- Kitoloho
Headlines News :
Home » »

Written By Msamaa on Thursday, August 22, 2013 | 12:25 PM

Ponda asomewa mashtaka wodini

Share bookmark Print Email Rating
 
Na  Beatrice Moses na Aziza Masoud  (email the author)

Posted  Jumatano,Agosti14  2013.Mwananchi.
 
Dar es Salaam. Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda amesomewa mashtaka ya uchochezi akiwa kitandani katika Taasisi ya Mifupa ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (Moi).
Ponda aliyekuwa chini ya ulinzi wa polisi tangu Agosti 9 mwaka huu, alipofikishwa hospitalini hapo kwa matibabu, alisomewa mashtaka hayo na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Hellen Liwa.
Kiongozi huyo alifikishwa hospitalini hapo baada ya kudaiwa kupigwa risasi ambayo hata hivyo, si Moi wala Polisi waliothibitisha.

Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu, Dar es Salaam, ililazimika kuhamia hospitalini hapo kutokana na Ponda kulazwa.
Mwendesha Mashtaka na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Tumaini Kweka alisema Sheikh Ponda anatuhumiwa kufanya uchochezi katika maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Sheikh Ponda alikana shtaka hilo bila kuwapo wakili wake, Juma Nassor. Hivi sasa kiongozi huyo wa Kiislamu, anatumikia kifungo cha nje cha mwaka mmoja kutokana na kesi ya uchochezi iliyokuwa ikimkabili.

Habari zilizopatikana baadaye jana zilieleza kuwa, ilikuwa Sheikh Ponda aondolewe hospitalini hapo na kwenda jela, lakini Wakili Nassor alisema hali ya mteja wake haikuwa nzuri tangu asubuhi hivyo kuomba abaki hospitalini hapo.
“Hawezi kuondolewa kwa kuwa tangu asubuhi analalamika kuumwa kichwa, kizunguzungu na maumivu katika jeraha alilopata. Zaidi ya yote, ni mpaka atakapopata ruhusa ya daktari,” alisema wakili huyo.

Habari zaidi zilizopatikana jana jioni zinaeleza kuwa utaratibu unafanyika ili Sheikh Ponda apate ruhusa ya kutoka hospitalini hapo ndipo apelekwe gerezani hadi kesi yake itakapotajwa tena Agosti 28, mwaka huu.
Akizungumza baadaye jana, Wakili wa Ponda alisema: “Nilichelewa kufika, ningepinga mashtaka hayo lakini ninaandaa pingamizi nitakalowasilisha siku ya kutajwa kwa kesi; sikubaliani na mashtaka aliyosomewa mteja wangu na pia Mahakama ya Kisutu haina uwezo wa kusikiliza shtaka linalotajwa.”

Wafuasi wazua zogo.
Mapema ilipofika saa 10 jioni, wafuasi wa Sheikh Ponda walifika kwa wingi hospitali kumwona ikiwa ni muda wa kawaida wa kuona wagonjwa, lakini walizuiwa na polisi hali iliyosababisha kutokea kutokuelewana.

Hata hivyo, hali hiyo ilitulia baada ya polisi waliokuwapo kulinda usalama kuzungumza na baadhi ya waumini hao na kukubaliana utaratibu wa kumwona kiongozi wao.
Mmoja wa wafuasi hao ambaye jina lake halikufahamika mara moja, aliwaambia wenzake: “Jamani tulieni, hakuna haja ya kushindana nguvu na polisi kwani taratibu za Serikali zinaendelea, tumeshaweka utaratibu na wote tutakwenda kumwona Sheikh wetu.”
Baadaye wafuasi hao waliruhusiwa na askari hao kuingia kumwona Sheikh Ponda katika makundi ya watu watano watano.

Moro nao waigomea kamati.
Uongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Mkoa wa Morogoro, umegoma kushirikiana na kamati iliyoundwa na Polisi nchini kuchunguza tukio la kupigwa risasi kwa Sheikh Ponda.
Mwenyekiti wa Jumuiya na Taasisi Morogoro, Sheikh Ayubu Mwinge Salum alisema aliitwa na tume hiyo katika Ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Faustine Shilogile ambako imeweka kambi kuhoji na kusikiliza ushahidi wa tukio hilo na kuieleza kuwa hayuko tayari kushirikiana nayo.
“Tuliwaambia hatuko tayari kutoa ushahidi kwa kuwa hatuna imani na kamati hiyo kwani haiko huru kama tulivyotarajia.
“Sisi ndio tuliomba kuundwa kwa tume na kutaka iwe huru lakini tumeshangazwa na kuundwa na maofisa wa jeshi hilo wakati ndilo linalotuhumiwa kuhusika na tukio lenyewe,” Sheikh Salum aliwaambia waandishi wa habari juzi.
Alisema kuwa watakuwa tayari kutoa ushahidi katika kamati hiyo hadi itakapoundwa iliyo huru ambayo wajumbe wake watapatikana nje ya Serikali na nchi.
Shilogile agoma
Akizungumzia kauli iliyotolewa na Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata) Mkoa wa Dar es Salaam ya kumtaka ajiuzulu kupisha uchunguzi wa tukio hilo, Kamanda Shilogile alisema hana mpango wa kufanya hivyo.
Alisema hawezi kujiuzulu wala kujibu kauli za taasisi akisema zina uhuru wa kusema chochote. Hata hivyo, alizishauri kuiachia kamati iliyoundwa kuchunguza suala hilo ifanye kazi.
“Siwezi kuwazuia watu kusema, sitaki kuzungumza lolote wakati Kamati ya Haki Jinai imeundwa tayari na itafanya kazi yake na kubaini ukweli. Tusiingilie kazi ya tume hiyo,”alisema.
Polisi imeunda Kamati ya Haki Jinai inayoongozwa na Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Isaya Mungulu ili kuchunguza tukio hilo ambalo jeshi hilo linatuhumiwa kumjeruhi Sheikh Ponda kwa risasi katika bega lake la kushoto, Ijumaa iliyopita mkoani Morogoro.
Viongozi mbalimbali wa taasisi za kiraia na zile za dini pia wamemtaka Kamanda Shilogile ajiuzulu kutokana na tukio hilo na kuitaka Serikali kuunda tume huru badala ile ya Kamati ya Haki Jinai.
Nyongeza na Lilian Lucas
Share this article :

0 comments:

Speak up your mind

Tell us what you're thinking... !

ZILIZOSOMWA SANA.

Followers

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Proudly powered by Blogger
Copyright © 2011. Kitoloho - All Rights Reserved
Template Design by Creating Website Published by Mas Template