Ugonjwa wa Dk. Mwakyembe
Januari 3, 2012
HALI ya afya ya Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe,
ilikuwa inasikitisha kwani licha ya kupata matibabu nchini India na
kuendelea na tiba hiyo hapa nchini, hali yake haikuwa ya kuridhisha
kutokana na kunyonyoka nywele, kope, ndevu na vinyweleo vyote.
Majambazi yateka ndege
Januari 5, 2012
WATU wanne wanaosadikiwa kuwa majambazi wakiwa na silaha nzito za
kivita, walivamia Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) na kuiteka ndege ndogo
iliyokuwa imebeba dhahabu kwa ajili ya kuisafirisha kwenda nje ya nchi.
Madaktari 229 wafukuzwa Muhimbili
Januari 6, 2012
UONGOZI wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) uliwafukuza kazi
madaktari 229 waliokuwa katika mafunzo kwa njia ya vitendo kutokana na
mgomo wa siku nne wakishinikiza kulipwa posho zao za mwezi mmoja.
Umeme bei juu
Januari 14, 2012
WAKATI gharama za maisha kwa Watanzania wengi zikizidi kupanda kila
siku, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA),
iliidhinisha ongezeko la bei ya umeme kwa asilimia 40.29 kwa Tanzania
Bara na asilimia 28.21 kwa Zanzibar kuanzia Januari 15, 2012.
Askari aua nduguze na kujiua
Januari 22, 2012
ASKARI polisi wa kituo cha Magomeni jijini Dar es Salaam, Nicodemas
Senge (43), amewaua ndugu zake wawili na kisha kujiua kwa kujipiga
risasi wakati wakiwa kwenye kikao cha usuluhishi wa mgogoro wa ardhi ya
kijijini kwao Singida.
Madaktari waanza mgomo nchi nzima
Januari 23, 2012
JUMUIYA ya Madaktari Nchini, ilianza mgomo nchi nzima hadi pale
ambapo serikali ingeliridhia kulipa madai yao ndipo madaktari
wangelirudi kuendelea na kazi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Madaktari, Dk. Ulimboka Stephen, alisema mgomo
huo ungelikuwa wa nchi nzima kwa madaktari kutotoa huduma.
Wanafunzi wanane wafa maji Arusha
Februari 28, 2012
WANAFUNZI wanane kati ya kumi wa Shule ya Msingi Piyaya, wilayani
Ngorongoro, mkoani Arusha, walifariki baada ya kusombwa na maji ya
mafuriko ya Mto Radiru wakati wakitoka shuleni, jioni majira ya saa
11:30.
Azikwa akiwa hai
Aprili 29, 2012
WAKAZI wa Kitongoji cha Itezi Magharibi, Kata ya Itezi, jijini
Mbeya, walimzika mwenzao akiwa hai kwa kumtuhumu kuwa ni mchawi kwa
kumuhusisha na kifo cha mtoto wa mdogo wake.
Marian Girls kinara matokeo kidato cha sita
Mei 2, 2012
BARAZA la Mitihani la Tanzania, lilitangaza matokeo ya kidato cha
sita na kuonesha Shule ya Marian Girls kuongoza kwa ufaulu kwa kutoa
wasichana watano waliofanya vizuri katika masomo ya sayansi kwa
kombinesheni ya PCM.
Watu saba wafa ajali ya basi la NBS
Mei 3, 2012
WATU saba walikufa papo hapo na wengine 54 walijeruhiwa baada ya basi
la kampuni ya NBS lenye namba za usajili T 978 ATM lililokuwa likitokea
Tabora kuelekea Arusha kupinduka katika eneo la Jineri, nje kidogo ya
mji wa Igunga.
Dk. Ulimboka atekwa na kupigwa
Juni 28, 2012
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk. Steven Ulimboka,
alitekwa na watu wasiojulikana, kupigwa na kujeruhiwa sehemu mbalimbali
za mwili, kisha kutupwa katika msitu wa pande, nje kidogo ya jiji Dar es
Salaam.
Serikali yawashtaki madaktari
Julai 7, 2012
SERIKALI iliwashtaki katika Baraza la Madaktari Tanzania, madaktari
wanafunzi wa vitendo walioshiriki kwenye mgomo wa madaktari uliofanyika
nchini kwa tuhuma za kuhatarisha maisha ya wagonjwa na kukiuka maadili
ya taaluma yao.
Meli ya Mv Skagit yazama
Julai 18, 2012
Kisiwa cha Zanzibar kilikumbwa na msiba mzito kutokana na kuzama
kwa meli ya MV Skagit, mali ya Kampuni ya Seagull, iliyokuwa ikisafiri
kutoka Dar es Salaam ikiwa na abiria wanaokadiriwa kuwa 290 pamoja na
mizigo kuelekea Unguja, visiwani Zanzibar majira ya saa saba mchana.
Watu 63 walifariki, 146 wakiokolewa hai na 81 hawakupatikana.
Sheria ya mifuko ya jamii moto
Julai 27, 2012
VUGUVUGU la kupinga mabadiliko ya sheria za mifuko ya hifadhi ya
jamii ya mwaka 2012 lilichukua sura mpya baada ya wabunge kutaka
kuifanyia marekebisho mengine kwa sababu mwanachama hataruhusiwa
kuchukua mafao yake kwa sababu yoyote mpaka hapo atakapofikisha miaka 55
au 60.
Ugonjwa wa ebola waingia nchini
Agosti 5, 2012
UGONJWA hatari wa ebola ambao umeua idadi kubwa ya watu nchini Uganda
uliripotiwa kuingia nchini katika wilaya ya Kyerwa, kijiji cha Bulongo,
mkoani Kagera, ambapo mtoto wa miaka sita alionekana na dalili hizo.
Walimu watishia kuing’oa CCM
Agosti 6, 2012
WALIMU walipokubali kurejea kazini na kuendelea kutafakari amri ya
mahakama, mkakati mzito ulipangwa kuhakikisha hawakiungi mkono Chama cha
Mapinduzi (CCM) kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.
Polisi waua kikatili
Septemba 3, 2012
Jeshi la Polisi lilimuua mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni
cha Channel Ten, Daudi Mwangosi, aliyekuwa anaripoti habari za ufunguzi
wa matawi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), mkoani hapa.
Mwangosi alidaiwa kuuawa kwa bomu lililorushwa na polisi waliotaka kuizuia CHADEMA kufungua tawi katika kijiji cha Nyololo.
Waislamu waandamana Dar
Septemba 21, 2012
MAELFU ya waumini wa dini ya Kiislamu waliandamana na kukusanyika
kwenye viwanja vya Kidongo Chekundu jijini Dar es Salaam ambako walitoa
tamko dhidi ya wanaoshambulia na kunyanyasa Uislamu, hasa kwa Marekani
kutengeneza filamu ikimkashifu Mtume Muhammad (SAW).
Ajali yaua 10 Mbeya, mbunge anusurika
Oktoba 3, 2012
MBUNGE wa Viti Maalum Mbeya kupitia tiketi ya Chama cha Mapinduzi
(CCM), Dk. Mary Mwanjelwa, alinusurika kufa katika ajali iliyogharimu
maisha ya watu takriban 10.
Ajali hiyo ilitokea eneo la Mbalizi, wilaya ya Mbeya Vijijini. Gari la mbunge huyo liligongwa na kuteketea kwa moto papo hapo.
Kizaazaa cha mafuta Dar
Oktoba 3
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) baada ya
kushusha bei za mafuta ya petroli na dizeli nchini, baadhi ya
wafanyabiashara walizua kizaazaa kwa kuweka mgomo baridi wa kuuza mafuta
hayo.
Waislamu wachoma, wavunja makanisa
Oktoba 12, 2012
KUNDI kubwa la Waislamu wenye imani kali, lilizusha vurugu kubwa
zilizoambatana na kuchomwa moto na kuharibiwa makanisa manne huko
Mbagala jijini Dar es Salaam, katika kile kilichoelezwa kuchukizwa na
kitendo cha kijana mmoja wa Kikristo aliyedaiwa kukimwagia haja ndogo
kitabu kitakatifu cha Kurani.
Ponda akamatwa kwa uchochezi
Oktoba 17, 2012
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, lilimtia mbaroni
Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Issa Ponda Issa,
akikabiliwa na tuhuma mbalimbali za uchochezi.
Jeshi la Polisi lamjeruhi
mwandishi kwa risasi
Desemba 5 2012
JESHI la Polisi Mkoa wa Kinondoni jijini Dar es Salaam, liliingia
kwenye kashfa baada ya askari wake kumjeruhi kwa risasi mwandishi wa
habari wa gazeti la Tanzania Daima, Shabani Matutu, akiwa nyumbani
kwake.
Padri apigwa risasi Zanzibar
Desemba 26, 2012
PADRI wa Kanisa Katoliki lililoko Mpendae visiwani Zanzibar, Ambrose
Mkenda, alijeruhiwa kwa risasi na watu wasiojulikana nje ya nyumba yake
majira ya saa 12 jioni juzi wakati akitoka kanisani.
CHANZO:TANZANIA DAIMA.
|
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !