BAADA ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar (DDP) kulitaka Jeshi la Polisi
kumwachia mtuhumiwa Mussa Omar Makame kutokana na ushahidi kutojitosheleza,
jeshi hilo sasa limeingia kwenye mkorogano.
Wiki iliyopita jeshi hilo lilitangaza kumkamata Makame pamoja na watuhumiwa
wengine na kudai kuwa ndiye aliyemuua Paroko wa Parokia ya Mpendae, Padri
Evarist Mushi, kwa risasi huku wenzake wakitajwa kuhusika kuwajeruhi viongozi
wengine wa dini.
Tukio hilo pia liligusiwa na Rais Jakaya Kikwete katika hotuba yake ya mwisho
wa mwezi Machi, akisema limehusisha vyombo vya nje vikishirikiana na jeshi la
polisi nchini.
Hata hivyo, jeshi hilo jana lilikana kushirikiana na vyombo vya nje katika
uchunguzi huo uliomtia hatiani Makame baada ya ushahidi wao kukataliwa na
Mkurugenzi wa Mashataka, Ibrahimu Mzee Ibrahimu.
Katika mahojiano na gazeti hili, Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa A. Mussa,
alikanusha jeshi la polisi kushirikiana na kikosi cha upelelezi cha Marekani
(FBI) ili kumkamata Makame.
Kauli yake inakinzana na ile aliyoitoa Machi 23, mwaka huu aliposema
uchunguzi huo ulikuwa ukifanywa na makachero wa polisi kwa kushirikiana na
wapelelezi kutoka Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) na kufanikisha
kumkamata mtuhumiwa huyo.
Hatua hiyo ilikuwa ni baada ya jeshi hilo kulaumiwa na Askofu Mkuu wa Jimbo
Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polikarp Kardinali Pengo, kuwa limekuwa
kimya kuhusu matukio hayo na kusingizia kwamba yanafanywa na vikundi vya
wahuni.
“Mhusika wa mauaji ya Padri Mushi tayari amekamatwa na ametambuliwa na watu
walioshuhudia tukio hilo la kupigwa risasi na kusababisha kifo,” alisema Mussa
katika mkutano wa wanahabari.
Aliongeza kuwa picha ya kuchora ya mtuhumiwa huyo pamoja na taarifa za
kiintelijensia zimesaidia kwa kiwango kikubwa kukamatwa kwake.
“Baada ya kuitoa picha ya mchoro katika vyombo mbalimbali vya kiulinzi,
wananchi, vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, mtuhumiwa ametambuliwa,”
alisema.
Kamishna Mussa alifafanua kuwa mtu aliyesaidia kupatikana kwa mtuhumiwa huyo
atakabidhiwa zawadi yake ya sh milioni 10 kimya kimya kutokana na sababu za
kiusalama.
Katika mkorogano huo wa taarifa kuhusu Makame, tamko rasmi la Jeshi la Polisi
nchini lililotumwa kwa vyombo vya habari halikumtaja mtuhumiwa kwa jina likidai
uchunguzi unaendelea lakini Kamishna Mussa alimtaja kuwa ni Mussa Omar
Makame.
Kamishna Mussa jana alilieleza gazeti hili kuwa licha ya DPP kusema Makame
hana hatia, wataendelea kumshikilia kwa uchunguzi zaidi.
“Sisi tutaendelea kumshikilia hata kama DPP hakuridhika na upelelezi
tuliofanya, tuna taratibu mbalimbali ambazo si lazima kuzitaja kwa sasa,”
alisema.
Alipotakiwa kufafanua kama ni kweli FBI hawakushirikiana nao katika uchunguzi
huo, kamishna huyo aliomba apigiwe simu baadaye kwa madai kuwa alikuwa na kazi,
lakini alipotafutwa tena hakupokea simu.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini, Isaya Mungulu, alipotakiwa
kuzungumzia mkorogano huo wa kauli, alidai apigiwe Kamishna wa Zanzibar ndiye
anayejua vizuri. {CHANZO:TANZANIA DAIMA-Ijumaa 05.04.2013}.
|
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !