§ Yaahidi kupeleka Hati za Muungano bungeni kesho
MAKOMBORA ya maneno yaliyokuwa yakitolewa na msemaji wa taarifa
ya wachache bungeni, Tundu Lissu, juu ya muundo wa muungano, na kutokuwapo kwa
Hati za Muungano kumetikisa serikali ambayo sasa imeamua kuzitoa hadharani hati
hizo.
Lissu ambaye wiki iliyopita
alishindwa kumaliza ufafanuzi wake baada ya Bunge kuvunjika kutokana na Shirika
la Utangazaji la Taifa (TBC) lenye vituo vya redio na runinga kukatisha
matangazo ya moja kwa moja (live) akifafanunua maoni yao kuhusu muundo wa
muungano na hati zake, jana alikuwa mjumbe wa kwanza kupata fursa ya kumalizia
kutoa maoni ya watu wachache.
Huku akikatishwa mara kwa mara na
taarifa na miongozo kutoka kwa baadhi ya wajumbe waaumini wa serikali mbili,
Lissu alisema wajumbe wengi wamekuwa wakipotosha umma kwamba kukubali serikali
tatu ni kuvunja hati ya makubaliano ya muungano ambayo haipo wala haijawahi
kutolewa mbele ya hadhara.
“Swali la msingi linalohitaji
kuulizwa, je, hati hii ipo? Swali la
pili, je, hati hii ni halali? Swali la tatu, kama hati hii ipo na ni halali je,
Muungano huu ni halali?”
Lissu
alisema hakuna ushahidi kwamba kuna hati ya muungano kwa kuwa hata
Umoja wa Mataifa, kunakoelezwa ilipelekwa, wamethibitisha hakuna jambo
hilo.
“Hati ya
Muungano haipo Zanzibar wala Tanganyika, haipo UN wala bungeni, sasa hiki
kilichozungumzwa na wengi kuwa kuanzisha muundo wa serikali tatu ni kuvunja
hati hizo ni uongo tu, zama za uongo sasa zimefikia mwisho.
“Nusu
karne ya uongo sasa ikome, tuambiane ukweli hivi sasa, waliozoea vya kunyonga
kamwe hawawezi vya kuchinja, mimi nawataka wajumbe wenzangu tufikie mwisho wa
kudanganya.
“Ni nani
aliyeshuhudia wakati wa kutiliana saini makubaliano ya muungano? Hakuna
walioshuhudia, wale wote walioshuhudia jambo hilo waliuawa, sasa mnahofia nini
kuingia kwenye serikali tatu?” alisema.
Bunge la
Tanganyika lilithibitisha kuungana na Zanzibar lakini Zanzibar haikuridhia
jambo hilo kwa mujibu wa nyaraka mbalimbali zilizopo.
Lissu
alisema nyaraka zinaonyesha kuwa Aprili 4, mwaka 1964 siku moja baada ya
muungano, Mwanasheria Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Costantine Paulo, aliandika
barua kwa Ubalozi wa Tanganyika akiwaambia wamesikia kuwa wameungana na
Zanzibar wapeleke hati ya makubaliano hayo ili iweze kupata usajili wa Umoja wa
Mataifa, itambulike kwa mujibu wa sheria za kimataifa.
Alisema
Mei 6, mwaka huo huo siku kumi baadaye Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanganyika
ikapeleka tamko rasmi kwamba kweli wameungana na hati ya muungano
wameiambatanisha na ‘noticefication’.
Aliongeza
kuwa Mei 14, wiki moja baadaye mwanasheria huyo akaandika ‘telex’ kwa serikali
ya Tanzania akiwataka Watanzania wawatumie nakala mbili za hati ya makubaliano
ya muungano ili waisajili kwa mujibu wa ibara ya 102 ya United Nation Charter.
“Taarifa
hii inamaanisha kuwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania iliposema kwamba
tumewaleteeni, hawakupeleka sasa mwenyekiti ushahidi kwamba Umoja wa Mataifa haujawahi
kupelekewa hati ya muungano umepatikana Machi 3, 2009, wakati ofisa habari za
kisheria wa kitengo cha mikataba ya kitaifa wa Umoja wa Mataifa, ofisi
inayoshughulikia masuala ya kisheria alipomwandikia mtafiti mmoja aliyeandika
kitabu kwamba hakuna ushahidi wowote kwamba hati ya muungano ilisajiliwa kwenye
sekretalieti ya Umoja wa Mataifa.
“Kama
ingesajiliwa kungekuwa na hati ya usajili iliyoambatanishwa, nimeangalia hakuna
kitu kama hicho Mwenyekiti, hati ya makubaliano ya muungano haipo Umoja wa Mataifa
na haipo Tanzania na kuna ushahidi kwamba haipo Tanzania,” alisema.
Alisema
mwaka 2005 Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ilishitakiwa Mahakama Kuu ya
Zanzibar na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Idd Pandu Hassan, aliambiwa apeleke
hati ya makubaliano ya muungano yenye saini ya Nyerere na Karume.
“Maneno
ya Mwanasheia Mkuu wa Zanzibar yanasema hivi kwa barua yake ya tarehe
22/6/2005, anasema; ‘ofisi yangu haikuweka kumbukumbu ya mkataba wa asili
(original) wa muungano wa Tangayika na Zanzibar tarehe 26/4/19964’” alisema.
Serikali kutoa hati
Baada ya
makombora ya Lissu, Mwenyekiti wa Kamati Namba Sita, Stephen Wassira, alisema
hati ya Makubaliano ya Muungano ya Tanganyika na Zanzibar iliyosainiwa na
waasisi wa Muungano, Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Aman Karume,
ipo salama na itawasilishwa katika Bunge Maalumu la Katiba ndani ya siku
mbili zijazo.
Baada ya
Wassira kusimama alisema hapo wanazungumza na Watanzania na hivyo si vizuri
kuzungumza mambo ya uongo.
“Mheshimiwa
Mwenyekiti napenda kukuthibitishia kuwa Hati ya Makubaliano ya Muungano ipo na
ipo imehifadhiwa sehemu salama kwa muda wote wa miaka 50 ya Muungano kwa niaba
ya dola ya Tanzania, naomba kukuthibitishia kuwa Hati hiyo ya Muungano
itawasilishwa kwenye Bunge baada ya siku mbili,” alisema Wassira.
Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda, amesema kuwa ametumiwa nakala ya hati ya muungano kwa
nukushi (fax), kutoka Ikulu, Dar es Salaam na kwamba ataikabidhi kwa Mwenyekiti
wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta.
Alibainisha
kuwa nakala nyingine italetwa ikiwa imesainiwa na mwanasheria kuthibitisha
uhalali wa nakala hiyo.
Mara
baada ya taarifa hiyo, Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta, alisema
akiipata Hati ya Muungano iliyothibitishwa ataigawa kwa kila mjumbe ili
waendelee vizuri na majadiliano.
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !