‘Aqiqah AFANYIWAYO MTOTO MCHANGA.
- ‘Aqiqah ni
jina lililopewa kichinjwa (Mnyama) achinjiwacho mtoto mchanga aliyezaliwa
ni mamoja awe ni wa kike au wakiume.
- ‘Aqiqah ni
Sunnah si waajibu. Ushahidi wa hili uko katika maneno ya Mtume Swalla
LLahu ‘Alayhi Wasallama aliposema: “Atakayepata mtoto na akapenda
amchinjie basi na afanye hivyo, kwa mwana
- mume mbuzi
wawili na kwa mwanamke mbuzi mmoja”. Hadithi
hii imepokewa na maimamu Abuu Dawuud na Annasaai kutoka kwa Abdallah bn
Umar. Kauli ya Mtume; “na akapenda amchinjie” ni dalili kuwa ‘Aqiqah
si lazima bali ni jambo
linalopendeza mwislamu kulifanya. Lakini kwa mwenye uwezo wa kufanya hivyo
basi iliyo bora zaidi kwake ni kufanya. Ama yule asiye na uwezo wa kufanya
hivyo basi si lazima kwake maana
Mwenyezi Mungu haikalifishi nafsi yoyote ila yale yaliyo sawa na uwezo
wake na pia hakufanya uzito katika dini Yake.
- Imethibiti
kutoka kwa Mtume wa Allah kuwa yeye kasema: “kila mtoto azaliwaye
anafungamana na ‘Aqiqah yake, anachinjiwa siku ya saba, ananyolewa kichwa
chake na anaitwa jina
- ”.
Wanachuoni wamelizungumzia neno “kufungamana” hapa kuwa linaweza
kuwa linamaanisha mambo mengi, miongoni mwa mambo hayo ni;
- Anakuwa
kama mwenye kujisikia uzito na unyonge na mwenye kukosa wepesi na furaha maishani
hadi achinjiwe
- Anazuiwa
kuwaombea wazazi wake uombezi mwema wa siku ya Qiyama
- Ni deni
lililo mithili ya Rehani ambayo hulazimiana na mtu hadi ailipe.
- Iliyo bora
zaidi na timilifu ni kuwa wale mbuzi wawili ambao anatakiwa mtoto wa kiume
achinjiwe wanatakiwa wawe ni wenye kufanana au kukaribiana kufanana kimaumbile
na kiumri. Lakini kama itashindikana kuwapata mbuzi wawili wenye sifa kama
hizo itafaa hata kama watatofautiana kiumbile na kiumri maadamu tu wana sifa
zinazofaa kisheria kwa ajili ya ibada hii. Sifa hizo tutazitaja baadaye.
- Iliyo bora
zaidi na timilifu ni kumchinjia mtoto wa kiume mbuzi wawili lakini ikiwa
mtu atashindwa kabisa kuchinja mbuzi wawili kama kutokana na yeye kupata
mbuzi mmoja tu au kumiliki kiwango cha mbuzi mmoja tu basi huyo huyo mbuzi
mmoja atatosha.
- Sunnah ni
kumchinjia mtoto atakapofikisha siku ya saba kama ilivyokuja katika
hadithi ya Samrah, lakini ikiwa mtu hakuweza kuchinja siku ya saba basi na afanye hivyo siku ya kumi na nne na ikiwa atashindwa
siku ya kumi na nne basi na afanye hivyo siku ya ishirini na moja na ikiwa atashindwa siku ya ishirini na moja
basi na afanye hivyo siku yeyote.
- Ibada hii
ya kuchinja hufanyika hata kama mtoto kafariki maadamu tu alizaliwa hai au
hata kama mimba ilitoka lakini mtoto tayari alikuwa ameviviwa roho yaani
alikuwa amefikisha miezi minne au siku mia na ishirini na kuendelea
lakini kama alikuwa hajafikisha miezi minne au siku mia na ishirini hapo
hatafanyiwa ‘Aqiqah.
- Kuna imani
imeenea kwa watu wengi kuwa kichinjwa cha ‘Aqiqah hakivunjwi mifupa hii ikiwa
kama ishara ya kumtakia mtoto salama na asivunjike maishani mwake. Hili si
sahihi wala halina mashiko katika Qur’an wala Sunnah. Kwa hiyo ieleweke wazi
kuwa mifupa ya ‘Aqiqah inafaa kuvunjwa wala hii haitakuwa sababu ya
kuvunjika kwa mtoto hata kama itatokea kama watu wanavyoamini. Vile vile
kuna jambo jingine nalo ni kuwa nyama ya ‘Aqiqah huchanganywa au hupikwa
kwa maji yaliyotiwa vitu vitamu vitamu kama sukari au huchanganywa na
asali wakati wa kuliwa, hii ikiwa ni kama ishara ya kumtakia mtoto tabia
njema; hili nalo pia halina mashiko. Hivyo iwekwe chumvi na kupikwa kama
nyama ya kawaida.
- Kinachotakiwa
kuchinjwa katika ‘Aqiqah ni wanyama ambao kisheria wanaitwa Bahiimatul
An’aam ambao ni; mbuzi, kondoo, ng’ombe na ngamia. Kwa mantiki hii
haifai kumchinja farasi kwa ajili hii, wala swala hata kama anafugwa na
amekuwa kama mbuzi kitabia na pia haifai kuchinja kuku wala bata kwa ajili
ya ibada hii.
- Ama
kuhusiana na umri unaofaa wa kichinjwa hichi ni miaka mitano kwa ngamia
na miaka miwili kwa ng’ombe, dume la mbuzi na dume la kondoo ni mwaka mmoja na mbuzi
jike na kondoo jike ni miezi sita.
- Ni sharti
katika kichinjwa cha ‘Aqiqah kiwe kimesalimika na aibu mbalimbali. Kwa
kifupi kabisa kichinjwa hichi kinafanana na kichinjwa cha Iddil adh’haa au
iddi kubwa yaani kisiwe chongo cha wazi, kiguru cha wazi, kilichokonda
sana, wala kisiwe ambacho kimetobolewa masikio yake, wala kilichokatwa
mkia au kukatika pembe.
- Ikiwa mtu
anamiliki takribani wanyama wote wanaofaa kuchinja kwa ajili ya ‘Aqiqah kiasi
kuwa anaweza akitaka akachinja ng’ombe au ngamia au kondoo au mbuzi, iliyo
bora zaidi kwake ni kuchinja mbuzi maana ndiyo aliyetajwa katika hadithi.
- Inafaa mtu
kuipika nyama ya ‘Aqiqah au kuigawa pasina kuipika lakini iliyo bora zaidi
ni kuipika nyama hiyo kuliko kuigawa kwa kuwa kwa kufanya hivyo
utawarahisishia masikini na majirani gharama za kupika.
- Hakuna
ubaya wowote katika kula nyama ya ‘Aqiqah kwa aliyechinja, kwani kwa
hakika hii ni nyama kwa ajili ya kumshukuru Allah na kile ambacho ni kwa
ajili ya kumshukuru Allah kinafaa kuliwa kisheria wala hapana ubaya bali
hii ni kama nyama ya iddil adh’haa.
- Pia inafaa
kuiweka nyama ya ‘Aqiqah katika jokofu pasina kuigawa lakini iliyo bora
zaidi na timilifu katika ibada hii ni kuigawa kwa mafaqiri, masikini,
majirani na marafiki hata kama ni kidogo.
- Haifai
kununua mbuzi aliyechinjwa na kumfanya kuwa ni ‘Aqiqah bali ni lazima
kumununua mbuzi aliye hai na kisha kumchinja kwa nia ya ‘Aqiqah.
- Ikiwa baba
hayuko kama kwa mfano kafariki mama atasimamia jukumu la kufanyia mtoto ‘Aqiqah.
- ‘Aqiqah ni
Sunnah kwa baba kumfanyia mtoto wake lakini kama mtoto hakufanyiwa ‘Aqiqah
na akapenda ajifanyie mwenyewe inafaa hata kama ni kitambo kirefu kimepita
na umri ukawa mkubwa.
- Inafaa
kumchinjia mtoto wa kiume mbuzi hao wawili kwa utaratibu wa kugawa kwa
maana ya kuwa anamchinja mbuzi mmoja mwezi huu na mwingine akamchinja
mwezi mwingine wala haishurutishwi wachinjwe mara moja, bali inafaa kwa
mtoto akajichinjia mbuzi mwingine ikiwa baba alimchinjia mbuzi mmoja kwa
sababu ya hali yake kifedha wakati huo. Bali inafaa kumchinjia mbuzi mmoja
sehemu moja na mwingine sehemu nyingine, wala si sharti wachinjwe wote
sehemu moja wala si sharti wachinjwe sehemu alipo mtoto anayefanyiwa.
- Haifai
kisheria kupigia thamani ya mbuzi wa ‘Aqiqah na kuwapa kiwango hicho cha
fedha masikini bali ni lazima achinjwe mbuzi
- Haifai
kushirikiana watoto katika ‘Aqiqah kwa mantiki ya kuwa wachangie kwa mfano
mbuzi wawili watoto wawili wa kiume. Watoto wawili wa kiume wanapaswa
wachinjiwe mbuzi wanne hata kama ni mapacha. Kama ni mapacha wawili wa
kike watachinjiwa mbuzi wawili, kama mmoja ni wa kike na mwingine ni wa
kiume watachinjiwa mbuzi watatu. Bali ngamia na ukubwa wake hafai
kuwachinjia watoto wawili na ikifanyika hivyo inazingatiwa ni kwa ajili ya
mtoto mmoja. Bali haitofaa kwa watoto wawili ambao hawakufanyiwa ‘Aqiqah
kwa wao kujiamulia kuchinja ngamia mmoja ili awe ni ‘Aqiqah kwa wote
wawili. Bali ngamia huyo atazingatiwa kuwa ni kwa ajili ya mtoto mmoja tu.
- Si lazima
wakati wa kumchinja mnyama wa ‘Aqiqah kusema kuwa hii ni ‘Aqiqah bali
inatosha mtu kunuia moyoni mwake na kilicho lazima kutamka ni Bismillah
Rahmaan Raheem wakati wa kuchinja.
- Si lazima kuwaambia
waliohudhuria kuwa watakula nyama ya ‘Aqiqah, lakini ni vizuri kuwaambia
ili wamuombee mtoto dua njema, uongofu, Uchaji Mungu, kutengenekewa na
kheri za dunia na akhera.
‘Aqiqah ni mnyama ambaye huchinjwa kwa ajili ya mtoto
mdogo kama tulivyotangulia kusema. Jambo hili ni katika mlango wa kumshukuru
Allah. Kuna pia vyakula vingine ambavyo ni katika mlango huu wa kumshukuru
Allah na vinafaa kuliwa kisheria navyo ni;
1.
Walima ambacho chakula
au karamu ya harusi
2.
Qiraa ambacho chakula cha mgeni, kile cha
mgeni njoo wenyeji tupone!
3.
Maadaba ambacho
ni chakula cha mwaliko
4.
Tuhfa ambacho
ni chakula cha mwenye kutembelea pahala.
5.
Khiraasu
ambacho ni chakula cha mwanamke aliyejifungua.
6.
Ghadiira
ambacho ni chakula cha wakati wa khitaani au kutahiri wanawake au wanaume.
7.
Naqiigha
ambacho ni chakula cha anayekuja kutoka safari.
8.
Wakiira
ambacho ni chakula baada ya kumaliza kujenga.
Vyakula vyote vilivyotajwa hapo juu ni halali isipokuwa
chakula cha msibani au chakula cha siku ya tatu
au chakula cha khitimah au chakula
cha arobaini, vyakula hivi haviifai
kuvila kisheria kama hakuna dharura ya kufanya hivyo. Jariri Ibn ‘Abdillah
anasema kuwa kukusanyika kwa wafiwa na kupikiwa chakula ni miongoni mwa mambo
aliyokataza Mtume wetu Mtukufu na ni sawa na kuongeza msiba.
Wabillah Tawfiiq.
Chanzo:MUM Lecturer.
Je naweza kumfanyia hakika mtoto ambaye amefkisha miaka minne?
ReplyDeleteInawezekana kabisa kumfanyia aqiqa mtoto aliyefikisha miaka minne kwasababu Aqiqa ni moja katika sunna kubwa lakini kufanywa kwake kunategemea na uwezo wa kiuchumi au kumiliki mnyama mwenyewe.
ReplyDeleteA'alleykum, nyama ya aqiqah ni lazima ichemshwe tu, je vingo Kama tangawizi inafaa kuwekwa?..
ReplyDeletenaam. nyama hii kama ilivyonukuliwa hapo juu yakuwa hufuata taratibu zakawaida kabisa kimaandalizi mfano wa yale ya wakati wa eid kubwa.
DeleteJe nikwamba unauwezo wa ukipika pamoja na Michele yaani pilau Au ukipika rosti ya mchuzi
DeleteAsalam aleikum warahmatullah wabarakatuh :jee inafaa kufanya aqiqah ukaleta wanafunzi wa madrasa kusoma dua?
ReplyDeleteUwezo wangu ni mbuzi mmoja na mtoto wangu niwakiume je itaswii nikimchinjia mbuzi mmoja Kwny kisomo cha aqiqah?
ReplyDeleteNa keep!? Naweza kumfanyia aqiqah mtoto siku ya Arobaini?
Kama mbuzi ni wa kiume unaweza kuchinja huyo mmoja baadae ukaja kumalizia mmoja tena.asante
DeleteAsalam alaikum sheikh; je Ni kisomo kipi kinacho stahiki siki ya Aqiqah maana bidaa zimekuwa nyingi naomba unielezee utaratibu wake wote kwa ujumla (A-z)
ReplyDeleteMtt wangu wa kiume na uwezo wangu mbuz mmoja je itaswih kumfanyia hakika?
ReplyDeleteJe kuna dua maalum ya siku ya akika kama ipo ni sura gani
ReplyDeleteHakuna Dua ndugu zangu, ibada Ni kuchinja tu. Kisha kugawa au Kula.
DeleteHakuna Dua yoyote
Je naweza kujifanyia Aqiqah mwenyewe endapo sikufanyiwa nikiwa mtoto?
ReplyDeleteJe kumfanyia mtoto aqiqah ni miaka mingapi?
ReplyDeleteAsallaam aleykum vp kuhusu mtoto ambaye ajazaliwa kwenye ndoa naomba kufahamu maana naumiza kichwa hapa
ReplyDeleteMwisho kumfanyia haqiqa mtoto ni umri gani?
DeleteJe, inajuzu kumfanyia Aqiqah mtoto wa nje ya Ndoa?
ReplyDeleteJe mtoto wa kiume anatakiwa kuchinjiwa mbuzi wa kiume na wakike kuchinjiwa mbuzi wa kike wakati wa aqiyqah???
ReplyDelete