Ijumaa, Aprili 19, 2013 05:54
Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam {MTANZANIA}
HUKUMU dhidi ya Katibu Mkuu wa Jumuiya na
Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda na wenzake 49,
imeahirishwa hadi Mei 9, mwaka huu. Hukumu hiyo, iliahirishwa kusomwa jana
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mjini Dar es Salaam na Hakimu Mkazi,
Aloyce Katemana kwa sababu Hakimu Victoria Nongwa anayesikiliza kesi hiyo
hakuwepo.
“Hakimu Nongwa, alitakiwa kusoma hukumu leo (jana), lakini hayupo hivyo hukumu yenu itakuwa tayari Mei 9, mwaka huu na itatajwa Mei 2, mwaka huu, washtakiwa waliokuwa nje kwa dhamana wataendelea kuwa nje na waliokuwa rumande watabaki huko,”alisema Katemana.
Mahakama hiyo jana ilifurika watu waliofika kwa ajili ya kusikiliza hukumu hiyo, lakini hawakufanikiwa kuingia ndani ya maeneo ya mahakama karibu na jengo la Maktaba Kuu ya Tanzania.
Hakuna mtu aliyeruhusiwa kuingia katika eneo la mahakama zaidi ya washtakiwa, mbwa na farasi kwa ajili ya kulinda usalama walikuwepo katika maeneo hiyo.
Hukumu hiyo, ilitakiwa kusomwa baada ya pande zote mbili zinazopingana kumaliza kusikiliza ushahidi na majumuisho ya kesi hiyo waliyowasilisha kwa ajili ya kuisaidia mahakama katika kutoa uamuzi.
Sheikh Ponda na wenzake, wanakabiliwa na mashtaka matano ya kula njama, kuingia kwa jinai katika uwanja namba 311/3/4 kitalu T uliopo Markaz Chang’ombe, wizi wa mali zenye thamani ya Sh milioni 59 mali ya Kampuni ya Agritanza Limited.
Kesi ilifikshwa mahakani kwa mara ya kwanza Oktoba 18, mwaka mjana na ilianza kusikilizwa kwa upande wa mashtaka kuleta mashahidi 16 mahakamani kwa ajili ya kuthibitisha tuhuma dhidi ya washtakiwa wote wakiongozwa na Wakili wa Serikali, Tumaini Kweka.
Sheikh Ponda na wenzake, wanatetewa na mawakili Juma Nassoro pamoja na Yahaya Njama ambao kwa kutaka kuionyesha mahakama kwamba wateja wao hawakutenda makosa hayo waliita mashahidi 52, wakiwemo washtakiwa.
Upande wa mashtaka, uliwasilisha mahakamani majuisho ya mwisho ukiiomba Mahakam a iwatie hatiani washtakiwa wote kwa sababu upande huo, umeweza kuthibitisha mashtaka bila kuacha shaka.
Wakili Nassoro, aliomba mahakama iwaachie huru wateja wake kwa sababu upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha makosa dhidi yao bila kuacha shaka.
Oktoba 18, washtakiwa walisomewa mashtaka na wakili Kweka ambapo alidai, Oktoba 12, mwaka jana katika eneo la Markaz Chang’ombe, lililopo Wilaya ya Temeke, kwa jinai na pasipo sababu za msingi washtakiwa hao walivamia kiwanja namba 311/3/4 kitalu T kinachomilikiwa na Kampuni ya Agritanza Ltd kwa nia ya kujimilikisha isivyo halali.
Kweka alidai washtakiwa hao, walitenda kosa hilo la kuingia kwa nguvu kwa nia ya kutenda kosa, kinyume na Kifungu cha 85 na 35 cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Alidai kati ya Oktoba 12 na 16, mwaka jana katika eneo hilohilo, washtakiwa hao pasipo uhalali wowote na hali iliyosababisha uvunjifu wa amani, walijimilikisha ardhi hiyo mali ya Agritanza Limited.
Shtaka la tano, linamkabili mshitakiwa wa kwanza, Ponda Issa Ponda na Shekhe Swalehe Mkadamu ambapo walidaiwa kuwa kati ya Oktoba 10 na 16 mwaka jana, Chang’ombe Markaz, walishawishi wafuasi wao kutenda makosa hayo.
Washtakiwa wote walikana mashtaka na kukubaliwa dhamana kwa masharti ya kuwa na mdhamini mmoja wa kuaminika atakayesaini dhamana ya Sh milioni moja, wote walitimiza masharti na kuwa nje kwa dhamana isipokuwa Ponda na Mkadamu ambao dhamana yao ilizuiliwa.
Kweka aliwasilisha mahakamani hati ya kuzuia dhamana iliyotoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) chini ya kifungu cha sheria namba 148(4) cha sheria ya makosa ya jinai.
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !