Pingamizi la CCT dhidi ya OIC & Mahakama ya Kadhi - Kitoloho
Headlines News :
Home » » Pingamizi la CCT dhidi ya OIC & Mahakama ya Kadhi

Pingamizi la CCT dhidi ya OIC & Mahakama ya Kadhi

Written By Msamaa on Friday, March 15, 2013 | 1:47 PM



PINGAMIZI LA UANZISHWAJI WA MAHAKAMA YA KADHI KIKATIBA LILILOTOLEWA NA JUMUIA YA KIKRISTO TANZANIA (CCT)-OKTOBA 2008 (OPPOSOTION OF THE SHARIAH COURT SYSTEM CONSTITUTIONALY, BY THE CHRISTIAN COUNSEL OF TANZANIA (CCT)




Siku za hivi karibuni zimeanza kusikika kauli toka kwa watu mbali mbali kuhusu uwezekano wa kuanzishwa kwa mahakama ya Kadhi ambayo hiyo ni maalum kwa Waislamu peke yao . Lakini zipo juhudi mbalimbali zinazofanywa hata na baadhi ya viongozi wa juu wa Kisiasa katika kulishughulikia suala hilo kana kwamba Katiba inawaruhusu kufanya hivyo. Mambo hayo yalikwisha amuliwa katika vikao vya Bunge lililopita kuwa yafanywe na Waislamu wenyewe katika dini yao. Hivi karibuni tumemsikia Makamu wa Rais Dk. Bilal, akiwapa tumaini Waislamu kuwa jambo hilo linawezekana. Hoja yangu ni kwamba kauli ya Makamu wa Rais aliitoa kama mtu binafsi au kama Kiongozi wa ki-Taifa? Kitaifa ilikwisha amuriwa tayari. Kumekuwepo na hoja kuwa suala la udini katika nchi yetu linaota mizizi na kuhatarisha amani ya nchi. Kama viongozi wao ndiyo wanaolichochea unategemea nini kitatokea ? Hii ndiyo iliyonisukuma kukurushia kumbukumbu ya Tamko la CCT-JUMUIA YA KIKRISTO TANZANIA walilolitoa mwaka 29008 kuhusiana na kadhia hiyo. Lisome halafu tafakari kauli zinazotolewa na viongozi wa upande wa Waislamu kuhusu Mahakama ya kadhi

JUMUIYA YA KIKRISTO TANZANIA (CCT)
PINGAMIZI DHIDI YA UANZISHWAJI WA MAHAKAMA YA KADHI NCHINI NA TANZANIA KUJIUNGA KATIKA USHIRIKIANO NA JUMUIYA KIMATAIFA YA KIISLAMU.

Sisi Maaskofu na Viongozi wa makanisa na mashirika wanachama wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) tumetafakari kwa Roho ya Kiutume na Kinabii kwa nchi yetu juu ya Uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi nchini na Tanzania kujiunga katika ushirikiano na Jumuiya ya Kimataifa ya Kiislamu (OIC).

Tunazingatia na kutambua kwa dhati na fahari kubwa kuwa nchi yetu haina dini na kwamba jambo hili limekuwa ni mojawapo ya tunu na misingi imara ya umoja na utaifa na amani ya nchi hii. Tumeipongeza Serikali yetu mara nyingi kwa kuingiza katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 19 (2) kama ifuatavyo:- Kazi ya kutangaza dini , kufanya ibada na kueneza dini itakuwa ni huru na jambo la hiari ya mtu binafsi, na shughuli na uendeshaji wa jumuiya za dini zitakuwa nje ya shughuli za mamlaka ya nchi. [Sheria ya Mabadiliko ya Kumi na Nne katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Na ya 2005]. Ibara hii imekuwa ni ya muhimu kwa ajili ya kusimamia na kuhakikisha kwamba mambo ya dini yanatenganishwa kabisa na shughuli za uendeshaji wa nchi yetu.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ndiyo sheria mama ya sheria nyingine zote, imeendelea kuzingatia umuhimu huu. Hifadhi ya haki zilizotajwa katika ibara hii itakuwa chini ya taratibu zilizowekwa na sheria ambazo ni muhimu katika jamii na umoja wa kitaifa. Haya yamewekwa wazi katika Ibara ndogo ya (3) katika Ibara ya 19 [Sheria ya Mabadiliko ya Kumi na Nne Katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania . Na. 1 ya 2005]

Sheria ya Vyama vya siasa [Sura ya 258 R.E 2002] imetii na kuheshimu tuliyoyataja na kuyanukuu hapo juu katika kifungu cha 9 (2) (a) (i) ambacho kinasema; Without prejudice to subsection (i) of this section, no political party shall qualify for provisional registration if by its constitution or policy (a) it aims to advocate or further the interests of – (i) any religious belief or group. Maana yake (tafsiri ni yetu) ni kwamba chama chochote cha siasa hakitakubaliwa usajili wa muda endapo kwa kufuatana na katiba au sera ya chama chicho kinalenga kutetea au kuendeleza maslahi ya imani au kikundi chochote cha kidini.

Siku za hivi karibuni Bunge la Tanzania na vyombo vingine vya serikali vimekuwa vikijadili juu ya uwezekano wa kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi na nchi kujiunga katika ushirikiano wa OIC. Maswala haya yanapojadiliwa inaashiria uwezekano wa kukubalika kwa mambo haya mawili. Kukubalika kwake ni kwenda kinyume na vifungu vya Katiba na sheria tulizotaja au kunukuu hapo juu. Si hivyo tu, bali pia ni kuruhusu kubomoka na kuvunjika kwa amani ya nchi yetu kwa sababu yanagusa hisia na itikadi za Watanzania wote.

Tunatambua kuwa vyama vya siasa katika kueleza sera na ilani zao vinajitahidi kuvutia wapiga kura wengi ili viweze kupigiwa kura ili kuchukua au kuendelea kushika uongozi wa nchi. Lakini kamwe na ni hatari isiwe ni ili mradi kushika uongozi wa nchi hata kama ni kwa gharama ya kuvunjika kwa umoja wa kitaifa na amani ya nchi hii! Hili ni jambo tusilolikubali kwa vyovyote vile kwa Chama chochote cha kisiasa kitakachokubali mambo haya mawili. Hata kama uhusiano wetu na chama hicho ni mzuri kwa sasa itabidi tufikirie upya uhusiano huu! Tunatoa tahadahari kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali yake kuacha mara moja kuruhusu majadala na kukubalika kwa mambo haya.
Msimamo wetu kuhusu mambo haya mawili ni kuyakataa; na mamlaka yoyote ya nchi kuendelea kukaribisha mjadala huu ili hatimaye yakubalike ni kupoteza muda wa wenye dhamana ya mamlaka ya nchi hii na raslimali za nchi hii. Tuna uhakika wa yaliyomo katika nyaraka anzilishi za taasisi hizo na ni hatari kabisa endapo yakikubalika nchi itaingizwa katika migogoro itakayoua maridhiano, mshikamano, amani, utangamano na umoja wa kitaifa. Kama ilivyokuwa wakati wote tangu kupata Uhuru wa nchi hii hadi sasa mambo ya imani zao bila ya kuingiza mamlaka za nchi katika gharama na kutumia rasilimali na muda ambavyo ni muhimu kwa maendeleo ya /na ustawi wa familia, umma na Taifa kwa ujumla.

Tunaendelea kuweka mkazo kwamba yale mambo yote ambayo yamekuwa ni tunu kwa Taifa hili tangu kuasisiwa kwake yasitikiswe wala kuhojiwa kwa makusudi ya kuyaondosha au kudhoofisha umuhimu wake.

Kwa kuzingatia wajibu wetu wa Kinabii na Ki-utume, Jumuiya ya Kikristo Tanzania inatoa wito kwa Bunge letu lisikubali kamwe kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi nchini kwa kupitia mchakato wa utendaji wa mamlaka ya nchi, wala kuridhia uanachama wa Tanzania katika OIC. Tanzania yenye amani imetokana na ni tunda la uhuru wa dini, itikadi, makabila, rangi na jinsia zote.

MUNGU IBARIKI TANZANIA, MUNGU IBARIKI AFRIKA.

Pingamizi hili limetolewa leo tarehe ……………………… Oktoba, 2008



Hii imekopiwa kutoka http://findtruefaith.blogspot.com/2010/12/pingamizi-la-uanzishwaji-wa-mahakama-ya.html
Share this article :

0 comments:

Speak up your mind

Tell us what you're thinking... !

ZILIZOSOMWA SANA.

Followers

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Proudly powered by Blogger
Copyright © 2011. Kitoloho - All Rights Reserved
Template Design by Creating Website Published by Mas Template