- Msamaa.
Headlines News :
Home » »

Written By Unknown on Friday, April 19, 2013 | 7:21 AM


 
IMEANDIKWA NA:   Mohamed Said
BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM
Imebidi kuandika makala hii kutokana na makala iliyoandikwa na Kaanaeli Kaale yenye kichwa cha habari 'Kusigana kwa matokeo baina ya shule za Kikatoliki na Kiislamu' (Mwananchi 17 Oktoba 2006). Makala ilikuwa inaeleza yaliyojadiliwa katika mkutano ulioandaliwa na Shirika la Elimu ya Sheria Tanzania (TANLET) katika moja ya harakati za kumuenzi hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Katika mkutano huo, ilielezwa kuwa shule za Kikatoliki ndiyo shule bora zinazoshika nafasi 'kumi bora' kwa kutoa matokeo mazuri ya mitihani na shule za Kiislam ndiyo 'zinazoshika mkia' katika kutoa matokeo mabaya. Ama taarifa hizo za shule za Wakatoliki kufanya vyema katika mitihani si habari mpya ni jambo linalotangazwa na vyombo vya habari kila mwaka kwa hiyo linafahamika. Ila kitu cha kushangaza ni kuwa kimezidi nini hii leo hadi ikawa ni muhimu kujadili ufanisi wa shule za Waislam hadharani kisha tukapewa ushauri kuwa Waislamu tujifunze kutoka kwa Wakatoliki ili nasi shule zetu zifanye vyema kama zao ili huu upogo wa elimu kati ya Waislam na Wakristo utoweke?

Ushauri huu umenitia simanzi kubwa na ndiyo hasa sababu ya kuandika makala hii. Bubu alizungumza kwa uchungu wa mwanaWe ni msemo mashuri. Leo hii sisi Waislam tumekuwa watu wa kusaidiwa na Wakatoliki tuelimike! Waswahili tuna msemo 'Akutukanae hakuchagulii tusi.'

Laiti hao wanaotushauri wengeijua tarikh (historia) yetu wasingetamka hayo. Wamishionari wameingia nchi hii wamewakuta babu zetu pwani yote ya Afrika Mashariki na bara kulikokuwa na Uislam wakijua kusoma, kuandika na kuhesabu. Lakini haya tuyaache yanahitaji muda kueleza.Turudi kwenye mada husika.

Awali ya yote ni kumkejeli hayati Mwalimu Julius Nyerere kwa kuadhimisha kifo chake kwa mkutano wa kuzungumza kubaki nyuma kwa Waislam katika elimu kwa kuwa, kwa kauli yake mwenyewe alisema kuwa upogo katika elimu baina ya Waislam na Wakristo uliorithiwa na serikali yake kutoka kwa Waingereza yeye ameuondosha katika kipindi cha utawala wake. Kauli hii aliitoa Novemba 5, 1985 katika hotuba aliyoitoa Ukumbi wa Diamond Jubille akiwaaga Wazee wa Dar es Salaam. Kabla hajastaafu urais, Mwalimu Nyerere alikuwa na haya ya kueleza kuhusu suala la elimu ya Waislam:

"Waislam wametupa nafasi kupitia sera yetu ya elimu, kurekebisha upogo. Sasa nipo katika hali ya kufurahia kwa kuwa wakati mwingine sielewi kama mbunge mpya, waziri, au katibu mkuu katika wizara zetu za serikali, ni mwislam au mkristo au hana dini labda pale jina lake la kwanza linapotoa utambulisho. Na hata hivyo hiyo siyo njia ya kuaminika kutoa utambulisho wa dini kwa kuwa tuna wakristo wenye majina ya Kiislam, na waislam wenye majina ya Kikristo. Kuvumiliana huku ndiyo sababu; nilichofanya mimi ni kuzungumzia maadili haya kwa niaba yenu." Sasa ikiwa Baba wa Taifa keshawanyanyua Waislam katika elimu na kafurahishwa na kazi yake nzuri, hawa wanaokuja leo na kusema kuwa Waislam wako nyuma wanataka kumshika uongo Mwalimu Nyerere? Wanataka hii leo kumsimamisha Baba wa Taifa kizimbani ajibu tuhuma za kuwakandamiza Waislam katika elimu?

Kwa hakika si adabu wala ustaarabu kupinga kauli ya Mwalimu Nyerere kuwa hakusema kweli katika tatizo la elimu ya Waislam. Je, hawa waliokuja na hoja hii nyeti wanatambua uzito wa kauli zao hasa katika kipindi hiki ambapo Kanisa Katoliki lipo katika mchakato wa kumfanya Mwalimu Nyerere kuwa mtakatifu? Hivi hawasikii nchi nzima inavyomtukuza Mwalimu Nyerere kwa sifa za uadilifu? Majibu wanayo wenyewe. Hili la kwanza.

Waswahili tuna msemo mwingine "Asiekujua hakuthamini.' Historia ya kupigania uhuru wa Tanganyika ni ushahidi wa juhudi za Waislam katika kujitafutia elimu. Wakati wa kupigania uhuru wa Tanganyika tatizo la elimu ya Waislam ndiyo chanzo cha kuanzishwa chama cha upinzani Tanganyika All Muslim National Union (AMNUT) pale akina Ramadhani Mashado Plantan na wenzake walipotoka TANU mwaka 1958, sababu kuu wakihofu Wakristo waliokuwa na elimu kuja kushika madaraka peke yao katika Tanganyika huru na kuwaweka Waislam pembeni.

Suala hili lilileta mjadala mkubwa katika TANU. Ukipenda unaweza ukarejesha msuguano huu ndani ya TANU nyuma kidogo mwaka huo huo wa 1958 pale Sheikh Suleiman Takadir (aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa TANU Dar es Salaam) alipomkabili Nyerere uso kwa uso na kumtuhumu kwa udini. Haya yalitokea baada ya Uchaguzi wa Kura Tatu pale TANU ilipoteua Wakristo kusimama kugombea nafasi za Legislative Council na kuwaweka Waislam wana TANU pembeni. Lakini katika hili palikuwa na sababu maalum za msingi. Hapa si mahali pake kuzieleza. Kipande hiki cha historia kinaogopwa sana na kwa ajili hiyo nami sitokiendeleza.

Baada ya uhuru kupatikana mwaka 1961 Waislam kwa pumzi ile ile waliyopigania uhuru wakaingia katika harakati za kutafuta elimu. Hawakusubiri wajengewe shule na serikali. Wazee wetu waliitisha mkutano chini ya taasisi zao - Daawat Islamiyya (Mwito kwa Waislam), Jamiatul Islamiya fi Tanganyika (Umoja wa Waislam wa Tanganyika na Muslim Education Union kujadili nini kifanyike ili Waislam wapate elimu waliyodhulumiwa na wakoloni. Mipango ikatayarishwa ya kujenga shule Tanganyika nzima na mwishowe kujenga Chuo Kikuu cha kwanza kwa Waislam katika Afrika ya Mashariki. Huu ndiyo ukweli wa historia ya Waislam. Waislam hatuna sifa ya uvivu wala kusubiri misaada kutoka Ulaya. Ufupi wa maneno ni kuwa shule sabini zilijengwa na EAMWS na jiwe la msingi la Chuo Kikuu liliwekwa na Mwalimu Nyerere mwenyewe kwa mkono wake. Sasa la kujiuliza ni kuwa juhudi hizi zote za kutafuta elimu ziliishia wapi na nini sababu yake


Ufupi wa mambo ni kuwa Mwalimu Nyerere alipiga marufuku jumuia zote za Kiislam mwaka 1968 na akwaundia Waislam Baraza Kuu la Waislam Tanzania (Bakwata). Historia ya TANU na uhusiano wa Mwalimu Nyerere na Waislam ina majibu ya swali hili. Mzee Rashid Mfaume Kawawa yu hai na ni shahidi wa yote yaliyopita katika kipindi kile. Mzee Kawawa anaweza kutoa majibu ya kitendawili hiki.Hili la pili.

Waswahili tuna msemo mwingine 'Chokochoko mchokonoe pweza binadamu hutamuweza.' Imekuwa vyema leo hii, hili tatizo la elimu ya Waislam limesemwa na wasiokuwa Waislam maana laiti tungelisema Waislam tungeambiwa 'siasa kali' tunataka kuvuruga 'amani na utulivu' kama alivyosakamwa marehemu Profesa Kighoma Abdallah Ali Malima alipoionya serikali kuhusu hujuma dhidi ya Waislam kama alivyoikuta ndani ya Wizara ya Elimu. Mwaka 1987 Profesa Malima aliteuliwa kuwa Waziri wa Elimu akiwa Muislam wa kwanza kushika nafasi hiyo. Mawaziri wanane waliopita walikuwa Wakristo. Kulikuwa na malalamiko kutoka kwa Waislam kuwa wizara hiyo imegeuzwa jimbo la Wakristo hasa Wakatoliki, maana ilifika hadi padri (Simon Chiwanga) kuteuliwa na Mwalimu Julius Nyerere kuongoza wizara hiyo.

Profesa Malima aliposhika wizara hiyo aliona upo umuhimu wa kufanya marekebisho kadhaa ili kurejesha imani ya Waislam katika wizara hiyo.

Kulikuwa na tuhuma kuwa Wizara ya Elimu ilikuwa ikiwabagua vijana wa Kiislam kupata nafasi katika vyuo vya elimu ya juu na ilikuwa ikizuia kupanda vyeo kwa Waislam. Tatizo hili liliwekwa wazi kwa mara ya kwanza mwaka 1981 na wanafunzi wa Sheikh Malik na ndiyo ikawa sababu ya yeye kufukuzwa nchini.Profesa Malima alipoona dhulma ile iliyokuwapo katika wizara ile dhidi ya Waislam, aliwateua Waislam wanne kushika nafasi katika kurugenzi mbalimbali. Hali kadhalika Profesa Malima alibadili mtindo uliokuwapo wa kutumia majina badala ya namba katika mitihani. Baada ya mabadiliko yale mwaka ule idadi ya wanafunzi Waislam walifaulu kuingia sekondari ilipanda kwa asilimia 40. Profesa Malima akaandika taarifa ya siri kwa Rais Ali Hassan Mwinyi kumtaarifu udini ulioota mizizi Wizara ya Elimu.

Katika taarifa ile kwa rais Mwinyi, Profesa Malima alieleza kuhusu kudumazwa kwa Waislam kwa makusudi katika mgawo wa elimu. Taarifa hii ilivujishwa kwa vyombo vya habari na kwa Wakristo wengine.

Katika watu walioipata taarifa hii ni Mwalimu Nyerere akiwa mstaafu lakini akiwa Mwenyekiti wa CCM. Hiki kisa ni kirefu inatosha tu kusema kuwa yaliyomkuta Profesa Malima kwa kutaka kutenda haki hakuna asiyeyajua. Alisimamishwa kizimbani mbele ya Kamati Kuu ya CCM kwa udini na akatolewa Wizara ya Elimu.

Lakini kabla hatujatoka katika nukta hii ningependa kueleza kuwa katika moja ya sababu kuu iliyofanya serikali ikifungie kitabu kilichoandikwa na Profesa Hamza Mustafa Njozi Mwembechai Killings and the Political Future of Tanzania ni kule kuanika hadharani mbinu zinazotumika nchini kuwanyima Waislam elimu. Profesa Njozi's aliandika:

"…Arabia (May, 1985) wrote under the heading "A Closed Door to the Corridors of Power": 'The majority of pupils in Tanzanian primary schools are Muslim (80 percent), a percentage which dwindles to 15-20 percent in secondary schools, sinking to a mere five percent at University level'. Almost fifteen years later, on 2 February, 1999 the Member of Parliament for Kigamboni Hon. Kitwana Kondo told the parliament that out of every 100 students who sat for the standard seven examination in Dar es Salaam in the year 1998, 71 were Muslim and 29 Christian. But out of every 100 students selected to join government secondary schools only 21 were Muslim while 79 were Christian. The MP wanted to know whether Muslim children were inherently dull (An-Nuur, February 5-11, 1999).

Yaliyomfika Mzee Kondo nayo yanafahamika. Yapo mengine mengi yaliyofichuliwa katika kitabu hicho yanayohusu mbinu zinazotumiwa katika kuhakikisha Waislam wanabaki nyuma lakini hapa hii leo si mahali pake. Hili la tatu. Sasa leo Waislam tunaambiwa tukajifunze mbinu za Wakatoliki ili tuboreshe shule zetu…tukajifunze mbinu gani? Kuhodhi madaraka na nafasi katika Wizara ya Elimu na kujipendelea kwa kuwanyima Wakristo nafasi za elimu ya juu? Hili ni muhali kwa Waislam.

Hata kama tungekuwa na uwezo nalo Uislam unakataza vyote kudhulumu na halikadhalika kukubali kudhulumiwa. Kwa Waislam elimu ni fardh jambo ambalo ni lazima litekelezwa na kwa kushindwa kufanya hivyo mja huandikiwa dhambi. Hatuhitaji kujifunza kwa yeyote yule kuhusu umuhimu wa elimu. Historia ya Waislam wa Tanganyika inapingana na dhana hiyo. Sasa tuzungumze kuhusu matokeo mabaya ya shule za Waislam. Kwangu mimi kwa uzoefu wangu na yale ambayo nayaelewa kuhusu historia ya Waislam wa Tanganyika hili linahitaji uchunguzi zaidi ili tudhihirishe kuwa kweli shule za Waislam zinashika mkia na za Wakatoliki ndiyo zinazotawala 'kumi bora' miaka nenda miaka rudi kwa haki au ndiyo hizo hizo mbinu alizotahadharisha marehemu Profesa Malima na Mzee Kondo akahoji katika Bunge na zilizosababisha kitabu cha Profesa Njozi kifungiwe na serikali ya Rais Benjamin William Mkapa?

Katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia, Wajerumani walikuwa wakiwakamata Wayahudi Poland na kwingineko Ulaya wakawatoa katika nyumba zao nzuri na kuwarundika katika ghetto. Umati mkubwa wa watu waliokuwa na nafasi na heshima zao katika jamii wakajikuta wanaishi katika sehemu finyu, chafu isiyo na mifereji ya maji taka wala maji safi. Wajerumani wakawa wanatuhumu na kuwakashifu Wayahudi kwa uchafu. Katika hali kama hiyo vipi utategemea mtu awe msafi? Huu ndiyo mfano wetu Waislam hii leo. Hatuna fursa sawa kama walizonazo Wakristo, shule zetu duni na juu ya hayo bado tunahujumiwa kisha tunalaumiwa kwa kutotoa matokeo mazuri.

Hili la nne ambalo ningependa lizingatiwe.
Kwa taarifa kwa wale wasiojua ni kuwa Organisation of Islamic Conference (OIC) walitaka kujenga Chuo Kikuu Dar es Salaam. Watendaji Wakristo katika Wizara ya Elimu walipiga vita mradi huo na mwisho chuo hicho kikajengwa Mbale, Uganda. Darul Iman ya Saud Arabia ilitaka kujenga shule ya ufundi Kibaha na yale yaliyoikuta OIC na wao yaliwafika sawia. Huu ndiyo ukweli wa nchi yetu. Waswahili tunapokabiliwa na mtu mwingi wa mbinu na ghilba tuna msemo maarufu tunautumia kumweleza mtu huyo. Tunasema 'Kwa nyakanga hakwishi nyimbo.'

Kichwa kinaniuma kutaka kujua hii agenda ya kudumazwa kwa Waislam katika elimu iliyozuka ghafla bin vuu ni ya nani hasa, yao wenyewe TANLET au wametumwa na mtu? Kama wametumwa, nani huyu kawatuma na kwa maslahi ya nani? Agenda hii si ndiyo iliyomfanya Profesa Malima aandamwe na hatimaye kufukuzwa Wizara ya Elimu? Agenda hii si ndiyo iliyomfanya Mwalimu Nyerere amfukuze Tanzania Bara Mufti Sheikh Hassan bin Ameir na kumrejesha Zanzibar chini ya ulinzi mkali na kuwaweka kizuizini wafuasi wake?

Agenda hii si ndiyo iliyomfanya Sheikh Hussein Malik afukuzwe nchini na serikali ya Mwalimu Nyerere baada ya wanafunzi wake kupitia taasisi yao ya Waandishi wa Kiislam (Warsha) kuzungumza kuhusu tatizo la elimu ya Waislam? Hii leo kimebadilika nini? Wakati una majibu kwa kila jambo, Waislam tusubiri.
MWISHO


 
 
 
 

 
Share this article :

0 comments:

Speak up your mind

Tell us what you're thinking... !

ZILIZOSOMWA SANA.

Followers

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Proudly powered by Blogger
Copyright © 2011. Msamaa. - All Rights Reserved
Template Design by Creating Website Published by Mas Template