Ponda Dar mpaka Moro kwa Helikopta
Katibu wa Taasisi na Jumuiya za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda
Issa Ponda alisafirishwa jana kwa helikopta kutoka Dar es Salaam kwenda
Morogoro na kupandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa kujibu
mashtaka yanayomkabili.
Ponda jana alianza kwa kufikishwa katika Mahakama
ya Hakimu Mkazi wa Kisutu asubuhi na kufutiwa mashtaka ya uchochezi
yaliyokuwa yakimkabili baada ya kusomewa mara ya kwanza Agosti 14, mwaka
huu akiwa kitandani katika Taasisi ya Mifupa ya Hospitali ya Muhimbili,
baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kuwasilisha hati ya kutokuwa na
nia ya kuendelea kumshtaki.
Alidaiwa kutenda makosa hayo katika maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Muungano kati ya Juni 2 na Agosti 11 mwaka huu.
Ponda alifikishwa mahakamani hapo saa 12 asubuhi
na baadaye alipandishwa kizimbani na kufutiwa kesi hiyo, baada ya Wakili
Kweka kuwasilisha hati hiyo ya DPP chini ya Kifungu cha 91 (1) cha
Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).
Hata hivyo, baada ya kufutiwa mashtaka hayo,
aliendelea kushikiliwa na kisha akachukuliwa na kupelekwa Morogoro
ambako pia alisomewa mashtaka ya uchochezi.
Kuwasili Moro
Sheikh Ponda aliwasili kwa helikopta ya polisi na
kutua kwenye Uwanja wa Gofu, Morogoro akiwa chini ya ulinzi wa polisi na
alipakiwa kwenye gari maalumu ambalo liliongozana na magari mengine
matatu ya polisi huku ulinzi ukiwa umeimarishwa katika eneo la Mahakama
ukiwajumuisha askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), askari wa
upelelezi, Usalama wa Taifa pamoja na mbwa wa polisi na kusababisha
shughuli za kazi katika Mahakama hiyo na ofisi za jirani kusimama kwa
muda.
Baada ya kufika mahakamani saa tano asubuhi,
magari yalisimama kwa takriban dakika 30 kabla ya kumtoa na kumwongoza
kwenye Mahakama ya wazi ambayo tayari ilikuwa umejaa watu.
Baada ya kumalizika kusomwa kwa kesi hiyo, msafara
uleule ulimrejesha Uwanja wa Gofu saa sita mchana na kupandishwa kwenye
helikopta kurejea Dar es Salaam.
Mahakamani Morogoro
Ponda alisafirishwa kwa helikopta ya polisi hadi
Morogoro na kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi akiwa
chini ya ulinzi mkali.
Mara baada ya kumfikisha katika Mahakama hiyo iliyofurika mamia
ya waumini na wafuasi wake, Wakili wa Serikali, Bernard Kongola
alimsomea mashtaka matatu yanayomkabili.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Morogoro,
Richard Kabate alisema: “Agosti 10, mwaka huu katika eneo la Kiwanja cha
Ndege, Manispaa ya Morogoro Ponda Issa Ponda, aliwaambia wafuasi wake.
“Ndugu Waislamu, msikubali uundwaji wa Kamati za
Ulinzi na Usalama za misikiti kwani kamati hizo zimeundwa na Bakwata
ambao ni vibaraka wa CCM na Serikali na kama watakuja kwenu na
watajitambulisha kwamba wao ni Kamati za Ulinzi na Usalama za misikiti,
fungeni milango na madirisha ya msikiti yenu na muwapige sana.”
Kongola alisema kauli hiyo ilikuwa ikiumiza imani
za watu wengine na kwamba hatua hiyo ni kinyume cha agizo la Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu lililotolewa na Hakimu Victoria Nongwa Mei 9, mwaka
huu ikimtaka kuhubiri amani ndani ya mwaka mmoja na kwenda kinyume na
kifungu cha Sheria namba 124 cha mwaka 2002, shtaka ambalo Ponda
alikana.
Katika shtaka la pili, Ponda anadaiwa Agosti 10
mwaka huu katika eneo la Kiwanja cha Ndege Manispaa ya Morogoro
aliwaambia Waislamu kuwa Serikali ilipeleka jeshi Mtwara kushughulikia
vurugu iliyotokana na gesi kwa kuwaua, kuwabaka na kuwatesa wananchi kwa
sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni Waislamu.
Alisema Serikali haikufanya hivyo kwa wananchi wa
Loliondo walipokataa Mwarabu asipatiwe kipande cha ardhi ya uwindaji
baada ya kudai ni mali yao kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni
Wakristo na kuwa maneno hayo yaliumiza imani za watu wengine jambo
ambalo ni kinyume cha Kifungu cha Sheria 129 cha mwaka 2002, shtaka
ambalo pia alikana.
Shtaka la tatu linafanana na lile la pili lakini
na upande wa mashtaka ulieleza kuwa maneno hayo yaliumiza imani za watu
wengine na kwamba kufanya hivyo ni kinyume cha Kifungu 390 cha Sheria na
Kanuni ya Adhabu namba 35 cha mwaka 2002, shtaka ambalo Sheikh Ponda
alilikana. Baada ya kusomwa kwa mashtaka yote matatu, wakili wa Serikali
aliiambia Mahakama kuwa upelelezi wa kesi umekamilika na kupanga kesi
kuanza kusikilizwa Septemba 2 mwaka huu. Upande wa utetezi uliomba
Mahakama kupanga kuanza kusikilizwa kwa kesi Agosti 26, mwaka huu.
Hakimu Kabate aliwapa mawakili kujadiliana na baadaye kuomba kesi hiyo ianze kusikilizwa Agosti 28 mwaka huu.
Wakili alalamika
Akizungumza Dar es Salaam jana, Wakili wa Ponda,
Juma Nassoro alilaani kitendo cha kuondolewa kwa mteja wake gerezani na
kwenda kusomewa mashtaka mapya Morogoro bila taarifa.
Alidai kuwa polisi wanaendelea kukiuka taratibu za
kumshikilia kiongozi huyo kutokana na kufanya mambo kinyume na sheria
kwa lengo la kutaka waumini kufanya vurugu ili waendelee kumshikilia
kiongozi huyo.
“Kitendo cha kumuondoa mteja wangu gerezani na kwenda kumsomea
shtaka jingine Morogoro nimelilaani. Sijalipenda. Polisi hawakuwa na nia
nzuri na Ponda kwa sababu sheria zinajulikana na kila mtu ana haki ya
kutetewa,” alisema Nassoro.
Akizungumzia kufutiwa kesi Mahakama ya Kisutu,
Nassoro alisema Serikali imeamua kufuta kesi kabla ya kusikilizwa baada
ya kuona imeelemewa kwani alishapeleka maombi ya kuirudisha Mahakama Kuu
kutoka Kisutu kutokana na Mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza
kesi hiyo na maombi hayo yalipewa namba 11/2013.
Msemaji wa familia, Isihaka Rashidi alisema: “Hawa
jamaa wamempeleka Morogoro kwa siri kwa sababu jana (juzi) tulikwenda
Segerea hakukuwa na hizo taarifa. Tumekuja kushtuka asubuhi baada ya mke
wake kwenda kumpelekea chai na kuambiwa ameondolewa na kupelekwa
Morogoro.”
Alisema baada ya kupata taarifa hizo iliwalazimu
kuwasiliana na ndugu zao waliopo Morogoro kwa ajili ya kwenda mahakamani
kusikiliza kesi hiyo.
*Imeandikwa na Lilian Lucas na Hamida Sharrif (Morogoro), James Magai, Aziza Masoud na Aidan Mhando, Dar.
Posted Jumatatu,Agosti19 2013 saa 20:9 PM:MWANANCHI.
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !