§ TBC yamzimia matangazo ya moja kwa moja
MAKOMBORA ya maneno
yaliyokuwa yakitolewa na msemaji wa taarifa ya wachache bungeni, Tundu Lissu,
juu ya muundo wa muungano, hati na nukuu mbalimbali za viongozi wa kitaifa
yalisababisha kuvunjika kwa kikao cha Bunge Maalumu.
Kuvunjika kwa Bunge hilo kulitokana na taarifa zilizotolewa kwa
Mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta, kuwa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC)
lenye vituo vya redio na runinga limekatisha matangazo ya moja kwa moja (live).
Mjumbe wa Bunge Maalumu, Freeman Mbowe, ndiye aliyeanzisha hoja
hiyo baada ya kusimama na kuomba mwongozo wa Mwenyekiti wa Bunge juu ya hatua
hiyo ya TBC kukatisha matangazo yake wakati Lissu akitoa ufafanuzi wa taarifa
ya walio wachache.
Mbowe alisema mjadala wa Katiba mpya ni muhimu kwa taifa lakini
kituo cha runinga cha TBC ambacho ni cha taifa kimekatisha matangazo ya moja
kwa maoja, jambo linalowanyima fursa wananchi kujua kinachoendelea bungeni.
“Mheshimiwa Mwenyekiti naomba mwongozo wako ni hatua au jambo
gani tutalifanya baada ya televisheni na radio ya taifa kukatisha matangazo ya
moja kwa moja ambayo imekuwa ikiyafanya tangu tuanze mkutano huu,” alisema.
Akijibu mwongozo huo Sitta, alisema kuwa taarifa hiyo inashtua
kwakuwa Bunge limeingia mkataba na serikali na TBC unaotaka matangazo ya vikao
vya Bunge ni lazima yaonekane na kufika kwa wanachi.
Sitta, alisema walifanya hivyo kwa kuwa mchakato wa uandikaji wa
Katiba mpya ni shirikishi hivyo wananchi wana haki ya kushiriki na kujua kila
kinachofanyika ndani ya Bunge.
“Naomba Katibu achunguze mara moja kuhusu kukatishwa kwa
matangazo ya TBC tujue kuna tatizo gani kwakuwa jambo hili linawanyima wananchi
haki za kusikia na kuona kile kilichotokea hapa bungeni,” alisema.
Mara baada ya taarifa hiyo, Sitta aliwataka wajumbe watulie kwa
muda afuatilie jambo hilo na atawapa taarifa baada ya muda mfupi.
Baada ya dakika chache Sitta aliwaambia wajumbe kuwa amepata
taarifa kwamba hali ya hewa Dar es Salaam ni mbaya kutokana na mvua kubwa
iliyokuwa ikinyesha hivyo kuathiri matangazo ya moja kwa moja ya vituo vya
runinga na radio vya TBC .
Sitta alisema kutokana na kukatika huko kwa matangazo ya moja
kwa moja, Bunge Maalumu haliwezi kuendelea na mijadala yake kwa kuwa wananchi
watakosa fursa ya kuona na kusikia kile kilinachojadiliwa.
“Kwa sababu yoyote ile hatuwezi kuendelea, natoa maelekezo kwa
Katibu kuangalia muda ambao matangazo yaliyokatika na alipoishia Lissu, wakati
jambo hilo likitokea….., ninawahakikishia tukianza kikao Jumatatu mtu wa kwanza
atakuwa Tundu Lissu,” alisema.
Mara baada ya kutoa kauli hiyo wajumbe kutoka vyama vya upinzani
walikuwa wakishangilia huku wengine wakipiga vigeregere na kuimba:
“Sitta….Sitta….Sitta wewe ni Mwenyekiti wa viwango na leo ndiyo umetuonyesha
viwango vyako.”
Uamuzi huo, ulionekana kumkera Hamisi Kingwangala, ambaye
alisimama na kutaka utaratibu akitumia Kanuni ya 52, (8), kuhoji
kanuni ipi iliyotumiwa na Sitta kuahirisha Bunge kabla ya muda unaotakiwa
ilhali pia halikuwa limemaliza shughuli za siku husika.
Kigwangala alisema Kanuni ya 32 inazungumzia mijadala au
ufafanuzi wa taarifa za kamati lakini hakuna hata eneo moja linataja kuwa
shughuli za Bunge zinaweza kuahirishwa kwa sababu ya kituo fulani hakijaonyesha
matangazo ya moja kwa moja.
Kauli hiyo iliwafanya wanjumbe wenzake wamzomee huku wakimuita
msaliti lakini Kingwangala aliwajibu: “Haya ndiyo matatizo ya Bunge Maalumu
kuwa na wanasiasa makanjanja.’
Sitta
amkata maini
Akitolea ufafanuzi Mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta, alisema
jambo linalofanyika hivi sasa katika Bunge Maalumu ni kubwa sana ndiyo maana
limewekewa bajeti ya kuwashirikisha kwa kupitia vyombo vya umma vinavyolipwa
fedha.
“Wananchi wanaofuatiliana kwa hamu yanayotokea hapa ndiyo maana
tunasema Bunge Maalumu ni shirikishi sasa kama wananchi hawaoni huo ushirikishi
unatoka wapi?
“Mimi nataka kutenda haki na ionekane imetendeka, hivi matangazo
yamekatika na watu hawaoni utawezaje kuzuia hisia za wengine kutotendewa haki?
Tukiendelea itatafsiriwa kuna ubaguzi fulani….mimi sitaki niwe mbaguzi,
nimeapa kutenda haki,” alisema.
Sitta alibainisha kuwa ametumia kanuni ya 85 ambayo inampa
mamlaka mwenyekiti kuamua jambo au kuvunja kanuni kutokana na sababu
mbalimbali.
“Mimi nataka kutenda haki, msemaji yeyote ikitokea hali kama ya
leo nitasitisha kidogo na tutaendelea tena hapo baadaye…. katika kulifanya hilo
sitajali vyeo au kundi fulani,” alisema.
Mara baada ya kauli hiyo ukumbi wa Bunge ulilipuka kwa vifijo na
vigeregere kutoka kwa wajumbe waliokuwa wakimshangilia Sitta, kwa uamuzi
waliouita wa busara.
Hoja za
Lissu
Awali Lissu wakati akianza kusoma maoni ya walio wachache,
yaliyokuwa yametawaliwa na nukuu za viongozi mbalimbali pamoja na vitabu
alivyokuwa navyo, alisema waliozoea vya kunyonga vya kuchinja hawawezi,
waliozoea vya haramu vya halali hawawezi.
Alisema walipeleka mapendekezo kwamba maoni ya wachache yasomwe
na wachache lakini waliozoea vya haramu wakayakataa kwa hoja kuwa wanataka
wayasome wao kama watakavyosoma yao.
Kauli hiyo ilimfanya Sitta, kumkatisha na kumtaka aache
kuwatuhumu wenzake waliomo ndani ya ukumbi wa Bunge ambao wamekwenda pamoja.
“Sisi sote tumekuja pamoja kuwaita wengine kuwa wamezoea vya
haramu unaamua wewe, hututendei haki hata kidogo kwasababu ya usioelewana nao
basi wamezoea vya haramu, sasa mjadala hauwezi kwenda hivyo, ondoa hayo maneno
ya waliozoea vya haramu,” alisema Sitta.
Baada ya maelekezo hayo Lissu alikubali kuyaondoa na kuingiza
mengine ambapo alisema waliozoea kuishi kwa uongo na udanganyifu hawawezi
kujifunza kuishi katika kweli.
Lissu alisema Katika kitabu kinachoitwa Panafricanism cha
Profesa Issa Shivji katika ukurasa 93 wa kitabu chake amesema kwamba hati ya
makubaliano ya muungano haikuwahi kuthibitishwa na Baraza la Wawakilishi
Zanzibar kwa miaka yote 50 tangu muungano uzaliwe.
“Alibainisha kuwa nyongeza zote za mambo ya muungano tangu
mwaka 64 hadi leo ni haramu na ni batili lakini leo Shivji ndiye mpiga
debe mkubwa wa CCM na muungano huu wa serikali mbili, mfano wa pili uko katika
kitabu kinaitwa ‘Tanzania’s 8th Constitutional Amendment and its implications
of constitutionalism democracy and union question,’ kilichoandikwa na Dk.
Mwakyembe 1995”
Alibainisha kuwa Dk. Mwakyembe, aliandika kitabu hicho kama
sehemu ya shahada yake ya uzamivu ya Chuo Kkikuu cha Humbarg, Ujerumani na
kwenye kitabu chake alisema kuwa hoja ya Dkt. Wolfgang Dourado kuhusu muungano
kiuhalisia hati ya makubaliano ya muungano ilitengeneza muundo wa serikali 3
lakini utekelezaji wake umekuwa tofauti, ukurasa wa 184.
Lissu alibainisha kuwa kwenye ukurasa 195 Dk. Mwakyembe, alisema
mfumo wa shirikisho la serikali 3 kama ilivyopendekezwa na tume ya Nyalali na
kuungwa mkono na vyama na makundi ya upinzani unaonekana ndio njia pekee katika
hali ya sasa ya Tanzania.
Alisema kitabu hicho kinasema mfumo huo unaweza kutoa kile
ambacho kimekosekana kwa utaratibu wa sasa yaani wa wazi wa mamlaka kati ya nchi
washirika na kati ya muungano na washirika wake.
Lissu alisema Dk. Mwakyembe ni mjumbe wa kamati namba 4 aliyomo
yeye na ni mmoja wa wajumbe walio wengi katika kamati hiyo wamekataa shirikisho
na wamekataa muundo wa serikali 3, ambao wamezoea kuishi kwa uongo hawawezi
kujifunza kusema ukweli.
Aliongeza kuwa mfano wa tatu unahusu walioandika kitabu
kitachoitwa ‘Mali kuhusu rasimu ya katiba’ na kimeandaliwa na wahadhiri wa
sheria wa vyuo vikuu 15 vya Tanzania ambapo katika ukurasa wa pili wa kitabu
wamejadili rasimu hiyo inayobeba muundo wa serikali tatu wanayoitaka wananchi
na wanaunga mkono muungano wenye muundo wa shirikisho lenye serikali tatu.
Alibainisha kuwa mfano wa nne unamuhusu baba wa taifa, Julius
Nyerere mwaka 1968, akizungumza na gazeti la Observer la London alizungumzia
habari za muungano kwa maneno kuwa iwapo uma wa Zanzibar bila ya ushawishi
kutoka nje na kwa sababu zao wenyewe wataona kuwa muungano una hasara kwa uhai
wao hatowapiga mabomu, kuwalazimisha, muungano utakuwa hauna tena sababu ya
kuendelea iwapo washiriki wake wataamua kuukana.
Lissu aliongeza kuwa mwaka 1984 Wazanzibari walipohoji
muungano Alhaji Abood Jumbe akafukuzwa kazi amewekwa kizuizini katika eneo la
Mji Mwema jijini Dar es Salaam anakoishi mpaka sasa huku Wolfgang Dourado
akawekwa kizuizini na baadaye kupelekwa Ghana.
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !