- Msamaa.
Headlines News :
Home » »

Written By Unknown on Thursday, May 2, 2013 | 7:14 AM

Aliyoyasema KK bungeni .
{Mauaji ya Mwembechai 1998}
 
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana
Mheshimiwa Spika. Mbunge mwenzetu wa Jimbo la Ukerewe ana maneno ambayo huyasema mara kwa mara.Ni maneno ya busara na mimi ningeomba niyanukuu hapa leo. Anasema hivi "Simple minds discuss people…ordinary minds discuss events…..great minds discuss ideas" (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Nabii Mussa Alayhis-Salaam alipopewa kazi ya kwenda kuwarudisha Mayahudi kule Misri alimwambia Mungu "Ewe Mola wangu mimi nina kigugumizi, kazi hiyo siiwezi peke yangu nakuomba unipe Haroun anisaidie". Mungu akampa na kazi ikafanyika. (Kicheko)
Mheshimiwa Spika, kuna methali ya Kiswahili inayosema "Kikulacho kimo nguoni mwako". Kuna methali ya Kiswahili inayosema "Laumu ulikojikwalia, usilaumu ulikoangukia". (Makofi)
 
Mheshimiwa Spika, hivi karibuni mimi nilifanya Press Conference kule Dar es Salaam. Katika Press Conference yangu nilisema niliwaomba Polisi waache kuwashtaki Waislamu kwa kosa la kusema "Yesu si Mungu". Kwa sababu maneno yale yamo ndani ya Qur-an. Kama kwa bahati mbaya Waislamu hao wakipata ‘conviction’ itabidi I proscribe dini ya Kiislamu, wanaiona hatari yake. Nikawaomba pia Polisi wawape dhamana hawa watu maana yake waliokuwa wakipiga kelele wasipewe dhamana, wasipewe dhamana ni Polisi, wapewe dhamana hawa watu.
Baada ya siku chache Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani akatoa kauli akasema Mbunge anayo haki ya kutoa fikra zake, lakini baadaye Waziri mwenyewe akatoa kauli akasemaMbunge anatafuta umaarufu. Hili suala la umaarufu katika kitabu hiki Waziri amelitaja mara tatu. Sasa kwanza mimi nataka nimwambie Waziri kwamba mimi sitafuti umaarufu Dar es Salaam.Mimi Dar es Salaam maarufu. Mimi Dar es Salaam nina wastaha. (Makofi)
 
Mheshimiwa Spika,katika maisha yangu yote nimekuwa msema kweli na wewe unajua. Nimekuwa msema kweli kwa kiongozi wa Awamu ya Kwanza, mbele yako, nimekuwa msema kweli kwa Kiongozi wa Awamu ya Pili na nimekuwa msema kweli kwa Kiongozi wa Awamu hii. Sasa kama kusema kweli kwa viongozi wako ndiyo kulitakiaTaifa mabaya basi chama changu kitanihukumu.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nataka nirudie tu niliyoyasema na nipate maelezo kutoka kwa Waziri. Hivi karibuni hapa Dodoma askari wawiliwaliacha malindo yao wakaadhibiwa kwa kufukuzwa kazi. Nilipochangia hoja ya Waziri Mkuu niliuliza habari ya Chuki Athumani amekaa na pingu miezi minne na hakufunguliwa pingu ingawa Rais alimpa ruhusa alitoa amri aachiliwe,
 
Mheshimiwa Waziri Mkuu alikubali kwa naam". Chuki amekaa miezi minne na hakuachiliwa mpaka Waziri mwenyewe alipokwenda Dar es Salaam tarehe 17/6/98. Sasa mimi ninachotaka kujua kama hawa askari wawili hawakukaa kwenye malindo wamefukuzwa, wale ambao waliokiuka na kukataa kufuata amri ya Rais wamefanywa nini. Ni kina nani hao? Narudia kule kule kwa uwazi na ukweli. Ningeomba Waziri aseme anaogopa nini kwani na yeye anahusika. Amri imetolewa na Rais, watoto wote watolewe pamoja na Chuki Athumani. Chuki amekaa miezi minne gazeti la Observer linasema kama angetolewa wakati ule huenda hali yake isingekuwa kama ilivyo sasa. Sasa tujue Imam wa Msikiti Bet-il-Mukadas, Mussa Katambo ana umri wa miaka 83. Rais amesema atolewe, amekaa mahabusu miezi mitano ametolewa juzi tu na hajulikani hivi sasa kama ataishi au atakufa. Imam wa Msikiti wa Kinondoni Mtambani,Chata Abdallah ana umri wa miaka 78 amekaa ndani miezi mitano hakutolewa mpaka juzi wiki iliyopita. Ninachotaka kujua, sitaki mimi kujua, wengi wanahitaji kujua. Umma wa Watanzania wanataka kujua, je waliohusika nakukataa amri ya Rais ni kina nani, wamefanywa nini au watafanywa nini? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hawa ambao hawakutekeleza wajibu wao ndio wasiolitakia mema Taifa letu. Kwa sababu kama wale Maimam wangefia jela ghasia zake zisingekuwa ndogo, hivyo Waziri halijui hilo.
 
Sasa la pili nataka kulisema hili jambo la "Yesu si Mungu". Cardinal wa Kanisa Katoliki Pengo amesema ya kwamba kwa Muislamu kusema Yesu si Mungu si kashfa dhidi ya Ukristo na ameendelea kusema kwamba kwa Mkristo kusema ya kwamba Muhammad si Mtume wa mwisho si kashfa kwa Muislamu. Ma-Bishop wa Pentecosti wamesema hivyo hivyo. Sasa kwa nini Polisi walikuwa wakiendelea kukamata watu, kuwashtaki kwa kosa hilo hilo, dhidi ya dini nyingine, dini gani tena. Dini ndio hizo, Catholic na Prostestant wote wanasema si kosa. Sasa hawa ndio wasioliombea Taifa letu mema. (Makofi)
 
Mheshimiwa Spka, kama ujuavyo babu zangu, babu yangu mmoja hapa na wengine wamesaidia sana alhamdullilah. Rais akawatoa wote wale. Leo Dar es Salaam hakuna tena mtuhumiwa wa kesi za Mwembechai aliyekuwa mahabusu na wachache waliobakia wameshatolewa kwa dhamana. Lakini msikitini Mwembechai kuna askari juzi nakuja huku nimewakuta 14 wengine wana bunduki, jana nimepiga simu naambiwa wako tisa na bunduki wanalinda nini. Mahakimu wanasema ya kwamba mambo haya yamekwisha ndiyo maana wakawapa dhamana hawa. Sasa wale askari waliokuwa Mwembechai mpaka leo na bunduki wanalinda nini. Waislamu wa pale wanasema wanawazuia Waislamu wasisali kwa sababu mle ndani kulikuwa na darasa la watu wazima, kulikuwa na darasa la wanawake na kulikuwa na madrassa ya watoto hakuna kwa sababu ya kuogopa askari.
 
Mheshimiwa Spika, tuambiwe basi, siku ya Ijumaa msikiti ule ulikuwa unajaa watu tele ndani, nje unajaa. Leo wanaosali katika msikiti ule safu mbili, safu kwa Wasukuma, Wanyamwezi na Wadigo wasioelewa maana ya safu ni mistari. Mistari miwili siku ya Ijumaa mistari minne, jumla sita, sababu ya kuogopa askari. Sasa ningeomba Wziri atueleze kama Mahakimu wanasema pale ghasia imekwisha, Rais ametoa watu wote wale askari pale mpaka leo wanafanya nini?
 
Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala la parole nataka nimwambie Waziri kwamba "Kikulacho kimo nguoni mwake". Hiyo kengele? Lahaula!! Parole watu wake Waziri wamempelekea majina ya jamii moja. Waziri atanabahi akayakubali,akamshawishi na Waziri Mkuu kwenda kuzindua. Baraza Kuu na Taasisi za Kiislamu wamepiga kelele. Rais amefuta akamwambia aunde upya akizingatia uwiano wa jamii. Sasa mimi nasema wale waliombambikia yale majina ndio wasiolitakiaTaifa mema. (Makofi)
 
Sasa Waziri anasema ya kwamba kazi hiyo ataifanya katika kipindi cha mwaka 1998/99. Kazi iliyokuwepo ni kupunguza katika wale ishirini wa jamii moja akapunguza akaweka wengine wa jamii nyingine ni kazi ya siku mbili. Inakuwaje ichukue mwaka mzima. Sasa ndiyo namwambia tufuate mfano wa Nabii Mussa kama yeye hawajui hao wa jamii nyingine wenye elimu ya kutosheleza kuwa wenyeviti arudi kwa bwana mkubwa. Bwana wewe umenipa kazi hii lakini hii jamii nyingine siwajui waliosoma kiasi hiki,utampa Haroun. (Makofi/Kicheko).
 
Mheshimiwa Spika, nimesema mwaka jana kwamba mimi ni askari wa zamani kwamba nalipenda sana jeshi langu. Lakini ni wajibu wa mtu yoyote kama unampenda mtu umwambie kweli. Polisi hivi sasa wana makosa, nitoe mfano wamekwenda kumkamata Magezi msikiti wa Mwembechai baada ya salat alasiri, watu wamejaa pale.
 
Walikazania nini kama siyo ghasia? Wamekwenda kumkamata Ponda Issa Ponda, baada ya swalat I-jumaa ikatokea ghasia. Walitazamia nini? Hawa Masheikh wengine walikwenda kuwakamata nyumbani hakuna ghasia iliyotokea. Wamekwenda kumkamata Bishop Mugala kule Kurasini ndani ya kanisa. Taadhima gani hii? Kwa bahati nzuri waumini wake wakaanza kuimba nyimbo za dini. Lakini kuna wengine hawaimbi nyimbo za dini, hawakubali. Sasa mimi nasema Waziri ajue kwamba hawa wanaowasema wasiolitakia Taifa mema anao. Mimi tabia yangu husema kweli na sisemei uchochoroni. Ninapokuwa na jambo nakwenda kwa Kiongozi wangu, namwambia niliyokuwa nayo.Inawezekana nikakosea. (Makofi).
 
Sasa kama kwa kusema kweli, kumwambia kiongozi wako ni kukosa kulitakia mema Taifa, basi chama changu na serikali yangu wataamua. Lakini nitaendelea kufanya hivyo kila ninapolipata neno. Nilikuwa nikifanya hivyo katika awamu ya kwanza, katika awamu ya pili na nitafanya hayo katika awamu ya tatu. Tuzungumze kama anavyosema huyu Mbunge mwenzangu wa Ukererewe kwamba tuzungumze ideas. Let us not discuss people; let us not discuss events; let us discuss ideas. Hili lipo tulifanyeje. Watu wananung’unika Mwembechai. Watu wameuawa. Waziri kasema atafanya uchunguzi mpaka leo hakuna uchunguzi. Hapa anatueleza maneno mengi., ameyapata wapi?
 
Mheshimiwa Spika, nasema na nimesema mara nyingi kwamba nchi hii hakuna ghasia za kidini. Kuna ghasia zinazoonyesha insensitivity ya askari wake. Sasa ningemwomba Waziri leo afanye kama vile wanavyofanya kwa wengine. Kama kulikuwa na Tume mbili za kuchunguza ghasia za Arumeru ambako hakufa hata mtu mmoja, kama kulikuwa na shughuli za kelbu, mbwa, immigration, mpaka Jaji Mkuu akatoa kauli, aunde Tume ya kuchunguza mauaji ya Mwembechai. Halafu ile Tume impe ripoti na ripoti ya Tume ile ndiyo ailete atuambie Tume imeniambia hivi na hivi. Kukosa kufanya hivyo ni hatari. (Makofi)
 
Mheshimiwa Spika, muda wenyewe umekwisha. Kengele sijaisikia. Niongee dakika moja.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa muda wangu umekwisha nataka kusema kwamba naunga mkono hoja ya Waziri lakini natazamia kwamba haya niliyomwuliza atayajibu kwa sababu yapo katika manufaa yake, manufaa ya Taifa na manufaa yetu wote.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi).
Share this article :

0 comments:

Speak up your mind

Tell us what you're thinking... !

ZILIZOSOMWA SANA.

Followers

Blog Archive

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Proudly powered by Blogger
Copyright © 2011. Msamaa. - All Rights Reserved
Template Design by Creating Website Published by Mas Template