Hofu ya Uislam Kuwa na Nguvu Zanzibar ya Serikali Tatu - Kitoloho
Headlines News :
Home » » Hofu ya Uislam Kuwa na Nguvu Zanzibar ya Serikali Tatu

Hofu ya Uislam Kuwa na Nguvu Zanzibar ya Serikali Tatu

Written By Msamaa on Thursday, April 17, 2014 | 2:37 AM



Written By Mohamed Said on Monday, February 17, 2014 | 6:10 AM
Hofu ya Uislam Kuwa na Nguvu Zanzibar ya Serikali Tatu

Kila siku nchini petu hukosi kukutana na mambo ambayo yatakushangaza pakubwa ukiwa wewe ni Muislam unaejitambua. Gazeti la leo la Mwananchi (Jumatatu, Februari 17 2014) uk. wa 3 kuna makala, ''Wasomi waianzia Rasimu ya Katiba Dar.'' Makali hii inaeleza kuwa wasomi na wanazuoni wapatao 300 wanakutana Dar es Salaam kujadili Rasimu ya Katiba. Wasomi hawa katika yote hofu yao iko katika Uislam. Wanauliza vipi Zanzibar ambayo ni nchi ya Waislam wengi kupita kiasi itajiepusha na udini? Hapa ndipo palipo cha kushangaza. Hivi huu udini ulifurtu ada Tanzania Bara hawa wasomi na wanazuoni hawauoni? Wao wenyewe katika hicho kikao chao hawajioni kuwa wako Wakristo watupu? Imekuwaje ikawa hivyo? Mbona hawajajiuliza vipi wao watajiepusha na udini? Lakini Waislam tujiulize kweli hii ni agenda ya kutia hofu udini wa Zanzibar katika serikali tatu ni agenda yao hawa wasomi au kuna mtu anaikoleza kwa kuilipia? Tujiulize swali lingine. Kwani Uislam kuwa na nguvu Zanzibar hairuhusiwi? Haiyumkiniki ikawa leo Wazanzibari watatishwa na Uislam unaoshamiri katika jamii. Huyu anaetishwa na Uislam Zanzibar kiasi cha kukosa usingizi ni nani? Waarabu wana msemo, ''Ukiijua sababu ile ajabu inaondoka.'' Kumbe siku zote hizi vurugu zote na mauaji Zanzibar kinachowatisha ni kuwa utaingia uongozi ambao utaharibu maslahi ya Kanisa....
Annur Ilipozungumza Mwaka 2000

Vurugu za kisiasa Zanzibar: 
Serikali ya Mkapa inawasha moto ambao haitaweza kuuzima

MZIMU wa uhasama wa kisiasa na kijamii uliovikumba visiwa vya Zanzibar baada ya uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyamavingi Oktoba 25, 1995 bado unaendelea kuviandama visiwa hivyo.
Tukiwa tumebakiza muda mfupi kufikia siku ya uchaguzi mkuu wa pili wa vyama vingi wa Oktoba 29, 2000 zimeanza kuonekana dalili za kuibuka kwa mgogoro mkubwa wa kisiasa na kijamii. Mgogoro mkubwa wa kisiasa unovinyemelea visiwa vya Zanzibar unatokana na kuwepo kwa ukiukwaji wa makusudi wa sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi unaofanywa na serikali ya CCM kupitia vyombo vyake vya dola. Serikali ya Mkapa inaonekana imedhamiria kumpeleka Karume Ikulu kwa njia yoyote ile, hata kama ni kwa njia isiyo halali kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi zilizowekwa. Nia ya Seriakali kumpeleka Ikulu kinyume cha sheria mgombea wa Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Amani Karume imeanza kujionyesha kuanzia kwenye zoezi la uandikishaji wapiga kura lililoanza Agosti 8, 2000 na kumalizika Agosti 21,2000. Kwa mfano, serikali ya Mkapa ilipeleka vikosi vingi vya polisi na ulinzi visiwani Zanzibar mara tu baada ya kuanza kwa uandikishaji wapiga kura kwa kisingizio cha kuimarisha ulinzi na usalama ili kudumisha amani na utulivu wakati wa uchaguzi. Lakini yapo madai kuwa polisi hao wamepelekwa visiwani Zanzibar kujiandikisha kupiga kura ili kumnufaisha mgombea wa CCM.

Imedaiwa kuwa askari hao wameandikishwa kupiga kura kwenye makambi yao, na raia wa kawaida pamoja na wawakilishi wa vyama vya siasa hawakuruhusiwa kusogelea vituo hivyo. Zipo habari zinazosema kuwa polisi hao waliopelekwa Zanzibar walitumiwa kuwazuia kujiandikisha kupiga kura wanachama na wafuasi wa CUF. Mbali na hilo, polisi pia walitumiwa kuwanyanyasa na pengine kuwafukuza toka vituoni wawakilishi wa chama cha CUF. Vile vile zipo taarifa za kuaminika zinazosema kuwa tangu kuanza kwa zoezi la uandikishaji wapiga kura visiwani Zanzibar Polisi wamekuwa wakiwanyanyasa na kuwakamata bila sababu za msingi wanachama na wafuasi wa CUF. Taarifa zinasema kuwa mpaka sasa zaidi ya wana-CUF 300 waliwahi kukamatwa. 
Yapo madai kuwa wamepelekwa wapiga kura bandia toka Tanzania Bara. Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) haijasema imechukua hatua gani kuwazuia mamluki hao wasitekeleze mpango wao.
Vitendo vya polisi kuwanyanyasa viongozi na wanachama wa CUF havijaishia kwenye zoezi la uandikishaji wapiga kura tu, bali vinaendelea kwa kasi na nguvu kubwa zaidi wakati huu wa kampeni za uchaguzi. Polisi wameripotiwa kuendeleza vipigo na kamatakamata za bila sababu miongoni mwa viongozi na wanachama wa CUF. Pamoja na ukweli kuwa katiba na sheria za Tanzania na Zanzibar zote zinaruhusu uhuru wa kukutana, uhuru wa kukusanyika na kampeni za nyumba kwa nyumba, polisi wameripotiwa kuwazuia wana CUF kukutana na kukusanyika wakiwa zaidi ya watu watatu kwa madai kuwa kufanya hivyo ni kukusanyika bila kibali kinyume cha sheria. Polisi wamewazuia wana CUF kutembea wakiwa kwenye makundi ya zaidi ya watu watatu kwa madai kuwa kufanya hivyo ni kuandamana bila kibali kinyume cha sheria, lakini wana CCM wanaruhusiwa. 
Polisi wameanzisha zoezi la kuwapekua wana CUF wote wanaokwenda kwenye mikutano yao ya kampeni kwa madai kuwa wamekuwa wakienda mikutanoni na silaha kama vile visu na mawe, lakini upekuzi huo haufanywi kwa wana CCM. Na la kutisha zaidi kuhusu hali ya baadaye ya Zanzibar ni wimbi la maaskari wa Jeshi la wananchi kutoka bara kupelekwa Unguja na Pemba ikidaiwa ni uhamisho wa kikazi. Kusema kweli hali ya kisiwa visiwani Zanzibar ni tete. Matumizi ya nguvu yanayofanywa na polisi dhidi ya wana CUF ni ya kutisha. Vitendo wanavyotendewa wana CUF na polisi havitofautiani na vitendo walivyokuwa wanatendewa wazalendo wa Afrika ya Kusini na polisi wa Makaburu, vitendo vilivyopingwa na kulaaniwa na mataifa mengi duniani yakiongozwa na Tanzania. Ni jambo la aibu sana leo kuona hali kama hio inatokea Tanzania na Afrika Kusini wanafurahia uhuru wao.

Hali ya sasa ya kisiasa visiwani Zanzibar inachochewa na matumizi ya nguvu kuzidi kiasi yanayoendeshwa na polisi dhidi ya CUF. Uhasama uliokuwepo kati ya wana CUF na wana CCM sasa umekuwa kati ya polisi na CUF hali mbaya zaidi itakayosababisha janga la kisiasa na jamii. Wana CUF wanaliona jeshi hilo kama jeshi la CCM kutokana na kuwapendelea wana CCM. Polisi sasa hawana tofauti na vile vikosi vya vijana wa CCM vya maskani ambavyo vimekuwa na uhasama mkubwa na vijana wa "Blue Guards" wa CUF. Kwa jinsi hali mbaya ya kisiasa ilivyo ni vigumu kujua mustakabali wa visiwa vya Zanzibar. Hakuna dalili kama hali ya kisiasa visiwani Zanzibar itakuwa shwari siku za usoni kutokana na serikali kujihusisha kikamilifu na vurugu hizo. Kauli za ubabe na kejeli dhidi ya wapinzani zinazoendelea kutolewa na viongozi waandamizi wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wakiongozwa na Rais mwenyewe zina madhara makubwa. Pia kauli ya baadhi ya viongozi kwamba majeshi ya ulinzi na usalama yameandaliwa vya kutosha kupambana na wapinzani kwa kutumia vifaru vya kijeshi ni ya kushitua na kusikitisha sana.

Hali inakuwa mbaya zaidi pale inapoonekana kuwa wanaCUF wamefikia kikomo cha uvumilivu na sasa wako tayari kwa lolote. Kwa jumla jamii ya Wazanzibari inaelekea kwenye mgogoro mkubwa wa kisiasa na kijamii ambao haujapata kutokea katika historia ya jamii hiyo baada ya mapinduzi ya umwagaji damu ya 1964. Kwa Mtanzania yeyote anayekereketwa na kuheshmu haki za binadamu, hasa haki ya kuishi hapaswi kushangilia vitendo vya kikatili vinavyofanywa na serikali dhidi ya wapinzani kupitia jeshi la polisi. Watanzania tunapaswa kuacha kushangilia vitendo hivyo eti tu kwa sababu vinawapata wapinzani wetu kisiasa. Tukumbuke kuwa matokeo au athari za mgogoro wowote katika jamii huwapata watu wote bila kujali vyama vyao. Mgogoro wa kisiasa utakaoibuka Zanzibar utawadhuru wana CCM na wana CUF na hautakuwa wa Wazanzibari peke yao bali utasambaa kwa Watanzania wote na hivyo kuisambaratisha nchi.Pia nawakumbusha viongozi wa serikali kuwa mgogoro wanaoupalili visiwani Zanzibar una madhara hata kwao kwani pamoja na kuwa wanaweza kuendelea kutawala, lakini hawatawatawala kwa raha kama ilivyo sasa.
Imekwishathibitika duniani kuwa hakuna jeshi la serikali linaloweza kupigana vita vya wenyewe kwa wenyewe na kushinda. Mifano ni Msumbiji, Angola, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Rwanda, Burundi, Uganda, Sudan, Liberia, Algeria, Sierra Leone na kwingineko. Kinga ni rahisi kuliko kuponya. Serikali iliyoko madarakani ndio pekee yenye uwezo wa kuzuia jambo baya lisiipate Zanzibar na Tanzania kwa ujumla. Serikali inatakiwa kuthamini maisha ya watu wake kwa kuwaepusha na vita vinavyonukia sasa ili kuhakikisha kuwa maelewano ya kisiasa na kijamii yanarejea visiwani Zanzibar ni muhimu viongozi wa serikali iliyoko madarakani wawe na dhamira ya kisiasa (political will). Dhamira ya kisiasa ni muhimu sana katika kufanikisha mambo mengi. Dhamira ya kisiasa huwezesha kujenga uhusiano wa usawa kati ya vyama vya siasa. Dhamira ya kisiasa huwafanya viongozi wa chama tawala wakubali ukweli kuwa katika mfumo wa vyama vingi, kila chama kina nafasi sawa ya kuweza kuchaguliwa na kuunda serikali, na kwamba hakuna chama chenye haki ya kuendelea kutawala milele, isipokuwa tu ikiwa haki hiyo inatokana na ridhaa ya wananchi kutokana na uchaguzi huru na wa haki (uchaguzi unaoendeshwa katika mazingira ya haki, usawa na uhuru kwa wote wanaojishirikisha na uchaguzi huo), hivyo wakubali kushindwa kama inatokea kuwa hivyo. Mlolongo wa matukio ya kuvunja sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi unaofanywa na serikali kwa makusudi ya kupata ushindi unaonyesha jinsi gani serikali iliyopo madarakani isivyo kuwa na dhamira ya kisiasa, na hivyo haiko tayari kukubali kushindwa.
Pia serikali ya CCM inatakiwa kuviamini vyama vingine juu ya suala la muungano ambalo linaonekana kuwa sababu ya CCM kuendelea kuulinda na kuudumisha muungano huo. Kimsingi hakuna chama chenye wazo la kuuvunja muungano huo pindi kikichaguliwa kuongoza, bali tofauti iliyoko kati ya CCM na vyama vya upinzani juu ya muungano ni muundo wa muungano huo, jambo linaweza kumalizwa kwa majadiliano kati ya wananchi wa Tanganyika na Zanzibar. CCM haiwezi kuulinda muungano kwa mtutu wa bunduki, mifano imeonekana sehemu nyingi duniani kama Urusi ya zamani, Yugoslavia, Ethiopia, Timor ya Mashariki na sehemu zingine nyingi waliojaribu kulinda miungano yao kwa bunduki. Jambo lingine muhimu ambalo CCM inatakiwa kufanya ni kutangaza hadharani kama itakubaliana na matokeo yoyote ya uchaguzi ujao, ili kuondoa uvumi ulioenea kuwa CCM haiwezi kukubali kuachia madaraka hata kama kitashindwa. Rais Mkapa atoe kauli hadharani kuwa akishindwa uchaguzi atakabidhi madaraka kwa aliyemshinda.

Ikumbukwe kuwa uvumi huu unapata nguvu kutokana na historia ya CCM katika uchaguzi wa 1995 ambapo ilitangaza kutoyatambua matokeo yalioonyesha kuwa chama cha CUF kilikuwa kimeshinda uchaguzi huo, lakini baadaye kikayakubali matokeo yaliyokirudisha chama hicho madarakani. Jambo hilo lilithibitisha kuwa CCM haiwezi kukubali kushindwa hata kama kweli itatokea hivyo. Msimamo wa CUF unaeleweka. CUF ilikwisha tangaza kuwa ipo tayari kukubaliana na matokeo yoyote ya uchaguzi ikiwa tu chama hicho kitathibitishiwa kwa vitendo na serikali ya CCM kuwa uchaguzi ujao utakuwa huru na wa haki. Na ikaongeza kuwa haiwezi kuvumilia ikiwa itadhulumiwa ushindi wake kama ilivyotokea mwaka 1995 kwa Zanzibar. Ni ada kwetu kunena, lakini watekelezaji wa ushauri huu ni serikali ya CCM. Serikali ya  CCM ndio mwamuzi wa mustakabali wa nchi. Lakini serikali lazima ikumbuke kuwa moto inaouwasha haitaweza kuuzima baadaye kama itauacha sasa ukolee.


Share this article :

0 comments:

Speak up your mind

Tell us what you're thinking... !

ZILIZOSOMWA SANA.

Followers

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Proudly powered by Blogger
Copyright © 2011. Kitoloho - All Rights Reserved
Template Design by Creating Website Published by Mas Template