- Msamaa.
Headlines News :
Home » »

Written By Unknown on Thursday, August 22, 2013 | 12:13 PM

Matukio ya Kijamii yaliyotikisa 2012

Shehe Semtawa

Ugonjwa wa Dk. Mwakyembe
Januari 3, 2012

HALI ya afya ya Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe, ilikuwa inasikitisha kwani licha ya kupata matibabu nchini India na kuendelea na tiba hiyo hapa nchini, hali yake haikuwa ya kuridhisha kutokana na kunyonyoka nywele, kope, ndevu na vinyweleo vyote.

Majambazi yateka ndege
Januari 5, 2012

WATU wanne wanaosadikiwa kuwa majambazi wakiwa na silaha nzito za kivita, walivamia Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) na kuiteka ndege ndogo iliyokuwa imebeba dhahabu kwa ajili ya kuisafirisha kwenda nje ya nchi.

Madaktari 229 wafukuzwa Muhimbili
Januari 6, 2012

UONGOZI wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) uliwafukuza kazi madaktari 229 waliokuwa katika mafunzo kwa njia ya vitendo kutokana na mgomo wa siku nne wakishinikiza kulipwa posho zao za mwezi mmoja.

Umeme bei juu
Januari 14, 2012

WAKATI gharama za maisha kwa Watanzania wengi zikizidi kupanda kila siku, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), iliidhinisha ongezeko la bei ya umeme kwa asilimia 40.29 kwa Tanzania Bara na asilimia 28.21 kwa Zanzibar kuanzia Januari 15, 2012.
 
Askari aua nduguze na kujiua
Januari 22, 2012

ASKARI polisi wa kituo cha Magomeni jijini Dar es Salaam, Nicodemas Senge (43), amewaua ndugu zake wawili na kisha kujiua kwa kujipiga risasi wakati wakiwa kwenye kikao cha usuluhishi wa mgogoro wa ardhi ya kijijini kwao Singida.

Madaktari waanza mgomo nchi nzima
Januari 23, 2012

JUMUIYA ya Madaktari Nchini, ilianza mgomo nchi nzima hadi pale ambapo serikali ingeliridhia kulipa madai yao ndipo madaktari wangelirudi kuendelea na kazi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Madaktari, Dk. Ulimboka Stephen, alisema mgomo huo ungelikuwa wa nchi nzima kwa madaktari kutotoa huduma.

Wanafunzi wanane wafa maji Arusha
Februari 28, 2012

WANAFUNZI wanane kati ya kumi wa Shule ya Msingi Piyaya, wilayani Ngorongoro, mkoani Arusha, walifariki baada ya kusombwa na maji ya mafuriko ya Mto Radiru wakati wakitoka shuleni, jioni majira ya saa 11:30.

Azikwa akiwa hai
Aprili 29, 2012

WAKAZI wa Kitongoji cha Itezi Magharibi, Kata ya Itezi, jijini Mbeya, walimzika mwenzao akiwa hai kwa kumtuhumu kuwa ni mchawi kwa kumuhusisha na kifo cha mtoto wa mdogo wake.

Marian Girls kinara matokeo kidato cha sita
Mei 2, 2012

BARAZA la Mitihani la Tanzania, lilitangaza matokeo ya kidato cha sita na kuonesha Shule ya Marian Girls kuongoza kwa ufaulu kwa kutoa wasichana watano waliofanya vizuri katika masomo ya sayansi kwa kombinesheni ya PCM.

Watu saba wafa ajali ya basi la NBS
Mei 3, 2012

WATU saba walikufa papo hapo na wengine 54 walijeruhiwa baada ya basi la kampuni ya NBS lenye namba za usajili T 978 ATM lililokuwa likitokea Tabora kuelekea Arusha kupinduka katika eneo la Jineri, nje kidogo ya mji wa Igunga.

Dk. Ulimboka atekwa na kupigwa
Juni 28, 2012

MWENYEKITI wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk. Steven Ulimboka, alitekwa na watu wasiojulikana, kupigwa na kujeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili, kisha kutupwa katika msitu wa pande, nje kidogo ya jiji Dar es Salaam.

Serikali yawashtaki madaktari
Julai 7, 2012

SERIKALI iliwashtaki katika Baraza la Madaktari Tanzania, madaktari wanafunzi wa vitendo walioshiriki kwenye mgomo wa madaktari uliofanyika nchini kwa tuhuma za kuhatarisha maisha ya wagonjwa na kukiuka maadili ya taaluma yao.

Meli ya Mv Skagit yazama
Julai 18, 2012

Kisiwa cha Zanzibar kilikumbwa na msiba mzito kutokana na kuzama kwa meli ya MV Skagit, mali ya Kampuni ya Seagull, iliyokuwa ikisafiri kutoka Dar es Salaam ikiwa na abiria wanaokadiriwa kuwa 290 pamoja na mizigo kuelekea Unguja, visiwani Zanzibar majira ya saa saba mchana. Watu 63 walifariki, 146 wakiokolewa hai na 81 hawakupatikana.

Sheria ya mifuko ya jamii moto
Julai 27, 2012

VUGUVUGU la kupinga mabadiliko ya sheria za mifuko ya hifadhi ya jamii ya mwaka 2012 lilichukua sura mpya baada ya wabunge kutaka kuifanyia marekebisho mengine kwa sababu mwanachama hataruhusiwa kuchukua mafao yake kwa sababu yoyote mpaka hapo atakapofikisha miaka 55 au 60.

Ugonjwa wa ebola waingia nchini
Agosti 5, 2012

UGONJWA hatari wa ebola ambao umeua idadi kubwa ya watu nchini Uganda uliripotiwa kuingia nchini katika wilaya ya Kyerwa, kijiji cha Bulongo, mkoani Kagera, ambapo mtoto wa miaka sita alionekana na dalili hizo.

Walimu watishia kuing’oa CCM
Agosti 6, 2012

WALIMU walipokubali kurejea kazini na kuendelea kutafakari amri ya mahakama, mkakati mzito ulipangwa kuhakikisha hawakiungi mkono Chama cha Mapinduzi (CCM) kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.

Polisi waua kikatili
Septemba 3, 2012

Jeshi la Polisi lilimuua mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha Channel Ten, Daudi Mwangosi, aliyekuwa anaripoti habari za ufunguzi wa matawi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), mkoani hapa.
Mwangosi alidaiwa kuuawa kwa bomu lililorushwa na polisi waliotaka kuizuia CHADEMA kufungua tawi katika kijiji cha Nyololo.

Waislamu waandamana Dar
Septemba 21, 2012

MAELFU ya waumini wa dini ya Kiislamu waliandamana na kukusanyika kwenye viwanja vya Kidongo Chekundu jijini Dar es Salaam ambako walitoa tamko dhidi ya wanaoshambulia na kunyanyasa Uislamu, hasa kwa Marekani kutengeneza filamu ikimkashifu Mtume Muhammad (SAW).

Ajali yaua 10 Mbeya, mbunge anusurika
Oktoba 3, 2012

MBUNGE wa Viti Maalum Mbeya kupitia tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. Mary Mwanjelwa, alinusurika kufa katika ajali iliyogharimu maisha ya watu takriban 10.
Ajali hiyo ilitokea eneo la Mbalizi, wilaya ya Mbeya Vijijini. Gari la mbunge huyo liligongwa na kuteketea kwa moto papo hapo.

Kizaazaa cha mafuta Dar
Oktoba 3

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) baada ya kushusha bei za mafuta ya petroli na dizeli nchini, baadhi ya wafanyabiashara walizua kizaazaa kwa kuweka mgomo baridi wa kuuza mafuta hayo.

Waislamu wachoma, wavunja makanisa
Oktoba 12, 2012

KUNDI kubwa la Waislamu wenye imani kali, lilizusha vurugu kubwa zilizoambatana na kuchomwa moto na kuharibiwa makanisa manne huko Mbagala jijini Dar es Salaam, katika kile kilichoelezwa kuchukizwa na kitendo cha kijana mmoja wa Kikristo aliyedaiwa kukimwagia haja ndogo kitabu kitakatifu cha Kurani.

Ponda akamatwa kwa uchochezi
Oktoba 17, 2012

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, lilimtia mbaroni Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Issa Ponda Issa, akikabiliwa na tuhuma mbalimbali za uchochezi.

Jeshi la Polisi lamjeruhi mwandishi kwa risasi
Desemba 5 2012

JESHI la Polisi Mkoa wa Kinondoni jijini Dar es Salaam, liliingia kwenye kashfa baada ya askari wake kumjeruhi kwa risasi mwandishi wa habari wa gazeti la Tanzania Daima, Shabani Matutu, akiwa nyumbani kwake.

Padri apigwa risasi Zanzibar
Desemba 26, 2012

PADRI wa Kanisa Katoliki lililoko Mpendae visiwani Zanzibar, Ambrose Mkenda, alijeruhiwa kwa risasi na watu wasiojulikana nje ya nyumba yake majira ya saa 12 jioni juzi wakati akitoka kanisani.

CHANZO:TANZANIA DAIMA.
Share this article :

0 comments:

Speak up your mind

Tell us what you're thinking... !

ZILIZOSOMWA SANA.

Followers

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Proudly powered by Blogger
Copyright © 2011. Msamaa. - All Rights Reserved
Template Design by Creating Website Published by Mas Template