MAKOMBORA ZA LISSU MOTO - Kitoloho
Headlines News :
Home » » MAKOMBORA ZA LISSU MOTO

MAKOMBORA ZA LISSU MOTO

Written By Msamaa on Thursday, April 17, 2014 | 1:58 AM


§  TBC yamzimia matangazo ya moja kwa moja
13/04/2014 Posted by Salehe Mohamed | Tanzania Daima


MAKOMBORA ya maneno yaliyokuwa yakitolewa na msemaji wa taarifa ya wachache bungeni, Tundu Lissu, juu ya muundo wa muungano, hati na nukuu mbalimbali za viongozi wa kitaifa yalisababisha kuvunjika kwa kikao cha Bunge Maalumu.
Kuvunjika kwa Bunge hilo kulitokana na taarifa zilizotolewa kwa Mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta, kuwa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) lenye vituo vya redio na runinga limekatisha matangazo ya moja kwa moja (live).
Mjumbe wa Bunge Maalumu, Freeman Mbowe, ndiye aliyeanzisha hoja hiyo baada ya kusimama na kuomba mwongozo wa Mwenyekiti wa Bunge juu ya hatua hiyo ya TBC kukatisha matangazo yake wakati Lissu akitoa ufafanuzi wa taarifa ya walio wachache.
Mbowe alisema mjadala wa Katiba mpya ni muhimu kwa taifa lakini kituo cha runinga cha TBC ambacho ni cha taifa kimekatisha matangazo ya moja kwa maoja, jambo linalowanyima fursa wananchi kujua kinachoendelea bungeni.
“Mheshimiwa Mwenyekiti naomba mwongozo wako ni hatua au jambo gani tutalifanya baada ya televisheni na radio ya taifa kukatisha matangazo ya moja kwa moja ambayo imekuwa ikiyafanya tangu tuanze mkutano huu,” alisema.
Akijibu mwongozo huo Sitta, alisema kuwa taarifa hiyo inashtua kwakuwa Bunge limeingia mkataba na serikali na TBC unaotaka matangazo ya vikao vya Bunge ni lazima yaonekane na kufika kwa wanachi.
Sitta, alisema walifanya hivyo kwa kuwa mchakato wa uandikaji wa Katiba mpya ni shirikishi hivyo wananchi wana haki ya kushiriki na kujua kila kinachofanyika ndani ya Bunge.
“Naomba Katibu achunguze mara moja kuhusu kukatishwa kwa matangazo ya TBC tujue kuna tatizo gani kwakuwa jambo hili linawanyima wananchi haki za kusikia na kuona kile kilichotokea hapa bungeni,” alisema.
Mara baada ya taarifa hiyo, Sitta aliwataka wajumbe watulie kwa muda afuatilie jambo hilo na atawapa taarifa baada ya muda mfupi.
Baada ya dakika chache Sitta aliwaambia wajumbe kuwa amepata taarifa  kwamba hali ya hewa Dar es Salaam ni mbaya kutokana na mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha hivyo kuathiri matangazo ya moja kwa moja ya vituo vya runinga na radio vya TBC .
Sitta alisema kutokana na kukatika huko kwa matangazo ya moja kwa moja, Bunge Maalumu haliwezi kuendelea na mijadala yake kwa kuwa wananchi watakosa fursa ya kuona na kusikia kile kilinachojadiliwa.
“Kwa sababu yoyote ile hatuwezi kuendelea, natoa maelekezo kwa Katibu kuangalia muda ambao matangazo yaliyokatika na alipoishia Lissu, wakati jambo hilo likitokea….., ninawahakikishia tukianza kikao Jumatatu mtu wa kwanza atakuwa  Tundu Lissu,” alisema.
Mara baada ya kutoa kauli hiyo wajumbe kutoka vyama vya upinzani walikuwa wakishangilia huku wengine wakipiga vigeregere na kuimba: “Sitta….Sitta….Sitta wewe ni Mwenyekiti wa viwango na leo ndiyo umetuonyesha viwango vyako.”
Uamuzi huo, ulionekana kumkera Hamisi Kingwangala, ambaye alisimama na kutaka utaratibu akitumia Kanuni ya 52, (8),  kuhoji  kanuni ipi iliyotumiwa na Sitta kuahirisha Bunge kabla ya muda unaotakiwa ilhali pia halikuwa limemaliza shughuli za siku husika.
Kigwangala alisema Kanuni ya 32 inazungumzia mijadala au ufafanuzi wa taarifa za kamati lakini hakuna hata eneo moja linataja kuwa shughuli za Bunge zinaweza kuahirishwa kwa sababu ya kituo fulani hakijaonyesha matangazo ya moja kwa moja.
Kauli hiyo iliwafanya wanjumbe wenzake wamzomee huku wakimuita msaliti lakini Kingwangala aliwajibu: “Haya ndiyo matatizo ya Bunge Maalumu kuwa na wanasiasa makanjanja.’
Sitta amkata maini
Akitolea ufafanuzi Mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta, alisema jambo linalofanyika hivi sasa katika Bunge Maalumu ni kubwa sana ndiyo maana limewekewa bajeti ya kuwashirikisha kwa kupitia vyombo vya umma vinavyolipwa fedha.
“Wananchi wanaofuatiliana kwa hamu yanayotokea hapa ndiyo maana tunasema Bunge Maalumu ni shirikishi sasa kama wananchi hawaoni huo ushirikishi unatoka wapi?
“Mimi nataka kutenda haki na ionekane imetendeka, hivi matangazo yamekatika na watu hawaoni utawezaje kuzuia hisia za wengine kutotendewa haki?  Tukiendelea itatafsiriwa kuna ubaguzi fulani….mimi sitaki niwe mbaguzi, nimeapa kutenda haki,” alisema.
Sitta alibainisha kuwa ametumia kanuni ya 85 ambayo inampa mamlaka mwenyekiti kuamua jambo au kuvunja kanuni kutokana na sababu mbalimbali.
“Mimi nataka kutenda haki, msemaji yeyote ikitokea hali kama ya leo nitasitisha kidogo na tutaendelea tena hapo baadaye…. katika kulifanya hilo sitajali vyeo au kundi fulani,” alisema.
Mara baada ya kauli hiyo ukumbi wa Bunge ulilipuka kwa vifijo na vigeregere kutoka kwa wajumbe waliokuwa wakimshangilia Sitta, kwa uamuzi waliouita wa busara.
Hoja za Lissu
Awali Lissu wakati akianza kusoma maoni ya walio wachache, yaliyokuwa yametawaliwa na nukuu za viongozi mbalimbali pamoja na vitabu alivyokuwa navyo, alisema waliozoea vya kunyonga vya kuchinja hawawezi, waliozoea vya haramu vya halali hawawezi.
Alisema walipeleka mapendekezo kwamba maoni ya wachache yasomwe na wachache lakini waliozoea vya haramu wakayakataa kwa hoja kuwa wanataka wayasome wao kama watakavyosoma yao.
Kauli hiyo ilimfanya Sitta, kumkatisha na kumtaka aache kuwatuhumu wenzake waliomo ndani ya ukumbi wa Bunge ambao wamekwenda pamoja.
“Sisi sote tumekuja pamoja kuwaita wengine kuwa wamezoea vya haramu unaamua wewe, hututendei haki hata kidogo kwasababu ya usioelewana nao basi wamezoea vya haramu, sasa mjadala hauwezi kwenda hivyo, ondoa hayo maneno ya waliozoea vya haramu,” alisema Sitta.
Baada ya maelekezo hayo Lissu alikubali kuyaondoa na kuingiza mengine ambapo alisema waliozoea kuishi kwa uongo na udanganyifu hawawezi kujifunza kuishi katika kweli.
Lissu alisema Katika kitabu kinachoitwa Panafricanism cha Profesa Issa Shivji katika ukurasa 93 wa kitabu chake amesema kwamba hati ya makubaliano ya muungano haikuwahi kuthibitishwa na Baraza la Wawakilishi Zanzibar kwa miaka yote 50 tangu muungano uzaliwe.
“Alibainisha kuwa nyongeza zote za mambo ya muungano tangu mwaka  64 hadi leo ni haramu na ni batili lakini leo Shivji ndiye mpiga debe mkubwa wa CCM na muungano huu wa serikali mbili, mfano wa pili uko katika kitabu kinaitwa ‘Tanzania’s 8th Constitutional Amendment and its implications of constitutionalism democracy and union question,’ kilichoandikwa na Dk. Mwakyembe 1995”
Alibainisha kuwa Dk. Mwakyembe, aliandika kitabu hicho kama sehemu ya shahada yake ya uzamivu ya Chuo Kkikuu cha Humbarg, Ujerumani na kwenye kitabu chake alisema kuwa hoja ya Dkt. Wolfgang Dourado kuhusu muungano kiuhalisia hati ya makubaliano ya muungano ilitengeneza muundo wa serikali 3 lakini utekelezaji wake umekuwa tofauti, ukurasa wa 184.
Lissu alibainisha kuwa kwenye ukurasa 195 Dk. Mwakyembe, alisema mfumo wa shirikisho la serikali 3 kama ilivyopendekezwa na tume ya Nyalali na kuungwa mkono na vyama na makundi ya upinzani unaonekana ndio njia pekee katika hali ya sasa ya Tanzania.
Alisema kitabu hicho kinasema mfumo huo unaweza kutoa kile ambacho kimekosekana kwa utaratibu wa sasa yaani wa wazi wa mamlaka kati ya nchi washirika na kati ya muungano na washirika wake.
Lissu alisema Dk. Mwakyembe ni mjumbe wa kamati namba 4 aliyomo yeye na ni mmoja wa wajumbe walio wengi katika kamati hiyo wamekataa shirikisho na wamekataa muundo wa serikali 3, ambao wamezoea kuishi kwa uongo hawawezi kujifunza kusema ukweli.
Aliongeza kuwa mfano wa tatu unahusu walioandika kitabu kitachoitwa ‘Mali kuhusu rasimu ya katiba’ na kimeandaliwa na wahadhiri wa sheria wa vyuo vikuu 15 vya Tanzania ambapo katika ukurasa wa pili wa kitabu wamejadili rasimu hiyo inayobeba muundo wa serikali tatu wanayoitaka wananchi na wanaunga mkono muungano wenye muundo wa shirikisho lenye serikali tatu.
Alibainisha kuwa mfano wa nne unamuhusu baba wa taifa, Julius Nyerere mwaka 1968, akizungumza na gazeti la Observer la London alizungumzia habari za muungano kwa maneno kuwa iwapo uma wa Zanzibar bila ya ushawishi kutoka nje na kwa sababu zao wenyewe wataona kuwa muungano una hasara kwa uhai wao hatowapiga mabomu, kuwalazimisha, muungano utakuwa hauna tena sababu ya kuendelea iwapo washiriki wake wataamua kuukana.
Lissu aliongeza kuwa mwaka 1984 Wazanzibari  walipohoji muungano Alhaji Abood Jumbe akafukuzwa kazi amewekwa kizuizini katika eneo la Mji Mwema jijini Dar es Salaam anakoishi mpaka sasa huku  Wolfgang Dourado akawekwa kizuizini na baadaye kupelekwa Ghana.


Share this article :

0 comments:

Speak up your mind

Tell us what you're thinking... !

ZILIZOSOMWA SANA.

Followers

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Proudly powered by Blogger
Copyright © 2011. Kitoloho - All Rights Reserved
Template Design by Creating Website Published by Mas Template