarisha kidemokrasia.  Inakubalika kwa wengi kuwa kukosekana kwa matayarisho bora ya chaguzi ikiwa ni pamoja na mazingira (ya kisheria) yasio ya haki na sawa kumekuwa ndio sababu ya wazi ya kulemaza demokrasia na kuendeleza migogoro ya kisiasa.  Tunatanabahisha tu kwamba sura hii haitaji kila kitu katika historia ya kisiasa ya Zanzibar isipokuwa tu, ile hali iliopelekea heka heka, machafuko, magomvi, migogoro, unyanyasaji na hata upoteaji wa mali na maisha ya watu na namna tawala na dola za wakati huo zilivyojitahidi kushughulikia kadhia za namna hio.

Maelezo ya ushahidi yanayofuata yanazidi kuonesha kwamba, hata vyama vingi vya siasa vya zamani vilivyojengeka wazi wazi katika misingi ya makundi ya kikabila havikuwa na uhasama ulioashiria kwamba Zanzibar baada ya ukoloni ingebakia katika matatizo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii kama iilivyo leo.  Licha ya misuguano ambayo ni ya kawaida katika siasa za ushindani popote pale, lakini kulikuwa pia na aina ya mashirikiano na makubaliano baina ya vyama katika masuala muhiimu ya hatma ya Zanzibar.  Ama ushahidi upo kwamba kipindi cha vyama vingi vya awali kuanzia kutumiwa na wanasiasa wa nje ya Zanzibar kupandikiza mbegu za fitna na hasama miongoni mwa Wazanzibari ili kuanza kile leo kinachojidhihirisha kama mradi wa muda mrefu kuimaliza Zanzibar kisiasa, kijamii na hata kiuchumi.  Katika ujumla wa mambo basi, matukio yote ya unyanyasaji, udhalilishaji na umwagaji wa damu za watu unaoendelea Zanzibar ni matokeo ya utumiaji wa nguvu wa vyombo vya dola vya Serikali ya Muungano dhidi ya jitihada za Wazanzibari kuizuia Tanganyika (iliyojificha ndani ya koti la Muungano)  kuimaliza Zanzibar na kuitoa katika ramani ya dunia.  Na hivyo, sababu za kihistoria hutumiwa tu kama chaka la kuendeleza maovu ili kuendeleza mradi huo.  Ama tukiangalia nafasi ya vyombo vya dola katika siasa ni dhahiri kwamba vyombo vya dola katika siasa za baada ya uhuru hadi leo katika mfumo mpya wa vyama vingi ni maalum kwa unyanyasaji, udhalilishaji na hata uuaji kuliko katika mfumo wa siasa za Zanzibar katika historia.

Kwa hivyo, tunazidi kubainisha kuwa, kupotosha na kusingizia historia katika matatizo ya Zanzibar, sio tu kuwa unatumiwa ili kuisambaratisha na kuimeza Zanzibar lakini vile vile, ni mkakati wa kudumu wa kukifanya chama tawala CCM kuendeleza ukiritimba wa utawala baada ya ule uliodumu kwa zaidi ya miaka 30 ya mfumo wa chama kimoja baada ya uhuru.  Kwa hivyo, aina ya mapambano na migogoro ya kisiasa huchukuwa sura ya wazi ya upinzani dhidi ya ukiritimba wa utawala unaoendelezwa na CCM ambao huwa haufanikiwi bila ya dola kuendeleza unyanyasaji na umwagaji damu.  Hivyo ni kusema, mikakati hii ya vyombo vya dola kung’ang’ania kuiweka CCM katika madaraka kwa nguvu, nayo ni sababu tosha ya migogoro ya kisiasa na mauji katika visiwa vya Zanzibar.  Tunachambua kwa ajili ya kuzidi kuweka bayana kuwa historia ya kisiasa ya Zanzibar ni kisingizio (scape goat) tu cha kuendeleza hali mbaya ya kisiasa, kijamii na kiuchumi kwa Zanzibar, na kamwe si kiini cha mfululizo wa matatizo na migogoro ndani ya siasa za Zanzibar ya leo kama tutakavyoona katika maelezo yafuatayo.  Maelezo haya yamejikita kwenye chaguzi kwani ni wakati na baada ya chaguzi ndipo migogoro na maafa ya kisiasa yanaposhamiri katika visiwa vya Zanzibar.

2.1.3    Uchaguzi wa kwanza, Septemba 1957

Katika uchaguzi huu vyama vitatu vilishiriki, yaani ASP, ZNP na Indian Association.  Uchaguzi ulikuwa wa kugombania viti 6 vya Baraza la Kutunga Sheria na ambapo viti vingine 6 vilitengwa kwa ajili ya uteuzi.  Masharti ya uchaguzi yalikuwa mabaya kwani mpiga kura alitakiwa awe na mali ya angalau shilingu elfu tatu, kipato cha Shilingi elfu moja na mia tano na ajue kusoma na kuandika kizungu, au Kiswahili au kiarabu.  Kwa mwenye kuchaguliwa masharti yalikuwa magumu zaidi.  Pia wanawake hawakuruhusiwa kupiga kura.  Haya yalikuwa ni masharti yaliouweka uchaguzi kufanyika katika mazingira magumu.  Kulikuwa pia  na sharti kwamba mpiga kura lazima awe ni raia wa Sultani.  Ilichukuliwa hivyo kwa kuwa raia waliokuwa wa Sultani kwa vile ufalme ulikuwa na milki juu ya kila kitu kinyume na mfumo wa kidemokrasia unaosimamiwa na katiba kuliko amri.  Hatupingani kwamba mfumo wenyewe wa usultani ndio mbaya kwani ulikuwa wa kikoloni na ndio maana tukauondoa.  Hata hivyo, dhana ya kuwa haki ya kupiga ni lazima uambatane  na haki ya kiraia ni ukweli usiopingika duniani kote.  Kwa hapa Zanzibar, leo inatakiwa kwa chaguzi za Zanzibar.  Utata wa Katiba ambao ni sehemu ya mkakati wa kuimaliza Zanzibar unaifanya Zanzibar ionekane kama si dola na hivyo kwa mujibu wa baadhi ya Wanasiasa na hata Wanasheria wa Tanzania wanaelekeza kwamba hapana dhana ya uraia Zanzibar isipokuwa ukaazi tu.  Hata ni ajabu ya kujitawala kwani wakati nchi zote duniani hujitawala ili kujenga dola, Zanzibar ilijitawala ili kuondosha dola.  Haya ndio maana na maajabu ya uhuru kwa Zanzibar.

Haki ya kupiga kura imetajwa katika Kifungu cha 7(1) cha Katiba ya Zanzibar, lakini katika kifungu cha 7(3) cha Katiba hiyo, Bunge linapewa uwezo wa kutunga sheria inayohusu uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Wabunge na sheria hizo kutumika Zanzibar kwa kulingana na masharti ya Kifungu cha 132 cha Katiba hiyo.  Kwa mwanya huu, Bunge katika mwaka 2000 lilipitisha sheria ya kuchanganya tarehe za uchaguzi wa Jamhuri na ule wa Zanzibar siku chache kabla ya uchaguzi wa pili wa vyama vingi wa mwaka huo wa 2000.  Hili lilisababisha usumbufu mkubwa kwa wapiga kura wa Zanzibar, ingawa ilifanywa maksudi ili kuvikaribisha vyombo vyote vya dola kuchafua mwenendo wa uchaguzi mkubwa baadae.  Sheria hii iliwafanya Wazanzibar kupiga kura 5 kwa wakati mmoja wakati Watanzania Bara wakipiga kuwa 3 tu.  Kwa hivyo, mwanzo wa kuharibika uchaguzi wa mwaka ule ulianzishwa na Bunge la Muungano.  Haya yalifanywa kimkakati ili kuithibitishia duania kwamba Zanzibar si dola na kwa hivyo raia si suala la kuzingatia.  Hata hivyo, hapa pia  pana shahidi kwamba Muungano wetu unatumiwa na wanasiasa wa CCM hasa wa upande wa pili wa Muungano kutuanzishia matatizo na migogoro ya kisiasa Zanzibar.  Katika historia ya kisiasa ya mfumo wa kwanza wa vyama vingi, siasa kama hizo hazikuwepo nap engine ndio maana hali ya migogoro ya kisiasa kwa wakati huo haikuwa ikipata kichocheo cha vyombo vya dola kama ilivyo leo.

Umuhimu wa suala la uraia katika uchaguzi haujaanza kuonekana leo.  Minael Hosanna Mdundo [a999], akimnukuu Sheikh Thabit Kombo Jecha aliekuwa Katibu Mkuu wa mwanzo wa ASP, anasema kuwa Waafrika waliudhiwa sana na suala la uraia wakati wa ukoloni kama sharti moja wapo katika chaguzi.  Maoni haya yanafurahisha sana kwani si wakati huo wa ukoloni tu, lakini hata baada ya Mapinduzi na hadi leo, wako baadhi ya Wazanzibari ndio kwanza wanaoendelea kukerwa sana na suala la uraia (Uzanzibari).  Kwa mfano, kwa kuwa Uraia ni suala la Muungano, Utanzania badala ya Uzanzibari ndio unaotumiwa kuleta mitafaruku na dosari nyingi katika chaguzi zinazoihusu Zanzibari peke yake – yaani uchaguzi wa Rais wa Zanzibar na ule wa Baraza la Wawakilishi.  Kwa ujumla kwa Tanzania, Uraia pia umekuwa ukitumiwa na viongozi wa CCM kama kete yao ya kisiasa.  Kwa mfano imekuwa ikitokea mara nyingi kwa mtu ambae alishawahi hata kuwa Mbunge au Balozi (katiika nchi za kigeni) kwa miaka mingi tu kukataliwa uraia wakati akitiliwa mashaka kwamba anapingana na maoni ya Serikali.  Kwa hivyo, wakati kwa Tanzania uraia ni fimbo inayotumiwa kuwaadabisha wanaopinga Serikali, kwa Zanzibar uraia umekuwa ukitumiwa kuwapotezea Wazanzibari utambulisho wao wa haki za kuchagua.

Haikuwa bahati mbaya basi, wakati Baba wa Taifa Mwalim Nyerere aliposema kwamba Uzanzibari sii chochote ila ni ukabila na udini tu.  Mwalim anamaanisha kwamba mtu wa kabila lolote katika Tanzania nap engine popote Afrika (ilimradi tu mweusi) basi angekuwa na haki ya kushiriki katika chaguzi na harakati nyengine za kisiasa katika visiwa vya Zanzibar bila kuhojiwa.  Nchi ya aina hii haijatokea duniani na ndio maana hali hii haikubaliki kwa Wazanzibari.  Kosa la Wazanzibari hadi kufika kuuliwa na dola ya Muungano ni kutetea ukweli huu.  Kama kweli akina Mbita wanaamini historia inaibua ya zamani wakubali kwamba Zanzibar ilikuwa na uraia ambao ni utambulisho wake ingawa pengine mashartu ya kuwa raia wa Zanzibar ndio yaliyoonekana kuwa na matatizo.  Ama kwa kweli hapana angetarajia kwamba ukoloni ungekuwa na matakwa na masharti bora kwa watu unaowatawala.

Hata hivyo, iwapo bado tunaona kasoro kubwa katika suala la uraia katika historia, swali la kujiuliza ni jee, kama ni ukolonii ambao ulikuwa chini ya sultani na kwa kuwa leo baada ya miaka 40 ya uhuru bado suala la uraia ndio kwanza linazidi kuwa ni kipingamizi kikubwa cha demokrasia ya kweli na kwa kuwa utawala upo, jee sultani ni yupi?   Basi iwapo historia ndio chanzo cha kusababisha migogoro na mauaji Zanzibar, na iwapo wanapaswa kubeba lawama ni utawala wa kikoloni katika historia, jee kwa mabaya ya leo, nani alaumiwe kama si utawala uliopo madarakani?  Ikumbukwe kwamba utawala wa kisultani wa Zanzibar ulikuwa na fungamano na usultani wa Oman, leo pamoja na kuwa bado Oman kuna usultano lakini wananchi wan chi hiyo wana haki ya kupiga kura wakiwa popote katika ulimwengu wa kiarabu lakini Zanzibar yenye uhuru na utawala wa wengi bado mwananchi ananyimwe kura hata katika jimbo na kijiji wanachoishi?  Si hayo tu, kwa kuwa mikakati ya Serikali za CCM ni kutotenda haki katika chaguzi, basi zimeweka sheria kwamba mtu yeyote anaetaka kudai haki kama amedhulimiwa katika uchaguzi, ni shaeti kwanza aweke dhamana ya Shilingi milioni tano mahkamani, ingawa wastani wa kipato cha Mzanzibari ni chini ya Shilingi laki tatu.  Licha ya kwamba hiki ni kiwango kikubwa mno kuliko hata wakati wa ukoloni, malalamiko yanayokubaliwa ni ya Ubunge na Uwakilishi tu na sio malalamiko ya Urais.

Uchaguzi wa rais hauhojiwi katika mahakama yoyote ya sheria Tanzania ingawa watawala wanajigamba kila siku kwamba hakuna kitachokuw ajuu ya Sheria.  Hii ndio demikrasia ya Tanzania ambayo inasifiwa sana na hata mataifa makubwa ya ulimwengu tena yanayojitangaza kama kigezo cha mabadiliko na demokrasia.  Tumechukua muada mkubwa kuelezea kipengele cha uraia kwa kuwa watawala.

Tanzania wanakitumia kwa madai ya kuimarisha Muungano ingawa ukweli kinatumika kuwaondoshea Wazanzibari utambulisho wao ili mwishowe suala la uchaguzi lifanywe kuwa la Muungano na iwe ndio ‘msumari wa mwisho katika jeneza’ la Zanzibar.  Kwa maelezo hayo, huu ni ushahidi mwengine kuwa hata kama historia yetu ilikuwa na matatizo, lakini si chanzo cha matatizo ya leo.  Ni uongozi mbaya wa CCM ndio chanzo cha matatizo yetu Zanzibar.

Tukirudi sasa katika uchaguzi wa 1957, matokeo yake ni kwamba ASP ilipata ushindi wa viti 5 na kiti kilichobakia kikachukuliwa na Indian Muslim Association.  ZNP hawakuambulia kitu.  Kwa mujibu wa masimulizi ya Mzee Thabit Kombo, Mdundo (1996:75), anamnukuu Mzee Thabit akisema, “tuliahidiwa na bwana Coutts kwamba chama kitakachoshinda kitapewa fursa ya kuunda Serikali.  ASP tulishinda vizuri sana lakini hatukukabidhiwa Serikali”; mwisho wa kunukuu.  Kwa maoni yetu, hili la kutokabidhiwa Serikali baada ya kushinda lilikuwa ni jambo baya na ni kinyume na misingi ya demokrasia.  Hata hivyo, pamoja na masimulizi haya ya Mzee Thabit Kombo (ambae Mdundo kamsifu kama mtu mkweli na mwenye kumbukumbu mzuri wakati wa uzee wake), bado inashangaza kuwa utawala huu unaosimulia ubaya wa kunyimwa nafasi ya utawala baada ya kushinda uchaguzi ndio huu huu leo unayafanya yale yale, tena kwa Waafrika wenzao.  Kwa hili jambo hili ovu lilifanywa na Mkoloni, jee anaefanya hili hili leo anatafauti gani na mkoloni?  Jee, uhuru na ukombozi wa Zanzibar ni kitu gani na kinamsaidia nani?

Katika uchaguzi huo, tunaelezwa na Mzee Thabit kwamba katika zile nafasi 6 za kuteuliwa na Serikali, basi Mkoloni aliteua Waarabu 4 na Wahindi 2 kuingia katika baraza la Kutunga Sheria. Hili liliwafanya Waafrika walalamike sana, lakini anazidi kusimulia kwamba, baad ya malalamiko yao Mkoloni aliwasikiliza na hapo ndio wakatengewa viti viwili ambavyo waliteuliwa Sheikh AMeir Tajo na Sheikh Muhammed Shamte kuingia katika Baraza hilo.

Kitu cha kushangaza lakini chenye kufurahisha katika masimulizi ya Sheikh Thabit Kombo ni kuwa ingawa hawa mabwana Tajo na Shamte ndio waliokuwa viongozi wa Jumuiya ya Washirazi na ambapo Ushirazi ulikua ni ukabila, lakini bado waliteuliwa kama Waafrika ili wakiwakilishe Waafrika.  Ushahidi upo kwamba hakukuwa na mtu miongoni mwa wale waliojiita Waafrika (kama kabila lao) walioweza kuweka pingamizi kuwa hawa Tajo na Shamate si jamii ya Waafrika, wala hakuna aliewahi kusema kuwa huyu Shamte hafai kuwawakilisha Wazanzibari kwa kuwa ni Mpemba.  Huo tunaoutaja ulikuwa ni wakati wa Ukoloni ambapo Zanzibari ilikuwa haiku pamoja na Tanganyika na zaidi ilikuwa ikitawaliwa na sultani chini ya hivyi vyama vilivyojijenga kimakabila.  Ajabu ni kwamba leo, baada ya miaka 40 ya Uhuru na Muungano bado Mzanzibari ambae utungo wa mababu na mabibi (manyanya) wake wamezaliwa Zanzibar, bado anajengewa hoja kwamba hana sifa ya kuwaongoza Wazanzibari.  Hata akikubaliwa na wenziwe kupitia sanduku la kura, Serikali ya Muungano iko tayari kuuwa watu ili kuhakikisha kwamba Mzanzibari anetakiwa na Wazanzibari wengi haiongozi Zanzibar na yule asiekubalika hata katika chama chake ndie apandikizwe ili kuharakisha kuimaliza Zanzibar kiuchumi na kisiasa.  Wazanzibari leo tumetumbukia katika mtego wa kibaguzi waliotutegea Waafrika wenzetu.

Awali ya kuundwa CUF, Watanzania walihofishwa kwamba hiki ni chama cha kiislamu kama vile uislamu ni haramu na marufuku Tanzania.  Vyombo vya dola ndivyo vilivyoushauri Utawala, nao bila kisisi ukapanda majukwaani na kuwakhofisha Watanzania kwamba CUF ni chama kibaya.  Utawala uliozoea kudanganya watu wake hauna haya wala hauoni vibaya, kwani ukikitangaza chama Fulani kwamba ni cha wafuasi wa aina Fulani pia.  Viongozi wa CUF hawakutaka kuendeleza malumbano na CCM katika suala la kidini kwani tunafahamu nchi nyingi duniani zilivyopata maafa ya kuuwana na kugawana kwa sababu ya ajenda za dini.  Busara za viongozi wa CUF zilipelekea zaidi kuwafahamisha Watanzania kuwa hiki si chama cha kidini.  Tulijuwa kuwa Watanzania wengi wangechelewa kutufahamu na ni kweli ingawa imechukua miaka kumi kufahamu, lakini wamegundua nani mkweli.  Sasa Watanzania wengi bado hawajafahamu uhusiano wa matatizo yetu ya kimaisha na utawala.  Hawafahamu kwamba ukiwa na uongozi na utawala mbaya, basi hakuna maendeleo na maisha yanazidi makali.  Hata hivyo, tunaamini haitofika 2005 kabla hawajafahamu uhusiano huu muhimu.

Ama katika kuzidi kutumia sialaha ya kikoloni ya “wagawe uwatawale”, Watawala wa Tanzania wamezidi katika kutupandikiziya yale yale ya Uarabu na Uafrika; Upemba na Uunguja na hata Ukusini na Ukaskazini ilimradi tu tusambaratike tubaguane na nchi itokomee.  Tunazidi kuwathibitishia Watanzania kwamba si kweli kwamba historia yetu ilikuwa mbaya kuliko tawala za leo Tanzania.  Hii ndio maana wakati Taji na Shamte walipoingizwa katika Baraza la Kutunga Sheria kuwawakilisha Waafrika, Mzee Karume alieuchukulia Uafrika kama kabila lake hakumkana Shamte (Mpemba) wala Tajo (Mmakunduchi) lakini Karume wa leo kwa kuwa tu ni Mtawala katika CCM bado anawachukulia wajukuu, vilembwe na hata sahiba (hatusemi watoto) wa Tajo, Shamte, Ali Muhsini na Babu kuwa bado ni maadui wa Zanzibar.  Ndio maana wakati Sultani (Mwarabu) alichaguwa Waafrika wawili katika Baraza ili kumridhisha Karume wa kale; wakati Karume wa leo hataki kumchagua Mwafrika mwenziwe mmoja tu kuingia katika Baraza kama lile la katika historia.  Jee, ni historia yetu ni ya matatizo Mwenyezi Mungu kauleta Muafaka ili kututahini na Watanzania wamjue mkweli na mnafiki.  Jee, bado Watanzania hawajafahamu ukweli?  Tutabaki hadi karne ipi tuwe watu wa kudanganywa?  Turudi tena katika uchaguzi ambao eti ni sehemu ya kihistoria inayoendelea kutuangamiza Wazanzibari.

Katika uchaguzi wa 1957 hakukuwa na purukushani za magomvi na vita, lakini kulikuwa na malalamiko ambayo yalisikilizwa na inatudhihirikia kwamba angalau kuwa katika siku za ukoloni, pamoja na kwamba ukoloni hauwezi kusifiwa kwa kuwatendea haki watawaliwa, lakini hardali ya ukweli inabakia kuwa kuna kiwango Fulani cha malalamiko ya watawaliwa kiliweza kusikilizwa na Mkoloni na marekebisho kufanywa ili kuepusha migogoro.  Jambo jengine la wazi ni kuwa kama tulivyoona, jamii ya Wazanzibari ilikuwa na uvumilivu mkubwa zaidi na ikipenda umoja zaidi licha ya kwamba kulikuwa na kiny’ang’anyiro cha kuwania si  tu utawala lakin utawala ndani ya uhuru.  Hii ndio maana malalamiko na madai ya kila pande yaliweza kupatiwa ufumbuzi na makabila yakachanganyika kufanya kazi pamoja.

Afanalek! Pamoja na Karume wa katika historia kutulazimisha tukubali kuwa uafrika ndio kabila letu Wazanzibari lakini bado Karume wa leo anatugawa, kutunyanyasa na kutuuwa.  Ndio maana katika hyo historia ya Mbita hapakuwahi kuuliwa Wazanzibari kiholela kwa uchaguzi hadi alipokamata utawala Karume wa leo.  Jee, ni historia ndio tatizo letu au Watawala wa CCM?  Inasikitisha kwamba leo katika miaka 40 baada ya Uhuru wanaolalamikia uchaguzi jaza yao kutunguliwa risasi.  Ni kweli ukoloni ni mbaya, lakini utawala usio jail maisha ya watu wake ni mbaya kuli ukoloni.  Kwa ujumla basi, katika muda wote wa ukoloni wa sultani na Muingereza Serikali zao haikupatapo kufanya mauaji ya kinyama katika kiwango kinachokaribia mauaji yanayofanywa na Serikali za CCM baada ya Mapinduzi na Uhuru.

Leo, katika Tanzania anaeunga mkono upinzania huambiwa anataka kumrejesha Mwarab arejeshe utumwa, lakini huyo anaetaka kuleta utumwa akisema sasa anaomba Wazanzibari wawe na Serkali ya Umoja wa Kitaifa ili kuondosheana dhana mbaya na woga hudhaniwa Uafrika wake haujatimilia (maana uafrika wake una mchanganyiko wa damu ya Kiarabu, Kingazija, Khindi au Kishirazi).  Kazi yote ya Mzee Karume ya kuwataka Wazanzibari waowane bila ubaguzi il wachanganyike haijawasaidia CCM, leo baada ya miaka 40, bado inawaona wengine Waafrika zaidi kuliko wengine.  Na bado tunaambiwa ili tukubali kuwa CCM inatokana na fikra za ASP ambazo mwasisi wake ni huyo Mzee Karume.  Wacha turudi tena katika uchaguzi wa enzi ya kihistoria.

Kitu kimoja cha kufurahisha katika uchaguzi huu ni Kwamba, ulielezewa kama uchaguzi uliofaniikiwa kiusalama ijapokuwa kidemokrasia haukufana.  Na kwa maneno ya Ayany (1970:59), anasema; “Kutokana na hali ya matukio, uchaguzi ulikuwa wa amani katika historia ya kikatiba”.  Haya yote yakitokea Mtawala wa wakat ule ni Mkoloni, tafauti na leo ambapo Mtawala ni Mwafrika anaetarajiwa kuwatendea haki Waafrika wenziwe.  Brigedia Mbita haoni haya kusema historia yetu ndio jeneza letu.

2.1.4    Uchaguzi wa Pili, Januari 1961

Katika uchaguzi huu vyama vilivyoshiki ni ASP, ZNP na ZPPP.  Kabla ya uchaguzi, Waziri wa Makoloni wa Uingereza Sir Lan Macleod aliunda Tume ya kuchunguza taathira ya mabadiliko ya kisiasa ama kiutawala baada ya uhuru.  Katika uchunguzi huo vyama vilipewa nafasi ya kushauri juu ya hali hii ya baadae.  ASP kwa upande wao walisema walipendekeza kuwe na kipindi cha mpito kuliko uhuru wa moja kwa moja.  Vile vile walitaka kuwe na kipindi cha madaraka ya ndani na baadae uhuru kamili.  ZNP ilitaka uhur utolewe mara moja bila kuchelewa.  ZPPP ilitaka, kwanza utayarishe mfumo kamili wa Serikali na Mawaziri wake, ambao utazingatiwa mara tu baada ya uchaguzi.  Hii ndio ilikuwa mitazamo yao, lakini wote walitaka uhuru, na ndio lilikuwa lengo moja japo si la pamoja.

Sisi hatuna hoja ya kusema nani alikuwa na sera bora na sababu nzito zaidi kuliko mwengine, lakini angalau tunaweza kusema tu kwamba vyama vyote vilikuwa na sababu nzuri.  Kwa upande wa ZSP walitaka hivyo ili wapate nafasi ya kujenda uwezo wa Waafrika katika masuala ya Utawala na uendeshaji Serikali ingawa pia mtu anaweza kujiuliza tu iwapo, hiko kipindi cha mpito kingekuwa cha muda gani wakati Waafrika walikuwa wamechishwa na ukoloni.  ANP waliona kwa Zanzibar kuwa uhuru mara moja ndio muhimu kwa nchi iliyopita  kwenye ukoloni wa maonevu mazito ya mufa mrefu, ingawa hili lilionekana na wengine kama ni aina Fulani ya mbinu ya kutaka kuendeleza utawala wa kisultani.  Kitu cha kujiuliza ni jee, nini kilihakikisha kwamba ZNP ingeshinda wakati uchaguzi wa kwanza ulionesha namna ambavyo ASP ilijidhatiti.  Tukumbuke tu, hadi wakati huu umoja wa ZNP na ZPPP ulikuwa haujaundwa.  Kwa mujibu wa Sheikh Thabit ni kwamba, mbinu ya Mkoloni ya kuongeza majimbo kutoka 6 hadi 22 katika uchaguzi huo ilimaanisha kukipatia ushindi ZNP

Hata hivyo, kwa kuwa haya yote yalikuwa yapatikane kupitia sanduku la kura, bila shaka uchaguzi na namna ambavyo ungeendeshwa ndio hasa iliyokuwa shaka ya kila chama.  ZPPP haikutamka uhuru mara moja lakini hili ndio jibu la kimya kimya ingawa kubwa waliloona lizingatiwe ni vipi nchi itawaliwe baada ya uchaguzi unaoshindanisha vyama ambavyo vimejengeka kitabaka za kikabila.  Kuna malalamiko kwamba Mkoloni alikipendelea ZNP.  Hatuwezi kupingana na hisia hii, lakini ni kweli pia kwamba Mkoloni aliweza kukaa na vyama na kushauriana navyo kwa mambo ya msingi hasa yahusuyo chaguzi.  Imechukuwa miaka 10 katika mfumo wa leo wa vyama vingi, Serikali za CCM hawakupenda hata kusalimiana na Wapinzania licha ya kushauriana.  Haya ya leo ni mazingira ya uhasama na uadui mkubwa na inapotokezea CCM wamechanganyikiwa namna ya kusafisha masingira ya chuki waliyoyajenga wenyewe, basi huona njia pekee ni kutumia bunduki kwa kile kinachoitwa ‘kutuliza fujo’.  Na hivi ndivyo walivyofanya Januari yaliyoendelea kuathiri vibaya siasa na uchumi wetu.

Tukirejea katika Tume ya uchaguzi ya Mkoloni, tunaarifiwa kwamba mapendekezo matano yalifanywa.  Kwanza, Sultani aendelee kuwa mkuu wan chi lakini asie na madaraka ya kisiasa.  Pendekezo hili liliashiria kuendeleza usultani kwa upande mmoja, lakini pia lilimpunguzia SUltani madaraka na kuufanya utawala wake kuwa wa mpitao zaidi kuliko wa kujizatiti.  Yaonesha kwamba ni aina Fulani ya maafikiano ya ‘awamu ya mpita’ hasa ikizngatiwa kwamba sasa kulikuwa na jitihada za kuwa na Serikal ya Umoja wa Kitaifa.  Pili, ilitakiwa kuwe na Baraza la Kutunga Sheria lenye viti 22 (Unguja 13 na Pemba 9) vya kuchaguliwa na 5 vya kuteuliwa na liwe na Spika wake.  Tatu, ilikubaliwa na Tume hiyo kuwa na Waziri Mkuu na Mawizara mbali mbali.

Huku pia kulikuwa kunamaanisha kufifiliza kwa utawala wa kurithiana na kisultani.  Pendekezo la nne la Mkoloni, lilikuwa kwamba kwa chama ambacho hakiko Serikalini kuwe na Upinzani na Kiongozi wake apangiwe mshahara maalum.  Leo, mbinu moja ya CCM ni kuiba kura na kuhakikisha kwamba hakuna upinzani mkubwa au hata ulio rasmi katika Bunge na Baraza la Wawakilishi.  Na pendekezo la mwisho, lilitaka kwamba Zanzibar iruhusiwe kushiriki katika mazungumzo ya kuanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki.  Leo, ingawa Zanzibar ina Rais na Mawaziri 12 lakini haiwezi hata kuwa msikilizaji licha ya mshiriki katika mazungumzo kama hayo ingawa katika mpira Zanzibar inakubaliwa na Muungano kuwa mshiriki kamili anaejitegemea katika mashirikiano ya Afrika Mashariki kama nchi.  Tunaruhusiwa Zanzibar kuwa Taifa  katika mpira kwa sababu una gharama.  Ni kwenye suala la mapato tu ndio Muungano uimarishwe il udugu watu wa asili ustawi.

Kama mtu angetaka kujifunza zaidi mahusiano ya Muungano wa Tangayika na Zanzibar, basi hadithi za Abunuas zatosha kutuelimisha.  Katika maendeleo ya biashara, na uchumi haya kufanyika ili kuisaidia Zanzibar yanaonekana ni kuvunja Muungano.  Sisi tunaotetea haya tunaambiwa tunataka kuvunja Muungano na kwa kuwa Watanzania tumezoea kudanganywa, basi hatuna hoja baada ya Watawala kusema hivyo!  Maana ya serikali tatu si kuvunja Muungano, bali ni kupunguziana ajenda za malumbano na manung’uniko ili Watanzania wafikirie misingi ya kisasa ya maendeleo kuliko kutumia mufa mwingi kuchambua ngano za kisiasa.  Ustaarabu wetu leo unafikia kutukanana katika mabunge na majukwaa ya siasa sio tu kwa sababu chama kilicho na aila zao, wendelee kutawala namna na kadri watakavyo.  Haya yanaweza kuondoka kama Watawala wa CCM wangetaka, lakini kwa kuwa watawala hawataki, basi Watanzania wanaweza kuirejeshea nchi hii sifa na hadhi yake kwa siku moja.

Tukirudi katika makubaliano yale ya zama za kihistoria ya vyama vya zamani, Sheikh Thabit Kombo katika masimulizi yake yaliyonakiliwa na Mdundo, anasema kwamba baada ya mapendekezo haya ya kikatiba, vyama vyote vilifurahi isipokuwa ZNP ambacho kilichukia sana kumalizwa umaarufu wa Mamwinyi na Sultani.  Mzee Thabit hakutoa  uthibitisho wa dhana hii ambayo mtu mwengine angehisi kama ni maoni yake binafsi.  Kwa maoni yetu, hakuna mazungumzo na mapatano ya kutafuta suluhu yatakayomfurahisha kila mtu kwa kila kitu hasa kwa vile suluhu yoyote ni ‘nipe nikupe’.  Hata hivyo, inaonesha kwa mara nyengine kwamba hata kama Mkoloni alifanya upendeleo kwa baadhi a vyama wakati wa siasa za kihistoria lakini pia, nia ya kisiasa ilikuweko na haki kwa kiwango cha kufaa ilizingatiwa katika kusuluhisha migogoro wakati huo wa kiza katika historia yetu.  Hili la kusuluhisha migogoro kistaarabu ni jambo la kihistoria lililo jema lisiloweza kutarajiwa katika siasa za kale kwani ukoloni katika ujumla wake ni kutawaliwa na kutawaliwa kumeambatana na ukandamizaji na unyanyasaji.  Hizi za baadae si sifa njema kwa watawaliwa lakini zilikuwepo kwa kuwa ndizo zilizoutambulisha ukoloni sio tu Zanzibari, bali duniani kote.  Wazanzibaari tunachukua muda kuwalaumu ZNP kwa kuchukia kwa kumalizwa umaarufu wa Mamwinyi, lakini tunafurahia kumalizwa umaarufu wa ZanzibarKama kweli historia ndio tatizo letu kwa kuwa wanahistoria wanaamini historia hujirejea, basi irejee historia yote mbaya na ile njema.

Tukirejea kwenye uchambuzi wa uchaguzi ule, tutaona kwamba katika uchaguzi huo wa Januari 61, yako matatizo mengine zaidi yaliyojitokeza wakati wa matayarisho yake.  Kwa mfano, majimbo yalikatwa upya hasa pale ambapo vyama vilikweishajitayarisha kwa majimbo mengine.  Hili lilionekana dhambi kubwa kwa ASP lakini lilionekana zuri kuvifanyia vyama vya upinzani mwaka 2000 kwa kukata majimbo upya kihistoria.  Ukoloni, tunasema tena kwamba ni mbaya lakini ukoloni si rangi kama wanavyoamini Watanzania wengine, na iwapo pia kuwa ukoloni ni ukatili na unyanyasaji tu, basi bado Tawala za Tanzania baada ya uhuru hazijawacha tabia mbaya ya kuwanyanyasa na kuangamiza raia.  Mkoloni katika uchaguzi huu aliahidi kwamba atakaeshinda atapata nafasi ya kuunda Serikali, lakini matokeo yalikuwa kwamba ASP ilipata viti10, ZNP viti 9 na ZPPP viti 3.  baada ya matokeo haya ZNP ilikubaliana na ZPPP wachanganye vitti vyao ili kuwa na Serikali ya Pamoja, na kati ya viti 3 vya ZPPP, viwili vya vilikubali lakini kimoha kilikataa na kwenda ASP.  Hapa kila upande ukawa na viti 11.

Kwa matokeo hayo, jaribio lilifanywa na mkoloni kumpa fursa ya kwanza Mzee Karume wa ASP ya kuunda Serikali, lakini alishindwa kwani Baraza la Kutunga Sheria halikurishia.  Hivyo hivyo, fursa kama hiyo alipewa Mzee Ali Muhsini ZNP lakini misingi hiyo hiyo hakuweza kuunda Serikali.  Kama mkoloni angetaka kufanya vitimbi na vishindo vya kisiasa kama ilivyo leo katika CCM nani anaebisha kwamba asingeweza; hasa kwa vile amri ndio iliyoikichukua nafasi ya utaratibu na sheria kama tawala za kikoloni! Hapana ; baada ya sakata hili kukaa njia panda, sasa likawa tatizo la kisiasa ambalo lilihitaji kushughulikiwa.  Kwa mujibu wa Sheikh Thabit, “ikabaki njia moja tu kumaliza mgogoro huo, nayo ni kuunda serikali ya mseto ya pande zote mbili.  Serikali hiyo iliundwa; na Chief Secretary wa Serikali ya Mkoloni akateuliwa kushika nafasi ya Waziri Mkuu.  Kutoka ASP akateuliwa Sheikh karume kuwa Waziri wa Afry na Mambo ya Wenyeji na Ali Sharriff kuwa Waziri wa Kazi na Mawasiliano.  Kutoka ZNP/ZPPP Sheikh Ali Muhsin alikuwa Waziri wa Elimu na Ustawi wa Jamii na Sheikh Muhammed Shamte akawa Waziri wa Kilimo’.  Katika hili, mwisho Sheikh Thabit Kombo anasema hivi, “pamoja na mapendekezo kwamba Sultani asijiingizwa katika mambo ya siasa, lakini wazi wazi aliviunga mkoni vyama vya ZNP/ZPPP na kuvipa nafasi ya kutumia vyombo vya dola kuwatisha wananchi waliowapinga wakati wa uchaguzi ule”.  Mwisho wa kunukuu maneno ya Mdundo.

Hapo pana ushahidi kwamba kumbe suala la Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa Zanzibar sio tu kwamba ni la utashi wa kisiasa, lakini lilionekana kuwa ni la muhimu kusuluhisha migogoro ya kisiasa japo kwa muda Fulani huku ufumbuzi wa kudumu ukizingatiwa.  Mkoloni (mbaya) alilitumia na Waafrika tulikubaliana nalo.  Leo chini ya utawala wa Muungano hili ni dhambi na anaezungumzia Serikali ya Umoja wa kitaifa anatangazwa kuwa ni mroho wa madaraka  na Watanzania tunapiga kofi, lakini anang’ang’ania akae pekee yeye hapendi madaraka.  Watanzania tunaamini haya! Ndio tukasema, ukitaka kujua namna CCM inavyowachezea Watanzania soma hadithi za Abunuas.

Tujikumbushe hebu, pale wananchi wa kijiji cha Abunuas walipokubaliana kwamba watu wote wachote maji asubuhi ili kufanya mgao kutokana na uhaba wa maji.  Abunuas alikuwa akijificha usiku na kuchota maji.  Jitihada zote za kumdowea Abunuas akamatwe zilishinda.  Siku moja watu wakatega urimbo kwenye kinyago.  Abunuas kwa ujanja wake alikitambua haraka kuwa kile kilikuwa ni kinyago lakini pamoja na ujanja wake wote alishindwa kujua kuwa kina urimbo.  Kwa ujanja na jeuri yake akakipiga teke na akakanda hadi asubuhi na ukawa mwisho wa wivi wa Abuhuas.

Hivyo pamoja na tabaka katika enzi ya ukoloni lakini mashauri ya pamoja yaliwezekana na waliotafautiana kwa rangi na nasaba walikubaliana kukaa pamoja na kuendesha dola kwa pamoja.  Pana ushahidi kwamba uhasama wa vyama haukuwa kwa kiwango cha kutisha kama leo.  Pana ushahidi wa kuvumiliana kisiasa na hivyo kuubakisha utabaka katika hisia tu na sio katika maadili na hata itikadi za vyama.  Hapa historia si tatizo, lakini inafanywa ionekane kuwa tatizo.  Pamoja na madhila na matatizo yote katika ukoloni, bado hatujaona ushahidi wa wazi wa ukatili wa dola hata kufikia kiwango cha kuuwa na kuhajisi wanawake mithili ya majogoo wa alfajiri kama ilivyo leo Tanzania.  Huu ni utawala gani usio na haya wala usio juwa vibaya! Bado twaambiwa Lipumba mbaya, Sefu mbaya.

Tunachokiona kwa dhahiri ni kwamba, leo sio tu utawala wa Jamhuri ya Muungano unaipendelea CCM lakini kila uchaguzi ukifika Utawala unatoa silaha na askari kutia watu khofu, kutisha pamoja na kunyanyasa ilimradi tu uchaguzi usitoe matokeo ya haki na CCM iendelee na unyanyasaji wake.  Na unyama usiosahaulika ni yale yalioambatana na mauaji ya Januari 26/27. 2001.  watanzania waelewe tu kwamba mkakati na mbinu hizi za uovu zinatumia fedha nyingi sana kuliko fedha zote kupambana na Umasikini ni kupambana na CCM kwanza.

Tujikumbushe tu kwamba mauaji ya Januari 26 na 27 ni kilele tu cha unyama wa dola kwa sababu harakati za dalili mbovu zilionekana mapema sana pale Polisi walipoanza kupiga watu ovyo katika mikutano ya kampeni.  Waliwahi kuwafyatulia risasi watu katika mikutano ya Kampeni katika sehemu za Darajani, Kilimahewa na Kwahani.  Mjumbe mmoja wa Kamati Kuu ya CCM yeye alikuwa na mkia wa taa ambao alikuwa akiwashtukia wapiti njia Pemba na kuwacharaza bila sababu huku akilindwa na magari matatu ya polisi wenye silaha nzito.  Jee, haya yalifanyika katika historia?  Hii si haki ya kuwatendea Watanzania ambao baada ya madhila ya ukoloni ya muda mrefu mwishowe tumejitawala na tunaambiwa uhuru ni wa watu wote.  Yote Sultani aliyofanya ya kupendelea ZNP lakini Sheikh Thabit hakusema watu wangapi Sultani aliuwa kuulinda utawala wake kupitia chaguzi.

Leo tawala za Tanzania zinaendelea kujidhatiti katika madaraka kwa kuua na mwisho wa vituko vyote vya dola, walioshiriki kuuua wanapongezwa kwa kupandishwa vyeo na kupatiwa hifadhi Bara ili wasionekane na hapo hapo walioathirika kwa kunajisiwa, kupigwa na kuuliwa waume na watoto wao wanaambiwa wasamehe na wavulie.  Wakati tunaambiwa tusameheane bado mazingira ya kisiasa Tanzania hayajaonesha kuwa chaguzi na ubadilishanaji wa madaraka ambayo ndio vyanzo vya yote hayatarejesha ya nyuma.  Ikiwa leo kwa mambo madogo tu ya muafaka, hayatekelezi au yanatekelezwa kwa shida, vipi wananchi watahakikisha kwamba ‘lishalo limeshapita?’  bado kazi ipo, tena kubwa na bila  ya kutega urimbo, Abunuas kamwe hakamatiki.

2.1.5    Uchaguzi wa Tatu, June 1961

Kwa kuwa uchaguzi wa Januari 1961 haukuzaa Serikali ya kuchaguliwa ambayo ndio iliyotarajiwa hata na Mkoloni pamoja na wapiga kura kuwa iwe ya kukamilisha uhuru ili kuendeleza demokrasia ya kweli, ilibidi ufanyike uchaguzi mwengine mwaka huo huo wa 1961 katika mwezi wa Juni.  Jimbo moja zaidi liliongezwa na kwa mujibu wa Sheikh Thabit, eti liliongozwa Mtambile kwa sababu kulikuwa na ZPPP wengi.  Angalau Sheikh Thabit anatufahamisha sisi wanasiasa wachanga kwamba Watawala wakitaka kuhodhi madaraka hutumia mbinu mbaya ili wanavyopenda ndio moja ya mikakati yao ya kulazimisha ushindi.  Hata hivyo, Sheikh Thabit anaamini kumfanyika ASP tu wakati ule wa ukoloni ndio ni jambo baya, lakini CCM kuwafanyia wapinzani leo si tatizo!  Hatuwezi kumshukuru Mkoloni wala kumsifu kwani Ukoloni ulishapigwa muhuri wa ubaya, lakini tunaweza kusema kwamba kwa nafasi ya Mkoloni, tena sultani (ambae ni mtawala wa amri), basi iwapo angetaka ufalme uendelee angalau kupumuwa kwa miaka mengine zaidi za mbeleni, basi uchaguzi huu ungefanywa baada ya ule muda ambao angependa ufalme uvute pumzi hasa kwa vile sheria zilikuwa mali ya watawala hao zaidi kuliko zilivyo leo Tanzania.

Baada ya kuuharibu uchaguzi wa 2000 na hatimae kuua, serikali ya CCM ilipitisha sheria ya kurudia uchaguzi wa majimbo 17 ya Zanzibar baada ya miaka miwili.  Watawala hasa wanaojigamba kuwapenda watu waliamua kuwakosesha haki wananchi wa Pemba kwa kuwafukuza Wawakilishi na Wabunge wao kwa miaka miwili, ambapo Mkoloni alirudia uchaguzi baada ya miezi sitaru (kuanzia Januari 1961 hadi Juni 1961).  Ndio kusema kwamba katika wakati wa madhila kkwetu sisi Waafrika, Serikali ya kikoloni ilifanya chaguzi mbili katika kipindi cha mwaka mmoja ikiwa kama njia ya kutuliza amani na kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya uchaguzi sio ulioharibika, bali uliokosa kutoa mshindi safi.  CCM kwa upande wao baada ya kuuharibu (kwa maksudi) uchaguzi wa 2000, walitumia fedha nyingi na miezi kadhaa hadi kufikia angalau kukubali tu kuwa kuna matatizo ya uchaguzi.  Leo Taifa kukaa makambini kupaga namna ya kuharibu chaguzi za kidemokrasia, huku baada ya kila uchaguzi nchi inaendelea kutumia mamilioni mengine kuishawishi dunia kwamba hakuna tatizo la uchaguzi.  Umasikini ndio jaza ya Watanzania baada ya kila miaka 5 ya madaraka ya kulazimisha ya CCM.  Si hasha basi, kwa kuwa Watanzania ni waja wa sahau, hili laweza kujiweza kujirejea kwa mara ya tatu mfululizo.

Tukirejea tena katika uchaguzi ule wa Juni 1961 tutagundua kwamba kila uchaguzi una mikakati na mbinu.  Sheikh Thabit (1996: 112) anasema tena kwamba, “kama kawaida yetu sisi wa ASP tulilazimika kufanya maandalizi mapya ya kukabiliana na uchaguzi huo.  Kutokana na uzoefu tulioupata katika uchaguzi wa 1957 na ule wa Januari 1961, ASP ililazimika kubuni mbinu mpya za kuzuia uibaji wa kura au kupiga kura mara mbilimbili kama walivyofanya wapinzani wetu ZNP na ZPPP.  Anaendelea, ‘maana ile mbinu ya kuchovya dole gumba katika kopo la wino usiofutika haikufaa kitu  na kwa hivyo, tulijiandaa kwa namna nyengine”, mwisho wa kunukuu.  Sisi tunashukuru kwamba Mzee wetu Thabit kaondoka lakini katuachia hazina  ya mafunzo.  Kumbe CCM inakubali kwamba kupiga kura mara mbili mbili ni dhambi na kuiba kura pia ni dhambi lakini dhambi hii isingestahiki kwa wao kufanyiwa na Wakoloni tu, wao kuwafanyia Wapinzani leo ni jambo zuri.  Hivi ndivyo historia inavyojirudia, yaani kwa mabaya tu na sio kwa mema, lakini ilivyokuwa wanaofanya ubaya huu ni chama cha Mbita, hapa historia haina dowa.

Hata hivyo, pamoja na CCM kujua dhana ya dhambi lakini bado inasikitisha kwamba haijui dhara ya dhambi, na dhio maana ikapeleka Pemba vijana zaidi ya elfu 3,000 na kuwapandikiza katika baadhi ya majimbo kama vile Mkoani, Mkanyageni, Chonga, Wawi na Vitongoji ili kuendeleza madhambi.  Ni bahari mbaya kwamba wapiga kura kuwa harama walikuwa wakisafirishwa na kulindwa na vikosi vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania.  Inashangaza kwamba baada ya dhambi zote za wazi wazi, bado wako wanavyuoni wana maoni kwamba CCM imeshinda majimbo ya Mkoani, Mkanyageni na Wawi mwaka 2000 kwa kuwa eti kuna Waafrika wengi asili ya Bara.

Mmoja wa watoa maoni kama haya ni Profesa wa Chuo Kikuu katika nchi yetu.  Kwa mfano, [Maliyamkono, 2000], akiuelezea uchaguzi wa kwanza wa 1995 anasema; “Conversely, a strong electoral performance by CCM on Pemba occurred only in those constituencies in which there are large numbers of (Mainland) Africans, i.e, Wawi, Mkoani and Mkanyageni”.  Maana yake ni kwamba; “kwa upande mwengine CCM ilipata ushindi mkubwa zaidi mule mwahala mwenye Waafrika wa (Tanganyika), ambamo ni Wawi, Mkoani na Mkanyageni”.  Sisi tunajiuliza ni kwa nini wataalamu waseme CCM inapigiwa kura na Watanganyika tu na huku wanatueleza CCM ndio Mkombozi wa Wazanzibari?  Iwapo kauli hizi za wasomi ni kweli, kwa nini siku zote Waafrika hao wanaowaita wa Tanganyika wawe na hisia na maamuzi tafauti na Waafrika Zanzibar juu ya hatma ya Zanzibar?  Maoni kama ya Maliyamkono ndio yanayokumbusha ya nyuma na kurejesha hisia.  Iwapo pia Mbita ‘anazo hisi’ kwamba hisia za kisiasa za zamani ndio chanzo na sababu za mauaji basi angalau aeleze pia, vyanzo vya kuleta hisia za zamani.

Turudi tena kwa Sheikh Thabit bin Kombo, ambae anaendelea kusema “kwanza tulijua kuwa ZNP walikuwa na mtindo wa kujiandikisha katika vituo viwili au zaidi, kwa sababu wengi wa watumishi wa Serikali walikuwa ndio waandishi wa wapiga kura na ndio waliokuwa wanakipendelea Hizbu”.  Sisi tuulize basi jee katika kipindi ambacho wanaodhaniwa wanaipendelea CUF walikwisha kufukuzwa katika kazi, jee waliobakia walipendelea chama gani hata ikawa ndio wanaofaa kuandikisha wapiga kura?  Kwa nini ovu hili, pamoja na kuzungumzwa na kigogo wa CCM mwenyewe lakini hata wataalamu wetu hawaoni kuwa ni baya ili waone haja ya kuishauri Serikali juu ya madhara ya baadae katika jamii isiyotendewa haki?  Taaluma, hekima na busara za baadhi ya wanavyuoni zitatumika lini kuisaidia Tanzania kwa mambo mema?  Historia yetu inaborongwa ili kuendeleza ubaya.

Sheikh Thabit anamalizia kwa kusema “Afro Shiraz, tuliruhusiwa kuweka mashahidi tu katika kila kituo, kama vile vile walivyoruhusiwa vyama vingine”.  Mwisho wa kunukuu.  Tulisema tueleze sana kuhusu mazingira ya uchaguzi kwani yakiwa machafu (kama ambavyo  Thabit anasema yalikuwa), basi uchaguzi huwa na migogoro na kusababisha fujo na mauaji.  Bila shaka kukosekana kwa mazingira bora ya uchaguzi ndio kulikopelekea mauaji ya Januari 26/27, kwani mauaji tarehe 26 yalitokana na khfu iliyojengwa na usalama wa Taifa na kuishauri dola imalize udhia kwa ukatili wa mauaji.  Ama kwa yale mauaji ya tarehe 27, haya yalitokana na umma kupinga (kwa amani kabisa), kuvurugwa  kwa demokrasia kupitia zoezi la uchaguzi zinazosimamiwa na dola.  Kama kusingekuwa na uvurugaji wa uchaguzi kusingekuwa na malalamiko na kusingekuwa na mauaji.  Leo anatokea Mtanzania ‘saba na akili’ anasema mauaji yalitokea kwa sababu za kihistoria.  Huyu kalipwa umuluku wa fedha za umma ili aseme hivyo.  Ama lazima tumshukuru Marehemu Thabit kwa kusema kwamba, vyama kwenye uchaguzi kushindana kwa mbinu.  Lakini basi, ni bora mazingira yaruhusu ili kila chama kitumie mbinu zake, na mtutu wa dola usiwekwe kwenye orodha ya mbinu hizo kama ambavyo ‘Mkoloni asilia’ hakufanya.

Katika uchaguzi huu, ASP ilipata viti 10, ZNP viti 10 na ZPPP viti 3, na hivyo umoja wa ZNP/ZPPP ndio uliokuwa na wingi wa viti 13 dhidi ya 10 vya ASP, na hivyo umoja huo kupewa uwezo kisherua wa kuunda Serikali na Sheikh Mohammed Shamte wa ZPPP akawa Waziri Mkuu wa Kwanza, Mwafrika.  Ni kwa nini Shamte aliekuwa na viti kidogo kuwa na nafasi kubwa katika Muungano wao wa vyama ndio suala jengine.  Ingawa kila mtu atakuwa na maoni yake, lakini kitu kimoja kiko wazi; dalili ya haja ya umoja wa Kizanzibari ilikuwa dhahiri.  Funzo jengine tunalolipata katika sehemu hii ya historia ni kuwa ukitaka kujenga umoja wa Kizanzibari lazima maoni ya wananchi wa visiwa vyote viwili yatumike na yaheshimike kuunda utawala.  Kauli za huyu au yule ni mlafi wa madaraka ni poroja tu za kisiasa zinazotumiwa na mwanasiasa aliefilisika kimawazo.  Hakuna mtu au chama kinachoingia katika uchaguzi ikawa hakina uchu (hamu) wa madaraka.  Watanzania lazima tuzindukane.

Tukirudi kwenye uchaguzi wa Juni 1961, itaonekana kwamba nao ulilalamikiwa kama ule wa Januari 1961.  ASP ilisema kwamba haukuwa wa haki na huru na huku na baadae ukafuatiwa na fujo zilizoambatana na vifo vya raia wengi.  Kati ya watu 68 waliokufa, 65 walikuwa ni Waarabu na 3 Waafrika (Okello, 1967).  Kwa maoni ya takwimu hii, inaonesha kwamba kama Serikali  ya wakati ule (ambayo iliangalia zaidi maslahi ya Waarabu) ingekuwa na ghamiza ya matumizi mabaya ya silaha kwa raia kama ilivyo katika Serikali ya CCM, basi isingevumilia  kuona Waarabu 65 wakipotea mbele ya Waafrika 3 bila ya kulipiza kisasi kwa njia wanayoijuwa wenyewe.   Lakini haikuwa hivyo.

Januari 26 – 27 2001, huko Pemba, CCM ikiongoza vyombo vya ukandamizaji vya dola iliua zaidi ya watu 70 kwa kulipiza ‘eti kisasi cha askari mmoja’ ambae walisema kachinjwa na CUF.  Hiki kilikuwa kisingizio cha kufanya ufisadi na ushenzi wa kivita kwa raia wasio silaha.  Jee, tuwaulize wataalamu wetu na hasa Mbita, nini kibaya kwa Wazanzibari kati ya historia ya kisiasa ya uchaguzi wa Juni 1961 na vitendo vya CCM pamoja na dola yake vilivyoondosha watu kama kumbi kumbi katika maandamani ya amanni ya Januari 27?  Vikosi vya ulinzi bado vinaendeleza mauaji ya raia wasio hatia kwa kulinda utamu wa madaraka wa mabosi wengine?  Hivyo, Mbita na wenziwe wanatuona tu mbumbumbu sana hata Wazanzibari tuamini kwamba historia yetu ya kisiasa ndio tishio zaidi la maisha yetu katika demokrasia ya leo kuliko bunduki ya CCM inayotumiwa vibaya na dola.  Hii ni dhama potofu ya kihistoria.

Kufuatia machafuko hayo ya Juni 61, na mauaji ya watu, wengi wao wakiwa Waarabu, kulikamatwa wanachama wengi wa ASP.  Mtu asingefikiria kwamba wakati ule utamuuwa Mwarabu halafu utiwe rumane utoke ukiwa hai.  Yawezekana pengine, Waarabu wale waliokufa hakuna hata mmoja aliechanganya damu na Sultani, lakini walikuwa watu wa tabaka moja kwani utabaka ulijengwa kikabila.  Baadae kulikuwa na kesi na ni vyema kuangalia hukumu ilikuwaje..  [Mdundo, 1996:117], akimnukuu Mzee Thabit anasema “wakati wote huo wanachama wetu zaidi ya elfu wako ndani.  Othman Shariff, Mjumbe wa Baraza la Kutunga Sheria kwa upande wa ASP, akatangaza hadharani kuwa ASP italisusia Baraza la Kutunga Sheria ikiwa Serikali haitawafikisha Mahkamani wote waliotiwa kizuizini kutokana na machafuko na iwapo Mahakimu watakao sikiliza kesi hizo hawatatoka nje ya Zanzibar”.  Anaendelea Mzee Thabit, “British Resident akazipata habari hizo akatuita haraka na kutuambia kuwa amekwisha agiza Wanasheria na Mahakimu kutoka London tayari kuunda Tume ya Kuchunguza Machafuko na kuendesha kesi”.

Katika kulalamikia chaguzi za 1995 na zile za 2000, CUF ilifanya hivi hivi vilivyoahidiwa kufanywa na ASP katika enzi ya historia yetu na Serikali ya Muungano nay a Zanzibar zikaamua kuwafukuza wawakilishi hao wa wananchi moja kwa moja bila kujali kwamba athari kwa wanaowakilishwa.  Mkoloni aliwaita ASP haraka kwani aliona uhusiano wa sheria, demokrasia na maendeleo.  Kwa Zanzibari, leo baada ya kujitawala, watu wanapakaziwa kesi tena za kuua na uhaini na halafu wanakaa gerezani miaka zaidi ya 3, na baadae hunyanyaswa na kutolewa na kuambiwa kirahisi kwamba hakuna ushahidi.  Baada ya kusikilizwa kesi ya iliyoitwa ya uhaini iliyosingiziwa viongozi na wanachama wa CUF ambao walisota gerezani miaka 4 bila hukumu, mwishowe Jaji aliamua kuwa “haiwezekani watiwe hatiani kwa uhaini kwa kuwa Zanzibar si dola”.  Si hilo tu, kesi hii iliyowahusu Naibu Katibu Mkuu wa CUF Mheshimiwa Juma Duni na wenziwe ilikuwa ya kisiasa lakini ikatafutiwa ushahidi wa kijinai,  na kesi ya mauwaji yaliyofanywa na Majeshi ya Ulinzi na Polisi ya tarehe 26/27 ni ya kijinai lakini imehukumiwa kisiasa kwa kutumia Tume ya Mbita.  Kichekesho ni kuwa maelezo ya hukumu ni kwamba waliouliwa ndio wakosaji na wauwaji walistahili kuua na mwishowe wanastahiki kusamehewa.  Mkoloni mbaya kweli, lakini kwa nini CCM chama cha ukombozi kifanye uovu mkubwa namna hii kwa raia zake?  Tulifundishwa kuimba mwaka 1977 kuwa CCM ndie baba sasa tunatanabahi kwamba baba katugeukia kwa kukusufia.   Kwa nini ulimwengu uendelee kuwapa Watawala wa Tanzania jukumu na heshima ya kuhukumu kesi za wahalifu wa kivita wa Rwanda na Burundi lakini wahalifu wake wenyewe waachiwe?  Hata sheria za kimataifa zina ubaguzi wa wazi kama hivi!  “Sisi sote tuna msiba kwa ndugu zetu walouliwa, na hatusahau maisha yetu kwa roho zao walotolewa”.

Picha za cini zifuatazo ni :  Watuhumiwa wa Kesi ya Uhaini ya Viongozi wa CUF, Walisota Jela miaka 3 (1997 – 2000) na kasha kuachiwa kwa vile Zanzibar eti si Dola.

Katika kesi ya Juni 1961 ya mauaji ya uchaguzi, ASP ilishitakiwa kwa kufanya njama za kuharibu uchaguzi na halafu kusababisha mauaji.  Katika kujenga hoja na ushahidi, Jaji alipewa barua ambayo iliandikwa na kutiwa saini na yeye Mzee Thabit, ambae hata katika mahojiano yake na Jaji alikiri kuandika barua kwa Tawi lao, Dar es Salaam kuagizia vijana kuja kwa wingi siku ya uchaguzi.  Mzee Thabit alisema aliwaalika vijana kutoka Bara kwa sababu uchaguzi ni kazi ngumu na walihitaji msaada wao, Mdundo [1996:120].  Alipoulizwa kazi ngumu maana yake nini,Mzee Thabit alijibu uchaguzi hapa ni kazi ngumu kwani mtu analazimika kuamka alfajiri sana ili kuwahi kukaa msongoni kungojea kupiga kura na hulazimika kubaki hadi saa 12 za jioni.  Kwa kuwa huu ndio ukweli wa mambo, na kwa kuwa Jaji aliamini kuwa hivi ndivyo ilivyokuwa na kwa kuwa hii kweli ni kazi ngumu na vile vile kwa hukumu ilitegemea ukweli sio amri ya utawala (kama leo Tanzania) bila shaka basi ASP ilishinda kesi kirahisi.

Kama kweli Mkoloni alikuwa pamoja na ZNP na ZPPP kwa kila kitu, hizi zisingekuwa sababu za kushinda kesi kirahisi.  Hata tuseme ndivyo ilivyokuwa siku hizo za ukoloni, lakini kwa Tanzania ya leo tuliojitawala inachukua miaka mitano na zaidi mtu anaburuzwa katika Mahkama za sheria na bado hapati haki, na kila akienda kesini anaambiwa ‘ushahidi bado’ na uchunguzi unaendelea.  Hapa pia Mzee Thabit anatufahamisha kwamba kumbe ASP ilihitaji nguvu kutoka Bara siku zote ndio ishinde.  Na ndio hivyo hivyo kwa mrithi wake CCM hadi leo.  Huu ndio udugu wa damu ambao huongezeka zaidi kwa kumwaga damu.  Lakini alipoulizwa Mzee Thabit ni kwa nini mlete vijana kutoka Bara, alisema hawa ni Wazanzibar wanaofanya kazi kule.  Hivi ndivyo ilivyokuwa wakati ule, lakini kwa leo hata Wazanzibari waliokwenda kutembea tu Bara muda mchache tu kabla ya kuandikishwa, wanaporudi kutumia haki yao huzuiliwa kupiga kura Zanzibar.  Na ikionekana Sheria hazisaidii udhalilishaji huu, basu zutapindwa na kukunjwa ili kuwanyima watu haki.  Vituo vyote hivi, bado tunasingizia historia.

Pengine simulizi la Juni 1961 kwa akina Mbita lionekane si muhimu sana kwa funzo la kihistoria.  Hata hivyo, bado wachunguzi wetu hawapati funzo la namna matokeo ya uchaguzi wa wakati ule yalivyoonesha jinsi jamii ya Wazanzibari ilivyogawana takriban katikati kwa maoni ya kisiasa?  Asilimia 42.9 za ASP (kwa mujibu wa Taarifa ya Msimamizi wa Uchaguzi, Mchapaji wa Serikali Uk. 27 – 29) haikuleta ushindi, lakini na Muungano wa ZNP/ZPPP uliopata asilimia 48.7 za kura zote haukuwa ushindi wa kujivunia kwa nchi iliyokuwa na vyama vingi vyenye suta ya vyama viwili vilivyokaribiana nguvu.  Kama kweli uchambuzi wa kitakwimu (ambao ni sehemu ya historia) unazingatiwa na wanaotoa maoni ya hali ya kisiasa, kwa Zanzibar wataona kirahisi na kukubaliana kwamba Zanzibar imegawika takriban katikati kuhusu mtazamo wa kiitikadi ya vyama jambo ambalo likizingatiwa, basi ni dhahiri kwamba mfumo wa utawala unaowafaa watu wa Zanzibar ni ule wa ushirikishwaji wa makundi yote katika Serikali.  Kwa vile mfumo wa Mapinduzi hautou nafasi hii ndio maana tukasema Mapinduzi ya Zanzibar (tafauti na nchi zote duniani), ni mabadiliko ya kuondosha tabaka na kuanzisha tabaka jengine na kamwe si amabadiliko ya kondoa utabaka katika ujumla wake kama inavyotangazwa usiku na mchana na watawala.

Kwa maoni hayo hayo ushindi wa viti 13 vya ASP mbele ya 12 vya ZNP katika uchaguzi wa Juni 1961, kwa hali halisi ya Zanzibar haukuwa mkubwa wa kukiwachia chama chochote kuwa na nguvu za kiutawala.  Tena, kwa Zanzibar wanasiasa wanapaswa kutafautisha kati ya dhana ya nguvu za kisiasa na ile dhana ya nguvu za kiutawala.  Uimara wa utawala wowote unategemea nguvu za kisiasa.  Kwa Zanzibar nguvu za kisiasa zimeathiriwa sana na jiografia ya visiwa na majimbo.  Hili pengine lilitiliwa maanani na wanasiasa wa wakati wa ukoloni na ndio maana Shamte aliekuwa na viti 3, tena alietoka Pemba ndie aliekabidhiwa usukani na Ali Muhsin ambae chama chake kilivuna zaidi katika umoja wao.  Iwapo Wanasiasa wa wakati ule wangetilia maanani hali halisi ya Zanzibar si kiuchumi tu na kijiografia bali zaidi kisiasa, basi wangeona walistahili kuwa na Serikali ya vyama vyote pamoja na ASP kuliko ile ya ZNP/ZPPP peke yao.  Pengine wakati ule washauri wa siasa za Zanzibar walikuwa hawajazaliwa na kwa hivyo; dharau ya umoja iliendeleza ufukunyuku hadi kuzaa Mapinduzi yaliyoondosha tabaka moja na kuanzisha tabaka jengine.  Mapinduzi ni ukombozi lakini pia ni mauaji na kuwafutia majonzi jamii ya watu walioathirika kwa Mapinduzi si kwa kuzidisha ghamiza ya sera za kiukandamizaji na mauaji.  Kinachotarajiwa ni kuwa na sera za nchi zinazolenga kuwaunganisha ya kale kwa maneno, wakati vitendo vilivyoambatana mauaji ya Januari 27, 2001, vilishuhudisha unyama (kunajisi kina mama) mwingi wa dola ukifanywa Machomane na Mkanjuni; sehemu zenye wakaazi wengi wenye asili ya kiarabu.  Vitendo hivi vilidhihirisha wazi kwamba bado CCM na dola yake ina chuki isiyokwisha juu ya watu kutokana na kabila zao.  Iwapo bado akina Mbita anaamini kwamba historia ni tatizo la Zanzibar, basi inaonekana wazi kwamba hapa kwetu haijirudii bali inarudishwa na CCM ili kukumbusha ya zamani kwa vitendo.  Nini sasa tatizo, ni historia, gazeti la Dira au CCM na tawala zake!

Tunamalizia hapa kwa kusema kwamba, kwa vile hakuna ushahidi wa dola kutumia silaha vibaya kwa matukio ya Juni 1961, historia hii ndio halisi na ndio iliyopaswa kuwafunza CCM kuzuia matumizi mabaya ya silaha na nguvu za ziada katika matukio ya Januari 26 na 27, 2001.  Hii ni kusema, ingawa historia inaonesha kwamba kulikuwa na fujo na mauaji wakati ule, lakini historia ile haikuwa msingi wa akina Mbita kusema kwamba mauaji yatokee tena, hasa kwa vile, yale ya zamani hayakufanywa na dola kama yale ya Januari 26 na 27, 2001.  Kama mauaji ya Januari 26 na 27 yana fungamano na historia, basi imekuwa ni mapambano kati ya CCM na CUF vyama ambavyo eti leo baada ya miaka 40 vinaibua hisia za zamani.  Kinyume cha ukweli wa kihistoria, mauaji ya tarehe 26 na 27 yalifanywa na dola dhidi ya raia, na kwa kuwa  yalifuatiwa na unyama na udhalilishaji mwingi, basi inaonesha wazi kuwa pamoja na ukombozi wa kiutawala (uhuru), siasa hazijakomboa fikra na mawazo ya watawala wa leo kujifunza ya nyuma kwa kurekebisha ya mbele.

2.1.6    Uchaguzi wa nne, Julai 1963

Baada ya uchaguzi wa Juni 1961, Serikali ya Muungano wa ZNP/ZPPP ilidumu kwa miaka miwili kabla ya uchaguzi mwengine ambao ndio ulikusudiwa uwe wa mwisho kuelekea uhuru.  Kwa hivyo, kipindi cha kuanzia Juni 1961 hadi Julai 1963 kilikuwa na umuhimu kwani ni kipindi cha mazungumzo ya Katiba mpya ya Zanzibar baada ya Uhuru.  Mkutano wa kwanza wa kujadili Katiba ulifanyika London mwaka 1962 na vyama vya kupigania uhuru vilishiriki.  Ujumbe wa ZNP/ZPPP uliwakilishwa na Sheikh Ali Muhsin na Sheikh Shamte, wakati  ule wa ASP uliongozwa na Mzee Karume na Othman Sharif.  Huko Lancaster House mazungumzo yalifanywa bila ya mafanikio.  ZNP/ZPPP walitaka kuweko na Serikali ya madaraka ya ndani na baadae uhuru bila uchaguzi kwa madai kwamba katika kipindi kifupi cha miaka miwili isingekuwa vizuri kufanya chaguzi 3, hasa kwa vile uchaguzi wa Juni 61 uliishia kwa vurugu na mauwaji.  Na zaidi walipendekeza katika kipindi hicho cha mpito Sultani aendelee kuwa kiongozi wa  nchi. ASP wao walikataa kuwa na Serikali bila uchaguzi na kuhusu Sultani kuendelea ndio kabisa walichokataa.

Picha juu:          Baraza la Kutunga Sheria baada ya uchaguzi wa 1963.  Katikati mwenye suti ni Marehem Karume.  Hii ni  tafauti na baada ya uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi 1995 ambapo Wawakilishi wa CUF hawakualikwa hata kuhudhuria sherehe za kumwapisha Raisi kwa tiketi ya CCM.

Baada ya mapendekezo ya kila chama kusikilizwa, Mkoloni aliamua kuwe na Serikali ya Umoja wa Kitaifa kushirikisha vyama vyote vitatu.  ZNP/ZPPP walikubali mara moja na kuahidi kutoa nafasi 3 za uwaziri kwa ASP kati ya zote 9.  hata hivyo ASP ilikataa Serikali ya Umoja wa Kitaifa na kuhiari kurudi nyumbani bila Madaraka ya Ndani wala uhuru.  Katika kuelekea uhuru, hapa inaonesha namna ambavyo ASP ilivyopania kuhakikisha kutokukubali kuunda utawala na tabaka nyengine za Wazanzibari.  Kwa mantiki hiyo inaonesha kwamba, katika kushika mamlaka ya dola ilihiari yapatikane kwa njia yoyote ilimradi tu uwe ni wao tena wao peke yao.

Hii ndio sera ya CCM (mrithi wa ASP) hadi leo, kwani kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kwa uchaguzi wa 1995 tuliambiwa kuwa CCM ilipata asilimia 50.2 ya kura na viti 26 na CUF asilimia 48.8 na viti 24, lakini bado CCM ilisema „mchele na chua havikai pamoja“.  Hizi ndio fikra za viongozi wa Kiafrika kuwaona baadhi ya wananchi wao kuwa ni chua kwa kuwa tu wanatafautiana kiitikadi.  Mwalim wa Chama cha Mapinduzi alisema maendeleo yanaletwa na watu, leo wanafunzi wake katika hiyo hiyo CCM wanasema baadhi ya watu ni sawa na chua tu kwenye mchele.  Haya ni maoni yenye kutafautiana sana ndani ya chama kimoja kinachoongoa umma mkubwa katika nchi yetu.  Kwa vyovyote vile, bado ushahidi unaonesha kwamba katika historia yetu ya siasa kuliwahi kuwa na juhudi za kuwaunganisha Wazanzibari ili kuendesha madaraka kwa pamoja licha ya kuwepo kwa utabaka.

Baada ya mkutano wa London kutofanikisha lengo la kupata Katiba ambayo ingefanikisha kupata Utawala wa Ndai na baadae Uhuru kamili, vyama vilirudi nyumbani.  Baadae Serikali ya Uingereza ilimleta Zanzibar Sir Robert Arundell kuja kuangalia mambo yanayoleta mfarakano katika vyama kiasi kwamba hawakubaliani hata katika masuala ya Utawala na Uhuru ambao ndio uliopiganiwa na vyama vyao na hata vya nchi vyengine barani Afrika.  Sir Robert alileta maamuzi mawili makubwa ambayo kila chama ‚kilinufaika na huku kikipoteza’ (give and take – quid pro quo).  Kwanza, alikubaliana na ASP kwamba majimbo ya uchaguzi yaongezwe kutoka 23 hadi 31.  Vile vile alikubaliana na wazo la wanawake kupiga kura na kuondosha vikwazo vya kipato kwa mpiga kura.  Pili, alikubaliana na wazo la ZNP/ZPPP la kuwa na madaraka ya ndani na hivyo Waziri wa Makoloni kutangaza rasmi tarehe 24 Juni 1963 kuwa ndio ya Utawala wa Ndani.  Na Serikali hii ya ndani ikawa ile ile iliokuwepo baada ya uchaguzi wa Juni 61, na hivyo Sheikh Shamte ikawa ile ile iliokuwepo baada ya uchaguzi wa Juni 61, na hivyo Sheikh Shamte aliendelea kuwa Waziri Mkuu katika Serikali ya Madaraka ya ndani.  Pia, papo hapo Mkoloni akatangaza kuwa uchaguzi wa kuelekea uhuru kamili uwe mwezi wa Julai 1963.

Katika uchaguzi huo wa Julai 1963, matokeo yalikuwa, ASP ilipata viti 13 (Unguja 11 na Pemba 2), ZNP ilipata viti 12 (Unguja 6 na Pemba 6) na ZPPP ilipata viti 6 vyote kutoka Pemba.  Na mchanganyiko wa ZNP/ZPPP ndio uliokuwa na viti 18 na hivyo kupewa uwezo wa kuunda Serikali, sasa ya kukabidhiwa Uhuru.  Na kwa hivyo, uhuru wa Zanzibar ulipatikana rasmi tarehe 10 Disemba, 1963 kutokana na matokeo ya uchaguzi huo Sheikh Muhammed Shamte Hamad akiwa Waziri Mkuu.

Katika harakati hizi za chaguzi za kuelekea uhuru na hata uhuru wenyewe, kuna mambo matatu ya msingi yanayotupa uzoefu wetu wa kisiasa.  Kwanza, ni namna ya kutokukubaliana na suala la madaraka na uhuru lilivyotokea huko London na namna lilivyoshughulikiwa.  Baada ya vyama kurejea nyumbani bila makubaliano Serikali ya Uingereza ilijua kwamba matatizo ya kisiasa ya Zanzibar yamo katika uendeshaji chaguzi pamoja na mgawanyo wa madaraka.  Mapendekezo yote ya ASP yalihusu namna ya kusafisha mazingira ya uchaguzi ili kutoa nafasi  kwa kila chama kutumia vizuri haki ya kidemokrasia.  Na hii ni dhahiri kwamba kwa maana halisi demokrasia ikikubaliwa na vyama vyote kuwa misingi yake ni chaguzi tena chaguzi za haki na huru.  Mtazamo na malalamiko ya ASP wakati ule ulikuwa ni kutoridhika na watu wasio Waafrika (kwa tafsiri yao) au Waafrika wanaoshirikiana na wasio “Waafrika halisi”, kushika madaraka ya Zanzibar hata kama wanakubalika na Sheria zote kuwa ni Wazanzibar.

Hili bila shaka ndilo lililopelekea Mapidnuzi maana haidhuru walikubaliana kuwa uchaguzi ule uwe ni wa uhuru, lakini kumbe ungekuwa wa uhuru iwapo tu ASP ingefanikiwa kuunda Serikali.  Hata leo, CCM inaamini kuwa uchaguzi ndio njia ya kubadilishana madaraka, lakini hawaamini kwamba madaraka kwenda kwa vyama vyengine ni haki inayostahili kuheshimiwa.  Iwapo ufukunyuku wa wakati ule ulileta mapinduzi yaliyomwaga damu nyingi ambayo hadi leo tunayashangilia kwa shangwe na vigelegele vingi, ni nini basi kingezuia dola kuchukua silaha na kuua kwa kile kinachofikiriwa kuhatarisha Mapinduzi na Muungano chini ya utawala wa Chama cha Mapinduzi Dola ya Tanzania ilifanya kila juhudi kutafuta kisingizio cha mauaji ya tarehe 27 Januari, 2001, lakini ukweli ni kwamba mauaji yaliendeshwa na Serikali za CCM kuuadabisha umma ambao ulikuwa ukitoa maoni yao kwa kudhani demokrasia imetoa fursa hiyo lakini kinyume chake hawakufahamu kwamba mapinduzi na demokrasia havijawahi kukaa nyumba moja.  Ilivyokuwa hali ya muundo wa kiutawala bado ni ule ule wa ‘demokrasia ya kimapinduzi’ bado utata unazidi kutanda juu ya hali halisi itavyokuwa katika chaguzi zinazofuata.

Pili, kunajitokeza swali jee, ni kwa nini Shamte (ambae ASP walimkubali kama mwafrika mwenzao) hakuungana na Waafrika wenziwe badala yake akaikumbatia ZNP (kilichopigwa muhuri na ASP kuwa ni cha Waarabu) ambao walikuwa na tafauti kubwa na ASP? Jibu limo katika manifesto ya ASP ya wakati ule.  Ukurasa wa 127 wa Kitabu cha Mdundo unaeleza mazungumzo ya Babu Thabit kama hivi „………., ASP ilitaka kuunda Serikali ya peke yake na wala isingewezekana kuingia katika serikali ya mseto na ZNP au ZPPP au hata wote kwa pamoja“.  Ukweli huu unato maoni kwamba, pamoja na kuwa vyama vilijengeka kitabaka na kuwa na tafauti kubwa kisera, lakini ASP ilikusudia kuendeleza utabaka na tafauti hizo kuanzia kwenye mfumo wa utawala bila kufikiria kwamba hili lingeiathiri jamii tunayoihitaji kwa maendeleo.  Kwa kuwa CCM inaenda vile vile kama ASP iliyozaa CCM, basi yatosha kwamba uzoefu wa wazi wazi wa miaka 40 ni bora zaidi kwa ushahidi kwamba katika kuiunganisha jamii ya Zanzibar CCM haina nia wala njia.  Baadhi ya wanasiasa na wachunguzi walijitahidi kupoteza muda kupotasha historia kwamba CUF ina uhusiano na Hizbu na ZPPP na kwamba eti inataka kuleta Waarabu ikiwa madarakani.  Hizi ni propaganda bobo za kisiasa na haziwezi kutolewa ushahidi na hao wahubiri.  Wazanzibari wakiendelea kusikiliza uzushi huu watachelewa sana kuona taa ya maendeleo.  Hili halitaki kusisitizwa kwani hata hii leo miaka 40 baada ya Mapinduzi bado wengi wa Wazanzibari wanalala na njaa, hawana ajira, hawana umeme, hawana maji ya kutosha yalio safi na salama na mahitaji mengi ya msingi bado yanakosekana.

Iwapo Sheria ya Usajili wa Vyama ya 1 992 inavitaka vyama kutokuwa na uhusiano na vyama vya zamani, na CUF ikavuuka kikwazo hicho na kusajiliwa, basi Msajili wa Vyama angekuwa amekiuka sheria.  Hili ni zinduo kwa Watanzania.  Akina Mbita wasiwaeleze Watanzania kwamba wanadhurika kwa historia.  Historia ya Zanzibar, kama nchi nyengine ina mabaya na mazuri, lakini hata kwa yale mabaya, basi hayawezi kuruka kama mkizi ikawa ndio sababu za kuuliwa ndugu na watoto wetu.  Hata hivyo, kwa kuwa tumeshaona baadhi ya mazuri katika siasa za zamani, basi nazo zijirudie kuwaendeleza Wazanzibari.  Maana yetu ni kwamba, mabaya ya zamani tuendelee kuyalaumu lakini yale mema pia tuyaendeleze.

Katika siasa za leo vyama vya ZNP na ZPPP havipo wala havirudi tena, lakini la kushangaza ni kwamba wachunguzi bado wanaendelea kuwalazimisha Wazanzibari wasio wanachama wa CCM kwamba wao ndio wanaostaiki kuwa warathi wa Hizbu na Shirazi.  Hii ni kashfa ya kisiasa na mwenye kutamka haya ni muflisi kisiasa, kwani kati ya vyama vya leo ni CCM peke yake ndio inayotokana na vyama vya zamani (ASP na TANU) ambavyo viliungana tarehe 7.7.1977.  Tunazidi kusisitiza kuwa Washauri wa CCM ndio wanaojenga chuki za kisiasa (na sio kamwe ukweli wa historia) kwani wataalamu hao ndio wanaowafahamisha wananchi kuwa miongoni mwa jamii kuna wengine ni maadui wa wengine.  Washauri hawajatoa rai ya maana ya kuuangalia mgawiko wa kijamii na kushauri njia bora za kuishi pamoja badala yake wanasingizia historia tu.  Ushauri wao humaanisha kuwapa mkakati CCM ili ing’ang’anie madaraka kwa nguvu, bila ya kujua kwamba popote penye kutumiwa nguvu, maafa na mauaji hayazuiliki.  Kwa mfano [Maliyamkono, 2000:61], katika kutoa maoni ya uharibifu wa uchaguzi wa 1995 anasema kwamba;


„One of the reasons behind the feeling that the 1995 Presidential election results were rigged is the narrow victory Dr. Salmin had over Seif Shariff Hamad”.  Maana yake ni kwamba:  “kati ya sababu zilizojenga hisia kwamba matokeo ya uchaguzi wa Rais wa 1995 yalighushiwa ni kutokana na ushindi mdogo Dr. Salmin aliopata dhidi ya Seif Sharif Hamad”.  Alichowashauri CCM hapa ni kwamba wakitaka kuvuruga na kuiba uchaguzi, basi wafanye kweli kweli kwa maana kwamba ushindi mdogo n rahisi kujengewa hoja na kulalamikiwa.  Ushauri huu ndio uliotumiwa katika uchaguzi wa Oktoba 2000, kwani mgombea wa CCM aliekataliwa na chama chake alitangazwa kuwa mshindi tena kwa asilimia kubwa kuliko hata 1995.  ingawa ushauri wa mtaalamu wa siasa ulifuatwa lakini Tanzania baadae ikaingia katika aibu kama alivyothibitisha Rais Mkapa katika hotuba ya kutia saini Muafaka.

Maliyamkono pia alipaswa kujua kwamba miaka mitano sio kwamba inafundisha njia za wizi wa kura tu, bali inafundisha hata namna ya kudai haki kwa wanaoibiwa kila mara.  Ushauri wake kama ungekuwa wa kujenga basi angesaidia kuijenga Zanzibar, lakini kwa sababu alikusudiwa kuharibu basi aliiharibu sio tu Zanzibar, lakini hata Tanzania, kwani bila ya kujua nae alishiriki kumkosesha Mkapa usingizi baada ya Wazanzibari wengi ilibidi kupoteza maisha.  Si hayo tu, Tanzania ambayo ilizoea kuhami wakimbizi nayo ilibidi mara hii isitiriwe.  Nyerere hakua na nia safi na Wazanzibari lakini hakupenda kuona ukandamizaji na uuaji wa halaiki hadharani na wawazi wazi.  CCM inaposema inamkumbuka Nyerere hatujui inamkumbuka kwa lipi?

Katika uchambuzi wetu wa uchaguzi wa 1963, pia tunaona dhahiri suala la Pemba ambako ASP ilipata viti 2, ZPPP viti 6 na ZNP viti 6.  Kiti kimoja ni cha Chake chake ambako ASP ilishinda kwa kura moja.  Ingawa ASP ilishinfa kiti hiki, lakini kimantiki na kitakwimu ni shida kukihakikishia chama hicho kuwa huu ni ushindi wa kutegemea;  kwani chaguzi ambazo hata zingefuata baada ya masaa machache licha ya miaka michache, ushindi wa kura moja ni rahisi kubadilika.  Hii ni kusema kwamba ASP ilipoteza umaarufu wa kisiasa tokea alfajiri huko Pemba.  Kwa vile hali hiyo bado inaendelea kwa kasi leo miaka 40 baada ya mabadiliko ni dhahiri basi, kama si maslahi ya vyama tu ndio yatakayozingatiwa sehemu hiyo ya Pemba haiwezi kuwa na maendeleo, kwa kuwa inachukuliwa kuwa ni sehemu inayopinga chama ambacho kimejijengea ukiritimba wa kutawala maisha tena bila ya kushirikisha walio weni na wenye fikra tafauti za kiitikadi.  Ama ni kwa nini watu wa Pemba waliichagua zaidi ZNP na ZPPP kuliko ASP ni suala jengine la historia lisilohitajika sana kujibika kwa manufaa ya kitabu hichi, kama lile suala ambalo haijibiki kirahisi ni kwa nini nayo ASP haikukubaliana na wazo la kuunda Serikali na vyama vilivyoungwa mkono kwa kiasi kikubwa na Wazanzibari.

Tunawajibu kujikubmusha kwamba, hata katika mfumo wa chama kimoja CCM ilikumbana na vikwazo vingi katika chaguzi kwa upande wa Pemba.  Ilikuwa ni mwaka 1984 ambapo Bwana Ali Hassan Mwinyi alipeta kwa ushindi mnono ambao hajawahi kuupata mgombea mwengine yeyote hadi leo.  Kampeni za mwaka ule zilionesha wazi wazi tokea awali nani angekuwa msaidizi wa Mwinyi baada ya uchaguzi, hivyo kuashiria kile kinachoonekana kama umuhimu wa mgawano wa madaraka baina ya visiwa vya Unguja na Pemba, kuwa miongonii mwa mambo muhimu ya kuzingatiwa kabla hata maandalizi ya chaguzi hayajaanza.  Huu ni ushahidi kwamba mgao wa madaraka katika siasa za Zanzibar una nafasi kubwa sana katika kuamua hatma ya kisiasa na maendeleo katika nyanja nyengine za kimaisha.

Tunazidi kusisitiza zaidi kwamba, kitu kikumbwa cha kuzingatia ni kwamba mgao huu wa madaraka kwa Zanzibar si suala linaloweza kupata jibu ndani ya chama chochote kinachotawala kwa kuangalia misingi na mtazamo wa itikadi moja.  Ukweli huu ukidharauliwa na mambo yakalazimishwa kwa utashi wa kiitikadi mfumo wa utawala hauwezi kuwa na ufanisi.  Kwa mfano, muda wote ambao marehemu Dr. Omar Ali Juma (ambar ni Mpemba) alikuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar, ulikuwa ni wakati wa misukosuko kwa siasa za Zanzibari, na kamwe hakuweza kusaidia umoja wa visiwa viwili vya Pemba na Unguja na hata ule wa Tanzania ambao aliuhubiri sana.  Kwa kuwa huu ulikuwa ni ukweli ulioonekana wazi na hata CCM yenyewe, ndio maana baada ya Dr. Omar kuwa Makamo wa Rais wa Muungano, nafasi ya Uwaziri Kiongozi haikwenda kwa Dr. Ali Moh’d Shein kama alivyoahidiwa wakati  wa uchaguzi wa 1995.  ilionekana hakuna tafauti iwapo nafasi hiyo itachukuliwa na mtu kutoka Unguja au mtu kutoka Pemba ilimtadi wote wanahubiri itikadi moja.

Halikadhalika, hali ilikuwa ni hivyo hata baada ya uchaguzi wa mwaka 2000 na zaidi katika kipindi hiki mambo yalichafuka zaidi kwani ndio kipindi kilichoshuhudia mauaji ya kinyama ya Januari 26 na 27, 20001.  Ni Muafaka peke ndio uliosawazisha hali hii mbaya na Muafaka umefanikiwa kwa sababu chombo chake kinaendesha kwa mabadilishano ya itikadi zaidi ya moja.  Ni maoni yetu kwamba hatma ya Zanzibar kisiasa na kiuchumi imo katika dhana ya mgao wa madaraka kuliko mvuto wa kiitikadi unaostawi hadi leo baada ya miaka 40 ya Mapinduzi.  Ama iwapo Watanzania tunaamini kwa vitendo kwamba maendeleo ni watu, basi nadharia ya siasa sasa inahitaji kuelekezwa katika kuwachanganya ili kuwashirikisha watu.  Ushirikishwaji unaohubiriwa kwa miaka 40 sasa haujafanikiwa na ukiwepo umejaa nyufa kwa sababu watu hawajachanganyishwa kupitia dhana ya madaraka.  Sera ya CUF ya kuunda Serikali kwa mujibu wa matokeo ya kura kati ya visiwa hivi imekusudiwa kutoa jibu kwa tatizo hili.

Katika kuelezea histori a ya kisiasa ya Zanzibar tumejaribu kuangalia iwapo kulikuwa na juhudi na majaribio kwa vyama zamani kwa kukaa pamoja na kuzungumza khatma ya nchi yao kwa  masuala yaliyo nje ya mipaka ya vyama vyao.  Tumegundua, hili lilizingatiwa pamoja na kwamba vyama vilikuwa vikitafautiana kwa misingi ya kikabila kuliko ya kisera na kiitikadi (kama ilivyo leo).  Hali hii iliweza kushusha joto, mori, munkari na mizuka ya kisiasa kila mara mivutano ilipojitokeza.   Kwa mfano, katika wakati wa kupigania uhuru, kulikuwa na juhudi za pamoja katika Bara la Afrika za kuunganisha nguvu za Waafrika ili kuharakisha uhuru kwa zile nchi zilizokuwa na vyama (vya kupigania uhuru) zaidi ya kimoja.  Matokeo ya juhudi hizi ni kuzaliwa kwa Jumuiya kama vile za PAFMECA na PAFMECSA>

Katika kutekeleza lengo hilo, chama cha TANU kilialika vyama vingine vya Afrika Mashariki, Kusini na Kati kwa ajili hiyo hiyo katika mkutano wake uliofanyika Mwanza, Septemba 1958.  Katika mkutano huo, vyama vya ASP na ZNP vilishiriki na vilikubali sio kuungana moja kwa moja, lakini angalau kuwa na kamati ya pamoja ya kuratibu shughuli zao.  Hata hivyo, haikuchukua muda, Mwalimu alianza kuutia kidomodomo, kasoto na chokochoko umoja huu haukuendelea.  Kwa mfano, alidiriki kusema “…….., kisiasa viongozi wa Zanzibar wanalengo moja lakini wanatofautiana kwa sababu ya ukabila”.  Kauli hii ilizua hisia tafauti miiongoni mwa ASP na ZNP na haikuchukuwa muda umoja wao ukafifia, kama taarifa ya PAFMECA ya mwaka 1959 inavyoonesha.  Twaweza kujiuliza  hapa, hivyo pale walipokubaliana hawakuwa na makabila?  Kwa nini ukabila iwe ndio sababu ya mkato kutoka kwa Nyerere baada ya vyama hivi kukubaliana kushirikiana?  Waswahili wanasema ‘mvumbua kijungu ndie mpishi’, na Nyerere ndie alieanza kupandikiza mbegu ya fitna ambayo leo inaimarishwa na warathi wake ambao wameapa kumuenzi na kumrithi kwa hali yoyote.  Huu waendelea kuwa ushahidi tosha kwamba tafauti zetu Zanzibar ni za kupandikizwa na wenzetu ambao wanakerwa sana na kuwepo kwetu kama nchi na kuwa na nguvu za kisiasa na kiuchumi.

Vile vile, kwa mujibu wa masimulizi ya Mzee Thabit, vyama vya ASP, ZNP, ZPPP na Umma vilihudhuria mkutano mwengine wa Katiba kuanzia tarehe 20 hadi 24 Septemba 1963.  Mzee Thabit anaeleza kwamba “Katika mkutano huo, wote tulikubaliana tunataka uhuru upatikane tarehe 10 Disemba, 1963.  Vile vile, pamoja na mvutano mkali, lakini hatimae tulikubaliana kuwa Sultani aendelee kuwa Mkuu wa Nchi na vile vile amteuwe mrithi wake baada ya yeye kuondoka”  Mdundo (1996:111).  Huu ni ushahidi mwengine wa makubaliano na uvumilivu wa kisiasa ambao ulikuwa haujaathiriwa sana na fitna za Muungano na uvumilivu wa kisiasa wale wanaolumbana kuhusu tarehe ya uhuru, pia huu ni ushahidi mwengine kuwa tarehe 10/12/1963 ndio tarehe vyama vilivyokubaliana kuwa iwe ya uhuru.  Ama iwapo uhuru wa tarehe 10 Disemba, 1963 ulikuwa wa watu wachache  au wa rangi Fulani au eneo Fulani, basi ni suala la mjadala mwenginei kabisa  ambalo hata likiamuliwa halitabadilisha ukweli wa kihistoria kuhusu uhuru wa Zanzibar.  Ama tuna maoni kwamba iwapo uhuru ule wa tarehe 10.12.1963 ungekabidhiwa ASP basi pengine hii hadi leo ingekuwa ndio tarehe halisi ya uhuru na pasingekuwa na haja hata ya kufanya Mapinduzi.

Tukimalizia maelezo ya vyama vya zamani, cha muhimu zaidi tulichojifunza si sera za vyama hivyo wala miundo iliyojenga vyama vyenyewe, lakini ni namna mazingira ya wakati ule wa kikoloni yalivyoweza alau kuruhusu utendajji wa shughuli za siasa ikiwa ni pamoja na kufanyika kwa chaguzi na kuwa makini na malalamiko ya pande zote.  Huwezi kuamini kwamba utawala  wa kikoloni (ambao umekuwa ukishutumiwa na kulaaniwa kwa mwisho wa laana)  ungweza kutoa fursa kwa vyama vya upinzani kueneza siasa kwa wasaa bila ya bughudha na vikwazo vya kupindukia kama vya leo.  Mzee Aboud Jumbe anaeleza katika kitabu chake maarufu cha ‘The Partner – Ship’ kwamba kila ASP ilipopata nuksani ya kupoteza uchaguzi, basi ujumbe mzito ulikuwa ukienda Pemba ili kuwatuliza wanachama.  Hakukuwa na pingamizi kule ya wapi pa kupita na lipi la kusema hata pale ilipofahamika wazi kwamba Pemba ilikuwa ngome ya vyama vyengine.

Ama katika kuzidi kutilia mkazo hoja hii, pia tuangalie mfano mwengine ambao ni ule wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Afro Shirazi mwaka 1961 uliofanyika katika jengo la Manispaa ya Mjini Unguja (ambalo ni jengo la Serikali) tena katika kipindi cha harakati za chaguzi.  Kuna ushahidi kwamba hakukuwa na shida wala vikwazo  vya kukikinga chama kisifaulu kueneza sera zake na kujitangaza.  Katika kipindi cha kuanzia mwaka 1995 hadi 2000 chama cha CUF  kimezuiliwa na Serikali za CCM, kufanya mikutano katika viwanja tu wala sio majengo, kwa zaidi ya mara mia moja na sitini.  Hata baada ya uchaguzi huo, bado utawala unavipangia vyama vya siasa mwahala mwa kueneza siasa.  Ni mzaha kusema historia ndio sababu na chanzo cha matatizo ya kisiasa yanayopelekea hata mauaji ya raia wasio hatia Zanzibar na hata Tanzania kwa ujumla.

Hapa ndipo  Watanzania wanapopaswa kujiuliza, ni kwa nini mauaji ya Januari 26 na 27 2001; ingawa yalitokea Tanzania mzima, lakini kwa Zanzibar iambiwe kuwa ni sababu ya kihistoria kama Tume ya Mbita inavyoeleza! Tunamalizia kwa kusema kwamba, historia si chanzo cha mauaji ya tarehe 26 na 27 Januari, 2001; na kwa hivyo mauaji hayo yangeweza kuepushwa na Serikali za CCM zilizotumia vyombo vya dola vibaya kwa hivyo basi, historia ni kisingizio tu cha kuwafanyia Wazanzibari mabaya na kibaya zaidi, sasa mbinu hii inataka kuenezwa Tanzania mzima.  Ni nini basi chanzo na sababu za mauaji ya tarehe 26 na 27, Januari 2001.  endelea kusoma ili uzidi kuelimika.

Sehemu ya 2: Chanzo na sababu za mauaji

Tulipokuwa tukizungumzia historia ya kisiasa ya Zanzibar ambayo Mbita anasema ndio chanzo cha mauaji, tulikuwa tukiangalia vigezo vingi.  Tumefanya hivyo ili kuangalia viwango na namna vigezo vilivyoathiriwa na maendeleo na mabadiliko ya kimfumo.

Vigezo tulivizingatia ni hivi vifuatavyo:

?          Uhasama wa kupindukia wa vyama vya siasa,

?          Mashirikiano na vyama vya siasa,

?          Aina ya migogoro na misuguano ya kihamasa,

?          Mazingira ya chaguzi,

?          Nafasi ya dola katika siasa,

?          Usuluhishi wa matatizo ya kisiasa,

?          Fitna kutoka nje ya siasa za Zanzibar na mwisho

?          Ukiritimba wa kung’ang’ania madaraka

Uchambuzi wetu umetuonesha kwamba:

?          Uhasama wa kisiasa ulikuwepo lakini ulikuwa ukipunguzwa na jitihada za dola katika kuvikutanisha vyama na kuzungumzia tafauti zao na zaidi uhasama huo haukuashiria kama ungedumu na kutufikisha pahala pabaya pabaya kama tulipo leo.

?          Kulikuwa na mashirikiano ya vyama kwa kiwango kizuri kuliko leo.

?          Misuguano na mapambano yalikuwa ndani ya wafuasi wa vyama, kuliko leo ambapo ni dola ya chama tawala dhidi ya upinzani.

?          Mazingira ya chaguzi yalikuwa bora kwa kiwango cha maendeleo ya demokrasia ya wakati ule.

?          Juhudi za usuluhishaji migogoro zilikuwa kubwa na makin zaidi kuliko leo na maafikiano hayakuwa yakichukua muda kama leo.

?          Mbegu za fitna zilianza kupandikizwa na Mwalimu Nyerere na wafuasi wake wa karibu.

?          Ukiritimba wa kung’ang’ania madaraka ulianza kupungua kila harakati za uhuru zilipokaribia mwisho.  Leo ukiritimba wa utawala umeikumba Tanzania na ustawi wake unawagharimu watu maisha na mali nyingi.

Kwa hivyo, kwa kiasi fulani hakukuwa na historia mbaya ya chaguzi inayopaswa kuwa kigezo cha uvurugwaji wa makusudi wa demokrasia nchi na kuwa chanzo cha mauaji katika mfumo wa leo.  Hata hivyo, iwapo vigezo vyote hivyo vilionesha athari mbaya zaidi zamani, basi hakukuwa na sababu kwa nini leo viendelee kuwepo hasa kwa vile walioshika mamlaka na madaraka ya dola ni CCM ambayo inaamini yaliyotokea katika historia ni mabaya matupu na ni CCM ndicho chama kilichorithi vyama vya ukombazi (ASP na TANU) vilvyoahidi kuondoa kila mabaya ya kikoloni.  Iwapo kazi ya ukoloni ilikuwa ni kuua raia, kwa nini CCM iendelee kufanya kazi chafu kwa raia wasio hatia?  Baad ya majumuisho haya ya kihistoria sasa ni pahala muafaka pa kuangalia maelezo kuhusu chanzo na sababu za mauaji hayo ya tarehe 26 na 27 Januari, 2001.

Mauaji ya tarehe 26 na 27 Januari ni tukio baya, la kikatili na la kutisha na kwa kweli ni mkasa usiosahaulika.  Hata hivyo, kila mkasa unakisa.  Kisa kikuuu kilichopelekea mauaji ni kule kudhihirika na kukataliwa kwa wazi (lakini kwa amani), kasoro na mapungufu ya maksudi ya misingi madhubuti ya kuendeleza demokrasia yanayojionesha wazi katika kila chaguzi za vyama vingi.  Kisa hiki kilipata nguvu kutokana na Serikali kukosa nia na uadilifu wa kuheshimu haki za binaadamu hasa haki za uhuru katika chauzi pamoja na haki za uhuru wa maoni.  Cham cha Mapinduzi kwa kujipa cheo cha chama tawala ndicho kinachoendesha Serikali inayosimamia vyombo vya dola vilivyohodhi uwezo, na mamlaka ya kusimamia demokrasia ya vyama vingi  na kulinda haki za binaadamu.  Kwa kujipangia majukumbu haya ya chama tawala na chama dola, hivyo CCM haiwezi kukwepa lawama panapotokea uharibifu, kama vile ambavy isingewacha kujilabu na kusifiwa iwapo ingefanikisha wajibu huo.

Katika Taarifa ya Tume ya mbita, Kifungu 183 kimeorodhesha msururu wa mambo ambayo ndio yaliyoitwa kuwa ni vyanzo na sababu (za muda mfupi) za matukio ya tarehe 26 na 27 kifungu hicho kinaeleza kwamba, baadhi ya sababu za mauaji hayo ni: udhaifu wa Tume ya ZEC vyama kutokubali kushindwa, uchaguzi mbaya usio wa haki, vyombo vya dola kuingilia siasa, serikali kutoheshimu maamuzi ya wananchi, kutotekelezwa kwa muafaka wa 1999, kutoeleweka vyema mfumo wa vyama vingi, kukosekana haki: bila ya haki amani haiwezi kutawala, maendeleo duni hususan kisiwa cha Pemba, kutokuwepo matayarisho ya kutosha juu ya kuendesha mfumo wa siasa ya vyama vingi, kuwepi dhana kwamba wapinzani wanaleta vurugu, Uunguja na Upemba: hisia kwamba Mpemba hawezi kutawala, vyama kuhoji uhalali wa Muungano, nia ya CUF ya kutaka kureeshwa kwa wenyewe mali zilizochukuliwa baada ya Mapinduzi, ……………. vyama vya siasa kutotii amri za Serikali, uchaguzi wa 1995, n.k“……..

Sehemu ya pili, pia kuna sababu za vyama na Polisi.  Sababu walizotoa CUF kuishutumu CCM ni : vyama visivyo na historia ya ASP na TANU haviwezi kutawala, nchi iliyopatikana kwa bunduki haiwezi kutolewa kwa vikaratasi na dhana ya Mapinduzi daima.  CCM iliishutumu CUF kwa kauli hizi:  ngangari, jino kwa jino, kukaa vizuka, kulala barabarani, kuwa vilema na damu kumwagika.  Jeshi la Polisi lilitoa kauli kwamba iwapo CUF wao ni ngangari basi Polisi wao ni ngunguri.  Haya yalisemwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi Inspekta General, Alhaj Omar Mahita.

Ukiangalia sehemu ya kwanza ya sababu hizi ambazo Tume ya Mbita ilipokea kutoka kwa wananchi, itaonekana kuwa ingawa kuna uzito katika kuelezea matukio ya mauaji, lakini pia kunaweza kuwa na kisa zaidi cha kuelezea kwa ninii yakajiri haya ambayo mwishowe yalisababisha matukio hayo thakili.  Kitu kimoja kimejidhihirisha katika maoni hayo ya kwanza.  Nacho, ni kuwa hakuna yale maoni ya kuonesha kwamba kwa kiasi kikubwa Wazanzibari wana maoni ya athari za siasa za zamani.  Kati ya maoni 23, yaani Kifungu 27 (a – w), ni maoni mawili tu yaani 27 (i na n) ndio yalionesha mnasaba wa khofu na hisia za siasa za zamani.  Huu ni ushahidi kwamba hisia za siasa za kale si sababu walizonazo watu katika kufanya maamuzi ya kisiasa na kamwe haziwezi kupewa uzito wa kuwa chanzo cha mauaji.  Tunachopaswa kujiuliza awali ni jee, iwapo hii ndio sampuli ya sababu walizozitaja waliohojiwa, jee hizi za siasa za zamani zilitoka wapi hata zikachukua nafasi kubwa na ya mbele katika ripoti yake ya mauaji!.

Sababu 21 zilizobzkia katika sehemu ya kwanza zinaweza kunasibika na siasa za malumbano na kimunkari hata zisizozingatia itikadi ya vyama.  Hizi ni siasa zenye kashfa, matusi, shutma nzito na zenye kuleta mgawiko na hasama.  Hata hivyo, ikumbukwe tu kuwa hali hii ilianzia tokea mwanzoni mwa majio ya vyama vingi katika mwaka 1992.  Wakati wote huo hakukuwa na mapambano ya dhahiri baina ya wafuasi wa vyama vilivyolumbana.  Tukio moja la mauaji lilitokea Shumba Mjin ambapo Omar Ali na mwenzake walipigwa risasi wakati wa kupachika bendera ya CUF mwanzoni mwa mwaka 92.  huyu hakuuliwa na mwana CCM, bali aliuliwa na Polisi (chombo cha dola).  Hii ni kusema, pamoja na mapambano ya matusi waliyonayo Wazanzibari (kama inavyodai ripoti ya Mbita) bado wanachama waliozoea kulumbana hawakuwahi kuamua kuuana.  Hiki ni kipimo cha uvumilivu wao na inaonesha wazi kwamba hata kutukanana na kuhasimiana basi kunaletwa na mazingira ambayo ndio hicho kisa tunachokitafuta.  Kutokana na mauaji ya Shumba Mjini, ni dhahiri kwamba kisa cha kwanza kinatokana na matumizi mabaya ya vyombo vya dola.

Tukija kwenye sehemu ya pili ya mauaji ya Tume ya Mbita, tunaona kuwa kuna aina 9 za sababu.  CUF imeishutumu CCM mara 3 kwa matamshi yanayotokana na wao wenyewe CCM.  Matamshi yote haya yana mnasaba na hisia za siasa za zamani.  Matamshi haya hayakuwa malumbano kama yale ya sehemu ya kwanza ingawa vile vile ni ya kihisia.  Zaidi ya yote maoni haya yalikuwa ni ya kisera kwani yalitangazwa hata ndani ya Baraza la Wawakilishi na kwenye mikutano mingi ya hadhara.  Imetokezea kwamba katika chaguzi zote mbili za awali CUF imenyang’anywa ushindi kama CCM ilivyo ahidi, kuwa nchi haitoki kwa vikaratasi kwa vile ni ya kimapinduzi daima na hasa kwa vile CUF haitokani na vyama vya ASP na TANU; ingawa si hivyo tu, CUF haitokani na chama chochote cha zamani.  Hapa tunaonesha dhahiri kwamba iwapo kuna hisia za siasa za zamani kama anavyoona Mbita, basi huu ni ushahidi kwamba, CCM ndio wanaoziendeleza kwa maslahi ya kisiasa.  Huku pia ni “kujizatiti kwa tabaka“ hata ndani ya CCM yenyewe kuliko kuichukulia kuwa ni dhana ya utabaka kwa ujumla wake katika Zanzibar.

CCM waliishutumu CUF kwa mambo sita, yaani jino kwa jino, ngangari, vilema, kukaa vizuka, kulala barabarani na damu kumwagika.  Itakumbukwa kwamba matamshi haya yalikuja baada ya kutolewa maoni kama haya na CCM.  Kuna wakati CCM walikuwa wakionesha kanda za mauaji ya Rwanda katika Televisheni ya Zanzibar.  Kuna wakati, Kiongozi mmoja wa CCM aliwahi kusema hadharani kwamba kuua watu wawili hadi kumi kwa kulinda amani ya wengi si tatizo.  Katika uchaguzi mku wa mwaka 1995, Rais Mstaafu Ali H. Mwinyi alikuwa akimnadi Dr. Omar Ali Juma wakati akiwania Umakamo wa Rais, kwamba yeye apewe kura kwa kuwa ni chinja chinja.  Maoni haya ndio yaliojibiwa kwa maoni kama hayo ya CUF.  Na ndio tukasema hata kama CUF na CCM walilumbana kwa vitisho vya kila aina, vitisho vya CCM vya mwaka 1996 vya kuuwa watu 2 hadi 10, lakini hapakufa watu waliouliwa hadi kufikia Januari mwaka 2001.

Mwisho, ni kuwa maoni ya Polisi yaliilenga CUF, tu kwa kusema iwapo CUF ni ngangari basi Polisi ni ngunguri.  Polisi haikuwahi hata kusikitika kwa kauli za CCM licha ya kukemea.  Polisi ndio waliokuwa mstari wa mbele kwa kuwafanyia CUF fujo tokea mwanzo wa vyama vingi hadi kilele cha mauaji.  CCM isingekuwa chama dola isingeingia katika uchafu huu wa kushiriki mauaji.  Kwa uchambuzi huu wa vyanzo na sababu za mauaji, ni dhahi basi dhima yote ya mauaji haikuwa kwa wanachama wa CUF na CCM wa hapa Zanzibar, isipokuwa ilikuwa kwa viongozi wa CCM ambao walitoa matamshi ambayo ni sawa na amri kwa vyombo vya dola ili iwe vitekeleza mauaji.  Kwa kuwa CCM ni chama dola, kila ukipanda juu ya uongozi ni dhahiri kwamba kiongozi wa Dola ndie huyo huyo wa CCM.

Kwa kuwa muhusika mkuu wa kutekeleza kwa mauaji ya tarehe 26 na 27 Januari, 2001 ni vyombo vya DOLA (hasa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Polisi na Usalama wa Taifa) ambavyo vyote ni mali ya CCM na Serikali zake, kwa hivyo Chanzo cha Mauaji ni matumizi mabaya ya vyombo vya dola.

Hivyo hivyo, kisa cha mauaji ni kukosekana kwa maadili bora ya uendeshaji wa kidemokrasia ya mfumo wa vyama vingi, kutoheshimiwa kwa haki  za binaadamu, mazingira mabaya yanayochochea matumizi mabaya ya vyombo vya dola na silaha.

Kwa hivyo sababu za mauaji zinatokana na kasoro nyingi ndani ya Katiba za nchi, Sheria za ukandamizaji na zile za uchaguzi zisizoendana na matakwa ya mfumo wa vyama vingi pamoja na uendeshaji na usimamizi mbaya wa chaguzi.

Ingawa mauaji ya tarehe January 26/27, 2001 yalitokea kufuatia kuvurugwa kwa uchaguzi wa pili wa vyama vingi, lakini hali ya kuzorota kwa maendeleo ya siasa ilitokea tangu kumalizika kwa uchaguzi wa kwanza ambapo nao pia ulivurugwa.  Hivyo ni mazingira ya kisiasa na kidemokrasia ndio chanzo kikuu cha mauaji na athari za siasa za ukoloni hazina nafasi wala mahusiano ya maana katika mauaji ya tareh 26 na 27 Januari, 2001.
Share this article :

1 comment:

 1. Attn:

  Usikose nje kutoka kutoa yetu mega kama wewe ni katika haja ya mkopo au kama wewe
  wasiwasi juu ya madeni yako na kuwa na historia mbaya ya mikopo, tuna
  vifaa katika nafasi ya kukusaidia kurejesha udhibiti wa fedha yako.

  Huduma zetu ni pamoja na:

  - Business mikopo kwa ajili ya kuanza-up na refinancing biashara zilizopo
  - Binafsi mkopo hadi $ 500,000
  - Home mkopo
  - Muda mfupi mkopo
  - Mkopo wa gari na mikopo kwa ajili ya madhumuni yoyote worthwhile.

  Pamoja na mchakato wetu masaa 24 ya uamuzi huo, tunaweza kufadhili kwa ajili yenu ndani ya 2 hadi 3
  biashara siku moja kwa moja kwenye akaunti yako ya benki. Sisi kufikiria ni
  radhi kufanya biashara na wewe.

  Alitaka kuokoka? sisi kutoa kwa kukodisha taratibu zetu
  wanatakiwa kupata mkopo mapema. Tuna mtandao unaweza kujiinua
  juu ya!

  Reply nyuma kama una nia ya lindomartinez67@gmail.com

  Regards,
  Global Finance Services

  ReplyDelete

ZILIZOSOMWA SANA.

Followers

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Proudly powered by Blogger
Copyright © 2011. Msamaa. - All Rights Reserved
Template Design by Creating Website Published by Mas Template