Dodoma.
Wakati U-unguja na U-pemba ukianza kuibuka bungeni,
mbunge wa Mwanakwerekwe (CCM), Haji Juma Seleweji, amesema wanaounga mkono
serikali tatu wasijute watakaporudi Zanzibar.
Wajumbe wengi kutoka Zanzibar, badala ya kujadili Rasimu
ya Pili ya Katiba ili kuiboresha, walishambuliana kwa maneno, wakishindwa
kuficha hisia za ubaguzi.
Kila kundi lilituhumu jingine kuwa lilikuwa pinzani hata
kabla ya mapinduzi. Haji Juma Seleweji alianza kwa kutahadharisha wanaoishi
Bara watajuta.
Aliwaonya Wazanzibari wanaunga mkono serikali tatu
bungeni, kuwa watakapofika Zanzibar wasizungumze lolote na wasijute kwani
watasulubiwa.
“Hata mkiingia shimoni, msije kujuta na kusema
hamkufahamu, tumewaonya lakini hamkusikia,”alisema .
Abubakari Hamisi, alisema kuna Wazanzibari ambao kwa
makusudi na kwa nia isiyo njema, wanaigawa Zanzibar ili waendelee kuikandamiza.
Naye Waziri Rajabu Salimu, aliwatuhumu wajumbe wanaounda
mkono serikali tatu, kwamba ni vizazi vya waliopinduliwa katika mapinduzi
matukufu mwaka 1964.
“Wapinzani wa Zanzibar kabla ya mapinduzi matukufu,
vizazi vyao vipo na ndivyo vinasumbua kwa kuwa wapinzani wa muungano hadi
sasa,”alisema.
Aliwatuhumu Wapemba kwamba, hawaoni hasara kuvunja muungano
kwasababu udugu wao na Watanganyika siyo wa karibu kama ilivyo kwa Waunguja
ambao udugu wao na Watanganyika ni wa damu.
Alisema Wapemba kubeba mizigo, maduka yao na kwenda kwao
siyo tatizo kama ilivyo kwa Waunguja ambao kwa vyovyote ilivyo, hawataweza
kugawanywa na Watanganyika.
Naye Issa Gavu, alisema wanaotaka serikali tatu wamekuwa
maadui wa mapinduzi ya Zanzibar, tangu enzi.
“Maadui wa Mapinduzi bado wapo, wanaendelea kuzaliwa kila
kukicha lakini haiwezekani na haitawezekana kuendelea na mpango huo,
tumechoka,”alisema Gavu.
Aliwataka Wajumbe kutoka Zanzibar kutozungumza
lolote kuhusu shida na raha za Wazanzibari, badala yake wamwachie Dk Ali
Mohamed Shein.
Chanzo: Mwananchi; 17/04/2014
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !