IJUE MAANA YA AQIQAH. - Msamaa.
Headlines News :
Home » » IJUE MAANA YA AQIQAH.

IJUE MAANA YA AQIQAH.

Written By Unknown on Saturday, March 16, 2013 | 10:00 PM


 

‘Aqiqah AFANYIWAYO MTOTO MCHANGA.

 

 • ‘Aqiqah ni jina lililopewa kichinjwa (Mnyama) achinjiwacho mtoto mchanga aliyezaliwa ni mamoja awe ni wa kike au wakiume.

 

 • ‘Aqiqah ni Sunnah si waajibu. Ushahidi wa hili uko katika maneno ya Mtume Swalla LLahu ‘Alayhi Wasallama aliposema: “Atakayepata mtoto na akapenda amchinjie basi na afanye hivyo, kwa mwana

 

 •  

 

 • mume mbuzi wawili na kwa mwanamke mbuzi mmoja”. Hadithi hii imepokewa na maimamu Abuu Dawuud na Annasaai kutoka kwa Abdallah bn Umar. Kauli ya Mtume; “na akapenda amchinjie” ni dalili kuwa ‘Aqiqah  si lazima bali ni jambo linalopendeza mwislamu kulifanya. Lakini kwa mwenye uwezo wa kufanya hivyo basi iliyo bora zaidi kwake ni kufanya. Ama yule asiye na uwezo wa kufanya hivyo basi si lazima kwake  maana Mwenyezi Mungu haikalifishi nafsi yoyote ila yale yaliyo sawa na uwezo wake na pia hakufanya uzito katika dini Yake.

 

 • Imethibiti kutoka kwa Mtume wa Allah kuwa yeye kasema: “kila mtoto azaliwaye anafungamana na ‘Aqiqah yake, anachinjiwa siku ya saba, ananyolewa kichwa chake na anaitwa jina

 

 • . Wanachuoni wamelizungumzia neno “kufungamana” hapa kuwa linaweza kuwa linamaanisha mambo mengi, miongoni mwa mambo hayo ni;

 1. Anakuwa kama mwenye kujisikia uzito na unyonge na mwenye kukosa wepesi na furaha maishani hadi achinjiwe
 2. Anazuiwa kuwaombea wazazi wake uombezi mwema wa siku ya Qiyama
 3. Ni deni lililo mithili ya Rehani ambayo hulazimiana na mtu hadi ailipe.

 

 • Iliyo bora zaidi na timilifu ni kuwa wale mbuzi wawili ambao anatakiwa mtoto wa kiume achinjiwe wanatakiwa wawe ni wenye kufanana au kukaribiana kufanana kimaumbile na kiumri. Lakini kama itashindikana kuwapata mbuzi wawili wenye sifa kama hizo itafaa hata kama watatofautiana kiumbile na kiumri maadamu tu wana sifa zinazofaa kisheria kwa ajili ya ibada hii. Sifa hizo tutazitaja baadaye.

 

 • Iliyo bora zaidi na timilifu ni kumchinjia mtoto wa kiume mbuzi wawili lakini ikiwa mtu atashindwa kabisa kuchinja mbuzi wawili kama kutokana na yeye kupata mbuzi mmoja tu au kumiliki kiwango cha mbuzi mmoja tu basi huyo huyo mbuzi mmoja atatosha.

 

 • Sunnah ni kumchinjia mtoto atakapofikisha siku ya saba kama ilivyokuja katika hadithi ya Samrah, lakini ikiwa mtu hakuweza kuchinja siku ya saba basi na afanye hivyo siku ya kumi na nne na ikiwa atashindwa siku ya kumi na nne basi na afanye hivyo siku ya ishirini na moja na ikiwa atashindwa siku ya ishirini na moja basi na afanye hivyo siku yeyote.

 

 • Ibada hii ya kuchinja hufanyika hata kama mtoto kafariki maadamu tu alizaliwa hai au hata kama mimba ilitoka lakini mtoto tayari alikuwa ameviviwa roho yaani alikuwa amefikisha miezi minne au siku mia na ishirini na kuendelea lakini kama alikuwa hajafikisha miezi minne au siku mia na ishirini hapo hatafanyiwa ‘Aqiqah.

 

 • Kuna imani imeenea kwa watu wengi kuwa kichinjwa cha ‘Aqiqah hakivunjwi mifupa hii ikiwa kama ishara ya kumtakia mtoto salama na asivunjike maishani mwake. Hili si sahihi wala halina mashiko katika Qur’an wala Sunnah. Kwa hiyo ieleweke wazi kuwa mifupa ya ‘Aqiqah inafaa kuvunjwa wala hii haitakuwa sababu ya kuvunjika kwa mtoto hata kama itatokea kama watu wanavyoamini. Vile vile kuna jambo jingine nalo ni kuwa nyama ya ‘Aqiqah huchanganywa au hupikwa kwa maji yaliyotiwa vitu vitamu vitamu kama sukari au huchanganywa na asali wakati wa kuliwa, hii ikiwa ni kama ishara ya kumtakia mtoto tabia njema; hili nalo pia halina mashiko. Hivyo iwekwe chumvi na kupikwa kama nyama ya kawaida.

 

 • Kinachotakiwa kuchinjwa katika ‘Aqiqah ni wanyama ambao kisheria wanaitwa Bahiimatul An’aam ambao ni; mbuzi, kondoo, ng’ombe na ngamia. Kwa mantiki hii haifai kumchinja farasi kwa ajili hii, wala swala hata kama anafugwa na amekuwa kama mbuzi kitabia na pia haifai kuchinja kuku wala bata kwa ajili ya ibada hii.

 

 • Ama kuhusiana na umri unaofaa wa kichinjwa hichi ni miaka mitano kwa ngamia na miaka miwili kwa ng’ombe, dume la mbuzi na dume la kondoo ni mwaka mmoja na mbuzi jike na kondoo jike ni miezi sita.

 

 • Ni sharti katika kichinjwa cha ‘Aqiqah kiwe kimesalimika na aibu mbalimbali. Kwa kifupi kabisa kichinjwa hichi kinafanana na kichinjwa cha Iddil adh’haa au iddi kubwa yaani kisiwe chongo cha wazi, kiguru cha wazi, kilichokonda sana, wala kisiwe ambacho kimetobolewa masikio yake, wala kilichokatwa mkia au kukatika pembe.

 

 • Ikiwa mtu anamiliki takribani wanyama wote wanaofaa kuchinja kwa ajili ya ‘Aqiqah kiasi kuwa anaweza akitaka akachinja ng’ombe au ngamia au kondoo au mbuzi, iliyo bora zaidi kwake ni kuchinja mbuzi maana ndiyo aliyetajwa katika hadithi.

 

 • Inafaa mtu kuipika nyama ya ‘Aqiqah au kuigawa pasina kuipika lakini iliyo bora zaidi ni kuipika nyama hiyo kuliko kuigawa kwa kuwa kwa kufanya hivyo utawarahisishia masikini na majirani gharama za kupika.

 

 • Hakuna ubaya wowote katika kula nyama ya ‘Aqiqah kwa aliyechinja, kwani kwa hakika hii ni nyama kwa ajili ya kumshukuru Allah na kile ambacho ni kwa ajili ya kumshukuru Allah kinafaa kuliwa kisheria wala hapana ubaya bali hii ni kama nyama ya iddil adh’haa.

 

 • Pia inafaa kuiweka nyama ya ‘Aqiqah katika jokofu pasina kuigawa lakini iliyo bora zaidi na timilifu katika ibada hii ni kuigawa kwa mafaqiri, masikini, majirani na marafiki hata kama ni kidogo.

 

 • Haifai kununua mbuzi aliyechinjwa na kumfanya kuwa ni ‘Aqiqah bali ni lazima kumununua mbuzi aliye hai na kisha kumchinja kwa nia ya ‘Aqiqah.

 

 • Ikiwa baba hayuko kama kwa mfano kafariki mama atasimamia jukumu la kufanyia  mtoto ‘Aqiqah.

 

 • ‘Aqiqah ni Sunnah kwa baba kumfanyia mtoto wake lakini kama mtoto hakufanyiwa ‘Aqiqah na akapenda ajifanyie mwenyewe inafaa hata kama ni kitambo kirefu kimepita na umri ukawa mkubwa.

 

 • Inafaa kumchinjia mtoto wa kiume mbuzi hao wawili kwa utaratibu wa kugawa kwa maana ya kuwa anamchinja mbuzi mmoja mwezi huu na mwingine akamchinja mwezi mwingine wala haishurutishwi wachinjwe mara moja, bali inafaa kwa mtoto akajichinjia mbuzi mwingine ikiwa baba alimchinjia mbuzi mmoja kwa sababu ya hali yake kifedha wakati huo. Bali inafaa kumchinjia mbuzi mmoja sehemu moja na mwingine sehemu nyingine, wala si sharti wachinjwe wote sehemu moja wala si sharti wachinjwe sehemu alipo mtoto anayefanyiwa.

 

 • Haifai kisheria kupigia thamani ya mbuzi wa ‘Aqiqah na kuwapa kiwango hicho cha fedha masikini bali ni lazima achinjwe mbuzi

 

 • Haifai kushirikiana watoto katika ‘Aqiqah kwa mantiki ya kuwa wachangie kwa mfano mbuzi wawili watoto wawili wa kiume. Watoto wawili wa kiume wanapaswa wachinjiwe mbuzi wanne hata kama ni mapacha. Kama ni mapacha wawili wa kike watachinjiwa mbuzi wawili, kama mmoja ni wa kike na mwingine ni wa kiume watachinjiwa mbuzi watatu. Bali ngamia na ukubwa wake hafai kuwachinjia watoto wawili na ikifanyika hivyo inazingatiwa ni kwa ajili ya mtoto mmoja. Bali haitofaa kwa watoto wawili ambao hawakufanyiwa ‘Aqiqah kwa wao kujiamulia kuchinja ngamia mmoja ili awe ni ‘Aqiqah kwa wote wawili. Bali ngamia huyo atazingatiwa kuwa ni kwa ajili ya mtoto mmoja tu.

 

 • Si lazima wakati wa kumchinja mnyama wa ‘Aqiqah kusema kuwa hii ni ‘Aqiqah bali inatosha mtu kunuia moyoni mwake na kilicho lazima kutamka ni Bismillah Rahmaan Raheem wakati wa kuchinja.

 

 • Si lazima kuwaambia waliohudhuria kuwa watakula nyama ya ‘Aqiqah, lakini ni vizuri kuwaambia ili wamuombee mtoto dua njema, uongofu, Uchaji Mungu, kutengenekewa na kheri za dunia na akhera.

 

‘Aqiqah ni mnyama ambaye huchinjwa kwa ajili ya mtoto mdogo kama tulivyotangulia kusema. Jambo hili ni katika mlango wa kumshukuru Allah. Kuna pia vyakula vingine ambavyo ni katika mlango huu wa kumshukuru Allah na vinafaa kuliwa kisheria navyo ni;

 

1.   Walima ambacho chakula au karamu ya harusi

2.   Qiraa ambacho chakula cha mgeni, kile cha mgeni njoo wenyeji tupone!

3.   Maadaba ambacho ni chakula cha mwaliko

4.   Tuhfa ambacho ni chakula cha mwenye kutembelea pahala.

5.   Khiraasu ambacho ni chakula cha mwanamke aliyejifungua.

6.   Ghadiira ambacho ni chakula cha wakati wa khitaani au kutahiri wanawake au wanaume.

7.   Naqiigha ambacho ni chakula cha anayekuja kutoka safari.

8.   Wakiira ambacho ni chakula baada ya kumaliza kujenga.

 

Vyakula vyote vilivyotajwa hapo juu ni halali isipokuwa chakula cha msibani au chakula cha siku ya tatu au chakula cha khitimah au chakula cha arobaini, vyakula hivi haviifai kuvila kisheria kama hakuna dharura ya kufanya hivyo. Jariri Ibn ‘Abdillah anasema kuwa kukusanyika kwa wafiwa na kupikiwa chakula ni miongoni mwa mambo aliyokataza Mtume wetu Mtukufu na ni sawa na kuongeza msiba.

 

Wabillah Tawfiiq.
Chanzo:MUM Lecturer.

 

 

 
Share this article :

8 comments:

 1. Je naweza kumfanyia hakika mtoto ambaye amefkisha miaka minne?

  ReplyDelete
 2. Inawezekana kabisa kumfanyia aqiqa mtoto aliyefikisha miaka minne kwasababu Aqiqa ni moja katika sunna kubwa lakini kufanywa kwake kunategemea na uwezo wa kiuchumi au kumiliki mnyama mwenyewe.

  ReplyDelete
 3. A'alleykum, nyama ya aqiqah ni lazima ichemshwe tu, je vingo Kama tangawizi inafaa kuwekwa?..

  ReplyDelete
  Replies
  1. naam. nyama hii kama ilivyonukuliwa hapo juu yakuwa hufuata taratibu zakawaida kabisa kimaandalizi mfano wa yale ya wakati wa eid kubwa.

   Delete
 4. Asalam aleikum warahmatullah wabarakatuh :jee inafaa kufanya aqiqah ukaleta wanafunzi wa madrasa kusoma dua?

  ReplyDelete
 5. Uwezo wangu ni mbuzi mmoja na mtoto wangu niwakiume je itaswii nikimchinjia mbuzi mmoja Kwny kisomo cha aqiqah?
  Na keep!? Naweza kumfanyia aqiqah mtoto siku ya Arobaini?

  ReplyDelete
 6. Asalam alaikum sheikh; je Ni kisomo kipi kinacho stahiki siki ya Aqiqah maana bidaa zimekuwa nyingi naomba unielezee utaratibu wake wote kwa ujumla (A-z)

  ReplyDelete
 7. Mtt wangu wa kiume na uwezo wangu mbuz mmoja je itaswih kumfanyia hakika?

  ReplyDelete

ZILIZOSOMWA SANA.

Followers

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Proudly powered by Blogger
Copyright © 2011. Msamaa. - All Rights Reserved
Template Design by Creating Website Published by Mas Template