- Kitoloho
Headlines News :
Home » »

Written By Msamaa on Tuesday, June 18, 2013 | 9:32 AM

‘Tanzania kubaki masikini miaka 190 ijayo’.

TANZANIA inaweza kuendelea kuwa masikini kwa miaka 197 ijayo, iwapo mwenendo wa sasa wa utekelezaji wa mipango ya maendeleo utaendelea kusuasua. Hayo yalibainika katika semina iliyoandaliwa na Mtandao wa Madeni na Maendeleo Tanzania (TCDD), Dar es Salaam jana iliyokuwa inaangalia kiwango cha misaada kinachotolewa na wahisani kama inaleta matokeo chanya kwa mwananchi.

Meneja wa Sera na Utetezi wa mwavuli wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali (TANGO), Zaa Twalangete, alisema kama wananchi hawatakuwa na sauti katika mipango na fedha zinazotolewa, umasikini nchini hautamalizika.

Alisema miradi inayoanzishwa katika maeneo mengi nchini haionyeshi kuleta tija kwa sababu haina ushiriki wa wananchi, lakini pia fedha kwa ajili ya miradi hiyo hazipelekwi kwa wakati.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Agricultural Non State Actors Forum, (ANSAF), Audax Rukonge, alisema Tanzania haitaweza kumaliza umasikni kama haitakuwa na uwekezaji wa kimkakati kwa ajili ya maendeleo.

Alisema unahitajika uwekezaji mkubwa katika sekta ya kilimo inayoajiri watu wengi vijijini kwa kuimarisha miundombinu ya barabara na nishati sambamba na elimu bora.

Rukonge alisema, hali ikiendelea kama ilivyo sasa, umasikini wa Tanzania utaweza kumalizika miaka 197 ijayo.

“Tafsiri halisi ya bajeti ya taifa inayotolewa kila mwaka, haionyeshi kuwakwamua wananchi na kuwaondolea umasikini.

“Mipango mingi ya maendeleo inatekelezwa kwa kiwango cha chini, bajeti ya kila mwaka inatekelezwa chini ya asilimia 40, lakini pia inaendelea kuwa tegemezi.

“Nchi wahisani wakichelewa kutoa fedha maana yake wakulima hawatapata pembejeo kwa wakati na hakutakuwa na mavuno yaliyotarajiwa, tutaendelea kulia njaa kila mwaka.

“Uwekezaji ndani ya nchi hauko kimkakati, hakuna matokeo chanya ya fedha zinazotoka kwa wafadhili, hazifiki kwa wakati, wananchi hawashirikishwi kikamilifu na hata misaada hiyo haionyeshi impact yoyote katika ngazi ya kaya,” alisema Rukonge.

Mkurugenzi wa TCDD, Hebron Mwakagenda alisema deni la taifa la Sh trillion 22 ni kubwa mno na kuna athari uchumi wa nchi kuporomoka zaidi.

“Hali ya deni ni mbaya, lazima kama taifa tufikirie zaidi hali itakuwaje katika siku zijazo, mjomba ambaye tunamtegemea atupatie misaada kila siku amebadili mipango yake, anataka kuingia kwenye biashara zaidi si kutoa misaada.”

“Katika miaka mitano ijayo, wafadhili wetu watajielekeza zaidi katika biashara, tuachane na mawazo ya mahusiano ya kuomba msaada bali kibiashara zaidi,” alisema Mwakagenda.

MTANZANIA.
Share this article :

0 comments:

Speak up your mind

Tell us what you're thinking... !

ZILIZOSOMWA SANA.

Followers

Blog Archive

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Proudly powered by Blogger
Copyright © 2011. Kitoloho - All Rights Reserved
Template Design by Creating Website Published by Mas Template