- Kitoloho
Headlines News :

Written By Msamaa on Thursday, June 6, 2013 | 2:16 PM

Rasimu ya Katiba yazua mjadala Zanzibar

Salim Said Salim

HATIMAYE baada ya kelele za miaka mingi na waliozitoa kuitwa wasaliti, si wenzetu, watu wenye nia mbaya na hawaitakii mema Tanzania inaonekana kuelekea kule ambapo nchi nyingi zinazojenga utawala wa kidemokrasia zimetangulia kuifanya safari hiyo.
Nayo ni kuwa na katiba mpya ambayo rasimu yake ilitolewa wiki hii na sasa kuwa mada kuu ya mazungumzo kila pembe ya Jamhuri ya Muungano.
Kwa hapa Zanzibar rasimu hii imepokewa kwa mitazamo tofauti, wengine kwa kuiona ni nzuri sana, wengine nzuri kiasi na  wengine kuiona haijakidhi haja na matarajio ya Wazanzibari. 

Wapo pia wanaoisifu au kuiponda, lakini ukitafakari utaona hata kilichokuwamo ndani hawakielewi isipokuwa wanajifanya wataalamu na ukichunguza utaona wanasukumwa na utashi wa kisiasa badala ya masilahi ya Zanzibar na Tanzania kwa jumla.
Ukweli ni kwamba mapokezi ya rasimu yameigawa  Zanzibar kwa mapande, makubwa na madogo. Lipo kundi linaloona maoni ya Wazanzibari hayakupewa uzito unaostahiki, lakini wengine wanahisi waliokuwa wakipinga katiba ya zamani na mfumo wake wa serikali mbili ‘wamepata zaidi’ kuliko wao waliotaka serikali mbili au mbili kuelekea moja.
Maeneo yaliyotawala mjadala ni pamoja na kwa kiasi gani Zanzibar itakuwa na mamlaka kamili juu ya masuala mbalimbali na hasa fedha na biashara.
Hapa inafaa kukumbusha kwamba ukiachilia mbali wafanyabiashara, Wazanzibari wengi, wakiwamo wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na wabunge, wamekuwa wakitaka suala la fedha kama ilivyokuwa wakati wa muungano ulipoundwa mwaka 1964 lisiwe la Muungano.
Kumbukumbu zinaonesha kuwapo kelele hata ndani ya Baraza la Wawakilishi, kutaka Mamlaka ya Mapato Zanzibar (TRA) ifunge virago vyake Visiwani kwa kile kinachoonekana na wengi hapa kuwa ni taasisi isiyokuwa na masilahi na Zanzibar.

Mjadala unaosikika hapa ni kwamba kwa suala la fedha kuwa  la Muungano Zanzibar bado itakuwa haina uwezo wa kujitutumua kiuchumi, hasa kwa vile mfumo wa kodi uliopo sasa wa Muungano unaonekana hauitendei haki Zanzibar.
Kwa miaka mingi Wazanzibari wamekuwa na unafuu mkubwa wa ulipaji kodi ukilinganisha na wenzao wa Bara, kwa  hiyo wengine wanahisi  kwamba fedha kuwa chini ya Muungano, Zanzibar itaendelea kusononeka na kuumia kiuchumi.

Eneo jingine ambalo watu wamekuwa na shauku nalo ni hili la Mambo ya Nje, hasa kwa vile haijaelezwa wazi kama ushirikiano wa kimataifa nao utakuwa katika kapu la Muungano.
Zanzibar imekuwa ikilalamika kuwa ushirikiano wa kimataifa uliingizwa kinyemela katika orodha ya mambo ya Muungano ili Zanzibar isinufaike na misaada kutoka nje. Eneo linalogusiwa sana ni kule kuzuiliwa kuijunga na Jumuiya ya nchi za Kiislamu (OIC).
Kinachowaumiza Wazanzibari ni kile wanachokiona kama kudanganywa na Serikali ya  Muungano kwamba suala hili lingeshughulikiwa kwa Tanzania kujiunga na OIC, badala ya Zanzibar peke yake. Lakini hili halijafanyika kwa zaidi ya miaka 15 sasa na hazisikiki habari zozote za Tanzania kujiunga na OIC.
Muundo wa kuwa na  Bunge dogo badala ya utitiri uliopo sasa, umewafurahisha wengi, lakini wapo wanaoona haki haikutendeka kwa Bara kuwa na wabunge 50 na Zanzibar wabunge 20.
Wengi wanahisi mfumo huu hauoneshi kwamba Muungano ni wa nchi mbili, sawa na wanaohisi angalau Bara ingelikuwa na Wabunge 45 na Zanzibar 25 .
Muda wa wabunge kuwa na kikomo cha vipindi vitatu umefurahiwa na wengi, lakini wapo wanaohisi viwili vingelitosheleza kama alivyowekewa rais.
Pendekezo la kulipa Bunge meno la kuidhinisha mawaziri na watendaji wakuu linaungwa mkono na wengi. Lakini wapo wachache (wahafidhina) wanaona rasimu haimtendei haki rais kwa vile mazoea yamewalemaza kuona rais hakosei na anayo haki ya kufanya maamuzi bila ya kuhojiwa au kukataliwa na yeyote yule katika nchi kwa kisingizio kwamba amechaguliwa na wananchi.
Watu hawa hawa wanafumbia macho ukweli kwamba wabunge nao wanachaguliwa na wananchi.

Kwa suala la Baraza la Mawaziri kuwa na mawaziri 15 tu karibu kila mtu ameipongeza Tume ya Katiba, kwani  wanahisi Tanzania hivi sasa inalo baraza kubwa kupita kiasi na hii inaigharimu nchi mabilioni ya shilingi.
Wapo wanaohisi Zanzibar nayo inafaa irekebishe sheria yake na iwe na mawaziri wasiozidi 10 na iondokane na kuwa na mawaziri wasiokuwa na wizara maalumu na utitiri wa manaibu mawaziri na washauri wa rais.
Kwa suala la kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi wengi wanasema tume imeona mbali na kuipongeza, lakini wahafidhina wanahisi muundo wa sasa wa rais kuchagua wajumbe ni sahihi.

Hoja ya watu hawa ni kwamba aliyekuwa mbele siku zote ndiye mshindi na si lazima apate zaidi ya asilimia 50 ya kura zote.
Lakini hapa baadhi ya wanasheria na watu ambao wanaona mbali wanasema lazima pawepo tafsiri inayoeleweka ya maana ya  zaidi ya asilimia 50 ya kura zote. Je, hii ni ya kura zilizopigwa, zile zilizokuwa halali  au ni pamoja na zilizoharibika?
Vile vile kipengele cha mgombea kuhoji matokeo ya uchaguzi wa rais mahakamani kimeleta furaha kubwa Zanzibar japokuwa watu wengi walikuwa na shaka kama mahakama za Tanzania zitakuwa na ubavu na kujiamini kuwa huru, hivyo kutenda haki na hasa kutokana na dhana iliyopo sasa kuwa mahakimu wetu bado hawaamini kama wanaongozwa na sheria na si mapendekezo ya viongozi.
Lililo muhumu, watu wengi wanasema ni kwa mahakama kuhakikisha sheria zinaheshimiwa na anayezivunja anawajibishwa kisheria, bila ya kujali nafasi yake katika jamii.
Kipengele cha rais kumpunguzia mamlaka ili asipande watu vichwani kimefurahisha wengi, hasa wapinzani. Hata hivyo wapo wanaohisi na rais naye aweze kushitakiwa kwa sababu akiwekewa kinga atakuwa na ubavu wa kutowatendea wananchi haki kwa mujibu wa sheria.
“Kama rais atakuwa na kinga, basi na mawaziri nao wawe na kinga na wananchi nao pia tuwe na kinga,” alisema kijana mmoja, Ali Mohamed  wa Michenzani.
Suala la umri wa kiongozi limeonekana kuleta mgawanyiko Zanzibar. Wapo wanaohisi miaka 40 ni mingi kwa vile wapo vijana wa chini ya umri huo wenye uwezo kuliko wakubwa wao kwa umri.
Katika hili wanatoa mfano wa Waziri Mkuu mstaafu na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Nchi za Kiafrika, Salim  Ahmed Salim, ambaye alichaguliwa balozi akiwa na miaka 21 na Nigeria ilipoongozwa na Yakubu kutoka mwaka 1966 akiwa na miaka 32 hadi mwaka 1975.
Rais Joseph Kabila wa Congo ambaye alichukua uongozi mwaka 2001 akiwa anakaribia umri wa miaka 30 na Muammar Gaddafi wa Libya aliyekuwa rais akiwa na  miaka 27.

Dada mmoja, Amina Suleiman wa Bububu  alielezea suala hili kwa hasira kwa kusema: “Tatizo lililopo katika nchi yetu ni wazee kuona wao tu ndio wenye akili, uwezo na busara. Mwenendo huu umepitwa na wakati.”
Kwa ujumla mapendekezo ya katiba yametoa mwanga wa matumaini palipokuwepo na giza. Lakini suala ni kwa kiasi gani mjadala wa hiyo rasimu utakuwa na maana na kuboreshwa katika mabaraza ya katiba ambayo hapa Visiwani yamelalamikiwa kuwa yameundwa kwa mizengwe na kudaiwa kuwa chama tawala cha CCM kilicheza mchezo mbaya.
Watanzania sasa wanajua wapi walipo, lakini safari ya huko wanakokwenda, hasa hapa Visiwani, bado ni ya milima na mabonde. Ni uzalendo tu na si utashi wa kisiasa ndio utakaosaidia kupiga hatua mbele.
Hongera Jaji Warioba na timu yako, lakini tume inapaswa kuwa makini na hayo mabaraza ya katiba, kwani kazi nzuri ambayo imefanywa inaweza kutiwa doa na kuchafuliwa na kunuka na kuwa sehemu mbaya ya historia ya nchi hii.
CHANZO:TANZANIA DAIMA.
5-june-2013
Share this article :

0 comments:

Speak up your mind

Tell us what you're thinking... !

ZILIZOSOMWA SANA.

Followers

Blog Archive

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Proudly powered by Blogger
Copyright © 2011. Kitoloho - All Rights Reserved
Template Design by Creating Website Published by Mas Template