- Msamaa.
Headlines News :
Home » »

Written By Unknown on Sunday, June 9, 2013 | 12:42 PM

Waziri Dossa Azizi: Shujaa aliyesahaulika

Na. Mohammed Said
Baada ya vita kuu ya pili (1938-1945) nchi nyingi zilizokuwa chini ya ukoloni hasa barani Afrika zilianzisha harakati za kudai uhuru.
Uongozi uliokuwepo Tanganyika wa chama cha Waafrika kilichojulikana kama African Association wakati ule ulishindwa kabisa kubuni mbinu mpya za kupambana na utawala wa kigeni.
Ili Tanganyika iende mbele ilikuwa ni lazima uongozi ule uondolewe madarakani. Sababu kuu za kuung’oa madarakani uongozi ni kule kushindwa kwake kupambana na mabadiliko ya siasa yaliyokuwa yakitokea dunia nzima.
Harakati za Waziri Dossa Aziz na kuweka wazi mali yake ili kupambana na dhuluma za Serikali ya Kiingereza katika Tanganyika zinaanza wakati huu. Dossa wakati ule alikuwa kijana mdogo wa miaka 25. 

Ili aweze kupata picha halisi ya siasa katika mji wa Dar es Salaam ni lazima msomaji afahamishwe hali iliyokuwepo Dar es Salaam katika miaka ya 1950.
Katika mji wa Dar es Salaam ya miaka 1950 kulikuwa na koo mbili maarufu. Ukoo wa Azizi Ali baba yake Dossa, Ramadhani na Hamza Azizi na ukoo wa Kleist Sykes baba yao Abdul-wahid (1924-1968), Ally na Abbas Sykes.
Wazee hawa wawili walikuwa marafiki na urafiki huu ulienea hadi kwa watoto wao. Watoto wao wakafanya mengi pamoja katika harakati za kudai uhuru wa Tanganyika; na ndiyo maana haiwezekani ikaelezwa habari za Dossa bila kugusa habari za akina Sykes.
Halikadhalika haiwezekani yakaandikwa maisha ya Nyerere au historia ya uhuru wa Tanganyika na mwandishi akapuuza mchango wa watu hawa. Watoto wa koo mbili hizi, Dossa akiwakilisha ukoo wa Azizi Ally na Abdulwahid na Ally Sykes wakiwakilisha ukoo wa Sykes ndiyo mwaka 1950 waliohusika na mapinduzi ya kuung’oa madarakani uongozi wa African Association wa wazee uliodumu kuanzia mwaka 1929 hadi 1950 rais wake wa mwisho akiwa Mwalimu Thomas Sauti Plantan. 

Muhimu katika mazingira ya siasa za wakati ule ni kuwa hakuna chochote ambacho kingeliweza kufanyika Dar es Salaam katika jitihada ya kupambana na Serikali ya kikoloni bila ya msaada wa Dossa na watoto wa Kleist Sykes kwa sababu hawa walikuwa kwanza na elimu ya kutosha na pili walikuwa na hazina ya kuendesha harakati za siasa.
Kleist Sykes (1894-1949) alikuwa mwajiriwa wa Tanganyika Railway kama mhasibu. Kleist alikuwa mwanasiasa muasisi wa African Association (1929) na Al Jamiatul Islamiyya (Muslim Association) (1933) katika miaka ya mwisho ya uhai wake Kleist akawa mfanyabiashara maarufu.
Azizi Ally alikuwa mkandarasi wa kujenga majumba. Lakini kwa kuwa Azizi Ali alikuwa Mwafrika wakoloni walimbagua wakakataa kumpa leseni ya ukandarasi wa daraja la juu ambayo ingelimwezesha kujenga majumba makubwa ya ghorofa. Leseni hizo walipewa Wahindi na Wazungu. Juu ya ubaguzi huu wote baba yake Dossa alifanya kazi ya ujenzi na akatajirika katika biashara kama alivyotajirika rafiki yake Kleist. Mali hii ndiyo iliyokuja kuwa mtaji wa kwanza waliotumia Waafrika wa Tanganyika katika miaka ya mwanzo kuanzia harakati za kudai uhuru.
Wakati ule mtu hakujiingiza katika siasa ili anufaike binafsi. Nafasi hiyo haikuwepo kwa kuwa hakukuwa na fedha katika siasa. Kila aliyeingia katika harakati aliingia kwa uchungu na mapenzi ya nchi. Kama alikuwa na mali basi aliingia ili atoe mali yake kuikomboa nchi. Kama hana mali basi alijitolea chochote katika vipawa alivyojaaliwa. 

Dossa aliingia katika harakati za siasa mwaka 1950 siasa ikiwa katika hali hii. Aliingia katika African Association na uongozi mpya wa vijana miongoni mwao akiwa Abdulwahid na Ally Sykes, Hamza Mwapachu (1918-1962), Tewa Said Tewa (1924-1998), Dk. Vedast Kyaruzi, Dk. William Mwanjisi, Dk. Luciano Tsere, na vijana wengine ambao ingawa hawakuwa Watanganyika walishiriki kikamilifu katika harakati za kudai uhuru. Hawa walikuwa Dennis Phombeah kijana wa Kinyasa kutoka Nyasaland (Malawi), Patrick Aoko na Dome Budohi kutoka Kenya na vijana wengine wengi.
Dossa aliguswa na madhila ya ukoloni kwa dhahiri yake mwaka 1947. Dossa pamoja na mtoto mmoja wa Mwarabu tajiri aliyekuwa akiishi Dar es Salaam, Ali Mmanga walichaguliwa kuhudhuria mahojiano Nairobi kwa ajili ya kozi ya urubani wa ndege. Walipowasili Nairobi wakoloni walikataa kumfanyia usaili Dossa kwa sababu alikuwa Mwafrika. Dossa alifahamishwa kuwa yeye kama Mwafrika hastahili kupewa ujuzi wa kurusha ndege. Dossa alifadhahika sana na alimweleza mwandishi wa makala hii kuwa alipiga simu kwa baba yake na akawa analia machozi kwa uchungu. Kwa kumuonea huruma baba yake alimtumia fedha ili anunue gari pale Nairobi kama zawadi ya kumfajiri. Hii ndiyo ilikuwa gari ya kwanza kuwa nayo Dossa na aliitumia hadi 1955 alipoitoa kwa TANU ili itumike kwa ajili ya kudai uhuru.
Lakini Dossa alipokwenda Nairobi alimkuta Ally Sykes yupo mjini hapo na tayari alikuwa akifahamiana na wanaharakati wa Kenya kama Jomo Kenyatta, W.W. Awori, Tom Mboya na wengineo. Ally alikuwa akihudhuria mikutano ya siasa ya Wakikuyu iliyokuwa ikifanyika kwa siri Limuru. 

Ally Sykes alimchukua Dossa katika moja ya mikutano ya hadhara ambao Kenyatta alikuwa anahutubia katikati ya Nairobi sehemu moja ijulikanyo kama River Road. Aliyoyaona pale yalimtosheleza kabisa Dossa kujua kuwa Tanganyika ilikuwa imechelewa katika harakati za kudai haki yake. Waafrika wa Kenya walikuwa wamefikia hali ya kuzungumza siasa kwenye majukwaa wakati Waafrika wa Tanganyika walikuwa bado wakifanya mikutano yao ndani ya kiofisi kile kidogo cha African Association chini ya uongozi dhaifu wa Thomas Plantan akiwa kama Rais na Clemet Mtamila kama Katibu. Dossa alifikisha yote aliyoyaona Kenya kwa wenzake.
Mzee Dossa alimfahamisha mwandishi wa makala hii kuwa ni katika kipindi hiki kati ya mwaka 1947-1950 ndipo njama za kupindua uongozi wa Africa Association zilipoanza washiriki wakuu wakiwa yeye mwenyewe Dossa, Abdulwahid na mdogo wake Ally na rafiki yao Hamza Kibwana Mwapachu. Huku akicheka Mzee Dossa alimfahamisha mwandishi kuwa:
"Ilikuwa kutokea Tanga Club, Club mahsusi ya vijana wasomi Waafrika iliyokuwepo New Street (hivi sasa Lumumba Str.) si mbali sana na ofisi ya African Association ndipo Abdulwahid na Hamza Mwapachu walipoivamia kwa nguvu ofisi ya African Association na kufanya mapigano ambayo yalimfanya Katibu Mzee Mtamila apigwe na kutupwa nje ya ofisi". 

Dossa anasema yeye ingawa alikuwa anauchukia ule uongozi wa wazee hakuwa na moyo wa kuwatoa wazee wale kwa nguvu na kwa taadhira, kwa ajili hii basi alibaki nje akawa anaangalia sakata ile kwa mbali. Uchaguzi ulifanyika na wazee wakang’olewa madarakani. Dk. Kyaruzi akachaguliwa Rais na Abdulwahid akiwa Katibu wake.
Kuanzia wakati huu mikutano ya siasa ikaanza kufanyika Ilala Commuity Centre ambako Hamza Mwapachu alikuwa akifanya kazi kama Assistant Welfare Officer. Nyakati za jioni mijadala hii ikawa inahamia nyumbani kwa Dossa Mtaa wa Mbaruku Gerezani au Tanga Club, Agenda kuu ikiwa namna ya kuwaunganisha Watanganyika chini ya chama cha siasa ili kudai uhuru.
Mwaka wa 1950 Gavana Edward Twining alipoteua Kamati ya Katiba (Consitutional Development Committee) ili kukusanya mapendekezo ya Waafrika ni vipi wangependa katiba ya nchi iwe, Dossa alisema kuwa hapo ndipo Waingereza walipopata kwa mara ya kwanza kuhisi kuwa uongozi mpya wa vijana katika African Association ulikuwa umepania kuleta mabadiliko katika nchi. Uongozi wa akina Dossa uliihimiza Serikali ya kikoloni kuhusu umuhimu wa kuwa na uwakilishi wa Waafrika katika Baraza la Kutunga Sheria, uwakilishi wa kuchaguliwa na wananchi wenyewe badala ya ule uwakilishi wa kuchaguliwa na Gavana rangi ya mtu zaidi kuliko sifa nyingine yoyote.
Kipindi hiki cha mwaka 1950-1954 kilikuwa kipindi kigumu sana kwa kuwa kwanza chama kilikuwa hakina fedha kikitegemea sana msaada wa Dossa. Wakati ule chama kilitegemea sana fedha za Dossa katika shughuli za kuendesha ofisi na gari yake katika kutimiza majukumu yake ya kila siku.
Kwa kipindi kirefu wakati wa uongozi wa wazee kulikuwa hakuna mawasiliano yoyote kati ya Waafrika wa Tanganyika kupitia African Association na Baraza la Udhamini la Umoja wa Mataifa ambalo ndilo lililokabidhi Tanganyika kwa Waingereza wailee nchi hadi hapo Waafrika watakapokuwa tayari kujitawala. Kwa bahati mbaya Waingereza hawakutoa umuhimu wowote katika kuwafahamisha Waafrika mapatano hayo kati yake na Umoja wa Mataifa. Vijana walichukua nukta hii kama kazi ya kwanza kwa umuhimu katika chama na walipeleka barua nyingi sana katika matawi ili kuyaamsha kwa kuwa yalikuwa yamelala kwa muda mrefu.
Kati ya mwaka 1950-1952 Dossa alishiriki katika mikutano kati ya TAA na Earle Seatonn mwanasheria kutoka Bermuda aliyekuwa akikishauri chama katika masuala mbali mbali ya Katiba na sheria, kutayarisha mapendekezo kwa Constitutional Developmet Committee na katika mgogoro wa ardhi ya Wameru. 

Vile vile Dossa alishiriki katika kutuma ujumbe wa TAA ulioongozwa na Abdulwahidi kwenda Kenya ambao ulikutana na uongozi wa KANU wa Jomo Kenyatta, Fred Kubai, Bildad Kaggia na Kungu Karumba mwaka 1951.
Halikadhalika Dossa alikuwa mjumbe wa TAA uliokuwa ukutane tena na Kenyatta kwa mazungumzo ya siri Arusha mazugumzo yaliyoombwa na KANU. Wajumbe wengine wakiwa Abdulwahid na Stephen Mhando.
Katika salaam alizoleta Kenyatta kwa TAA alihimiza kuwa kila mjumbe wa TAA asije mkutanoni ila awe amebeba silaha. Ujumbe huu ulikuwa uondoke kwa siri mmoja mmoja ili kukwepa makachero.
Dossa alikuwa wa kwanza kuondoka kuelekea Arusha akiwa na bunduki. Wakati ule ili kwenda Arusha njia ilipita Dodoma. Mkutano huu haukufanyika kwa kuwa Kenyatta na wenzake walikamatwa kwa makosa ya kuwa wafuasi wa Mau Mau.
Akiwa Dodoma Dossa alifahamishwa na Ali Juma Ponda katibu wa TAA Dodoma kuwa mkutano hautakuwepo kwa kuwa viongozi wa KANU wote wametiwa mbaroni. Akiwa njiani kwenda Arusha palitokea mapigano kati ya Mau Mau na askari wa kikoloni.
Tarehe 20 Oktoba, 1952 serikali ya kikoloni Kenya ilikuwa imeshindwa kabisa kupambana na Mau Mau, kwa sababu hii basi serikali ilitangaza hali ya hatari, Kenyata na Uongozi mzima wa KANU ukatiwa kizuizini ( tarehe 8 Aprili 1953)wakahukumiwa kifungo cha miaka saba kazi ngumu). Dossa aliamua kwenda Mwanza ambako alipokewa na Dk. Joseph Mutahangarwa, Makamo wa Rais wa TAA Lake Province. Dk. Mutahangarwa aliulaumu uongozi wa Makao Makuu kwa kuunganisha harakati za TAA na KANU kwa hofu ya kusababisha kamata kamata kama ile iliyokuwa ikiendelea Kenya. 

Dossa Azizi alikwenda Bukoba ambako alipokelewa na Chief Rutinwa na viongozi wengine wa TAA kama Ali Migeyo na Suedi Kagasheki.
Mwaka 1953 Dossa alihusika na uamuzi wa kuupeleka ujumbe wa TAA wa Saadan Abdu Kandoro, Japhet Kirilo na Abbas Sykes utembee nchi nzima kuwaeleza wananchi kile kilichopitika Umoja wa Mataifa kuhusu kesi ya ardhi ya Wameru. Vile vile katika mwaka huo huo Dossa alihusika katika uamuzi wa kuupeleka ujumbe wa TAA Southen Rhodesia (Zambia) kuhudhuria mkutano uliojulikana kama Pan African Congress uliotayarishwa na mwanasiasa mmoja aliyeitwa David Keneth Kaunda aliyekuwa Katibu wa African National Congress. Wajumbe waliochaguliwa kuiwakilisha TAA katika mkutano huu walikuwa Ally Sykes na Denis Phombeah. Katika harakati hizi zote zilipotakikana fedha kwa ajili ya kufanikisha hili au lile jukumu lilimwangukia Dossa. Dossa alitoa fedha zake kwa ukarimu na bila kinyongo. 

Mwaka wa 1951 wakati Dossa na wenzake wako katika juhudi za kuipa uhai mpya TAA Dossa aliandikiwa barua na V.M. Nazerali aliyekuwa mjumbe wa Baraza la Kutunga Sheria akimuomba aunge mkono juhudi zake na za Ivor Bayldon na Brig. Scupham za kutaka kuunda chama cha siasa kitachowashirikisha watu wa rangi zote. Bayldon na Birg. Scupham walikuwa kama alivyokuwa Nazerali, wajumbe wa Baraza la kutunga sheria.
Wanasiasa wengine walioombwa kuunga mkono juhudi hizi walikuwa Chifu Kidaha Makwaia. Liwali Yastio Mponda wa Newala. Dk. Joseph Mutahangarwa, Chifu Abdieli Shangali wa Machame, Chifu Thomas Marealle wa Marangu, Chifu Adamu Sapi Mkwawa, Chifu Haru Msabila Lugusha, Dk. Wiliam Mwanjisi, Abdulkarim Karimjee, Dk. Vedast Kyaruzi, Liwali Juma Mwindadi, H.K. Viran, Stephen Mhando, Ally Sykes na Abdulwahid Sykes.
Dossa na wenzake waliikataa ghilba hii kwa kuwa lengo lao lilikuwa ni kuanzisha chama cha siasa cha Waafrika wa Tanganyika kwa minajili ya kudai uhuru.
Itaendelea toleo lijalo
Share this article :

0 comments:

Speak up your mind

Tell us what you're thinking... !

ZILIZOSOMWA SANA.

Followers

Blog Archive

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Proudly powered by Blogger
Copyright © 2011. Msamaa. - All Rights Reserved
Template Design by Creating Website Published by Mas Template