WAKATI Katibu wa Jumuia na Taasisi za Kiislam, Sheikh Ponda
Issa, akilazwa katika Kitengo cha Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI)
kutibiwa jeraha alilodai kupigwa risasi na polisi, jeshi hilo limemruka.
Licha ya polisi kukwepa kumjeruhi kiongozi huyo, taarifa zinadai kuwa
yalikuwepo mawasiliano baina yao mkoani Morogoro kuhusu Ponda kuhudhuria
mhadhara ulioandaliwa na taasisi ya masheikh.
Akizungumza hospitalini hapo jana, mpwa wa Sheikh Ponda, Is-haq Rashid
alidai mjomba wake hakuwahi kupata wito wowote wa kuhitajika polisi
kabla ya tukio la kupigwa risasi.
Alisema kuwa hata waliposikia taarifa za kutafutwa kwake katika vyombo
vya habari walimuuliza Sheikh Ponda kama alishapewa taarifa hizo
kisheria.
Alifafanua kuwa Ponda aliwaeleza kuwa hajawahi kupata wito wowote
kutoka polisi wala ujumbe wa kuitwa kupitia kwa mwanasheria wake hali
iliyomfanya aendelee na ratiba yake ya kutembelea misikiti mbalimbali
baada ya kutoka gerezani.
Mpwa huyo aliongeza kuwa katika kudhihirisha Ponda hakuwa mtu wa
kujificha kama ilivyoelezwa na polisi, siku ya Idd Mosi alishiriki
mhadhara wa wazi kwenye msikiti wa Kichangani na siku iliyofuata
aliwasili mkoani Morogoro huku polisi wakiwa na taarifa zake.
“Walioandaa mkutano waliwaeleza polisi mkoani Morogoro juu ya Sheikh Ponda kuhudhuria na kuwa mgeni rasmi.
“Sasa tunashangaa kwa nini walitumia njia hiyo ya kumpiga risasi kwa
kweli hatujui dhamira yao ilikuwa ni ipi,” alisema Is-haq.
Aliongeza kuwa baada ya Ponda kupigwa risasi kulikuwa na mabishano
baina ya mfyatua risasi hiyo aliyevalia kiraia na askari waliovaa sare
hali inayowathibitishia kuwa risasi hiyo ilitoka kwa mmoja wa askari
waliolizunguka gari alilopanda mjomba wake.
“Kinachotusikitisha ni kauli ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro,
Faustine Shilogile, kuwa ndugu yao hakupigwa risasi na polisi na wala
jeshi hilo halimjui aliyerusha risasi hiyo,” alisema.
Akielezea tukio hilo, Is-haq alisema baada ya Ponda kumaliza mhadhara
na kuondoka, magari matatu ya polisi yaliizingira gari lake hali
iliyomfanya atelemke.
Baada ya kutelemka, mmoja wa askari alimpiga risasi iliyomfanya
aanguke chini na muda huo kukawa na mgongano baina ya mrushaji na
wenzake kisha watu walimuokota Ponda na kumuwahisha hospitali ya mkoa wa
Morogoro.
“Alipofikishwa hospitali askari walikuwa wengi na kwa kuwa wananchi
walioshuhudia tukio lile walishakuwa na wasiwasi, alitolewa pale na
kupelekwa katika zahanati binafsi kabla ya kufikishwa jana MOI,
Muhimbili, Dar es Salaam,” alisema.
Is-haq alidai kuwa baada ya tukio hilo polisi waliweka ulinzi na
kukagua kila gari lililokuwa likielekea jijini Dar es Salaam na kwamba
hata wao walikuwa katika hali ya taharuki bila kufahamu alipo Ponda hadi
walipopigiwa simu jana kuwa yuko Magomeni katika moja ya teksi.
Kwa mujibu wa mmoja wa wafanyakazi wa hospitali hiyo ambaye hakutaka
kutaja jina lake, Ponda amepasuka mfupa mkubwa wa upande wa mkono wa
kulia ambapo kwa wakati huo ulikuwa ukifanyiwa upasuaji.
Polisi waruka
Msemaji wa polisi, Advera Senso, katika taarifa yake kwa vyombo vy
habari alisema kuwa kongamano hilo lilifungwa saa 12:05 jioni amabpo
watu walianza kutawanyika na baadhi yao wakiwa wamezingira gari dogo
alilokuwa amepanda Sheikh Ponda.
“Baada ya kutoka eneo hilo, askari walilizuia gari hilo kwa mbele kwa
nia ya kumkamata Ponda ambaye mpaka sasa anatuhumiwa kwa kosa la kutoa
maneno ya uchochezi sehemu mbalimbali nchini yenye lengo la kuvunja
amani.”
“Baada ya askari kutaka kumkamata, wafuasi wake waliwazuia kwa
kuwarushia mawe askari. Kufuatia purukushani hiyo, askari walipiga
risasi hewani kama onyo la kuwatanwanya,” alisema.
Senso aliongeza kuwa katika vurugu hizo, wafuasi wa Ponda walifanikiwa
kumtorosha mtuhumiwa huyo na kwamba sasa imethibitika yuko Muhimbili
akitibiwa jereha katika bega linalodaiwa alilipata katika purukushani
hiyo.
Alisema kuwa timu inayowashirikisha wajumbe kutoka jukwaa la haki
jinai ikiongozwa na Kamishna Issaya Mungulu imeanza kufanya uchunguzi wa
tukio hilo.
Nao Umoja wa Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania (Hay – atul Ulamaa),
umeeleza kupokea kwa masikitiko makubwa habari za kushambuliwa na
kujeruhiwa kwa Sheikh Ponda.
Katika taarifa yao kwa vyombo vya habari jana, mwenyekiti wa umoja
huo, Sheikh Suleiman Kilemile, alisema Hay-atul Ulamaa, inaumia,
kushtusha na kuwa na fadhaa kama jamii nzima ilivyoshtushwa na matukio
mengine kama hili hapa nchini.
Tukio hilo linaashiria kuwa waliolitenda hawaitakii mema amani ya nchi yetu.
Chanzo:Tanzania Daima Jumatatu 12 Agost 2013.
|
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !