Ponda asomewa mashtaka wodini
Dar es Salaam. Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu
Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda amesomewa mashtaka ya uchochezi akiwa
kitandani katika Taasisi ya Mifupa ya Hospitali ya Taifa Muhimbili
(Moi).
Ponda aliyekuwa chini ya ulinzi wa polisi tangu
Agosti 9 mwaka huu, alipofikishwa hospitalini hapo kwa matibabu,
alisomewa mashtaka hayo na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Hellen
Liwa.
Kiongozi huyo alifikishwa hospitalini hapo baada
ya kudaiwa kupigwa risasi ambayo hata hivyo, si Moi wala Polisi
waliothibitisha.
Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu, Dar es Salaam, ililazimika kuhamia hospitalini hapo kutokana na Ponda kulazwa.
Mwendesha Mashtaka na Wakili Mwandamizi wa
Serikali, Tumaini Kweka alisema Sheikh Ponda anatuhumiwa kufanya
uchochezi katika maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Sheikh Ponda alikana shtaka hilo bila kuwapo
wakili wake, Juma Nassor. Hivi sasa kiongozi huyo wa Kiislamu,
anatumikia kifungo cha nje cha mwaka mmoja kutokana na kesi ya uchochezi
iliyokuwa ikimkabili.
Habari zilizopatikana baadaye jana zilieleza kuwa, ilikuwa Sheikh Ponda aondolewe hospitalini hapo na kwenda jela, lakini Wakili Nassor alisema hali ya mteja wake haikuwa nzuri tangu asubuhi hivyo kuomba abaki hospitalini hapo.
“Hawezi kuondolewa kwa kuwa tangu asubuhi
analalamika kuumwa kichwa, kizunguzungu na maumivu katika jeraha
alilopata. Zaidi ya yote, ni mpaka atakapopata ruhusa ya daktari,”
alisema wakili huyo.
Habari zaidi zilizopatikana jana jioni zinaeleza kuwa utaratibu unafanyika ili Sheikh Ponda apate ruhusa ya kutoka hospitalini hapo ndipo apelekwe gerezani hadi kesi yake itakapotajwa tena Agosti 28, mwaka huu.
Akizungumza baadaye jana, Wakili wa Ponda alisema:
“Nilichelewa kufika, ningepinga mashtaka hayo lakini ninaandaa
pingamizi nitakalowasilisha siku ya kutajwa kwa kesi; sikubaliani na
mashtaka aliyosomewa mteja wangu na pia Mahakama ya Kisutu haina uwezo
wa kusikiliza shtaka linalotajwa.”
Wafuasi wazua zogo.
Mapema ilipofika saa 10 jioni, wafuasi wa Sheikh
Ponda walifika kwa wingi hospitali kumwona ikiwa ni muda wa kawaida wa
kuona wagonjwa, lakini walizuiwa na polisi hali iliyosababisha kutokea
kutokuelewana.
Hata hivyo, hali hiyo ilitulia baada ya polisi waliokuwapo kulinda usalama kuzungumza na baadhi ya waumini hao na kukubaliana utaratibu wa kumwona kiongozi wao.
Moro nao waigomea kamati.
Hata hivyo, hali hiyo ilitulia baada ya polisi waliokuwapo kulinda usalama kuzungumza na baadhi ya waumini hao na kukubaliana utaratibu wa kumwona kiongozi wao.
Mmoja wa wafuasi hao ambaye jina lake
halikufahamika mara moja, aliwaambia wenzake: “Jamani tulieni, hakuna
haja ya kushindana nguvu na polisi kwani taratibu za Serikali
zinaendelea, tumeshaweka utaratibu na wote tutakwenda kumwona Sheikh
wetu.”
Baadaye wafuasi hao waliruhusiwa na askari hao kuingia kumwona Sheikh Ponda katika makundi ya watu watano watano.
Moro nao waigomea kamati.
Uongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Mkoa wa
Morogoro, umegoma kushirikiana na kamati iliyoundwa na Polisi nchini
kuchunguza tukio la kupigwa risasi kwa Sheikh Ponda.
Mwenyekiti wa Jumuiya na Taasisi Morogoro, Sheikh
Ayubu Mwinge Salum alisema aliitwa na tume hiyo katika Ofisi ya Kamanda
wa Polisi wa Mkoa, Faustine Shilogile ambako imeweka kambi kuhoji na
kusikiliza ushahidi wa tukio hilo na kuieleza kuwa hayuko tayari
kushirikiana nayo.
“Tuliwaambia hatuko tayari kutoa ushahidi kwa kuwa hatuna imani na kamati hiyo kwani haiko huru kama tulivyotarajia.
“Sisi ndio tuliomba kuundwa kwa tume na kutaka iwe
huru lakini tumeshangazwa na kuundwa na maofisa wa jeshi hilo wakati
ndilo linalotuhumiwa kuhusika na tukio lenyewe,” Sheikh Salum aliwaambia
waandishi wa habari juzi.
Alisema kuwa watakuwa tayari kutoa ushahidi katika
kamati hiyo hadi itakapoundwa iliyo huru ambayo wajumbe wake
watapatikana nje ya Serikali na nchi.
Shilogile agoma
Akizungumzia kauli iliyotolewa na Baraza Kuu la
Waislamu wa Tanzania (Bakwata) Mkoa wa Dar es Salaam ya kumtaka ajiuzulu
kupisha uchunguzi wa tukio hilo, Kamanda Shilogile alisema hana mpango
wa kufanya hivyo.
Alisema hawezi kujiuzulu wala kujibu kauli za
taasisi akisema zina uhuru wa kusema chochote. Hata hivyo, alizishauri
kuiachia kamati iliyoundwa kuchunguza suala hilo ifanye kazi.
“Siwezi kuwazuia watu kusema, sitaki kuzungumza lolote wakati
Kamati ya Haki Jinai imeundwa tayari na itafanya kazi yake na kubaini
ukweli. Tusiingilie kazi ya tume hiyo,”alisema.
Polisi imeunda Kamati ya Haki Jinai inayoongozwa
na Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Isaya Mungulu ili kuchunguza tukio
hilo ambalo jeshi hilo linatuhumiwa kumjeruhi Sheikh Ponda kwa risasi
katika bega lake la kushoto, Ijumaa iliyopita mkoani Morogoro.
Viongozi mbalimbali wa taasisi za kiraia na zile
za dini pia wamemtaka Kamanda Shilogile ajiuzulu kutokana na tukio hilo
na kuitaka Serikali kuunda tume huru badala ile ya Kamati ya Haki Jinai.
Nyongeza na Lilian Lucas
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !