Kupaa na kutunguliwa kwa Aboud Jumbe Mwinyi - Msamaa.
Headlines News :
Home » » Kupaa na kutunguliwa kwa Aboud Jumbe Mwinyi

Kupaa na kutunguliwa kwa Aboud Jumbe Mwinyi

Written By Unknown on Friday, May 10, 2013 | 1:31 PMNasaha za Mihangwa

Joseph Mihangwa
Toleo la 292&293
1&8 May 2013
Raia Mwema.
MIAKA 29 iliyopita, Januari 1984, Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama cha Mapinduzi (CCM), iliyoketi mjini Dodoma kwa dharura, ilimvua (ilimpindua?) nafasi zote za uongozi, Rais wa Awamu ya Pili wa Zanzibar, Alhaj Sheikh Aboud Jumbe Mwinyi kwa kutenda ‘dhambi kuu’ ya kuhoji muundo wa sasa wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Nyadhifa alizovuliwa kiongozi huyo na kubakia kuwa raia wa kawaida na kuwekwa chini ya kizuizi cha nyumbani kwake kwa kipindi kadhaa, ni pamoja na urais wa Zanzibar, uenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, umakamu wa Rais wa Tanzania na umakamu Mwenyekiti wa CCM Taifa.
Mkutano huo ulitawaliwa na kampeni chafu dhidi ya Jumbe, huku kambi mbili za Zanzibar zikiumana, kwa kambi moja kuunda tuhuma dhidi yake na nyingine kujibu mapigo, na hivyo kuchonga ufa na uhasama mkubwa miongoni mwa viongozi wa Zanzibar kati ya kambi mbili hizo kinzani; kambi iliyojiita ya ‘Wakombozi’ (Liberators), iliyoundwa na waliojiona kama watetezi halisi wa Mapinduzi ya 1964 na ile ya kambi ya ‘Wanamstari wa mbele’ (Front liners), iliyotaka mabadiliko ya sera visiwani.

Katika msuguano huo, Kamati ya Wakombozi ilishindwa na Rais Jumbe akatunguliwa kwa mzinga mzito, akaisha. Jumbe alikuwa mrithi wa Rais wa kwanza wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, aliyeuawa katika jaribio la mapinduzi ya kijeshi lililoshindwa, Aprili 7, 1972. Kabla ya hapo, Jumbe alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, akishughulikia mambo ya Muungano.

Kuuawa kwa Karume kulifikisha tamati ya utawala wa awamu ya kwanza kufuatia Mapinduzi ya 1964, utawala uliotawaliwa na vitisho, hofu, umwagaji damu na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu dhidi ya yeyote aliyetoa sauti kuhoji utawala huo, na au kwa aliyedhaniwa tu kuwa mpinzani wa Mapinduzi.

Uporaji huo wa demokrasia, ulitekelezwa na utawala wa Karume kupitia genge katili lilojulikana kwa jina la ‘The Gang of Fourteen (Genge la Watu 14), likiongozwa na Kanali Seif Bakari. Kugongewa mlango tu usiku na genge hilo enzi hizo, kulitosha mtu kupatwa hofu kabla ya kuhojiwa.
Genge hili na sehemu kubwa ya wajumbe wa Baraza la Mapinduzi, walitaka kuendelezwa kwa sera za Karume, na mtu pekee waliyeona angeweza kufanikisha hilo kama mrithi halali wa Karume, ni huyo Kanali Seif Bakari.

Hata hivyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa wakati huo, Mwalimu Julius Nyerere aliposikia hilo, akaona giza mbele. “Sera za Karume tena? Ukatili na mauaji ya kutisha kwa watu wasio na hatia? Hapana!” alisikika Mwalimu aking’aka mbele ya watu wake wa karibu, na kuamua kutokubaliana na pendekezo la Wazanzibari lililomtaka Kanali Bakari kumrithi Karume. Akajenga hoja nzito kupangua kisayansi hoja hiyo kwa kuhusisha na tukio la kuuawa kwa Karume!

Jaribio la mapinduzi lililoshindwa liliandaliwa na wanasiasa makini wa Kizanzibari kwa kuhusisha baadhi ya wanajeshi wa Jeshi la Zanzibar, ambalo hadi akiuawa, Karume alikuwa bado Amiri Jeshi Mkuu wake; kwa kushirikisha pia wanajeshi kadhaa wa Kizanzibari waliokuwa kwenye Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWT) kwa upande wa Bara.

Muuaji wa Karume, Luteni Hamoud Mohammed Hamoud, alikuwa wa Jeshi la Zanzibar. Alichukua hatua hiyo yeye mwenyewe baada ya kuhisi kwamba mpango wa mapinduzi umegunduliwa siku hiyo, na kwamba yeye na wenzake walikuwa wanatafutwa; na kwa sababu kikosi cha pili cha mapinduzi kutoka Dar es Salaam kilishindwa kufika Zanzibar muda uliopangwa, baada ya kuonywa kikiwa baharini juu ya kugunduliwa kwa mpango huo na kurejea hima Dar es Salaam.
Luteni Hamoud aliona kwa mikasa hiyo miwili, kwa vyovyote vile, angekamatwa na kuuawa kikatili. Akaamua na lolote liwe, na bila kupoteza muda akaamua kutekeleza mauaji hayo yeye mwenyewe na wenzake wengine watatu tu.

Imeelezwa kwamba ushiriki wa Luteni Hamoud katika jaribio hilo, mbali na kubeba hisia (sentiments) za kisiasa, pia alidhamiria siku nyingi tangu nyuma, kulipiza kisasi kwa Karume kwa kifo cha baba yake, Mzee Mohammed Hamoud, aliyeuawa kikatili na kiongozi huyo akiwa kizuizini kwa sababu za kisiasa.
Mwalimu Nyerere hakutaka mauaji ya Rais Karume yatafsiriwe au yahusishwe na jaribio la mapinduzi, bali alitaka yatafsiriwe kama mauaji ya kisiasa tu. Akasema, hatua yoyote ya kumteua Kanali Seif Bakari ambaye ni mwanajeshi, kuchukua nafasi ya Karume aliyeuawa na mwanajeshi pia, kungetafsiriwa kama Mapinduzi ya Kijeshi. Hapo, Wazanzibari wakanywea, wakatazamana kwa ishara bila kupata jibu kwa hoja ya Mwalimu Nyerere. Hawakuwa na namna isipokuwa kufuta pendekezo la uteuzi wa Kanali Seif Bakari kumrithi Karume.

Ndipo ikawadia zamu ya Mwalimu Nyerere kushawishi na kushauri nani ateuliwe. Akasema, pamoja na kuuawa kwa Karume, ambaye alikuwa mwasisi mwenza wa Muungano wa Tanzania, Muungano huo lazima uendelezwe bila kuyumba; na mtu pekee aliyefaa, kwa maoni ya Nyerere, alikuwa ni Aboud Jumbe Mwinyi, kwa sababu kuu tatu:-

Mosi, ni msomi na mwanasiasa mkongwe mwenye kuzielewa vyema siasa na migongano ya jamii ya Kizanzibari. Pili, ni mtu ambaye hakuwa na majungu wala makundi yenye kuhasimiana. Tatu, wadhifa wake wa Waziri wa nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais (Mambo ya Muungano) kwa muda mrefu, ilikuwa ni sifa ya ziada iliyompa uzoefu, na uwezo wa kuendeleza na kudumisha Muungano. Hoja ya Mwalimu ikapita; Jumbe akapaa, akawa Rais wa Zanzibar wa awamu ya pili.
Jumbe na Mwalimu Nyerere walifanana kwa mengi. Wote walikuwa wasomi waliosoma pamoja Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda, na kisha wote wakawa walimu wa sekondari. Kwa uhusiano mzuri huo, Jumbe alianza kulegeza mengi yenye ukakasi visiwani ambayo yasingewezekana enzi za Karume ambaye aligeuka mwiba kwa Mwalimu, akidai mara nyingi wavunje Muungano kwa kuwa uligeuka koti lililowabana Wazanzibari. Chini ya Jumbe, misuguano kati ya Bara na Visiwani ambayo kabla yake ilizua kero za Muungano, ilianza kutoweka.

Jumbe alianza kukubalika haraka kwa wengi Visiwani na Bara; akawa kipenzi cha Rais wa Muungano, naye akaanza kupaona Bara kama nyumbani kwake. Akajenga makazi yake eneo la Mjimwema, Dar es Salaam. Akilala Mjimwema na kila asubuhi aliruka kwa ndege kwenda Ikulu ya Unguja na kurejea tena jioni baada ya kazi. Ufanisi wake wa kuihudumia Zanzibar ulipungua kwa sababu ya kuweka nguvu kubwa zaidi kwenye Muungano. Na kadri alivyozidisha ziara za kirais Bara na nje ya nchi kumwakilisha Mwalimu, (majukumu ambayo Mwalimu hakuthubutu katu kumpa Karume), ndivyo alivyozidi kujiweka mbali na siasa za Zanzibar na Wazanzibari.
Kwa kutumia hali hiyo ya maridhiano, Mwalimu alizidi kuchanja mbuga kwenda mbele zaidi bila Jumbe kushuku kitu. Katika kikao cha pamoja cha NEC ya TANU cha Bara na NEC ya ASP cha Zanzibar, kilichofanyika Dar es Salaam, Septemba 5, 1975, Mwalimu Nyerere alipendekeza vyama hivyo viungane ili kuimarisha zaidi Muungano.

Jumbe alikubali kimsingi wazo hilo, lakini akataka ASP kipewe muda kufikiria zaidi. Mwaka mmoja baadaye, Oktoba 1976, maridhiano yakafikiwa ya kuunda Chama kipya ‘Chama cha Mapinduzi’ (CCM), kilichozinduliwa Februari 5, 1977, tarehe na mwezi sawa na ilipozaliwa ASP miaka 20 nyuma, mwaka 1957.
Licha ya Wazanzibari kushinikiza tarehe na mwezi wa kuzaliwa chama chao, yaani Februari 5, walishinikiza pia na kufanikiwa kubakiza neno ‘Mapinduzi’ yaliyoleta uhuru wao Januari 12, 1964, liwe sehemu ya jina la chama kipya. Kwa maana ya Chama cha Mapinduzi bila kuwa na tafsiri yake kwa lugha ya Kiingereza.

Na hizo ndizo zilikuwa karata mbili pekee kwa Wazanzibari kukubali kuunda Chama kipya, chama ambacho kilipewa ukuu wa kikatiba wa kushika hatamu zote za uongozi wa nchi na kuweza kumng’oa madarakani Jumbe miaka saba baadaye, mwaka 1984, kama kitanzi alichojitengenezea mwenyewe. Hata hivyo, kwa mujibu wa Hati (Mkataba) ya Muungano ya Aprili 22, 1964, vyama vya siasa si jambo la Muungano kuweza kusimamia mamlaka za Muungano. Hivyo utaratibu uliotumika kumng’oa Jumbe unahojika kisheria!

Kadri Jumbe alivyozidi kujiona kukubalika kwa Mwalimu Nyerere, ndivyo alivyojiona pia kama mrithi halali mtarajiwa wa Rais wa Muungano kuliko mtu mwingine yeyote, Bara na Visiwani. Lakini kutokuwepo kwake Zanzibar mara kwa mara kulizua ombwe la uongozi kwa kuwa kila kitu kilimsubiri yeye, hata kama ni idhini ya kukata mti. Na kwa jambo la dharura, Waziri mwenye dhamana ya dharura hiyo ilibidi amfuate Dar es salaam.

Kana kwamba ombwe hilo halikutosha, hofu ilitanda miongoni mwa Wazanzibari pale Mwalimu alipopendekeza mabadiliko zaidi ya Katiba kutaka kuunda Serikali moja badala ya Serikali mbili, wakihofia nchi yao kumezwa na Tanganyika. Hali hii ilimweka pabaya Jumbe Visiwani juu ya uswahiba wake na Nyerere, wakimwita ‘msaliti’ wa Mapinduzi ya Zanzibar na Wazanzibari.
uona hivyo, Jumbe alianza kugeuka nyuma kwa kuchanganyikiwa; akawa njia panda. Wakati hilo halijapoa, jingine kubwa zaidi lilikuwa njiani likija. Mwaka 1983, Edward Moringe Sokoine, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi wa Muungano, aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu. Sokoine alikuwa na mvuto wa watu, shupavu na mwadilifu kiasi kwamba katika kipindi kifupi tu alijidhihirisha kuwa chaguo la watu na mrithi halali wa Mwalimu, ambaye naye alimkubali kwa ishara na kwa vitendo.
Kwa kuridhika na Sokoine, taratibu Mwalimu alianza kumbeza Jumbe kwa sababu nyingi, lakini itoshe hapa kutaja mbili tu. Kwanza, alimwona kama kiongozi mpweke asiye na sapoti na aliyepoteza mvuto Visiwani, pia kama dikteta mkimya asiyeshaurika na watu wa chini yake.

Pili; Mwalimu aliudhika kwa Jumbe kugeuka mhafidhina wa kidini na mpambanaji wa Kiislamu katika Taifa lisilo na dini. Kwa hili, Jumbe alizuru nchi nzima akitoa hotuba kwenye misikiti, na Serikali ikalazimika kutoa Waraka mkali wa Rais, kuwakumbusha na kuwataka viongozi wa kitaifa kutojipambanua au kuendekeza mambo ya kidini. Jumbe alipuuza Waraka huo; kwake ndio kukawa kumekucha.

Habari za Mwalimu kupoteza imani na upendeleo kwa Jumbe hatimaye zilimfikia kiongozi huyo, zikamuuma sana na kumvunja moyo. Hapo uhasama ukazuka kati yake na Mwalimu kwa njia ya kukomoana. Kwa hasira na kukata tamaa, Jumbe akaanza maandalizi ya kuumbua Muungano, kwa minyukano na Mwalimu.
Kuanzisha minyukano hiyo, ilikuwa ni lazima kwanza Jumbe arejeshe imani yake iliyopotea kwa Wazanzibari, kutokana na hatua yake ya kuhamia Mji mwema, Kigamboni na kwa kuwatelekeza Wazanzibari. Baada ya kuridhika kwamba mambo ameyaweka sawa, aliomba mawazo ya Makatibu Wakuu wa Wizara zote na Watendaji Wakuu wengine wa Serikali, ni aina gani ya Muungano unaotakiwa.

Wote, isipokuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa Zanzibar, Damian Lubuva, walikataa muundo wa sasa wa Serikali mbili au wa Serikali moja uliokuwa umeanza kupigiwa upatu na Mwalimu na baadhi ya wanasiasa. Jumbe na watendaji wake hao ndani ya Serikali ya Zanzibar wakapendekeza muundo wa Shirikisho lenye Serikali tatu. Serikali ya Tanganyika, Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Muungano kwa mambo kumi na moja tu yaliyoainishwa katika Mkataba wa awali wa Muungano.
Mtizamo huo ndio aliouweka wazi Jumbe baadaye katika kitabu chake kiitwacho ‘The Partnership,’ yaani ‘Ubia kati ya Tanganyika na Zanzibar,’ kilichosambazwa mwaka 1984. Kuthibitisha hilo, ananukuu ibara ya tano ya Mkataba wa Muungano inayosema kwamba kufuatia kuundwa kwa Serikali ya Muungano, “Sheria za Tanganyika zilizopo na zile za Zanzibar, zitaendelea kuwa na nguvu katika nchi hizo.” (The Partnership, uk. 22).

Vivyo hivyo, anathibitisha kwa kunukuu Ibara ya Sita (a) ya Mkataba, inayotanabahisha kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano, atasaidiwa na Makamu wawili wa Rais (mmoja kwa ajili ya Tanganyika na mwingine kwa ajili ya Zanzibar), Mawaziri na Maofisa wengine anaoweza kuwateua kutoka Tanganyika na Zanzibar ambapo kufuatia uteuzi huo, utumishi wao utahamishiwa kwenye utumishi wa Serikali ya Muungano.

Anahoji: “Kwa kuwa Mkataba wa Muungano na Sheria ya Muungano Namba 22 ya 1964, vinatambua uwapo na kubakia kwa Serikali za Tanganyika na Zanzibar baada ya Muungano, kwanini Muundo uliokusudiwa usitafsiriwe kuwa Shirikisho? Kama Tanganyika na Zanzibar zinatajwa kuwa nchi ndani ya Muungano, lakini kwa vitendo na hulka kuna nchi ya Zanzibar pekee, Tanganyika ilikwenda wapi?

Hatua iliyofuata na aliyochukua Jumbe, ilikuwa ni kumrejesha kwao Tanzania Bara, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Damian Lubuva, akimwelezea kama mtumishi asiyeweza kusimamia maslahi ya Wazanzibari; na badala yake akamteua rafiki yake wa zamani, raia wa Ghana, Alhaj Bashir K. Swanzy kuwa Mwanasheria Mkuu.

Kuanzia hapo, madai ya Wazanzibari kutaka mabadiliko ya Katiba, huku wengine wakitaka warejeshewe Visiwa vyao (Zanzibar), kupitia mihadhara, magazeti na redio, yalipamba moto ambapo wanajeshi wa Kizanzibari nao walikuwa na malalamiko yao.

Mashambulizi yenye kashfa nzito nzito na matusi ya kisiasa yaliongozwa na redio ya ufichoni iliyopachikwa jina la ‘Kiroboto Tapes,’ hadi ilipogunduliwa na kuharibiwa na wanajeshi kutoka Bara. Mitafaruku yote hii ilikuwa na ridhaa ya Alhaj, Sheikh Aboud Jumbe Mwinyi.

Jumbe aandaa mashitaka dhidi ya Muungano
Kwa kumtumia Alhaj Bashir K. Swanzy, raia wa Ghana aliyemteua kuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar kushika nafasi ya Damian Lubuva, na kumpa uraia kwa njia ya usajili, Rais Jumbe aliandaa Hati ya Mashtaka kuhoji muundo na uhalali wa Muungano kwenye Mahakama Maalum ya Kikatiba ya Jamhuri ya Muungano, ambayo kwa mujibu wa Ibara ya 125 na 126 ya Katiba ya Muungano ya mwaka 1977, kazi yake pekee (nanukuu) “ni kusikiliza shauri lililoletwa mbele yake na kutoa usuluhishi juu ya suala lolote linalohusika na tafsiri ya Katiba; iwapo tafsiri hiyo au utekelezaji wake unabishaniwa kati ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.”

Katika hili, Mwanasheria Mkuu Mstaafu wa Zanzibar, Wolfgang Dourado (sasa marehemu), naye alishirikishwa. Hata hivyo, Hati hiyo ya mashitaka ilipotea mezani kwa Rais Jumbe katika mazingira ya kutatanisha, na hatimaye kuibukia mikononi mwa Mwalimu Nyerere (Ikulu, Tanzania Bara).
Mbali na Hati ya Mashtaka, Rais Jumbe aliandika pia barua ndefu kwa Mwalimu kubainisha jinsi Mkataba wa Muungano na Sheria ya Muungano zilivyoendelea kukiukwa na utawala wa nchi, na kuhoji pia mantiki ya kuunganishwa kwa TANU na ASP kuunda CCM, na mamlaka turufu Chama hicho kiliyojipa kusimamia Muungano, wakati vyama vya siasa si jambo la Muungano.
Kwa msaada pia wa Jaji Swanzy, Rais Jumbe alifanya rejea kwa kuhoji uhalali wa Sheria Namba 18 ya mwaka 1965, iliyoahirisha kwa kusogeza mbele muda wa kuitisha Bunge la Katiba, ubabe wa Katiba ya Muda ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1965 na ubatili wa Katiba ya Kudumu ya mwaka 1977 kwa namna ilivyobuniwa na kutungwa bila kuzingatia matakwa ya Mkataba na Sheria ya Muungano.

Kwa kuwa barua hiyo iliandikwa kwa lugha ya Kiingereza, alimwagiza aliyekuwa Waziri Kiongozi wake, Ramadhan Haji, ahakikishe imetafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili ili iweze kujadiliwa kikamilifu kwenye Baraza la Mapinduzi.
Kabla ya hapo, akihutubia kwenye kilele cha Sherehe za Mapinduzi Zanzibar, Januari 12, 1984, Rais Jumbe alionyesha kukerwa na jinsi Muungano ulivyokuwa ukiendeshwa na kuwataka Wazanzibari wavute subira wakati tatizo hilo likishughulikiwa, na kwamba bila ya mwafaka na maridhiano kati ya Zanzibar na Serikali ya Muungano juu ya muundo sahihi wa Muungano, Zanzibar ingekwenda Mahakamani.

Kwa mara nyingine, kama ilivyopotea Hati ya Mashitaka katika mazingira ya kutatanisha, ndivyo pia barua hiyo ndefu ilivyopotea hata kabla Rais Jumbe Mwinyi hajaitia sahihi na kuibukia mikononi mwa Mwalimu Nyerere.

Kwa kuona hatari mbele yake, haraka haraka kikaitishwa kikao cha dharura cha Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM mjini Dodoma kumjadili Rais Jumbe kwa dhambi kuu ya kuthubutu kutua mahali ambapo ‘Malaika’ waliposhindwa kutua.
Humo ndani ya kikao, mizinga ikalia. Mizinga ya piga nikupige, huku kambi mbili za Kizanzibari zikiumana kutaka kuangamizana. Kambi ya ‘Wanamstari wa mbele’ (Frontliners) ilitaka Rais Jumbe atoswe, huku ikimwelezea kama msaliti wa Muungano, kiongozi dhaifu na asiyekubalika Visiwani, mbinafsi na mwenye makundi.
Kambi ya pili, ya ‘Wakombozi’ (Liberators), iliona Rais Jumbe anazushiwa mengi na wabaya wake, wapinga Mapinduzi wasioitakia mema Zanzibar. Kanali Seif Bakari (marehemu), ambaye wakati huo alikuwa pia Naibu Waziri wa Ulinzi, alijitahidi mno kumwokoa Rais Jumbe kikaoni humo bila mafanikio, lakini baadaye akaishia kuwekwa chini ya ulinzi nyumbani, na hatimaye kutiwa kizuizini Tanzania Bara kwa zaidi ya miezi sita.

Kwa kutumia kofia yake ya Mwenyekiti wa CCM, na kwa kutumia pia udhaifu wa Wazanzibari, kama ulivyojidhihirisha wakati huo kwa utengano wao, wivu na chuki miongoni mwao kwa wao, ilikuwa rahisi kwa Mwalimu kumtungua Rais Jumbe bila sauti ya umoja kutoka Zanzibar, na saa ilipowadia; akavuliwa nyadhifa zake zote za uongozi kama tulivyoona katika sehemu ya kwanza ya makala haya.

Tetemeko na mafuriko yakawakumba pia wasaidizi wake wa karibu, wakiwamo aliyekuwa Waziri Kiongozi, Ramadhani Haji; Waziri wa Nchi wa Zanzibar, Aboud Talib, ambapo Mwanasheria Mkuu Mteule wa Rais Jumbe, Jaji Bashir Swanzy, alifukuzwa Zanzibar kwa taarifa ya saa 24 na kurejeshwa kwao Ghana.

Naye Jaji Dourado, kama ilivyokuwa kwa Rais Jumbe na Kanali Seif Bakari, aliwekwa kizuizini kwa miezi sita, kisha ikatangazwa sawia hali ya hatari kisiasa, maarufu kama ‘kuchafuka kwa hali ya hewa Visiwani.’ Mambo ya Usalama wa Taifa, ambayo kabla ya hapo hayakuwa jambo la Muungano (ilikuwa ni Ulinzi tu), yakaingizwa kwenye Katiba kuwa jambo la Muungano, na kwa hiyo ikasomeka ‘Ulinzi na Usalama’ ili kudhibiti zaidi hali hiyo. Kufikia hapo, ilikuwa ushindi mkubwa kwa kambi ya ‘Wanamstari wa mbele’ dhidi ya kambi ya ‘Wakombozi.’

Mwandishi wa makala haya, ambaye alikuwa mmoja wa Vijana wa CCM kutoka Tanzania Bara, walioshiriki kwenye zoezi la kulegeza na kudhibiti mkakamao wa hali hiyo tete Visiwani, kwa lengo la ‘kusafisha’ hewa iliyochafuka, alishuhudia jinsi kambi hizi mbili zilivyokamia kuumizana, licha ya Zanzibar kupata Rais mpya, Sheikh Ali Hassan Mwinyi; huku kambi ya ‘Wakombozi’ iliyoshindwa ikiapa kulipiza kisasi kwa ‘Wanamstari wa mbele’ na kwa Mwalimu Nyerere pia. Nafasi hiyo ilikuja pale Mwalimu Nyerere alipotangaza nia yake ya kung’atuka mwaka 1985 na kutafuta mrithi wake.

Nyerere aandaa mrithi wake
Kifo cha Waziri Mkuu, Edward Moringe Sokoine, ambaye nafasi yake ilichukuliwa na Dk Salim Ahmed Salim, kilimweka Mwalimu njia panda kuhusu uteuzi wa mrithi wake baada ya yeye kung’atuka. Ili kuweka mzani wa kidiplomasia za kimuungano sawa na kwa lengo maalum, iliazimiwa kwamba Rais wa Awamu ya Pili wa Jamhuri ya Muungano, atoke Zanzibar.
Na katika kutekeleza lengo hilo, nafasi za wagombea zilidhibitiwa kuwa watatu tu. Nao walikuwa ni Rais wa Zanzibar na Makamu wa Rais wa Muungano na pia Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa, Ali Hassan Mwinyi; Waziri Mkuu wa Muungano na Mjumbe wa NEC na Kamati Kuu (CC) ya CCM, aliyekuwa na nguvu kubwa kisiasa wakati huo, Dk Salim Ahmed Salim; na Mjumbe mwingine wa NEC na CC, aliyekuwa na nguvu kubwa pia kisiasa, Rashid Mfaume Kawawa.

Ukimwacha Kawawa ambaye alikuwa anatokea Bara, Mwinyi na Dk Salim ndio pekee walikuwa Wazanzibari, na hivyo kufifisha dhamira nzima kwamba Rais wa Awamu ya Pili atoke Zanzibar. Mwinyi, pamoja na kuzaliwa Kisarawe (Tanzania Bara), alikulia na kusomea Zanzibar. Na kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, Mtanzania yeyote aliyeishi Zanzibar kwa miaka sita mfululizo, anastahili kuitwa Mzanzibari; na ndivyo ilivyokuwa kwa Mwinyi.
Mwalimu Nyerere alikuwa na mtihani mgumu kumpata mrithi kutokana na vigogo hao watatu waliokuwa na sifa na nguvu sawa katika siasa za Tanzania enzi hizo. Kwa hiyo, akaanzisha mchezo wa karata na ushawishi katika ngazi za juu za Chama, lakini bila rushwa wala matumizi ya fedha kama ilivyo siku hizi ndani ya CCM.

Ikumbukwe kwamba katika ngazi hizo za juu, kwa maana ya NEC na CC ya CCM, zilikutanishwa kambi mbili zenye kuhasimiana juu ya ukuu wa kisiasa Zanzibar. Kambi hizo zilikuwa ni zile zile za ‘Wakombozi’ (Liberators), iliyoongozwa na Brigedia Abdullah Said Natepe. Wengine walikuwa ni Ali Mzee (aliyekuwa Waziri wa Nchi (Serikali ya Muungano), Hassan Nassoro Moyo (aliyekuwa Waziri wa Kilimo Zanzibar), Mohammed Seif Khatib (aliyekuwa Katibu Mkuu na Kaimu Mwenyekiti wa UVCCM), pamoja na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani wa Muungano, Dk Salmin Amour Juma.

Kambi hii ilikuwa pia na maofisa wastaafu wa Jeshi na Usalama wa Taifa. Hao walikuwa ni pamoja na Brigedia Mstaafu na Waziri Kiongozi wa zamani, Ramadhan Haji (aliyeng’olewa pamoja na Jumbe) na Mkuu wa Jeshi la Zanzibar, Brigedia Khamis Hemed.
Kambi hiyo ya Wakombozi ilikuwa bado ikipiga kampeni kushinikiza kuachiwa kutoka kizuizini mtu wao, Kanali Seif Bakari, pamoja na Mjumbe mwingine wa zamani wa Baraza la Mapinduzi, Hafidh Suleiman, ambao hao wawili walikuwa sehemu ya watesi maarufu (Genge la watu 14) na vinara wa ukiukaji wa haki za binadamu na mauaji enzi za utawala wa Abeid Amani Karume.
Kwa upande wa kambi ya ‘Wanamstari wa mbele’ ilikuwa na Dk Salim Ahmed Salim, Seif Shariff Hamad (wakati huo Waziri Kiongozi), Hamad Rashid) wakati huo Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani wa Muungano) na Khatib Hassan. Wengine walikuwa ni Kanali Adam Mwakanjuki, Isaac Sepetu, Shaaban Mloo, Ali Salim na Ali Haji Pandu, ambao wote walikuwa Wajumbe wa NEC ya CCM.
Kambi ya ‘Wakombozi’ ilijua mapema chaguo la Mwalimu Nyerere ni Dk Salim Ahmed Salim kuwa kumrithi wake. Kambi hiyo ikaona hiyo ilikuwa ni nafasi nzuri kulipiza kisasi kwa majeraha iliyopata kutokana na mtu wao Aboud Jumbe, kuondolewa madarakani.

Mwalimu akwaa kisiki kuteua mrithi
Tangu mwanzo, kambi hii ya ‘Wakombozi’ ilikuwa na chuki ya kudumu dhidi ya Dk Salim kwa sababu za kisiasa na kijamii. Mwaka 1982, wakati Dk Salim alipoteuliwa na Mwalimu kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Brigedia Natepe (wakati huo akiwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais (Usalama wa Taifa) na Ali Mzee (wakati huo akiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais), walikwenda kwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Sokoine, wakadai kwamba walikuwa na maagizo kutoka kwa Rais wa Zanzibar, Aboud Jumbe na Kanali Seif Bakari, ya kuzuia Dk Salim asiwe Waziri wa Mambo ya Nje.

Walitoa sababu mbili. Mosi, kwamba kuna makubaliano ya siri tangu enzi za Karume, kwamba wanachama wa zamani wa vyama vya zamani vya siasa mbali na ASP, na ndugu zao, wasipewe nafasi za uongozi katika Chama, Serikali ya Zanzibar wala katika Serikali ya Muungano; bali watumike kwa shughuli za kitaalam tu.

Dk Salim alikuwa mmoja wa viongozi wakuu wa chama cha siasa cha mrengo wa kushoto (Ki-Marxist/Kikomunisti) cha Umma Party kilichofanikisha Mapinduzi ya 1964 kwa kushirikiana na ASP, kisha akateuliwa na Karume kuwa Balozi wa Zanzibar nchini Misri, chini ya Serikali ya mseto kati ya ASP na Umma Party. Pili, walidai kwamba rangi ya ngozi ya Dk Salim iliwakumbusha Wazanzibari, kwa kilio cha kusaga meno, utawala wa Sultani aliyepinduliwa Januari 12, 1964.
Sokoine, Waziri Mkuu ambaye hakupenda mzaha wala majungu, aliwafukuzia mbali viongozi hao. Kuanzia hapo, nyota ya Dk Salim ilizidi kung’ara na hatimaye kumrithi Sokoine alipofariki kwa ajali ya gari miaka minne baadaye.

Mikakati ya ‘Wakombozi’ kumzuia Dk Salim asimrithi Mwalimu Nyerere ilikuwa thabiti ikihusisha vigogo wa Visiwani na Bara pia. Wasukaji wa mikakati Visiwani, walikuwa ni Hassan Nassoro Moyo, Natepe, Ramadhan Haji na Aboud Talib, kwa kumshirikisha mwanamkakati kiungo chao Tanzania Bara, Waziri wa Utalii wa wakati huo, Paul Bomani, aliyeunda na kuongoza kikosi cha Wajumbe wa NECwa Bara dhidi ya Dk Salim.
Mwalimu Nyerere alijua yote haya, lakini hakujihusisha kupiga kampeni kwa kuheshimu demokrasia na misingi ya uongozi bora. Mwinyi alifuatwa na ‘Wanamstari wa mbele’ siku ya uteuzi na kushauriwa, naye akakubali, kujitoa katikati ya mchakato ili kumwachia Mzanzibari mwenzake, Dk Salim.

Walidhani wamemshawishi vya kutosha kufikia uamuzi huo, lakini mambo hayakuwa kama walivyotarajia siku ya kikao cha Kamati Kuu ya CCM cha kuteua mgombea, hapo Agosti 12, 1985. Kawawa, kama ilivyotarajiwa, alijitoa kugombea, kwa hiyo wakabakia wawili. Mwinyi na Salim wakatoka nje ili wajadiliwe, lakini hadi hapo bila dalili zozote za Mwinyi kujiengua.
‘Wakombozi’ wa Visiwani na maswahiba wao wa Bara, walitumia vizuri nafasi waliyopewa na hivyo kutawala mazungumzo, huku Moyo na Natepe wakiongoza. Mjumbe mwingine aliyezungumza, alikuwa Getrude Mongella, wakati huo akiwa pia Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu (kikulacho kinguoni mwako?) na mpambe mku wa Bomani kwa kampeni za Bara.
Hoja ya Mongella ilikuwa kwamba kumwacha Mwinyi ambaye alikuwa Makamu wa Rais na Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa, na kumteua Dk Salim, kungetafsiriwa vibaya kitaifa na kimataifa kwamba Watanzania hawaheshimiani kiuongozi. Kamati kuu ikamteua Mwinyi. Kambi ya ‘Wakombozi’ ikachekelea kwa ushindi.

Bado ilitarajiwa kuwa Mwinyi angejitoa baada ya hapo, lakini hakufanya hivyo. Akajikausha chini ya mkazo wa macho ya ‘Wanamstari wa mbele’ waliotarajia afanye hivyo. Kinyume chake, alipojulishwa juu ya kuteuliwa kwake kikaoni humo, jibu lake lilikuwa rahisi na fupi. Alisema: “Kama hayo ndiyo matakwa ya watu, nakubali.” Mwenyekiti wa CCM, Mwalimu Nyerere hakupinga. Tayari alikuwa amekwaa kisiki cha ‘Wakombozi,’ wakafanikiwa kulipiza kisasi chao kwake.
Share this article :

0 comments:

Speak up your mind

Tell us what you're thinking... !

ZILIZOSOMWA SANA.

Followers

Blog Archive

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Proudly powered by Blogger
Copyright © 2011. Msamaa. - All Rights Reserved
Template Design by Creating Website Published by Mas Template