FALSAFA YA UDINI NA UGAIDI: Njia ya uongo uliofichwa - Msamaa.
Headlines News :
Home » » FALSAFA YA UDINI NA UGAIDI: Njia ya uongo uliofichwa

FALSAFA YA UDINI NA UGAIDI: Njia ya uongo uliofichwa

Written By Unknown on Tuesday, May 21, 2013 | 11:45 AM


 
 
Bakari M. Mohamed
UDINI na ugaidi ni uhalifu dhidi ya ubinadamu. Udini na ugaidi ni uhalifu unaoweza kubomoa mujtamaa wa maelewano baina ya mtu na mtu, au watu na watu na hata kundi moja la jamii ya watu na kundi jinigne! Udini na ugaidi ni silaha inayotumika kwa kificho na mtu na au watu wenye taathira ya woga na hutumia mbinu ya kuogepesha katika kutekeleza malengo yao.
Kwa vyovyote viwavyo, udini na ugaidi ni dhana zinazofanana isipokuwa tofauti ni jinsi ya utekelezaji wa malengo yake.
Kwa upande mmoja, tuanze mada hii kwa kuangalia dhana ya udini na kisha tuiunganishe na dhana na faslafa ya ugaidi katika kutoa mifano inayoweza kusaidia kuelezea hali halisi ilivyo na jinsi ilivyoasisiwa na kuwa taasisi inayotishia amani ya dunia na kuvuruga maisha ya binadamu katika nyanja za siasa, uchumi na jamii.
Udini (si dini) ni hali ya mtu mwenye dini (imani na njia ya maisha ya kiroho na ucha Mungu kwa mujibu wa imani yake) kupendelea dini yake na kuifanya dini yake ni bora na inayostahili kuwepo badala ya nyingine.
Udini ni hali ya upendeleo unaoatamiza fikira na mawazo ya kwamba: “Watu wa dini fulani ndio wenye uhuru na haki ya kuwa na satwa ya kutawala maisha yote ya jamii, siasa na hata uchumi inapobidi).
Udini ni imani ya kuwa bora kwa kundi moja la dini juu ya jingine! Udini ni ugonjwa wa kisaikolojia unaotokana na ubinafsi uliokithiri (kayaya) ambao humfanya binadamu kujiona yeye ni bora zaidi na anachokiamini mtu kuwa bora zaidi ya wanachoamini wengine hata pasipokuwa na hoja za kisayansi zilizofanyiwa utafiti, kujaribiwa na kukubalika ni haki na kweli.
Mazingira ya binadamu na kujipendelea ni asili ya binadamu kwa vile hutokana na hali ya ubinafsi (rejea kisa cha Kaini kumuua Habili – watoto wa baba mmoja na ndugu moja wa damu).
Udini hujionesha kwenye jinsi ya uendeshaji wa maisha ya kijamii, kiuchumi na kisiasa kwenye mazingira ya watu wenye mitazamo na falsafa tofauti juu ya imani na itikadi za dini (kwenye nchi ya dini mseto kama Tanzania).
Umbile la udini huumbwa juu ya misingi ya (1) dhana mbaya dhidi ya binadamu wengine, (2) roho ya chuki dhidi ya binadamu wengine, (3) tabia inayoongozwa na uadui dhidi ya binadamu wengine, na (4) mafundisho yasiyozingatia maisha huru, adilifu na yanayozingatia usawa.
Mafundisho yanayoatamiza fikira za udini huathiri wafuasi wa dini husika juu ya kuwatendea binadamu wengine kinyume na uhuru, haki, usawa, uadilifu, na insafu kwa mujibu wa ujenzi wa ‘jamii ya watu walio sawa na huru.’
Uhuru ni zao la nafsi; na mara zote nafsi huru ni ile inayojali nafsi za watu wengine katika kutamani kuwaona watu wengine wenye mitazamo ya kifalsafa na kiitikadi wakiishi maisha yenye staha na raha kama vile wanavyoishi wale wenye mitazamo ya falsafa kiitikadi inayotofautiana nao!
Huu ndio mwanzo wa maisha yanayozingatia thamani ya ubinadamu na utu wa watu wote kwa uhuru na haki ya kuishi kwa kutegemeana.
Sintofahamu, songombingo na sokomoko la kijamii, kisiasa na hata kiuchumi limewafanya binadamu kuwa kama wanyama wa mwituni wanaoishi pasipokufuata kanuni za kimaumbile kwa mujibu wa maisha ya asili ya binadamu!
Binadamu si mnyama na hawezi kuwa mnyama; japokuwa kifalsafa binadamu anaweza kuwa na roho mbaya zaidi ya mnyama!
Binadamu anaweza kumuua nduguye (kama alivyofanya Kaini kwa Habili), na ndio kusema kwamba ni muhali kumuona simba akimuua simba mwenzie na kumtafuna hata akiwa na njaa (ya kufa). Binadamu mwenye roho ya chuki, uadui na uuaji ni hatari kwa vile anapopata nafasi ya kuwa juu ya wengine ndivyo anavyoweza kutumia nafasi yake ya kuwa juu kuatamiza fikira zake za kujipendelea na kuwafanya wengine wasipate nafasi kama aliyo nayo yeye kwa mtazamo wa falsafa ya itikadi yake.
Kutokana na mfumo wa maisha mseto tunayoishi binadamu tangu azali (mwanzo wa uumbaji na asili ya binadamu) tumewekewa sheria, kanuni na taratibu za kimaumbile za kutofautiana kwa mitazamo ya kifalsafa na ya kiitikadi.
Hata hivyo tofauti zetu hazikuwekwa kwa minajili ya kuwafanya wengine waonekane duni, dhaifu au dhalili mbele ya wengine, hasha! Isipokuwa ni tofauti zilizowekwa na Mwenyezi Mungu mwenyewe ili kuwatofautisha binadamu wa jamii moja na wengine kwa mitazamo inayotofautiana lakini yenye asili moja.
Tofauti nyingi zinatokana na fikira za upembuzi juu ya muktadha wa kuyaendea mambo yanayohitaji akili angavu ya utambuzi na jinsi ya kujitambulisha kama binadamu huru katika jamii ya watu wenye mitazamo huru na inayohitilafiana!
Tofauti lazima ziwepo, na kwa tofauti hizo zinazoruhusiwa na akili angavu na ya kawaida ndizo zinazotufanya tuwe na “uhuru wa maoni.”
Kila mtu ana uhuru wa maoni na kueleza maoni yake kwa fikra huru zinazozingatia uhuru na haki ya watu wengine. Udini unachukua sura ya kuwafanya watu wengine walazimishwe kukubaliana na utashi wa mtu, watu au kundi la watu wenye mitazamo ya kifalsafa na kiitikadi inayotofautiana na watu wengine.
Udini umezalishwa na watu na unaenezwa na watu wenye nia ovu na roho mbaya zenye dhamira ya kupandikiza chuki ambayo ndiyo inayozaa uadui unaosababisha mbinu chafu za mapambano yanayogharimu maisha ya watu wasiokuwa na hatia.
Sasa turejee kwenye dhana ya ugaidi na jinsi unavyochukuliwa na hata kupewa maana. Hapa tutaangalia ugaidi ni nini, asili ya ugaidi na chimbuko lake kihistoria, na hata kuangalia baadhi ya mifano na mahusiano yake na udini. Ugaidi ni vitendo viovu vinavyotekelezwa na magaidi kwa mfano mauaji, wizi wa kimabavu, vitisho na kuwahangaisha watu ili kudumisha maslahi yao ya kibinafsi (tazama Kamusi ya Karne ya 21, Longhorn, 2011, ukurasa wa 518).
Ukiitazama maana hii utaguandua kwamba ugaidi ni ‘uovu’ na unafanywa na watu ‘waovu.’ Uovu ni roho chafu na ya kishetani; na hakuna dini (kama njia ya maisha inayokubaliwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu na wa kweli) inayoelekeza watu kuwa na nia ‘ovu’ na kufanya uovu! Hakuna dini inayofundisha uovu; na kama ipo, basi ni njia ya shetani aliyelaaniwa!
Maisha ya binadamu yamejengwa kwenye msingi wa utu (yaani, ubinadamu wake). Na ndiyo kusema kwamba binadamu aliyekamilika ni yule anayetambua ubinadamu wake na anayejitambulisha kwa ubinadamu wake huku akizingatia maisha yenye saada kimaanawi na kimaada kwa mujibu wa mwongozo wa haki unaotoka kwa Mwenyezi Mungu – Mwenyezi Mungu ambaye ndiye chanzo cha uhai!
Thamani ya binadamu ni uhai aliopewa na Mwenyezi Mungu Muumbaji; na hakuna awezaye kuchukua nafasi ya uumbaji wa thamani hii adimu na adhimu hata mwisho wa dahari!
Dini (kama njia) zimewekwa ili binadamu afuate utashi wa ucha Mungu na kuwatendea binadamu wengine vile apendavyo yeye (binadamu) kutendewa!
Kanuni ya thamani juu ya maisha ya binadamu ni kuishi kama mgeni au mpita njia anayetaraji kurejea kwa Mwenyezi Mungu kupokea malipo yake ya haki kwa mujibu wa maisha yake ya hapa duniani. Hakuna shaka yoyote kwamba ugaidi kama njia ya waovu ni kitisho cha dunia na ndio msingi wa mauti ya utu na ubinadamu!
Historia ya ugaidi inaanzia mbali sana; hata hivyo, matukio ya ugaidi yameendelea kurekodiwa kwa zama nyingi na kwa nyumati mbalimbali za binadamu.
Lipo tukio kubwa la kigaidi na ovu machoni pa wanandamu hata kama lilifanywa miaka zaidi ya elfu mbili iliyopita!
Hili ni tukio ovu la kuzima haki ya kuenea kwa falsafa ya ukombozi wa mwanadamu kutokana na uovu ulioenea zama hizo na ndio maangamizi ya kuenea kwake zama hizi.
Ukitazama historia ya ugaidi wa zama za karne ya 14 hadi 18 utagundua kwamba magaidi (watu waovu) walikuwa wakitumia mbinu za kufanya vitendo viovu vya kigaidi katika kufikia malengo yao ya kijamii, kisiasa na kijamii kwa kujenga mazingira ya hofu na kuwatia woga wahanga wao (rejea: www.research-terrorism.com).
Inawezekana sana, na hususan kwa wanagenzi wa historia wakadhani kwamba matukio makubwa ya kigaidi ni yale tu yaliyojitokeza 9/11 (Marekani), hasha!
Ugaidi umekuwapo duniani kwa muda mrefu na unaendelezwa kwa mtindo maalumu wenye kupangiliwa na kuwekewa mikakati maalumu ya utekelezaji na taasisi zenye malengo ya kimkakati katika kufanikisha mradi wenye malengo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii kadhalika.
Tuchukue dhana ya ugaidi inayopigiwa chapuo na Marekani na washirika wake ambayo ndiyo inayoatamizwa kuchukuliwa kama sehemu ya mafundisho ya mapambano na vita dhidi ya ugaidi wa dunia (international terrorism).
Sidhani kama wapo waliofanya utafiti wa kina na kujiridhisha pasipokuwa na shaka yoyote kwamba ni nani aliyeuanzisha ugaidi huu tunaouona leo unaodhaniwa kuwa ni matokeo ya kundi la al-Qaeda.
Nani ameanzisha kundi hili la al-Qaeda na kwa nini? Ni utafiti mpana unaoweza kuweka bayana uanzishwaji wake na malengo yake japokuwa ni nadra sana kukuta waandishi wameandika hususan wale wanaoandikia vyombo vya habari vya kimataifa vilivyoisukuma dhana hiyo!
Hakuna shaka yoyote kwamba, al-Qaeda ilikuwa inaongozwa na Osama bin Laden! Ni nani huyu Osama bin Laden? Ushahidi wa moja kwa moja unaopatikana kwenye vyanzo vinavyoaminika pamoja na uongozi wa Marekani kukiri (kama alivyofanya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekeni Bibi Hilary Clinton) kwamba al-Qaeda iliundwa na Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) na kupewa kiasi cha dola za Marekani bilioni tatu ($ 3bn/-) ili kundi hilo liendeshe vita dhidi ya Urusi (USSR) ya zamani iliyokuwa ikiikalia Afghanistan (rejea: www.theinsider.org, news.bbc.co.uk, na www.forbes.com).
Kiongozi wa al-Qaeda alipata mafunzo yake ya kigaidi chini ya usiamizi wa CIA na Marekani ilikuwa inajua malengo ya kuanzishwa kwakwe.
Hata hivyo, kwa Marekani urafiki wao ni wa kimasilahi zaidi kuliko wa kuendelea. Na ndivyo walivyoifanya al-Qaeda na kiongozi wake Osama bin Laden.
Waliitumia al-Qaeda kwa malengo ya kimasilahi na kimkakati zaidi na baadaye walipohitilafiana kimasilahi waliibatiza al-Qaeda jina la ugaidi na kuanzisha vita dhidi yake!
Ugaidi unaenezwa na taasisi zenye malengo mahususi; ninachotaka kuandika hapa ni kwamba, ‘ugaidi unapewa usaidizi wa hali na mali na taasisi maalumu kwa malengo maalumu.’
Hivyo ndivyo ugaidi ulivyoendelea kuatamizwa kwa masilahi na kwa nyakati tofauti za historia.
Tukiachilia mbali mfano wa gaidi namba moja (kama alivyobatizwa na Marekani na washirika wake) na ndivyo kundi la al-Qaeda lilivyofanywa lijulikane dunia nzima. Pamoja na al-Qaeda kuna makundi mengi yaliyoorodheshwa kwenye orodha ndefu ya makundi ya kigaidi duniani.
Hii orodha ni kwa mujibu wa nchi zenye masilahi yake kwenye hii via inayoitwa ya ugaidi duniani!
Pamoja na hayo, tusisahau kwamba hata hapa kwetu Afrika kulikuwapo na watu na makundi yaliyoitwa ya kigaidi enzi za harakati za kupigania uhuru miaka ya 1960 hadi mwishoni mwa miaka ya 1990.
Makundi kama vile UNITA lililoongozwa na Dakta Jonas Savimbi wa Angola, na kundi la RENAMO lililoongozwa na Alfonso Dhlakama wa Msumbiji.
Hata wakati mmoja mzee Nelson Mandela (Madiba) aliwahi kuwekwa kwenye orodha ya magaidi!
Kwa vyovyote vile ukimtazama aliyeitwa gaidi Dakta Jonas Savimbi wa UNITA alikuwa akipewa msaada na usaidizi wa kijeshi na Marekani kwa masilahi ya rasilimali za Angola. Ninachotaka kuandika hapa na kuwafanya wasomaji waelewe ni kwamba, ugaidi unaotangazwa ni ule unaotokana na harakati za watu na makundi yao katika kuendesha mfumo wa madai halali ya haki na yapo madai ya mfumo wa kigaidi unaoendeshwa kwa misingi ya masilahi ya kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Katika mifumo yote, matumizi ya mbinu za kigaidi ni ya aina moja kwa vile falsafa ya ugaidi ni kuwatia hofu na kuwajengea woga wahanga wa vitendo vya kigaidi. Na hata wakati mmoja wa kupigania uhuru wa Afrika Kusini, mzee Mandela aliwahi kusema kwamba: “Pale njia ya amani inaposhindwa kuleta uhuru, haki na usawa basi njia iliyopo ni kuendesha harakati za kudai uhuru, haki na usawa kwa njia ya mapambano.”
Pamoja na hali zote nilizozieleza hapo kabla, napenda niweke wazi kwamba, ‘kuna dhana mbili za ugaidi.’ Ugaidi unaoendeshwa na magaidi wanaotumiwa na watu au makundi ya watu (hata serikali) katika kufikia malengo ya kimkakati katika kutawala siasa, uchumi au jamii; na kuna ugaidi unaoendeshwa na watu mmoja mmoja katika kufanikishwa malengo ya kibinafsi au malengo ya kutumiwa na mtu au kundi la watu wenye mitazamo ya kifalsafa na kiitikadi kwa mujibu wa malengo yao ya kimkakati. Ugaidi utabaki na utaendelea kuwa ni uhalifu, uwe unafanywa na mtu, watu au kikundi cha watu kwa malengo yoyote yawayo! Na hapa ni vema tukiweka wazi kwamba: “Kuna watu wanaotumia ugaidi kuficha malengo yao.” Hii ni njia ya uongo uliofichwa!
Inawezekana wanaoficha uongo kwenye ugaidi wana dhamira ovu kama ilivyokuwa mwaka 2003 wakati Marekani ilipotengeneza uongo na kuivamia Iraq na kumuua Saddam Hussein kwa madai ya uongo.
Au kama Marekani ilivyotengeneza uongo dhidi ya Kanali Muammar Gaddafi na kumuua! Na vivyo hivyo, Marekani na baadhi ya tawala na mamlaka za nchi kote duniani zenye nia ovu zinavyotumia alama ya ugaidi kuwapa watu makosa ya ugaidi wasiokuwa na hatia ya ugaidi; ili kwa uongo huo wa kutengeneza waweze kuwahukumu na au kuwaua! Huu ni ushenzi na kinyume cha ustaarabu!
Au ndiyo kusema, baadhi ya watu wanavyoitumia alama ya ugaidi kuwanasibisha watu wa dini isiyokuwa yao ili wapate kuwatenga na hata kuwapiga vita na kuwaua pasipo na hatia ya ithibati ya dhamira ya kutenda makosa (mens rea) na au hata kutenda makosa (actus reus).
Mwisho, tuache njia ya uongo juu ya kuwasingizia ndugu zetu makosa wasiyokuwa nayo; hususan makosa ya ugaidi, kwa sababu zisizokuwa na mashiko ya kisayansi na kiuchunguzi (admissible evidence). Sisi sote ni ndugu wa baba na mama mmoja, ni wajibu wetu kuishi kama ndugu hata kama tunatofautiana mitazamo na falsafa na au hata itikadi. Tukumbuke; tunapoishi pamoja lazima tukubali tofauti zetu!
CHANZO:TANZANIA DAIMA{May, 21, 2013}

 

Share this article :

0 comments:

Speak up your mind

Tell us what you're thinking... !

ZILIZOSOMWA SANA.

Followers

Blog Archive

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Proudly powered by Blogger
Copyright © 2011. Msamaa. - All Rights Reserved
Template Design by Creating Website Published by Mas Template