Vilio tupu mazishi Arusha. - Msamaa.
Headlines News :
Home » » Vilio tupu mazishi Arusha.

Vilio tupu mazishi Arusha.

Written By Unknown on Saturday, May 11, 2013 | 2:22 AM


*Maaskofu watoa kauli nzito, wataka dola iamke
SIMANZI, majonzi na vilio vilitawala katika mazishi ya watu watatu waliokufa kwa mlipuko wa bomu katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Olasiti Arusha. Mazishi hayo, yalifanyika huku ulinzi ukiwa umeimarishwa katika kila kona ya kanisa hilo. Maelfu ya wakazi wa Arusha na vitongoji vyake, jana walijitokeza kuhudhuria ibada ya kuipumzisha miili hiyo.
Marehemu hao watatu, Regina Loning’o Laizer (50) mkazi wa Olasiti, James Gabriel Kessy (16) na Patrisia Joachim Assey (10) walizikwa katika makaburi matatu pembeni kidogo ya Kanisa hilo.

Ibada hiyo, iliongozwa na Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Dar es Salaam, Muadhama Kardinari Polycap Pengo.

Katika ibada hiyo, maaskofu mbalimbali nchini walitoa salamu za rambarambi wakishirikiana na viongozi wa dini ya Kiislamu.

MAKAMU MWENYEKITI

Akitoa salamu za umoja huo, Askofu wa Kanisa la Anglikani Dayosisi ya Mount Meru, Askofu Stanley Hotay, alisema, “Mtu akupigaye hatoi taarifa, mwizi hatoi kibali, mhalifu haombi ruhusa na muuaji hahitaji kusindikizwa”.

Alisema kuusitisha uhai wa watu walio zawadi ya kipekee kutoka kwa Mungu, hakupaswi kuchekewa.

“Tunatambua watu waliofanya matendo haya ni waoga, kwani mtu jasri hahitaji kukuvizia ili akuue.

“Maandiko matakatifu yanatueleza: ‘Heri wafu wafao katika Bwana.’ Sisi tunaomba kama hii ndiyo saa ya kufa kwetu kwa sababu yeyote si kwa hawa watatu tu pengine wengi watafuata, maangamizi haya yamefanywa na watu ambao siku zao nao ni chache.

“Sisi tunaamini Serikali yetu na vyombo vyake hawatawaonea haya wala aibu wauaji hawa, kwani muuaji akituua sisi atawafuata na wengine.

“Nchi yetu iliyoaminika kisiwa cha amani, hususani Mkoa wa Arusha, lango kuu la utalii hakika jambo hili limeleta fedheha na aibu kwetu.

“Tunatambua kwamba Kanisa halina dini, ila waumini wake ndio wenye dini, hivyo basi viongozi wa Serikali na vyama vya siasa tunawaomba msitugawe kwa sababu ya utashi wa nafasi au chochote.”

ASKOFU MALASUSA

Kwa upande wake, Asofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Alex Malasusa, akitoa salama zake kanisani hapo, alisema: “Ibada hii ya kipekee isiyo ya kawaida, tukiwa tumefurika hapa ili kuagana na Wakristo wenzetu kimwili.

“Ni ibada yenye mchanganyiko wa majonzi, lakini kwa sababu sisi Wakristo tunayo matumaini, ibada hii itakuwa yenye furaha, tunafahamu wenzetu waliolala watarithi uzima wa milele.

“Tukio hili la kikatili, lililoleta aibu kubwa katika taifa letu, Taifa lililojulikana kisiwa cha amani, lakini sasa amani hiyo imetoweka.

“Wakristo tunalo tumaini moja kwa sababu Yesu Kristo tunayemwamini yu hai, basi na sisi pia tutakuwa hai.

“Katika ibada hii, nitumie fursa kuwaambia tusiwe waoga kwa sababu Kristo alikufa kwa ajili yetu na sisi tunahitaji kumtangaza bila hofu yotote.

“Risasi zinazopigwa kwa ajili ya watumishi wa Mungu, mioto inayowashwa kwa ajili ya makanisa na kuteketeza makanisa kwa mabomu yanayorushwa ili kuwadhuru waliokusanyika kwenye Ibada yasitukatishe tamaa.”

BARAZA LA MAASKOFU WAKATOLIKI

Kwa upande wake, Rais wa Baraza la Maaskofu wa Katoliki na Askofu wa Jimbo Kuu la Iringa, Tarcsius Ngalalekumta, alisema: “Ndugu zangu, bado tunaendelea kuomba kwa Mungu Kanisa na waumini kuwa na ustahimilivu, kwani kwa muda mrefu kumekuwa na vitisho vikifuatiwa na uchomaji wa makanisa, mashambulizi na mauaji ya viongozi wa Kanisa.

“Mashambulizi haya, bila shaka ni muendelezo wa uovu huu unaoratibiwa na watu wasiolitakia mema Kanisa.

“Hapo nyuma kwa kipindi cha miongo takribani mitatu, uhusiano wa dini mbalimbali nchini umekuwa si mzuri wa kuridhisha. Mtiririko wa matukio unaonyesha, tangu zilipoanza chochoko za mihadhara ya kidini hali ilianza kubadilika.

“Viongozi hawa walizunguka nchi nzima kueneza uchochezi na kutangaza vita dhidi ya Wakristo, wakidiriki kusema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni kichaka cha mfumo Kristo,” alisema na kuongeza:

“Sasa basi kinachosikitisha sana ni kwamba Serikali yetu haijawahi kukanusha madai, tuhuma hizo wala kuwakamata watu hao.

“Tunavitaka vyombo vya dola, vitekeleze wajibu wake kwa kuzingatia weledi pasipo shinikizo lolote, vyombo vya Dola viendee mbali zaidi kwa kuwakamata wale wanaofadhili ugaidi huo nchini.”

KARDINALI PENGO

Akizungumza wakati mahubiri katika ibada hiyo, Kardinali Pengo alisema, uovu uliotendwa na watu dhidi ya waumini umetendwa kwa madhumini yanayojulikana kwao tu waliotenda ouvu huo.

“Bila kosa, bila kuchokozwa na yeyote kati yetu wakapoteza maisha ya watu na kujeruhi vibaya miili ya watu. Je, sisi tufanye nini?

“Lakini madai ya Kristo Yesu yanabakia yale yale katika maandiko Matakatifu kuwa, tusijaribu kuushinda uovu kwa uovu bali tuushinde uovu kwa kutenda mema, kwani tunaamini Kristo Yesu hakuua mtu ili kujenga Imani yetu ya Kikristo.

“Kama kiongozi wenu wa kiimani nisingependa kuingia na kuanza kuwaambia majukumu ya Serikali au Dola, kazi yangu hapa kwenu waumini tusilipe ovu kwa ovu.

“Kinyume chake tuliombee Taifa letu, uovu si kitu kinachopendeza, hata wale tunaouawa kwa sababu ya imani yetu si jambo linalojenga taifa lolote.”
Share this article :

0 comments:

Speak up your mind

Tell us what you're thinking... !

ZILIZOSOMWA SANA.

Followers

Blog Archive

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Proudly powered by Blogger
Copyright © 2011. Msamaa. - All Rights Reserved
Template Design by Creating Website Published by Mas Template