KATIBA IJAYO NI SUMU ILE ILE, IMEHAMISHIWA CHUPA NYENGINE TU. - Msamaa.
Headlines News :
Home » » KATIBA IJAYO NI SUMU ILE ILE, IMEHAMISHIWA CHUPA NYENGINE TU.

KATIBA IJAYO NI SUMU ILE ILE, IMEHAMISHIWA CHUPA NYENGINE TU.

Written By Unknown on Monday, June 17, 2013 | 12:22 PMNdugu zangu wapendwa, jukumu letu la kuelimisha jamii litaendelea siku zote mpaka mwisho wa uhai wetu kwani akili ya mwanadamu ili iwe na uwezo wa kutafakari vizuri na kwa kina, ni lazima ishibishwe tafakuri safi daima. Chakula cha kuiwezesha akili kufikiri sawa sawa na kufanya maamuzi sahihi ni elimu sahihi peke yake. Elimu sahihi huambatana na ukweli na siku zote ukweli ni jambo muhimu sana katika maisha ya mwanadamu maana akiujua humuweka huru.

Ila kuna sharti moja muhimu katika kuutafuta ukweli. Mtu anapaswa  kuacha ushabiki na mihemko ya kimakundi au kiitikadi ikiwa kweli anahitaji kuujua ukweli na pia kuukubali. Vyenginevyo anaweza kuujua ukweli lakini akasita kuukubali na hapo ndipo alama za nyakati zitakapomuhukumu baadae iwapo tu sharti lililotajwa awali ataliangalia kwa  jicho la dharau. Nawasihi wale wote watakaobahatika kusoma maelezo haya, wayasome kwa macho ya kujifunza ukweli na kuukubali hata kama watakuwa na imani tofauti za kidini na mwandishi.

Kwa kuweka maneno haya kuwa mafupi lakini yenye kueleweka, leo  ningehitaji kugusa jambo muhimu katika maisha ya sasa na hata yale ya baadae. Jambo hilo limo katika mchakato wa kuelekea kukamilishwa kwa katiba mpya. Ni vyema kufahamika  kwamba tukitaja “jambo”  katika makala hii fupi, tunakusudia mchakato wa kupata katiba mpya unaondelea sasa nchini Tanzania ambapo baada ya hatua ya ukusanyaji wa  maoni, tayari tume imeshaandaa “RASIMU” na kuiwasilisha kwa jamii ili ijadiliwe zaidi.

Kiudhati tume imefanya kazi kubwa na inafaa ipongezwe kwa hali moja au nyengine lakini bado kazi kubwa ipo kwa wananchi ambao wataijadili RASIMU na kugundua madhaifu na kupendekeza namna ya kuiboresha. Kiupande wangu kama raia mwenye haki ya kutoa maoni juu ya mwenendo mzima wa machakato wa upatikanaji wa katiba mpya, bado naona RASIMU ni “SUMU’’ ile ile dhidi ya Waislamu ispokuwa kilichofanyika, “SUMU” hii imebadilishiwa chupa na kuwekwa kwenye chupa nyengine mpya ila nguvu ya kuwauwa WAISLAMU ni ile ile kama ile iliyotokea Mwembechai mwaka 1998 na Januari 26 na 27 kule Unguja na Pemba mwaka 2001.

Naomba nikiri kwamba, kubwa ambalo limenisukuma kufanya uchambuzi huu ni kuona kwa asilimia kubwa kama si zote, mawazo ya Waislamu yametupwa kwenye kapu la taka na kupenyezwa vipengele ambavyo vitakuwa “SUMU” kali zaidi dhidi yao kwa miaka kadhaa ijayo.

“SUMU” ya kwanza ni Ibara ya 31 ibara ndogo ya tano inayopatikana katika sura ya nne, sehemu ya kwanza  ya RASIMU ya katiba mpya. Ibara inasema “Ni marufuku kwa mtu, kikundi au taasisi ya dini kutumia uhuru wa kutangaza dini kwa kukashifu imani na dini nyingine, kujenga chuki au kuchochea vurugu na ghasia kwa madai ya kutetea imani au dini”.
Ibara hii kwa bahati mbaya au kwa makusudi haikuwekewa tafsiri ya kuelezea maana ya  kashfa kama vile neno “dini” lilivyotolewa maana katika ibara ya 31(6), hivyo jambo hili limenitia wasiwasi mno na shaka kubwa. Wasi wasi wangu umekuja kwa sababu wanaosikika sana wakisema wanakashifiwa ni Maaskofu, Mapadri na Wachungaji na hivyo kuifanya hoja hii kubebwa na watu wa upande mmoja tu wa imani {WAKRSITO} na kupelekea wengine kuitwa vikundi vya watu wachache, wahuni na majina mengine mengi mabaya huku magereza yakawa halali kwao.

Nakumbuka kijana Khamisi Dibagula wa Morogoro na wengine pia wameshawahi kufungwa kwa kisingizio cha kukashifu dini za watu wengine na sababu iliyotolewa ni kwamba Dibagula alisema “YESU SIO MUNGU”.  Kusema “YESU SIO MUNGU” ni miongoni mwa nguzo kubwa katika imani ya Uislamu kwasababu hakuna MUNGU ispokuwa ALLAH mmoja tu. Ila jambo la kusikitisha zaidi maana ya kashfa ilikuwa haielezwi na mpaka sasa haijaelezwa rasmi kiasi kwamba  Wakristo huwa huru na kuonekana hawajakashifu dini za wengine pale wanaposema “YESU NI MUNGU”. Ambapo tamko hilo katika Uislamu ni kashfa kubwa na ni tamko la kumtukana MUNGU na kwasababu ya ubaya wa tamko hilo, mbingu hukaribia kupasuka kutokana na  hasira za ALLAH.

Siku zile katiba ilikuwa haijaweka rasmi kipengele cha kuwatia hatiani watu wanaokashifu dini za wengine, jee katiba ijayo si itakuwa ni halali Waislamu kujazwa magerezani kwa kupitia mgongo wa kuvunja katiba ya nchi iwapo kipengele hiki kitaendelea kuwemo?  Jee huku si kuwapendelea Maaskofu na wafuasi wao na kuwadharau Waislamu kwa kutupa hoja zao za kutambulika kwa mahakama ya kadhi kikatiba na uwepo wa ruhusa kwa nchi kujiunga na OIC?......Itaendelea.


Share this article :

0 comments:

Speak up your mind

Tell us what you're thinking... !

ZILIZOSOMWA SANA.

Followers

Blog Archive

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Proudly powered by Blogger
Copyright © 2011. Msamaa. - All Rights Reserved
Template Design by Creating Website Published by Mas Template