- Kitoloho
Headlines News :

Written By Msamaa on Saturday, June 8, 2013 | 4:44 AM

Rasimu ya Katiba yazidi kung’ata

Sura za Habari Hii
Rasimu ya Katiba yazidi kung’ata
MIIKO YA UONGOZI
Habari Yote
*Askofu Kilaini apinga mfumo wa Serikali tatu
*Asema utakuwa mzigo kiutendaji, aonya Watanzania
Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki, Jimbo la Bukoba, Methodius Kilaini
ASKOFU Msaidizi wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Bukoba, Dk. Methodius Kilaini, amepinga mapendekezo ya rasimu ya Katiba mpya yaliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, yakitaka uwepo muundo wa Serikali tatu. Akizungumza katika mahojiano maalum na MTANZANIA jana, Askofu Kilaini alisema kama Watanzania watakubali muundo wa Serikali tatu, utakuwa ni mzigo utakaowakandamiza wananchi wa kawaida. Mbali na kuwakandamiza wananchi, alisema Serikali hizo hazitakuwa na nguvu kama inavyotakiwa.

“Sikubaliani na wazo la kuanzisha Serikali tatu, huu ni mzigo kwa wananchi wa kawaida, hawa watawala wapo ambao hawatakuwa na nguvu za kiutawala.

“Wapo ambao watakosa hata amri au uwezo wa kuagiza barabara fulani ijengwe, sasa kama ni hivyo tunakwenda wapi, nawaomba Watanzania waliangalie jambo hili kwa umakini pindi muda utakapowadia,” alisema Askofu Kilaini na kuongeza:

“Kwa mawazo yangu, napenda Serikali mbili au moja, licha ya muundo wa sasa kukabiliana na changamoto nyingi.

“Naamini tukiwa na Serikali moja, ni kitu kizuri, tunaweza kusonga mbele bila matatizo yoyote kwani tumeona katika muundo wa Serikali mbili, bado watu hawakuridhika na changamoto nyingi zilizopo.

“Kumekuwa na ukakasi katika Serikali mbili, hivyo ni vema ukaondolewa kwa manufaa ya pande mbili,” alisema Askofu Kilaini.

Alisema kwamba, katika muundo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, unapaswa uwe mdogo na wenye kuzingatia maslahi ya wananchi.

“Kama tutafanikiwa kuwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano, basi tunahitaji kuwa na umakini wa hali ya juu kwenye muundo wake ambao utazingatia maslahi ya Watanzania, tusiwe na baraza la mawaziri kubwa ambalo litakuwa ni mzigo wa uendeshaji.

Kuhusu hatima ya Muungano uliopo, alisema utakuwa legelege kwa sababu utapoteza uhalisia wake.

“Ninavyoona Muungano wetu utakuwa legelege kidogo, ule uimara utapungua kwa sababu Rais atakuwa amepungukiwa na sehemu ya madaraka yake.

“Ukiangalia tunaweza kupata rais atakayekuwa anashughulikia vitu vidogo vidogo tu, sasa tangu lini ukaona duniani kiongozi wa juu anakosa madaraka ndani ya nchi yake,” alihoji Askofu Kilaini.

Alisema kama Serikali ya Tanganyika ikirudi, ni wazi itahitaji Katiba yake, jambo ambalo litaleta mgongano mwingine. 

MIIKO YA UONGOZI
Alisema kama kutakuwa na Serikali mbili au tatu, ni wazi kuna kazi kubwa ya kutengeneza miiko ya uongozi, itakayowabana viongozi wanaokiuka miiko ya uongozi.

“Jambo jingine kubwa ambalo tutalihitaji, ni kuwa na miiko ya uongozi ambayo itawabana viongozi wetu, tofauti na ilivyo sasa,” alisema.

Aliwataka Watanzania kuwa watulivu wakati huu ambao wanajiandaa kwenda kwenye mabaraza ya Katiba kutoa maoni yao.

“Nawaomba Watanzania wenzangu wawe watulivu kipindi hiki, wajitokeze kwa wingi kwenye Mabaraza ya Katiba pindi muda utakapowadia.

“Wakifika kwenye mabaraza haya, watoe hoja za msingi ili tupate kitu ambacho ni bora zaidi kwa manufaa ya Watanzania.

Juni 3, mwaka huu, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba aliweka hadharani rasimu ya Katiba mpya ikiwa na mapendekezo mbalimbali.

Miongoni mwa mapendekezo hayo, ni uanzishwaji wa Serikali tatu, uwepo wa mgombea binafsi, kufutwa kwa viti maalum bungeni na idadi ya mawaziri kupunguzwa.
MTANZANIA.
Share this article :

0 comments:

Speak up your mind

Tell us what you're thinking... !

ZILIZOSOMWA SANA.

Followers

Blog Archive

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Proudly powered by Blogger
Copyright © 2011. Kitoloho - All Rights Reserved
Template Design by Creating Website Published by Mas Template