- Kitoloho
Headlines News :

Written By Msamaa on Monday, June 10, 2013 | 10:33 PM

‘Madeni yameielemea Serikali’

Share bookmark Print Email Rating
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti na Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge 
Na Ibrahim Bakari  (email the author)

Posted  Jumatatu,Juni10  2013  saa 21:3 PM.
MWANANCHI.
 
Dodoma.

Zikiwa zimesalia siku mbili kabla ya Bajeti Kuu ya Serikali kusomwa, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti na Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge amesema Serikali imeelemewa na mzigo wa madeni.
Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa anatarajia kuwasilisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2013/14 keshokutwa.
Chenge alisema hayo juzi Mjini Dodoma baada wa mkutano wa majadiliano ya namna bora ya utendaji kazi baina ya Kamati ya Bunge ya Bajeti na kamati za Miundombinu, Ulinzi na Usalama, Mambo ya Nje, Hesabu za Serikali (PAC) na Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).
Alisema Serikali imeelemewa na madeni huku kila wizara ikitaka kukamilishiwa mafungu yake ya fedha jambo ambalo linashindikana kwa kuwa hazipo.
Kwa mujibu wa hotuba ya Kambi ya Upinzani ya Wizara ya Fedha, mpaka sasa deni la taifa limefikia Sh21.028 trilioni bila dhamana ya Serikali kwa mashirika ya umma na binafsi hadi kufikia Desemba 2012 na kati ya fedha hizo, asilimia 75.97 ni deni la nje.
Hata hivyo, katika majibu ya Serikali, Waziri Mgimwa alisema Serikali imeanza kulipa na kuanzia Julai 2012 hadi Aprili 2013, malipo ya madeni yamefikia Sh1,666.77 bilioni na kati ya hizo, deni la nje lililolipwa ni Sh213.57 bilioni.
“Unapoamua kuminya eneo moja kwa ajili ya kupeleka fedha eneo jingine, hapa panapominywa wanahangaika na wao wanahitaji fedha, inatakiwa kutafuta njia nyingine ya kupata fedha kwa ajili ya eneo hilo,” alisema Chenge.
Mwenyekiti huyo alisema wizara zote 32 zinahitaji fedha kulingana na bajeti wanazowasilisha bungeni wakati wizara nyingine zikihitaji fedha zaidi ili kukamilisha mipango kwa matumizi ya kawaida na maendeleo.
“Katika vikao vyetu vya ndani, tumezungumza na kila wizara. Zina matatizo mengi kweli... wanatutaka tuwaongezee kasma, sasa sisi siyo Serikali, tunachokifanya kamati ni kuishauri Serikali kuelekeza fedha eneo moja lenye mahitaji ya fedha nyingi kwa masilahi ya taifa.
“Tumeishauri Serikali kuondoa fedha maeneo kadhaa na kuitaka kutenga fedha kwa ajili ya mipango ya maendeleo, lakini wakati mwingine, hata hizo fedha zenyewe hakuna kwa kuwa tunachokitegemea zaidi hapa ni pato la ndani. “Sasa watu walipe kodi. Tabia ya ukwepaji kodi inasababisha Serikali kushindwa kukusanya mapato yake. Watu wanalalamika hakuna hiki na hiki, lakini wananchi na taasisi mbalimbali wenyewe ndiyo hao wanaokwepa kodi, sasa utapata wapi fedha za maendeleo?
Meghji: Bajeti ina presha.

Waziri wa zamani wa Fedha, Zakhia Meghji amesema kipindi cha kuelekea kwenye bajeti, kinakuwa cha ‘presha’ hasa ikiwa waziri hakujiandaa kisaikolojia.
Akizungumza kwenye Viwanja vya Bunge, Dodoma jana, Meghji ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Kuteuliwa, alisema: “Ninajivunia, katika kipindi changu kuanzia 2005-7 nikiwa Waziri wa kwanza wa Fedha mwanamke, nilikuwa naona fahari, ni heshima kubwa kwangu kusimama mbele ya wabunge kuwasilisha Bajeti.
“Nilikuwa nina hofu sana mwanzoni. Nilikuwa ninawaza jinsi ya kuwasilisha Bajeti, wabunge wananisikiliza, Watanzania wote wananisikiliza lakini nilichokuwa ninakifanya ni kurudia-rudia kuisoma.
“Kitu kilichokuwa kinanikwaza ni kutaja zile namba... ma-trilioni sasa nilichokuwa ninakifanya ni kuandika pembeni na kusoma moja kwa moja bila matatizo,” alisema huku akicheka.
Share this article :

0 comments:

Speak up your mind

Tell us what you're thinking... !

ZILIZOSOMWA SANA.

Followers

Blog Archive

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Proudly powered by Blogger
Copyright © 2011. Kitoloho - All Rights Reserved
Template Design by Creating Website Published by Mas Template