Polisi wakorogana mauji ya Padri Mushi. - Kitoloho
Headlines News :
Home » » Polisi wakorogana mauji ya Padri Mushi.

Polisi wakorogana mauji ya Padri Mushi.

Written By Msamaa on Friday, April 5, 2013 | 1:33 PM

Polisi wakorogana mauji ya Padri Mushi.

na Josephat Isango.
BAADA ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar (DDP) kulitaka Jeshi la Polisi kumwachia mtuhumiwa Mussa Omar Makame kutokana na ushahidi kutojitosheleza, jeshi hilo sasa limeingia kwenye mkorogano.
Wiki iliyopita jeshi hilo lilitangaza kumkamata Makame pamoja na watuhumiwa wengine na kudai kuwa ndiye aliyemuua Paroko wa Parokia ya Mpendae, Padri Evarist Mushi, kwa risasi huku wenzake wakitajwa kuhusika kuwajeruhi viongozi wengine wa dini.
Tukio hilo pia liligusiwa na Rais Jakaya Kikwete katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi Machi, akisema limehusisha vyombo vya nje vikishirikiana na jeshi la polisi nchini.
Hata hivyo, jeshi hilo jana lilikana kushirikiana na vyombo vya nje katika uchunguzi huo uliomtia hatiani Makame baada ya ushahidi wao kukataliwa na Mkurugenzi wa Mashataka, Ibrahimu Mzee Ibrahimu.
Katika mahojiano na gazeti hili, Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa A. Mussa, alikanusha jeshi la polisi kushirikiana na kikosi cha upelelezi cha Marekani (FBI) ili kumkamata Makame.
Kauli yake inakinzana na ile aliyoitoa Machi 23, mwaka huu aliposema uchunguzi huo ulikuwa ukifanywa na makachero wa polisi kwa kushirikiana na wapelelezi kutoka Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) na kufanikisha kumkamata mtuhumiwa huyo.
Hatua hiyo ilikuwa ni baada ya jeshi hilo kulaumiwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polikarp Kardinali Pengo, kuwa limekuwa kimya kuhusu matukio hayo na kusingizia kwamba yanafanywa na vikundi vya wahuni.
“Mhusika wa mauaji ya Padri Mushi tayari amekamatwa na ametambuliwa na watu walioshuhudia tukio hilo la kupigwa risasi na kusababisha kifo,” alisema Mussa katika mkutano wa wanahabari.
Aliongeza kuwa picha ya kuchora ya mtuhumiwa huyo pamoja na taarifa za kiintelijensia zimesaidia kwa kiwango kikubwa kukamatwa kwake.
“Baada ya kuitoa picha ya mchoro katika vyombo mbalimbali vya kiulinzi, wananchi, vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, mtuhumiwa ametambuliwa,” alisema.
Kamishna Mussa alifafanua kuwa mtu aliyesaidia kupatikana kwa mtuhumiwa huyo atakabidhiwa zawadi yake ya sh milioni 10 kimya kimya kutokana na sababu za kiusalama.
Katika mkorogano huo wa taarifa kuhusu Makame, tamko rasmi la Jeshi la Polisi nchini lililotumwa kwa vyombo vya habari halikumtaja mtuhumiwa kwa jina likidai uchunguzi unaendelea lakini Kamishna Mussa alimtaja kuwa ni Mussa Omar Makame.
Kamishna Mussa jana alilieleza gazeti hili kuwa licha ya DPP kusema Makame hana hatia, wataendelea kumshikilia kwa uchunguzi zaidi.
“Sisi tutaendelea kumshikilia hata kama DPP hakuridhika na upelelezi tuliofanya, tuna taratibu mbalimbali ambazo si lazima kuzitaja kwa sasa,” alisema.
Alipotakiwa kufafanua kama ni kweli FBI hawakushirikiana nao katika uchunguzi huo, kamishna huyo aliomba apigiwe simu baadaye kwa madai kuwa alikuwa na kazi, lakini alipotafutwa tena hakupokea simu.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini, Isaya Mungulu, alipotakiwa kuzungumzia mkorogano huo wa kauli, alidai apigiwe Kamishna wa Zanzibar ndiye anayejua vizuri. {CHANZO:TANZANIA DAIMA-Ijumaa 05.04.2013}.

 
Share this article :

0 comments:

Speak up your mind

Tell us what you're thinking... !

ZILIZOSOMWA SANA.

Followers

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Proudly powered by Blogger
Copyright © 2011. Kitoloho - All Rights Reserved
Template Design by Creating Website Published by Mas Template