Kashfa saba nzito nchini - Msamaa.
Headlines News :
Home » » Kashfa saba nzito nchini

Kashfa saba nzito nchini

Written By Unknown on Thursday, June 5, 2014 | 12:34 AM 
SOURCE: MWANANCHI.
Na Goodluck Eliona na Editha Majura, Mwananchi

Posted  Jumapili,Juni1  2014  saa 24:0 AM
Dar es Salaam. Serikali imepoteza zaidi ya Sh362.9 bilioni kutokana na baadhi ya kashfa kubwa za ufisadi na operesheni mbalimbali zilizoligharimu taifa tangu uhuru.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini taifa kukumbwa na kashfa mbalimbali za upotevu wa fedha au kuanzisha mipango ambayo utekelezaji wake ulisababisha maumivu kwa wananchi na hakuna awamu ya uongozi wa Serikali iliyokwepa hali hiyo.
Kuanzia awamu ya kwanza ya Mwalimu Julius Nyerere aliyeiongoza nchi toka mwaka 1961 ilipopata uhuru hadi 1986, Rais Ali Hassan Mwinyi (1986-1995), Rais Benjamin Mkapa (1995-2005) na Rais Jakaya Kikwete (2005-hadi sasa), kumeibuka kashfa mbalimbali, saba zikiwa kubwa na kulitikisa taifa.
Kashfa na operesheni saba kubwa zilizotikisa taifa ni pamoja na Operesheni Uhujumu Uchumi, ufisadi katika Mfuko wa Kuwezesha Uagizaji Bidhaa kutoka Nje ya Nchi (Commodity Import Support – CIS) na Kashfa ya Rada.
Nyingine ni ufisadi Akaunti ya EPA, kashfa ya Richmond, Operesheni Tokomeza Ujangili na ile ya uchotaji mabilioni katika akaunti ya Escrow.
Operesheni Uhujumu Uchumi
Mwaka 1984 Serikali ilianzisha Operesheni Uhujumu Uchumi, iliyoongozwa na Waziri Mkuu wa wakati huo, Edward Sokoine ili kutaifisha mali ambazo baadhi ya watu walidaiwa kujipatia kwa njia isiyo halali.
Operesheni hiyo ilishuhudia baadhi ya watuhumiwa wakimwaga fedha mitaani na majalalani, huku wengine wakitupa mali kuhofia kutiwa kwenye mkono wa sheria.
Hata hivyo, katika operesheni hiyo baadhi ya watendaji wa Serikali ambao hawakuwa waaminifu, waliitumia nafasi hiyo vibaya kutaifisha mali za baadhi ya watu, ambao hawakuwa wahujumu uchumi.
Zoezi hilo lilisababisha wananchi kadhaa hasa vijijini kuwekwa ndani na wengine kuachwa maskini baada ya kunyang’anywa mali zao ikiwamo mifugo na mashine za kusaga nafaka, kwa kudaiwa kuwa walizipata kwa njia isiyo halali.Mfuko wa Commodity Import Support (CIS)
Miaka 24 baadaye yaani mwaka 2008, liliibuka sakata jingine lililokuwa na harufu kubwa ya ufisadi wa mabilioni katika Mfuko wa Kuwezesha Uagizaji Bidhaa kutoka Nje ya Nchi (Commodity Import Support – CIS).
Sakata hilo liliwahusisha baadhi ya wanasiasa, wafanyabiashara maarufu nchini na wizara kadhaa za Serikali ya Muungano na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).
Kupitia mfuko huo, vigogo hao walichota zaidi ya Sh200 bilioni kwa kivuli cha uagizaji bidhaa kutoka nje ya nchi.
Mfuko huo wa CIS, ulianzishwa katika miaka ya 1980, ambapo baadhi ya nchi wafadhili ikiwamo Japan, zililenga kuipatia Tanzania fedha za kigeni za kununulia malighafi, vyombo vya usafiri wa barabara, vifaa vya kilimo, ujenzi na vingine mbalimbali. Mpango huo ulioanzishwa na Serikali uliendelea hadi mwanzoni mwa miaka 2000, ambapo nchi hizo wahisani ikiwamo Japan, Uingereza, Uholanzi, Saudi Arabia, Norway, Uswisi, Ubelgiji, Sweden na Denmark zilikuwa zikiipatia Serikali fedha za kigeni ili kuimarisha sekta za biashara.
Wizara zilizotajwa katika orodha ya wadeni wa CIS ni pamoja na iliyokuwa ya Mawasiliano na Uchukuzi, Wizara ya Kazi, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Maji na Wizara ya Mambo ya Ndani kwa Tanzania Bara, wakati Zanzibar zinatajwa Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi na Wizara ya Maji.
Rada
Mwaka 2011 Serikali ilikumbwa na jinamizi la ufisadi kwa mara nyingine. Safari hii uliibuka ufisadi wa mabilioni ya shilingi kupitia ununuzi wa rada kuukuu kutoka Kampuni ya BAE Systems ya Uingereza. Ununuzi wa rada hiyo unatajwa kutofuata taratibu sahihi, uliligharimu taifa Sh29.5 bilioni, wakati gharama halisi ilikuwa Sh21 bilioni.
Serikali ya Uingereza iliamua kurudisha fedha hizo kama chenji, huku ikisisitiza kuwa watuhumiwa wote wa hapa nchini waliohusika na ununuzi wa rada hiyo mtumba, washitakiwe Tanzania au Uingereza kutokana na kubainika dosari kwenye ununuzi huo.
Wakati Uingereza ikitaka watuhumiwa hao wafikishwe mahakamani, mtandao wa Wikileaks unaosifika kwa kufichua siri za ndani ya mataifa mbalimbali duniani, ulibaini kuwepo kwa harakati nchini za kutowafikisha mahakamani wahusika wa ufisadi huo.

EPA
Mwaka 2008 iliibuka kashfa nyingine ya wizi wa mabilioni katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu (BoT), ambapo vigogo kadhaa walitumia mbinu chafu kuchota zaidi ya Sh133 bilioni katika akaunti hiyo.
Katika wizi huo ulioitikisa nchi, wahusika walitajwa kutumia vivuli vya siasa katika kupitisha nyaraka bila kufanyiwa uhakiki wa nyaraka hizo.

Richmond
Mwaka 2006 baada ya Rais Jakaya Kikwete kuingia madarakani kulitokea tatizo kubwa la uhaba wa umeme.
Hapo ndipo Serikali ilipoanza kufanya mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutafuta njia za dharura za kutatua tatizo hilo.
Waziri Mkuu wa wakati huo Edward Lowassa alikuwa mstari wa mbele katika mikakati hiyo ndipo Kampuni ya Richmond Development (LLC) ilipewa zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura na kuliuzia Shirika la Ugavi wa Umeme nchini Tanesco.
Hata hivyo, baadaye ilibainika kuwa kampuni hiyo haikuwa na uwezo wa kuzalisha umeme kama ilivyodhaniwa, badala yake kulikuwa na michezo michafu iliyofanyika kwa masilahi ya wafanyabiashara na baadhi ya viongozi wa Serikali.
Mwaka 2007, sakata hilo lilifika bungeni na aliyekuwa Spika wakati huo, Samuel Sitta aliunda kamati iliyokuwa chini ya mbunge wa Kyela, Dk Harrison Mwakyembe ili kuchunguza suala hilo.
Kamati hiyo ilichunguza sakata hilo na kutoa taarifa ilionyesha kuhusika kwa viongozi wa juu wa Serikali akiwemo aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa na kusababisha kiongozi huyo, kujiuzulu pamoja na mawaziri wawili kung’oka madarakani.
Waliong’oka madarakani ni mawaziri wa Nishati na Madini kwa vipindi tofauti, ambao ni Naziri Karamagi na Dk Ibrahim Msabaha.

Operesheni Tokomeza Ujangili
Operesheni Tokomeza Ujangili iliyoanzishwa na Serikali kupambana na ujangili wa wanyama nchini mwaka jana iliwang’oa madarakani mawaziri wanne ambao wizara zao zilielezwa kushindwa kusimamia vizuri utekelezaji wa operesheni hiyo.
Kung’oka kwa mawaziri hao kulitangazwa bungeni na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, aliyeeleza kuwa Rais Jakaya Kikwete ametengua uteuzi wao baada ya kuwasiliana naye kwa mashauriano akiwa nchini Marekani.
Mawaziri waliong’olewa kutokana na ripoti ya kamati hiyo iliyoongezewa shinikizo na michango ya wabunge wengi ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamisi Kagasheki na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi. Wengine ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David Mathayo.
Operesheni hiyo inadaiwa kukiuka haki za binadamu ikiwamo watu 13 na askari sita kuuawa, utesaji wa kutisha wa watuhumiwa, ubakaji, rushwa na uporaji wa mali za wananchi.
Akaunti ya Esrow
Wakati kashfa ya Richmond haijasahaulika, mapema mwaka huu imeibuka kashfa ya upotevu wa mamilioni ya fedha kwenye Akaunti ya Esrow katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Kashfa hiyo inayolitikisa Bunge na Serikali sasa, imetajwa kuwa ni mwendelezo wa jinamizi la kashfa ikiwa ya saba kubwa kulikumba taifa hadi sasa.
Akaunti hiyo iliyokuwa na zaidi ya Sh200 bilioni, ilifunguliwa wakati kukiwa kuna mgogoro wa kisheria baini ya wabia wa zamani wa IPTL (VIP Engeneering and Marketing na Mechmar Corporation ya Malaysia) kwa upande mmoja, Tanesco na Independent Power Tanzania, IPT, kwa upande mwingine.
Wadau kwenye akaunti hiyo hawakupaswa kuchukua kitu chochote hadi pale mgogoro utakapotatuliwa. Hata hivyo, kitita hicho cha fedha kilichotwa.
Wazungumza
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Emmanuel Mallya alisema matukio ya ufisadi yanaongezeka nchini kutokana na Serikali kushindwa kuweka bayana hatua zinazopaswa kuchukuliwa watu wanapatikana na makosa hayo, ili iwe fundisho kwa wengine.
Alisema kila mara wizi wa fedha za umma unapotokea, Serikali hupata kigugumizi kuwawajibisha wahusika, hatua inayowafanya watu wengi kuamini kushindwa kwao kunatokana na woga wa kutekeleza azma zao.
“Hakuna uwajibikaji kama mtu kafanya jambo fulani, kuna kulindana sana, lakini kama wote wangechukuliwa hatua za wazi pengine ufisadi usingekuwa wa kiwango cha juu namna hii,” alisema.
Mhadhiri
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, (UDSM) Faraji Christoms, alishauri wenye dhamana ya kusimamia masilahi ya taifa wanatakiwa kujitathmini upya.
Alitaja maeneo yanayohitajika kufanyiwa tathmini kuwa ni uzalendo kwa taifa, elimu kwa maana ya uelewa wa mambo ya kisheria, lugha za kimataifa na umakini wakati wa majadiliano ya kimataifa na wanaposoma mikataba ya aina hiyo.
“Unakuta mtu badala ya kutuliza akili akasoma kwa makini mkataba kabla ya kuusaini, anaupeleka kwa msaidizi wake ukisindikizwa na memo (agizo la maandishi) “Please read carefully for advice,” (tafadhali soma kwa makini, shauri),” alieleza Christoms.
Alisema katika mazingira hayo, hatima ya usalama wa mkataba huo unakuwa mikononi mwa mwingine, tofauti na aliyepewa dhamana.
Christoms alisema mazingira yanaonyesha kuwa wanasheria serikalini wanashindwa na walioajiriwa kwenye kampuni za uwakili, hivyo kusababisha Serikali kupata hasara kwa kuingia katika mikataba isiyo na masilahi kwa taifa.
Profesa Gaudence Mpangala, wa Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCO) alisema historia ya ufisadi nchini inamnyima mtu yeyote makini, ujasiri wa kuishauri Serikali mbinu za kudhibiti vitendo hivyo vya rushwa.
Profesa Mpangala alisema vitendo vya rushwa haviepukiki katika jamii, lakini Serikali inapochukua hatua zinazothibitisha kuwa inavipiga vita, hali inakuwa shwari tofauti na ilivyo nchini ambapo rushwa ndogo na ufisadi vimeota mizizi huku hatua zinazochukuliwa zikiacha maswali mengi bila majibu.
Alitoa mfano wa serikali ya awamu ya kwanza, ilivyoshughulikia rushwa iliyokuwa inaelekea kwenye ufisadi kwa kuchukua hatua kali, chini ya hayati Edward Sokoine na Mwalimu Nyerere ambapo waliothibitika kuhusika pamoja na adhabu ya kifungo jela, walitakiwa kuchapwa viboko wakati wa kuingia na kutoka gerezani.

Share this article :

0 comments:

Speak up your mind

Tell us what you're thinking... !

ZILIZOSOMWA SANA.

Followers

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Proudly powered by Blogger
Copyright © 2011. Msamaa. - All Rights Reserved
Template Design by Creating Website Published by Mas Template