SOURCE: MWANANCHI.
Na Goodluck Eliona na Editha Majura,
Mwananchi
Posted Jumapili,Juni1 2014 saa 24:0 AM
Posted Jumapili,Juni1 2014 saa 24:0 AM
Dar es Salaam. Serikali imepoteza zaidi ya
Sh362.9 bilioni kutokana na baadhi ya kashfa kubwa za ufisadi na operesheni
mbalimbali zilizoligharimu taifa tangu uhuru.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini taifa kukumbwa na
kashfa mbalimbali za upotevu wa fedha au kuanzisha mipango ambayo utekelezaji
wake ulisababisha maumivu kwa wananchi na hakuna awamu ya uongozi wa Serikali
iliyokwepa hali hiyo.
Kuanzia awamu ya kwanza ya Mwalimu Julius Nyerere
aliyeiongoza nchi toka mwaka 1961 ilipopata uhuru hadi 1986, Rais Ali Hassan
Mwinyi (1986-1995), Rais Benjamin Mkapa (1995-2005) na Rais Jakaya Kikwete
(2005-hadi sasa), kumeibuka kashfa mbalimbali, saba zikiwa kubwa na kulitikisa
taifa.
Kashfa na operesheni saba kubwa zilizotikisa
taifa ni pamoja na Operesheni Uhujumu Uchumi, ufisadi katika Mfuko wa Kuwezesha
Uagizaji Bidhaa kutoka Nje ya Nchi (Commodity Import Support – CIS) na Kashfa
ya Rada.
Nyingine ni ufisadi Akaunti ya EPA, kashfa ya
Richmond, Operesheni Tokomeza Ujangili na ile ya uchotaji mabilioni katika
akaunti ya Escrow.
Operesheni Uhujumu Uchumi
Mwaka 1984 Serikali ilianzisha Operesheni Uhujumu
Uchumi, iliyoongozwa na Waziri Mkuu wa wakati huo, Edward Sokoine ili
kutaifisha mali ambazo baadhi ya watu walidaiwa kujipatia kwa njia isiyo
halali.
Operesheni hiyo ilishuhudia baadhi ya watuhumiwa
wakimwaga fedha mitaani na majalalani, huku wengine wakitupa mali kuhofia
kutiwa kwenye mkono wa sheria.
Hata hivyo, katika operesheni hiyo baadhi ya
watendaji wa Serikali ambao hawakuwa waaminifu, waliitumia nafasi hiyo vibaya
kutaifisha mali za baadhi ya watu, ambao hawakuwa wahujumu uchumi.
Zoezi hilo lilisababisha wananchi kadhaa hasa
vijijini kuwekwa ndani na wengine kuachwa maskini baada ya kunyang’anywa mali
zao ikiwamo mifugo na mashine za kusaga nafaka, kwa kudaiwa kuwa walizipata kwa
njia isiyo halali.
Mfuko wa Commodity Import Support (CIS)
Miaka 24 baadaye yaani mwaka 2008, liliibuka
sakata jingine lililokuwa na harufu kubwa ya ufisadi wa mabilioni katika Mfuko
wa Kuwezesha Uagizaji Bidhaa kutoka Nje ya Nchi (Commodity Import Support –
CIS).
Sakata hilo liliwahusisha baadhi ya wanasiasa,
wafanyabiashara maarufu nchini na wizara kadhaa za Serikali ya Muungano na ile
ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).
Kupitia mfuko huo, vigogo hao walichota zaidi ya
Sh200 bilioni kwa kivuli cha uagizaji bidhaa kutoka nje ya nchi.
Mfuko huo wa CIS, ulianzishwa katika miaka ya
1980, ambapo baadhi ya nchi wafadhili ikiwamo Japan, zililenga kuipatia
Tanzania fedha za kigeni za kununulia malighafi, vyombo vya usafiri wa
barabara, vifaa vya kilimo, ujenzi na vingine mbalimbali. Mpango huo
ulioanzishwa na Serikali uliendelea hadi mwanzoni mwa miaka 2000, ambapo nchi
hizo wahisani ikiwamo Japan, Uingereza, Uholanzi, Saudi Arabia, Norway, Uswisi,
Ubelgiji, Sweden na Denmark zilikuwa zikiipatia Serikali fedha za kigeni ili
kuimarisha sekta za biashara.
Wizara zilizotajwa katika orodha ya wadeni wa CIS
ni pamoja na iliyokuwa ya Mawasiliano na Uchukuzi, Wizara ya Kazi, Wizara ya
Kilimo, Wizara ya Maji na Wizara ya Mambo ya Ndani kwa Tanzania Bara, wakati
Zanzibar zinatajwa Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi na Wizara ya Maji.
Rada
Mwaka 2011 Serikali ilikumbwa na jinamizi la
ufisadi kwa mara nyingine. Safari hii uliibuka ufisadi wa mabilioni ya shilingi
kupitia ununuzi wa rada kuukuu kutoka Kampuni ya BAE Systems ya Uingereza.
Ununuzi wa rada hiyo unatajwa kutofuata taratibu sahihi, uliligharimu taifa
Sh29.5 bilioni, wakati gharama halisi ilikuwa Sh21 bilioni.
Serikali ya Uingereza iliamua kurudisha fedha
hizo kama chenji, huku ikisisitiza kuwa watuhumiwa wote wa hapa nchini
waliohusika na ununuzi wa rada hiyo mtumba, washitakiwe Tanzania au Uingereza
kutokana na kubainika dosari kwenye ununuzi huo.
Wakati Uingereza ikitaka watuhumiwa hao
wafikishwe mahakamani, mtandao wa Wikileaks unaosifika kwa kufichua siri za
ndani ya mataifa mbalimbali duniani, ulibaini kuwepo kwa harakati nchini za
kutowafikisha mahakamani wahusika wa ufisadi huo.
EPA
Mwaka 2008 iliibuka kashfa nyingine ya wizi wa
mabilioni katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu
(BoT), ambapo vigogo kadhaa walitumia mbinu chafu kuchota zaidi ya Sh133
bilioni katika akaunti hiyo.
Katika wizi huo ulioitikisa nchi, wahusika
walitajwa kutumia vivuli vya siasa katika kupitisha nyaraka bila kufanyiwa
uhakiki wa nyaraka hizo.
Richmond
Mwaka 2006 baada ya Rais Jakaya Kikwete kuingia
madarakani kulitokea tatizo kubwa la uhaba wa umeme.
Hapo ndipo Serikali ilipoanza kufanya mikakati
mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutafuta njia za dharura za kutatua tatizo hilo.
Waziri Mkuu wa wakati huo Edward Lowassa alikuwa
mstari wa mbele katika mikakati hiyo ndipo Kampuni ya Richmond Development
(LLC) ilipewa zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura na kuliuzia Shirika la Ugavi
wa Umeme nchini Tanesco.
Hata hivyo, baadaye ilibainika kuwa kampuni hiyo
haikuwa na uwezo wa kuzalisha umeme kama ilivyodhaniwa, badala yake kulikuwa na
michezo michafu iliyofanyika kwa masilahi ya wafanyabiashara na baadhi ya
viongozi wa Serikali.
Mwaka 2007, sakata hilo lilifika bungeni na
aliyekuwa Spika wakati huo, Samuel Sitta aliunda kamati iliyokuwa chini ya
mbunge wa Kyela, Dk Harrison Mwakyembe ili kuchunguza suala hilo.
Kamati hiyo ilichunguza sakata hilo na kutoa
taarifa ilionyesha kuhusika kwa viongozi wa juu wa Serikali akiwemo aliyekuwa
Waziri Mkuu Edward Lowassa na kusababisha kiongozi huyo, kujiuzulu pamoja na
mawaziri wawili kung’oka madarakani.
Waliong’oka madarakani ni mawaziri wa Nishati na
Madini kwa vipindi tofauti, ambao ni Naziri Karamagi na Dk Ibrahim Msabaha.
Operesheni Tokomeza Ujangili
Operesheni Tokomeza Ujangili iliyoanzishwa na
Serikali kupambana na ujangili wa wanyama nchini mwaka jana iliwang’oa
madarakani mawaziri wanne ambao wizara zao zilielezwa kushindwa kusimamia
vizuri utekelezaji wa operesheni hiyo.
Kung’oka kwa mawaziri hao kulitangazwa bungeni na
Waziri Mkuu Mizengo Pinda, aliyeeleza kuwa Rais Jakaya Kikwete ametengua uteuzi
wao baada ya kuwasiliana naye kwa mashauriano akiwa nchini Marekani.
Mawaziri waliong’olewa kutokana na ripoti ya
kamati hiyo iliyoongezewa shinikizo na michango ya wabunge wengi ni Waziri wa
Maliasili na Utalii, Khamisi Kagasheki na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk
Emmanuel Nchimbi. Wengine ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi
Vuai Nahodha na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David
Mathayo.
Operesheni hiyo inadaiwa kukiuka haki za binadamu
ikiwamo watu 13 na askari sita kuuawa, utesaji wa kutisha wa watuhumiwa,
ubakaji, rushwa na uporaji wa mali za wananchi.
Akaunti ya Esrow
Wakati kashfa ya Richmond haijasahaulika, mapema
mwaka huu imeibuka kashfa ya upotevu wa mamilioni ya fedha kwenye Akaunti ya
Esrow katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Kashfa hiyo inayolitikisa Bunge na Serikali sasa,
imetajwa kuwa ni mwendelezo wa jinamizi la kashfa ikiwa ya saba kubwa kulikumba
taifa hadi sasa.
Akaunti hiyo iliyokuwa na zaidi ya Sh200 bilioni,
ilifunguliwa wakati kukiwa kuna mgogoro wa kisheria baini ya wabia wa zamani wa
IPTL (VIP Engeneering and Marketing na Mechmar Corporation ya Malaysia) kwa
upande mmoja, Tanesco na Independent Power Tanzania, IPT, kwa upande mwingine.
Wadau kwenye akaunti hiyo hawakupaswa kuchukua
kitu chochote hadi pale mgogoro utakapotatuliwa. Hata hivyo, kitita hicho cha
fedha kilichotwa.
Wazungumza
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT),
Emmanuel Mallya alisema matukio ya ufisadi yanaongezeka nchini kutokana na
Serikali kushindwa kuweka bayana hatua zinazopaswa kuchukuliwa watu
wanapatikana na makosa hayo, ili iwe fundisho kwa wengine.
Alisema kila mara wizi wa fedha za umma
unapotokea, Serikali hupata kigugumizi kuwawajibisha wahusika, hatua
inayowafanya watu wengi kuamini kushindwa kwao kunatokana na woga wa kutekeleza
azma zao.
“Hakuna uwajibikaji kama mtu kafanya jambo
fulani, kuna kulindana sana, lakini kama wote wangechukuliwa hatua za wazi
pengine ufisadi usingekuwa wa kiwango cha juu namna hii,” alisema.
Mhadhiri
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, (UDSM)
Faraji Christoms, alishauri wenye dhamana ya kusimamia masilahi ya taifa
wanatakiwa kujitathmini upya.
Alitaja maeneo yanayohitajika kufanyiwa tathmini
kuwa ni uzalendo kwa taifa, elimu kwa maana ya uelewa wa mambo ya kisheria,
lugha za kimataifa na umakini wakati wa majadiliano ya kimataifa na wanaposoma
mikataba ya aina hiyo.
“Unakuta mtu badala ya kutuliza akili akasoma kwa
makini mkataba kabla ya kuusaini, anaupeleka kwa msaidizi wake ukisindikizwa na
memo (agizo la maandishi) “Please read carefully for advice,” (tafadhali soma
kwa makini, shauri),” alieleza Christoms.
Alisema katika mazingira hayo, hatima ya usalama
wa mkataba huo unakuwa mikononi mwa mwingine, tofauti na aliyepewa dhamana.
Christoms alisema mazingira yanaonyesha kuwa
wanasheria serikalini wanashindwa na walioajiriwa kwenye kampuni za uwakili,
hivyo kusababisha Serikali kupata hasara kwa kuingia katika mikataba isiyo na
masilahi kwa taifa.
Profesa Gaudence Mpangala, wa Chuo Kikuu cha
Ruaha (RUCO) alisema historia ya ufisadi nchini inamnyima mtu yeyote makini,
ujasiri wa kuishauri Serikali mbinu za kudhibiti vitendo hivyo vya rushwa.
Profesa Mpangala alisema vitendo vya rushwa
haviepukiki katika jamii, lakini Serikali inapochukua hatua zinazothibitisha
kuwa inavipiga vita, hali inakuwa shwari tofauti na ilivyo nchini ambapo rushwa
ndogo na ufisadi vimeota mizizi huku hatua zinazochukuliwa zikiacha maswali
mengi bila majibu.
Alitoa mfano wa serikali ya awamu ya kwanza,
ilivyoshughulikia rushwa iliyokuwa inaelekea kwenye ufisadi kwa kuchukua hatua
kali, chini ya hayati Edward Sokoine na Mwalimu Nyerere ambapo waliothibitika
kuhusika pamoja na adhabu ya kifungo jela, walitakiwa kuchapwa viboko wakati wa
kuingia na kutoka gerezani.
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !