- Msamaa.
Headlines News :
Home » »

Written By Unknown on Thursday, May 2, 2013 | 5:45 AM


MAKALA
KAMATI YA KINA MAMA WA KIISLAMU
TAARIFA YA MATUKIO JUU YA UNYANYASAJI WA POLISI DHIDI YA WANAWAKE WA
KIISLAMU KUFUATIA TUKIO LA UVAMIZI WA POLISI MSIKITI WA MWEMBECHAI TAREHE 12/02/98 - 29/03/98.
I. UTANGULIZI:
Hii ni taarifa iliyoandaliwa na Kamati ya Kupigania hHaki ya Kinamama wa Kiislamu kuelezea kwa mukhtasari madhila yaliyowapata Wanawake wa Kiislamu kuhusiana na kadhia ya mauaji ya Waislamu katika Msikiti wa Mwembechai.
MAUAJI YA POLISI
II. KADHIA YA MSIKITI WA MWEMBECHAI:
1. Asili ya tukio:
Kadhia ya mauaji yaliyofanywa na polisi katika msikiti wa Mwemebechai, jijini Dar es Salaam inafungamana na mambo mawili la kwanza la mambo hayo ni vita dhidi ya mihadhara ya Waislamu ya mlingano wa dini (comparative religion).
La pili ni jitihada za kujaribu kuvunja nguvu za Waislamu kwa njia mbalimbali ili kuondoa vikwazo na upinzani katika utekelezaji wa maelekezo na mikakati ya kuudhulumu na kuuhujumu Uislamu na Waislamu.Katika kutekeleza hili la pili, juhudi zimekuwa zikifanywa zisiweze kuwepo taasisi imara za Waislamu kama vile jumuiya huru na misikiti yenye msimamo wa kupigania maendeleo ya Uislamu. Ni katika hali hii ndio migogoro katika misikiti mbalimbali ikiwemo wa Mwemebechai imekuwa ikipewa nguvu.
2. MLOLONGO WA MATUKIO:
Mlolongo wa matukio yaliyopelekea kuuawa kwa Waislamu katika msikiti wa Mwembechai limeanza na tamko la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Benjamin William Mkapa, alilolitoa kule Tabora katika sherehe za Kanisa la Moravian ambapo aliahidi kwa hamasa kuwa atahakikisha kuwa anakomesha mihadhara.Haraka haraka ukafuata mkutano wa Waziri Mkuu Mh. Fredirck Sumaye na Wakuu wa wilaya na mikoa na kuwaagiza wahakikishe mihadhara haifanyiki katika maeneo yao. Baada ya hapo ukafuatia mkutano wa Mh. Waziri wa Mambo ya Ndani na viongozi wa Kikristo na Kiislamu kuzungumzia suala la mihadhara. Japo muafaka ulifikiwa katika mkutano huo kuwa si sawasawa kuipiga mihadhara marufuku, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mh. Yusuf Makamba akafuatia na amri ya kupiga marufuku katika mkoa wa Dar es Salaam.Amri hii ikafuatiwa na amri ya kuwakamata wahadhiri, viongozi wa vikundi vya mihadhara pamoja na maimamu wa misikiti inakofanyika mihadhara. Baada ya hapo, wahadhiri kadhaa pamoja na maimamu wa misikiti walikamatwa. Na msako wa kuwatafuta wengine ijapokuwa hakuna "arrest warrants" zilizotolewa dhidi ya watuhumiwa na zaidi ya hivyo ni kuwa taratibu zilizotumika zilikuwa ni za kutia mashaka. Taratibu kama vile watuhumiwa kufuatwa majumbani mwao usiku wa manane, n.k.Kilele cha mlolongo huu ilikuwa ni tarehe 12/2/98 siku alipokamatwa Ust. Magezi Shaaban pale katika msikiti wa Mwembechai. Hakuna anayepinga kuwa iwapo mtu anatuhumiwa kwa kosa lolote la jinai, hata akiwa kiongozi mkubwa wa kidini, ipo haki ya mtu huyo kutiwa mbarano. Tatizo la siku hii lilikuwa ni utaratibu walioutumia askari polisi waliokuja msikitini hapo kumkamata Ust. Magezi. La kwanza, hawakuwa na "arrest warrant". La pili hawakutumia utaratibu wa kawaida wa kipolisi wa kujitambulisha na kumweleza mtuhumiwa kuwa anawekwa chini ya ulinzi na kumpa haki ya kujua kwa nini anawekwa chini ya ulinzi. Hizi zote ni taratibu za lazima za kisheria, na sheria haikuziweka hizi bila sababu.Sababu za msingi ni kuzuia askari polisi kutumia vibaya nguvu zao za kisheria kuwanyanyasa raia. Pili, ili kuwatoa mashaka raia wanaohusika kuwa wao au jamaa zao hawatiwi nguvuni kwa lengo la kuwahujumu. Hivyo kuvunjwa kwa taratibu hizi siku hiyo ndiko kuliko sababisha ghasia zilizotokea siku hiyo.
Nini walifanya polisi hao siku hiyo ni kitendo kinachostahiki na kila mpenda amani kulaaniwa. Askari hao walikwenda katika eneo la msikiti huo ambapo walimkuta Sheikh Magezi. Wakaegesha gari lao, nalo pia la kiraia, karibu na pale alipo kisha wakamvamia ghafla na kumkwapua kwa nguvu juu juu na kumtupia garini na kuondoka naye ghafla kama walivyokuja.Wapo watu wengi walioshuhudia tukio hili ukianzia na waumini waliokuwepo nje ya msikiti huo pamoja na wapita njia.Tukio hili lilileta hali ya wasiwasi mkubwa juu ya nia yake na mashaka juu ya usalama wa Sheikh Magezi. Na lilikuwa ni tukio lililoamsha ari kwa waumini na wafuasi wa Sheikh Magezi kutaka kumtetea pengine kwa kutojua waliomkamata ni askari polisi. Na vipi watajua kwani si utaratibu wa kipolisi. Na kwa polisi kuja kumkamata kiongozi mkubwa wa kidini kama yeye mbele ya wafuasi wake na kwa utaribu huu wa kukwapuana kwa jinsi hii ni kuwachokoza Waislamu kwa makusudi. Kwa hivyo yale mawazo ya wengine wasemao ya kuwa tukio lile lilipangwa makhsusi ili liwe chanzo cha kuyatekeleza yale yaliyotekelezwa na polisi msikitini pale huenda yakawa kweli.Waislamu wakajitoa kwa ujasiri kumtetea kiongozi wao aliyekuwa akitekwa nyara na watu wasiowajua mbele ya macho yao. Purukushani likatokea lakini askari hao walifanikiwa kutoweka haraka na Bwana Magezi ndani ya gari yao. Baada ya tukio hili ambalo lilitokea majira ya saa tisa alasiri, gari kadhaa za polisi wenye silaha zilifika katika eneo la msikiti na askari wengi wakaletwa. Hali hii ilisababisha wasiwasi mkubwa na pia ilivuta watazamaji wengi waliokuwa wakishangaa kuna nini. Baada ya muda mfupi watu walikuwa wengi sana na askari kujikuta wamezungukwa kila upande. Pengine hali hiyo ndiyo iliyowatia hofu kiasi cha kuwafanya waanze kurusha mabomu ya moshi kuwatimua watu hao waliojaa hapo wakiwemo waumini wa Kiislamu, wa Kikristo na wengineo.
Wengi wanaamini kuwa iwapo askari hao wangeamua kuondoka, basi na kadamnasi yote ingetawanyika kimya kimya kwani wengi wao walikuja kwa kuwashangaa wao wakitaka kujua kuna nini. Hakukuwa na vurugu yoyote. Wakati askari hao wanafika ilikuwa Waislamu msikitini hapo wanaandaa ujumbe wa watu kwenda polisi kufuatilia dhamana ya Sheikh Magezi na kujua hatima yake. Hivyo kila mtu alishangaa ikiwa ni pamoja na Waislamu hapo msikitini.Vurugu kubwa ikatokea, watu waliokuwa wamekusanyika hapo walitawanywa kwa virungu, mateke na mabomu ya moshi (machozi). Baadhi ya vijana waliokumbwa na hali hiyo walianza kujitetea kwa kurusha mawe. Na wengine, pengine kwa kughadhibishwa na dhulma na uonevu huu dhahiri wa polisi dhidi ya raia wakaanza kupiga magari ya Serikali mawe.Watu wengine walikimbilia msikitini kujisalimisha wakawa pamoja na wale waliokuwemo humo baada ya swala ya alasiri wakiwemo wanawake. Baada ya watu kutawanyika, askari waliuzingira msikiti huo, wakabaki hapo hadi usiku wa manane. Wakati wa usiku umeme wa msikiti ulikatwa na msikiti ukabaki kiza totoro.Baada ya kukatwa umeme, askari wakachukua fursa hiyo kuuvamia msikiti na kuvunja milango. Kilichofuata walirusha mabomu mengi ya machozi pamoja na ya moshi wa kuwasha. Wengi katika wanawake waliwashwa sana kiasi hata cha kuvua nguo zote. Askari wakaingia msikitini kuwapiga kwa virungu, mateke, n.k. waliokuwemo ikiwa ni pamoja na wanawake. Wanawake wengine damu nyingi ziliwatoka kiasi cha kuchafua mazulia ya msikiti.Madhila mengi yalifanywa dhidi ya wanawake hao wa Kiislamu wakati wa kukamatwa ikiwa ni pamoja na mashambulio ya aibu (indecent assault na mengine ya aibu zaidi.Siku ya tarehe 13/2/ 98 ilikuwa ndio siku walipouawa Waislamu kwa kupigwa risasi makusudi na polisi. Mpaka leo bado idadi kamili ya waliouawa haijaweza kuthibitika kwa uhakika. Kinachojulikana kwa uhakika ni kuwa Waislamu wawili waliuawa kwa kulengwa shabaha na polisi. Muislamu mwingine mmoja alikufa kwa athari ya moshi baada ya kuangukiwa na bomu la machozi kifuani. Pia mtoto mmoja mchanga alifariki baada ya bomu la moshi kuanguka uani mwa nyumba ambako yeye na mamaye walikuwa wakati ghasia zikiendelea barabarani. Pia katika siku hii, kijana mdogo Chuki Athumani, mwanafunzi wa shule ya Alharamain alipigwa risasi kifuani na kujeruhiwa vibaya. Mpaka sasa kijana huyu bado yuko katika Hospitali ya Muhimbili akiendelea na matibabu huku akiwa na pingu kitandani.
Na taarifa za watu zaidi waliopigwa risasi zimepatikana ambapo wengine walitibiwa katika mahospitali binafsi kwa kuhofu kukamatwa.Chanzo cha vurugu za siku hii ya tarehe 13/2/98 hakitofautiani na cha jana yake. Yaani askari kuwachokoza Waislamu na raia wengine waliokusanyika hapo kwa kuanza kuwatupia mabomu ya moshi, kupiga risasi hewani na kuanza kuwaandama na kuwapiga. Watu hao walianza kujibu kwa kuwatupia mawe askari hao kuonyesha kukerwa kwao na tukio hilo. Zaidi ya hivyo waliyapiga mawe magari ya Serikali na mashirika ya umma. Walichoma moto matairi ya magari ili kupunguza athari za mabomu ya moshi.Vituo vya polisi (police posts) vilivamiwa na watu walioshiriki vurugu hizo, magari yanasemekana yalichomwa moto katika maeneo mbali mbali jijini tangu magomeni, manzese, Ubungo, Buguruni hadi Temeke.
Ghasia hizo zimeionyesha Serikali jambo moja kubwa nalo ni kuwa raia wake hawatokuwa tayari siku zote kuona dhulma ikitendeka. Na zaidi; Waislamu katika nchi hii hawatokubali kuonewa kila siku, hata kama muoneaji ni chombo chenye maguvu.Zaidi ya wale waliouawa na kujeruhiwa vibaya watu wengi walikamatwa na kuswekwa rumande. Idadi ya waliokamatwa katika matukio ya tarehe 12 na 13 Februari ni zaidi ya mia mbili (200).
III. UDHALILISHAJI WA POLISI DHIDI YA WANAWAKE WA KIISLAMU:
Katika kadhia hii, wanawake wa Kiislamu wameonyesha ujasiri mkubwa unaostahiki pongezi. Vile vile, wamepata madhila makubwa ambayo tunayasimulia hapa kwa mukhtasari kama ifuatavyo:(1) Kitendo cha askari wa kiume kuingia eneo la wanawake msikitini, tena wakiwa na viatu miguuni, ni unyanyasaji wa kijinsia. Zaidi ya hapo, askari hao waliwapiga kuwashikashika hata mpaka sehemu za siri wanawake hao, ikiwa ni pamoja na kuwavua nguo na kuwapiga mabomu ya kuwasha yaliyowalazimisha baadhi ya wanawake wafikie hata kuvua nguo bila kupenda.
(2) Wanawake hao walipofikishwa magerezani walivuliwa nguo zote na kupekuliwa hata sehemu za siri. Tena walifanyiwa hayo na askari wa kiume kinyume hata na taratibu, sheria na katiba ya nchi inavyoeleza kuwa ni haki ya kila raia kuheshimiwa utu wake na haramu kudhalilishwa au kuaibishwa. Pia, ni haramu kwa wanawake kupekuliwa na askari wa kiume, sembuse kuvuliwa nguo. La kusikitisha zaidi, kitendo hicho kimefanywa hadharani mbele ya watu wakiwemo mahabusu wenzao wa kiume. Kwa hili ni haki yetu kudai Mkuu wa Magereza ajiuzulu mara moja au afukuzwe kazi.Na tunahisi ya kuwa jambo hili limefanywa makusudi kutokana na chuki za makafiri juu ya utukufu wa HIJAB katika Uislamu na ili iwe njia ya kuwadhalilisha wanawake watukufu wa Kiislamu.
(3) Wanawake wa Kiislamu pia walipewa adhabu za kudhalilisha wakiwa mikononi mwa polisi na magerezani. Wanawake hao walirushwa kichura wakiwa uchi. Kwanza ni kosa kuwapa adhabu kwa kuwa mahabusu ni watuhumiwa tu, bado hawajapatikana na kosa lolote kisheria. Pili ni kitendo kiovu mno kuwavua nguo wanawake wa Kiislamu na kuwatweza adhabu juu yake ili kuwadhalilisha. Kwa tukio hili, ni haki yetu kumwelekea Mwenyezi Mungu (S.W.T) ili azielekeze ghadhabu zake dhidi ya wote waliohusika.Tunakumbusha pia kuwa, sababu iliyowafanya Waislamu kutangaza vita dhidi ya Mayahudi wa Banu Qainuqa wa Madina wakati wa Mtume (s.a.w) ni kitendo cha wanaume fulani wa Kiyahudi kumfunua nguo mwanamke wa Kiislamu sokoni huku wakimdhihaki na kumcheka. Kitendo walichofanya askari hawa ni kikubwa mara mia zaidi kuliko cha mayahudi wale. Basi vipi leo wanaume wa Kiislamu wanajibweteka tu hali ya kuwa sisi wanawake wa Kiislamu tunadhalilishwa kiasi hiki. Je hawaijui Aya ya Qur-an isemayo:Na mna nini hampigani katika njia ya Mwenyezi Mungu na (katika kuwaokoa) wale waliodhaifu katika wanaume na wanawake na watoto- ambao husema: "Mola wetu! Tutoe katika mji huu ambao watu wake ni madhalimu, na tujaalie tuwe tuna mlinzi anayetoka kwako na tujaalie tuwe na wa kutunusuru anayetoka kwako. (4:75)
(4) Pia, msiba mkubwa uliowakumba wanawake wa Kiislamu juu ya tukio hili ni kwa wake wa viongozi wa Kiislamu, kama vile Sheikh Omar Albashir na Ust. Ponda Issa Ponda, na wake wa watuhumiwa wengine wa Kiislamu wamekuwa wakiendewa majumbani mwao usiku wakati waume zao hawapo, kisha huchukuliwa na kupelekwa wasiko kujua jamaa zao wala ndugu zao. Na katika kisa kimoja, wake wa Sheikh Omar Albashir walitolewa usiku na nguo za ndani tu kuzungushwa mitaani.
(5) Katika jumla ya madhila haya ni pamoja na kusemezwa maneno ya kashfa, kukejeliwa na kudharauliwa wakiwa mikononi mwa polisi na magerezani.
(6) (i) La mwisho na kubwa zaidi, ni pale polisi Mkoa wa Dar es Salaam walipo jaribu kuwaziba midomo wanawake wa Kiislamu pale walipoupiga marufuku mkutano wao wa tarehe 29/3/98 uliopangwa kufanyika Diamond Jubilee jijini. Kitendo hicho kilivunja sheria na katiba ya nchi. Sheria ya nchi inatoa uhuru wa kujumuika, uhuru wa kukusanyika pamoja, na uhuru wa kupashana habari na uhuru wa mtu kutoa mawazo yake. Kitendo cha kuupiga marufuku mkutano ule kimekuwa na athari ya kumnyima mwanamke wa Kiislamu haki zake zote hizi za kikatiba. (ii) Mkutano ule ulikuwa ni halali kwa hali zote, moja umeitishwa na Kamati ya Kupigania Haki za Waislamu Tanzania ambacho ni chombo cha kisheria kuwa kimeundwa na taasisi za Kiislamu zinazotambulika kisheria. Pili, mkutano ule haukuhitaji kibali kwa kuwa ni mkutano wa ndani. Yaani ulikuwa ufanyike Diamond Jubilee Hall.
Tatu, kisingizio cha Kamanda Gewe cha kuupiga marufuku mkutano ule kuwa utavunja amani hakina mashiko ya kisheria. Kwa maelezo yake mkutano huo ungevuruga amani kwa kuwa eti ulikuwa na lengo la kujadili mauaji ya polisi Mwembechai. Anasahau ya kuwa sasa raia wana haki zilizo ndani ya katiba. Miongoni mwa haki hizo ni uhuru wa kuwasiliana na uhuru wa kubadilishana mawazo hata kama ni katika kukosoa vitendo vya Serikali. Hivyo ilikuwa ni haki kwetu kama ilivyo leo kujadili suala hili bila kipingamizi cha polisi. Hivyo ni kuonyesha kupitwa na wakati au ni kitendo cha makusudi cha ukandamizaji kwa Bwana Gewe kupiga marufuku mkutano wetu wa tarehe 29/3/98.
(7) Jambo la mwisho, ni kuwa kamati iliyoandaa taarifa hii imesikitishwa sana na kukatishwa tamaa na ukimya wa vyombo vya haki za wanawake juu ya suala hili. Hawakupatikana wa kujua kulikoni. Jambo hili limetutia unyonge na kutuondoa imani juu ya ukweli wa vyombo hivi kama kweli vinapigania haki za wanawake au ni vyama vya walaji tu.
Wabillah Tawfiiq.
Maazimio ya mkutano wa Akina mama1.
Kuunda Kamati ya kinamama wa Kiislamu ya kufuatilia maamuzi ya mkutano. Kazi ya Kamati hiyo zitakuwa:
(1) - Kukusanya na kuratibu taarifa za unyanyasaji wa Wanawake wa Kiislamu kuhusiana na tukio hili na kupendekeza hatua za kuchukuliwa.(2) - Kuyafikisha madai na walalamiko ya Wanawake wa Kiislamu kuhusiana na tukio hili kwa vyombo vinavyo husika Serikalini.
(3) - Kusambaza taarifa za tukio hili na za unyanyasaji na udhalilishaji wa Wanawake wa Kiislamu ndani na nje ya nchi.2. Serikali iwaombe radhi Waislamu na hususani kina mama wa Kiislamu kutokana na kitendo cha kudhalilishwa kina mama wa Kiislamu na watendaji wa Serikali hasa Polisi na askari magereza.3. Serikali iunde tume huru ya uchunguzi kuchunguza suala la udhalilishwaji na unyanyasaji wa wanawake wa Kiislamu katika suala hili na wanaohusika wote washitakiwe mahakamani4. Serikali iunde tume huru ya uchunguzi kuchunguza mauwaji yaliyofanywa Mwembechai na polisi na ukiukwaji wote wa sheria uliofanywa na polisi katika tukio hili na waliohusika wote wafikishwe mahakamani.5. Rais awafukuze kazi mara moja Waziri wa Mambo ya Ndani, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na Kamanda wa Polisi mkoa wa Dar es Salaam na Mkuu wa Magereza Tanzania.6. Kina mama wa Kiislamu tuunde taasisi huru ya kupigania haki za wanawake bila ubaguzi kutokana na ukweli kuwa taasisi zilizopo za haki za wanawake zimeshindwa au zimepuuza matatizo ya wanawake wa Kiislamu.
7. Wanawake wote waliohudhuria mkutano wawafikishie wale ambao hawakuhudhuria yale yote yaliyojadiliwa na kuazimiwa kwenye mkutano.8. Wanawake wa Kiislamu wajitahidi kuujua Uislamu vilivyo ili wasiyumbishwe na propaganda za ma adui wa Uislamu.
9. Kila mama wa Kiislamu ajitahidi kuwalea wanawe malezi ya Kiislamu na kwa kuanza kila mama ampeleke mtoto wake madrasa.
Share this article :

0 comments:

Speak up your mind

Tell us what you're thinking... !

ZILIZOSOMWA SANA.

Followers

Blog Archive

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Proudly powered by Blogger
Copyright © 2011. Msamaa. - All Rights Reserved
Template Design by Creating Website Published by Mas Template