Zanzibar na Bajeti ya 2014/2015 - Kitoloho
Headlines News :
Home » » Zanzibar na Bajeti ya 2014/2015

Zanzibar na Bajeti ya 2014/2015

Written By Msamaa on Thursday, May 15, 2014 | 12:21 AM



Zanzibar.
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) jana iliwasilisha bajeti yake ya Sh708.8 bilioni kwa mwaka 2014/2015 ambazo ni pungufu mara 28 ya Bajeti ya Jamhuri ya Muungano ya Sh19.7 trilioni inayotarajiwa kuwasilishwa mwishoni mwa Juni mwaka huu.
Sambamba na bajeti hiyo, SMZ imetangaza mikakati ya kukusanya fedha hizo kwa kupandisha kodi za leseni za udereva na ada ya usafiri wa anga kwa wasafiri wa ndani.
Waziri wa Fedha wa SMZ, Omar Yussuf Mzee alitangaza mpango huo jana alipowasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali katika kikao cha Baraza la Wawakilishi kinachoendelea Chukwani, Unguja.
Waziri Mzee alisema ili kuimarisha uwezo wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar na kutoa huduma bora, wasafiri wa ndani watalazimika kulipa Sh3,000 badala ya 1,000 na mabadiliko hayo hayatawahusu wasafiri wa nje ya nchi ili kutoathiri sekta ya utalii visiwani.
Pia ada za leseni ya udereva kwa miaka miwili italipwa kwa Sh35,000, miaka mitatu Sh45,000 na kwa miaka mitano kwa Sh60,000.
Alisema SMZ imeamua kufuta utaratibu wa kila mwaka kwa madereva kulipia leseni ili kuwaondolea usumbufu na sasa kuweka utaratibu wa kukata leseni za muda mrefu na utekelezaji wake utaanza mwaka huu wa fedha.
EFD zaingia Zanzibar
Pia Waziri Omar alisema ili kudhibiti ukwepaji kodi, SMZ inatarajia kuanzisha utaratibu wa stakabadhi kutolewa kwa mashine maalumu za (EFD) na wafanyabiashara wote watalazimika kuwa na mashine hizo kwenye maduka yao ambazo zitasaidia biashara kufanyika kisasa na kudhibiti mapato ya Serikali.
Hata hivyo, alisema bajeti ya mwaka huu ina nakisi ya Sh36 bilioni na kwamba Serikali itaziba pengo hilo kupitia mapato yatakayokusanywa kutokana na Kodi ya Wafanyakazi (Paye) wa Muungano walioko Zanzibar na Sh21 bilioni zitakusanywa kutoka vyanzo hivyo na Sh15 bilioni zitatokana na mikopo ili kuleta uwiano wa bajeti, mapato na matumizi yake.
Pia alisema Pato la Taifa limekua kutoka Sh1,342.6 bilioni mwaka 2012 hadi kufikia Sh1, 442.8 bilioni wakati pato la mtu binafsi limekua kwa asilimia 4.6 kutoka Dola za Marekani 656 hadi Dola 667 mwaka 2013.
Kuhusu deni la Taifa, Waziri Mzee aliwaeleza wajumbe wa Baraza hilo kwamba limeongezeka na kufikia Sh294.90 bilioni sawa na ongezeko la asilimia 17.0 ikilinganishwa na deni la Sh252.3 bilioni lilikuwapo hadi Machi mwaka jana.
Share this article :

0 comments:

Speak up your mind

Tell us what you're thinking... !

ZILIZOSOMWA SANA.

Followers

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Proudly powered by Blogger
Copyright © 2011. Kitoloho - All Rights Reserved
Template Design by Creating Website Published by Mas Template