Utangulizi
Sifa
njema anastahiki Allah aliyeumba na akafanya sawa sawa alivyoviumba, akakadiria
na akaongoza. Rehema na Amani zimwendee bwana wetu, kiongozi na mwalimu wetu Nabii
Muhammad, na juu ya Swahaba zake na Ahli zake.
Nimekuwa
nikiguswa sana na mambo mbalimbali yanayozungumzwa kuhusiana na mwanamke katika
Uislamu. Katika kitabu hiki
nitazungumzia jambo moja muhimu linalohusiana na mwanamke ambalo limekuwa ni
sehemu ya kejeli na hata kujadiliwa na watu mara nyingi. Tena kumekuwa na watu
wengi wakiuliza maswali kuhusiana na Uislamu unavyosema juu ya jambo hilo, nalo
ni MIPAKA YA KAZI ZA MWANAMKE KATIKA
UISLAMU.
Awali
ya yote ifahamike kuwa suala la mipaka ya kazi za mwanamke linakuja katika
Uislamu kama jibu dhidi ya kile kilichotokea Ulaya wakati wa Mapinduzi ya
Viwanda yaliyoteka huko Ulaya katika karne ya 19.
Kimsingi
kadhia na dhana nzima ya mwanamke kutoka na kwenda kufanya kazi nje ya nyumba
yake ni kadhia ambayo haiko katika kivuli cha Uislamu dini ambayo inajulikana
wazi kuwa inadhamini malezi ya mwanamke katika maisha yake yote tangu kuzaliwa
hadi kufa kwake.
Naingia
katika Maudhui hii kwa kuanza na kauli ya Ustaadh Muhammad Qutub katika kitabu
chake; "شبهات حول الإسلام" “Shubhaatun hawlal Islaam” ukurasa wa 108 hadi wa 111:
"إن الثورة الصناعية
شغّلت
النساء والأطفال، فحطمت روابط الأسرة وحلت كيانها. ولكن المرأة هى التى دفعت أفدح
الثمن من جهدها وكرامتها، وحاجاتها النفسية والمادية. فقد نكل الرجل عن إعالتها من
ناحية، وفرض عليها أن تعمل لتعول نفسها حتى لو كانت زوجة وأمًّا، واستغلتها
المصانع أسوأ استغلال من ناحية أخرى، فشغّلتها ساعات طويلة،
وأعطتها أجرًا أقل من الرجل الذى يقوم معها بذات العمل فى ذات
المصنع. ولا تسأل لماذا حدث ذلك، فهكذا هي أوروبا، جاحدة بخيلة، لا تعترف
بالكرامة للإنسان من حيث هو إنسان ولا تتطوع بالخير حيث تستطيع أن تعمل الشر وهى
آمنة. تلك طبيعتها على مدار التاريخ، في الماضي والحاضر والمستقبل إلا أن يشاء
الله لها الهداية والارتفاع. وإذا كان النساء والأطفال ضِعَافًا، فما الذي يمنع
استغلالهما والقسوة عليهما إلى أقصى حد؟ إن الذي يمنع شيء واحد فقط، هو الضمير،
ومتى كان لأوروبا ضمير؟!! ومع ذلك فقد وُجدت قلوب إنسانية حية لا تُطيق الظلم،
فهبت تدافع عن المستضعفين من الأطفال. نعم الأطفال فقط! فراح المصلحون الاجتماعيون
ينددون بتشغيلهم فى سن مبكرة، وتحميلهم من الأعمال ما لا تطيقه بنيتهم الغضَّة التي
لم تستكمل نصيبها من النمو، وضآلة أجورهم بالنسبة للجهد العنيف الذى يبذلونه.
ونجحت الحملات، فرفعت أجورهم، ورفعت رويدًا رويدًا سن التشغيل، وزادت الأجور وخفضت ساعات
العمل.أما المرأة فلم يكن لها نصير. فنصرة المرأة تحتاج إلى قدر من ارتفاع المشاعر
لا تطيقه أوروبا! لذلك ظلَّت في محنتها تنهك نفسها فى العمل – مضطرة لإعالة
نفسها - وتتناول أجرًا أقل من أجر الرجل، مع اتحاد الإنتاج والجهد المبذول. وجاءت
الحرب العظمى الأولى ثم الثانية، وقتل عشرات الملايين من الشباب الأوربيين
والأمريكان. وواجهت المرأة قسوة المحنة بكل بشاعتها. فقد وجدت ملايين من النساء
بلا عائل، إما لأن عائلهن قد قتل فى الحرب، أو شُوِّه، أو فسدت أعصابه من الخوف
والذعر والغازات السامة الخانقة، وإما لأنه خارج من حبس السنوات، يريد أن يستمتع
ويرفه عن نفسه، ولا يريد أن يتزوج ويعول أسرة تكلفه شيئا من
المال والأعصاب. ومن جهة أخرى لم تكن هناك أيدٍ عاملة من الرجال تكفى لإعادة تشغيل
المصانع لتعمير ما خرَّبته الحرب. فكان حتمًا على المرأة أن تعمل وإلا تعرَّضت
للجوع هي ومن تعول من العجائز والأطفال. وكان حتمًا عليها كذلك أن تتنازل عن أخلاقها.
فقد كانت أخلاقها قيدًا حقيقيًا يمنع عنها الطعام! إن صاحب المصنع وموظفيه لا
يريدون مجرد الأيدى العاملة، فهم يجدون فرصة سانحة، والطير يسقط من نفسه – جائعًا –
ليلتقط الحَب، فما الذي يمنع من الصيد؟
وما دامت قد وجدت – بدافع الضرورة – امرأة تبذل نفسها لتعمل، فلن يتاح
العمل إلا للتى تبذل نفسها للراغبين. ولم
تكن المسألة مسألة الحاجة إلى الطعام فحسب. فالجنس حاجة بشرية طبيعية لا بد
لها من إشباع. ولم يكن فى وسع الفتيات أن يشبعن حاجتهن الطبيعية ولو تَزَوَّج كل
من بقى حيًا من الرجال، بسبب النقص الهائل الذى حدث فى عدد الرجال نتيجة الحرب.
ولم تكن عقائد أوربا وديانتها تسمح بالحل الذى وضعه الإسلام لمثل هذه الحالة
الطارئة، وهو تعدد الزوجات. لذلك لم يكن بُدٌّ للمرأة أن تسقط راضية أو كارهة
لتحصل على حاجة الطعام وحاجة الجنس، وترضى شهوتها إلى الملابس الفاخرة، وأدوات الزينة،
وسائر ما تشتهيه المرأة من أشياء. وسارت المرأة فى طريقها المحتوم، تبذل نفسها
للراغبين، وتعمل في المصنع والمتجر، وتشبع رغباتها عن
هذا الطريق أو ذاك. ولكن قضيتها زادت حِدَّة. فقد استغلت المصانع حاجة المرأة إلى
العمل، واستمرَّت في معاملتها الظالمة التى لا يبررها عقل ولا ضمير، فظلت تمنحها
أجرًا أقل من أجر الرجل الذى يؤدى ذات العمل في ذات
المكان. ولم يكن بد من ثورة. ثورة جامحة تحطِّم ظلم أجيال طويلة وقرون. وماذا بقى
للمرأة؟ لقد بذلت نفسها وكبرياءها وأنوثتها، وحرمت من حاجتها الطبيعية إلى أسرة
وأولاد تحس بكيانها فيهم، وتضم حيواتهم إلى حياتها، فتشعر بالسعادة والامتلاء.
أفلا تنال مقابل ذلك – على الأقل – المساواة فى الأجر مع الرجل وهو حقها
الطبيعي الذي تقرره أبسط البديهيات؟ ولم يتنازل الرجل الأوربى عن سلطانه بسهولة.
أو قُلْ: لم يتنازل عن أنانيته التى فُطر عليها. وكان لا بد من احتدام المعركة،
واستخدام جميع الأسلحة الصالحة للعراك. استخدمت المرأة الإضراب والتظاهر. واستخدمت
الخطابة فى المجتمعات. واستخدمت الصحافة. ثم بدا لها أنها لا بد أن تشارك فى
التشريع لتمنع الظلم من منبعه، فطالبت أولاً بحق الانتخاب، ثم بالحق الذى يلى ذلك
بحكم طبائع الأشياء، وهو حق التمثيل فى البرلمان. وتعلمت بذات الطريقة
التي يتعلم بها الرجل؛ لأنها صارت تؤدى ذات العمل، وطالبت كنتيجة
منطقية لذلك أن تدخل وظائف الدولة كالرجل، ما داما قد أُعدَّا بطريقة واحدة، ونالا
دراسة واحدة. تلك قصة "كفاح المرأة لنيل حقوقها" فى أوروبا.
قصة مسلسلة، كل خطوة فيها لا بد أن تؤدى إلى الخطوة التالية، رَضِيَ الرجل أو كره،
بل رضيت المرأة أو كرهت، فهي نفسها لم تعد تملك أمرها فى هذا المجتمع الهابط المنحل الذى أفلت منه
الزمام. ومع ذلك كله فقد تعجب حين تعلم أن انجلترا – أم الديمقراطية – لا تزال
إلى هذه اللحظة تمنح المرأة أجرًا أقل من أجر الرجل فى وظائف الدولة، رغم أن فى
مجلس العموم نائبات محترمات!!"
Maneno haya yana maana ya kuwa; “Mapinduzi ya Viwanda yaliyofanyika huko Ulaya yaliwashughulisha
na kuwaathiri zaidi wanawake na watoto kuliko wanaume, hivyo yakawa ni sababu
ya kuvunja mafungamano na mifumo ya kijamii. Katika hali hii mwanamke ndiye
aliyelipa gharama kubwa zaidi kwa juhudi, heshima, na mahitajio yake ya kiroho.
Ni katika hali hii mwanamume, alizembea na kuacha kumhudumia mwanamke, hivyo
mwanamke akajikuta analazimika kufanya kazi ili aikimu nafsi yake hata kama
yeye ni mke wa mtu au ni mama mwenye watoto. Kwa upande mwingine viwanda
vilimtumia mwanamke vibaya sana, vilimtumia kikazi kwa mda mwingi zaidi huku
akipewa malipo kidogo kulingana na mwanamume anayefanya kazi kama hiyo katika
sehemu hiyo hiyo. Hilo si jambo la
kushangaza hata kidogo kwa Ulaya ambayo ilikuwa imegubikwa na ubakhili,
ukatili, ubinafsi, utimbakwiri, nk. Kwani historia inaonyesha dhahiri shahiri
kuwa kuna wakati Ulaya ilifika pahala ikawa haitambui utu wa mwanadamu, na
hivyo ikashindwa kumfanyia mwanadamu heri yoyote badala yake ikajikuta
ikimfanyia shari tena kwa kufurahia madhila hayo, na kuyafanya pasina kujisikia
tabu yoyote. Katika hali hii ambayo ndiyo ilikuwa kawaida ya Ulaya, wanawake na
watoto wadogo ambao kwa maumbile yao ni wanyonge walijikuta wakifanyiwa ukatili
wa kutisha na kutumiwa visivyo pasina kuwepo wa kuwatetea. Ambacho kingeweza
kuwanusuru na hali hii ni kitu kimoja tu nacho ni utashi na dhamira ya kweli,
ambavyo vyote viwili havikuwepo Ulaya. Kwa bahati nzuri wakapatikana watu
wachache waliokuwa na nyoyo zilizokuwa hai ambao hawakuweza kuona na kuvumilia
dhulma na hali hizi zikiendelea ambao kwanza walianza kuwatetea watoto. Wanaharakati
hawa walianza na masuala mazima ya kumfanyisha kazi mtoto katika umri mdogo,
kumfanyisha kazi ambazo umbile lake changa haliwezi kuzimudu, na ujira mdogo
anaopewa ambao haukuwa ukilingana na kazi nzito alizokuwa akifanyishwa.
Harakati hizi hatimaye zilifanikiwa, ikawa malipo ya kazi ya mtoto
yakapandishwa, kidogokidogo, umri wa kufanya kwake kazi ukaongezwa, na saa zake
za kufanya kazi zikapunguzwa. Ama mwanamke yeye hakuwa na wa
kumuokoa au kumunusuru. Maana kumunusuru mwanamke kulihitaji hisia kubwa ambazo
Ulaya haikuwa nazo. Hivyo mwanamke akajikuta akibaki kazini ili aweze kujihudumia,
huku akifanya kazi nzito na malipo yakiwa kidogo sana ukilinganisha na
mwanamume anayefanya kazi hiyo hiyo tena sehemu moja. Kisha vikaja vita vya
kwanza na vya pili vya dunia ambapo mamilioni ya vijana wa Ulaya na Amerika
waliouliwa. Hapo mwanamke akakabiliwa na tabu zaidi kutokana na mamilioni ya
wanawake kubaki pasina familia; kwa kuwa ima familia zao ziliuliwa vitani,
kuharibiwa kimwili na kisaikolojia kutokana na wasiwasi au gesi za sumu
zilizotumika katika vita hivyo, au kutokana na wanaume kutoka kizuizini ambapo
walikuwa kwa mda mrefu na hivyo wakawa wanataka wapumzike, wastarehe bila kuoa
na kuhudumia familia ambazo zingewagharimu mali na nguvu. Kwa upande mwingine,
hakukuwa na wafanya kazi wa kutosha wa kiume ili kuendesha viwanda na kujenga
majengo yaliyoharibiwa na kubomolewa na vita. Hivyo ikawalazimu wanawake kutoka
na kwenda kufanya kazi, la sivyo wangejikuta katika njaa na shida kubwa nao
wana watoto pamoja na vikongwe ambao hawakuwa na wa kumtegemea ila wao. Katika
mazingira haya wanawake walijikuta wakipoteza maadili yao. Kumbe wenye viwanda
hawakuwa wakitaka wafanyakazi tu ambao kwa sasa walikuwa wanawake bali walipata
fursa nyingine kwa wanawake hao nayo ni kutupa mbegu au punje katika mitego
mbele ya ndege wenye njaa ili wadonee mbegu hizo! Hivyo katika hali kama hiyo
watasalimikaje ndege hao na kudonoa mbegu hizo? Kwa kuwa wamepatikana katika
mlango wa dharura wanawake wanaojitahidi watoke ili wafanye kazi, na kazi nazo
sasa wakawa hawapewi ila wale wanawake ambao wanajitahidi wajitoe na kuwa
vyakula vya wenye kuwataka kijinsia. Kwa hiyo mas’ala hayakuwa ya haja ya
chakula tu basi bali maharamia waajiri wa wanawake walichukua fur’sa hii
kuwatafuna wanawake watakavyo. Matamanio ya kijinsia ni miongoni mwa mahitajio
ya kimaumbile ya binadamu ambayo ni lazima ayakidhi. Wala isingewezekana kwa
wanawake wakati ule kukidhi haja za maumbile yao hata kama kila mwanamme
aliyebaki hai wakati ule angeoa kutokana na upungufu mkubwa uliojitokeza wa
wanaume kwa sababu ya vita hivi. Kwa bahati mbaya zaidi itikadi na dini za
Ulaya hazikuwa ni zenye kuruhusu suluhisho lililowekwa na Uislamu katika hali
za dharura kama hizi ambalo ni kuoa mke zaidi ya mmoja. Hivyo ikawa hapana budi
kwa wanawake kuangukia kwa kupenda au kutokupenda katika Zinaa ili tumbo na
tupu zao zipate kushiba. Bali wakajikuta kuwa wanahitaji kuyaridhisha matamanio
yao ili wapate mavazi ya kifaghari, mapambo na vitu mbalimbali miongoni mwa
vitu walivyokuwa wakitamani. Wakawa wanawake hawana budi tena ila kutoa miili
yao kwa wanaowataka, na wakifanya kazi katika viwanda na sehemu nyingine pamoja
na malipo waliyokuwa wakiyapata wakawa pia wanaendelea kuyashibisha matamanio
yao ya kijinsia kwa njia za haramu. Tatizo
likazidi kuwa kubwa zaidi pale wenye viwanda walipochukulia shida ya wanawake
ya kutoka kwenda kufanya kazi kama fursa ya kuwatesa, kuwanyanyasa na
kuwadhulumu pasina sababu yoyote yenye maana kimantiki ya kuwafanyia hivyo
kiakili au kidhamira. Wakawa wakipewa ujira mdogo mno kuliko wanaume wanaofanya
nao kazi kama hiyo katika sehemu hiyo hiyo. Hapo ikawa hakuna budi lazima
yafanyike mapinduzi kuiondoa hali hii ya dhulma iliyodumu kwa mda mrefu tena
vizazi kwa vizazi. Lakini baada ya mageuzi haya wanawake walijitahidi kwa nafsi
zao, na kuonyesha kuwa nao wanaweza na hawashindwi kitu. Hapo wakajikuta wanazikimbia
haja zao za kimaumbile walizoumbiwa na Allah za kuhitaji familia na hivyo bila
wao kupenda wakajikuta wakiwakimbia watoto wao wenye kuwahitaji sana katika
sehemu za maisha yao ili waweze kukua vizuri. Wanawake wakaamua sasa wabaki
hivyo hivyo hata pale ambapo bado waliendelea kupata kiwango kidogo cha ujira
kulingana na wanaume wanaofanya nao kazi sehemu moja tena kazi moja. Wanaume
wa Ulaya kimaumbile walijikuta hawako tayari kuachia ngazi kirahisi na kuwa
sawa na wanawake katika mambo mengi. Hapo wanawake wakajikuta hawana budi
waingie katika migomo na maandamano, wapaze sauti katika makongamano, na vyombo
vya habari ili kuwashinikiza wanaume wawapatie fursa na haki sawa kama
walivyokuwa wakidai. Kisha baadaye wakaona kuwa hawana budi washiriki katika
rasimu za kutunga Sheria ili waweze kuizuia dhulma waliyokuwa wakiiona kuanzia
katika mzizi hadi katika matawi yake. Hapa wakadai
haki ya kushirikishwa katika chaguzi mbalimbali, na haki ya kushiriki
kuwakilisha bungeni. Wakajifunza kwa njia ile ile wanayojifunza mwanamume kwa
kuwa sasa wanafanya kazi ile ile wanayofanya wanaume. Kimantiki wakawa sasa
wanadai waingie katika shughuli za kiserikali kama wanaume maadamu wote yaani
wanaume na wanawake wameandaliwa kwa njia moja na wamepata somo moja. Hicho ndicho kisa
cha wanawake wa Ulaya katika kutafuta haki zao ambacho wanawake wetu
hawakifahamu. Kama ulivyoona kuwa ilikuwa ni hatua kwa hatua, hatua moja
ilipelekea hatua nyingine, wanaume wapende au wasipende, bali wanawake wapende
au wasipende walijikuta wanavutwa na hatua hizo. Pamoja na haya yote wanawake
hawakuzingatiwa kuwa wanamiliki nafsi zao katika jamii hii iliyokuwa
imeporomoka vibaya kimaadili na kupoteza mwelekeo kabisa. Pamoja na yote
haya utastaajabu kuona Uingereza ambayo inadai kuwa ni mama wa demokrasia
duniani bado hadi sasa inawapa wanawake ujira kidogo ukilinganisha na wanaume
katika kazi za serikali pamoja na kuwepo katika bunge la Uingereza wawakilishi
wa kike wenye kuheshimiwa”.
Tunaweza kuongeza katika haya aliyosema Muhammad Qutub
kuwa Mwanamke hadi sasa bado anapata
ujira mdogo Marekani na nchi nyingine nyingi za Ulaya wala si Uingereza tu, na bado
anapigania apate malipo sawa na mwanamume bila mafanikio yoyote.
Katika Suratu Yuusuf aya ya 111 Allah anasema: “Bila shaka katika hadithi zao hizi limo
fundisho kwa wenye akili. Si maneno yaliyozuliwa, bali ni hakikisho la yale
yaliyokuwa kabla yake (miongoni mwa vitabu vya Mwenyezi Mungu) na ni maelezo
pia ya kila kitu (kinachohitajiwa katika dini), na ni uwongofu na rehema kwa
watu wenye kuamini” (12:111)
MSIMAMO
WA UISLAMU KATIKA KUFANYA KAZI MWANAMKE
Msimamo wa Uislamu katika kufanya kazi mwanamke umewekwa wazi na
kisa cha Nabii Mussa na Mabinti Wawili wa Shu‘ayb ‘Alayhim Sswalaatu
Wassalaamu. Katika kisa hicho tunaona kuwa Nabii Mussa alitoka Misri hali ya
kuwa anakimbia kuadhibiwa na Firiawni. Kapita Nabii huyu wa Allah jangwa la
Sinai peke yake hali ya kuwa ni mwenye njaa na kiu kikali, huku akiogopa na
kugeukageuka kuangalia kama kuna mtu anayemfuata kwa nyuma au anamfukuza.
Akafika katika mji wa Madyani nje kidogo ya mipaka ya Mashariki ya mji wa
Misri. Hapo aliona pembeni kuzunguka kisima cha maji idadi kubwa ya wafugaji
wakisongamana na kusukumana katika kuwanywesha wanyama wao. Mbali
kidogo na vurugu na misongamano hii ya wachungaji katika kunyesha wanyama wao
aliwaona mabinti wawili wakiwaswaga na kuwazuia wanyama wao. Walikuwa wakifanya
hivi hadi watakapomaliza watu wengine kuwanyesha wanyama wao ndipo na wao
wapate kuwanywesha wanyama wao. Kwa kuwa Nabii
ni kama baba wa Umma aliwaendea wale
wasichana wawili ili apate kujua kulikoni na apate kutulizana kwa kuwasaidia
pale atakapojua nini shida yao. Wale wanawake wakamwambia kuwa baba yao ni mzee
sana na hali ya afya yake haimruhusu kuja na kuwanywesha wanyama. Hivyo
wamelazimika wao kufanya kazi ile kwa kuwa hawana kaka au waume wa kuwafanyia
kazi ile. Na pale walikuwa wanasubiri hadi watu wengine wanyeshe mifugo yao na
waondoke kisha na wao ndipo wanyweshe. Walikuwa wanafanya hivi kwa kuchelea
wasije wakasukumana na kuchanganyika na wanaume wasiokuwa maharimu wao. Kusikia
hivyo Nabii Mussa akawaonea huruma. Haraka haraka akawasaidia kunywesha mifugo
yao ili wapate kuondokana na tabu ili na kuchanganyika na wanaume. Mabinti wale
wawili wakamshukuru Nabii Mussa na kuondoka. Nabii Mussa akaelekea katika
kivuli cha mti akakaa chini ya kivuli hicho huku akimuomba na kumnong’oneza
Mola Wake.
Baada ya muda si mrefu akamuona mmoja kati ya wale mabinti
wawili akimjia tena karibu ajikwae na kuanguka kutokana na soni aliyokuwa nayo
wakati akija. Huku akiwa anaufunika uso wake kwa Niqaab na akishindwa
hata kunyanyua macho yake juu ya ardhi kutokana na haya iliyokithiri, alimwambia
Nabii Mussa kuwa baba yao ametambua alichofanya katika wema ule wa kuwahudumia
binti zake wawili na hivyo anapenda awe mgeni wake na amlipe kwa kazi ile nzuri
aliyofanya. Nabii Mussa alikubali na akaongozana naye kwenda kwa baba yao
lakini alimtangulia binti yule japo alikuwa hapajui kwao ila alimtaka binti
yule awe akimwambia apinde aidha kulia au kushoto hadi wafike nyumbani kwao.
Hapa yule binti aliyemwendea
Mussa na kumwambia kuwa baba yake anamuita, walipofika
kwao alitoa rai kwa baba yake kuwa amwajiri Mussa awe akichunga na kuwanywesha
wanyama wao badala yao. Pia alimweleza baba yake nguvu za Nabii Mussa na
Uaminifu wake; na hizi ni sifa mbili za msingi kwa mfanya kazi bora. Mwanamke
yule mwenye akili aliyajua yale kutokana na busara ya akili yake kuwa bila
shaka Nabii Mussa ana nguvu sana maana aliweza kunyanyua peke yake jiwe
lililokuwa likifunika mdomo wa kisima ambalo watu kadhaa walikuwa wakishindwa
kulinyanyua lakini yeye peke yake aliweza kulinyanyua. Ama Uaminifu wake dalili
yake ni kuwa Mussa alikataa binti yule amtangulie kutokana na kuhifadhi kwake
macho kwani kwa dada yule kutangulia ingeweza ikatokea upepo ukapepea nguo zake
na hivyo kumfanya Mussa ambaye si mahrimu wake aone maumbile yake. Baba wa
mabinti wale wawili ambaye ni Shu‘ayb alikubali fikra ile iliyotoka kwa mmoja
wa mabinti wake ya kumuajiri Nabii Mussa na wakakubaliana na Mussa afanye kazi
ile miaka minane ambayo pia ndiyo itakuwa ndiyo mahari ya mmoja wa binti zake
wale kama alivyopendekeza mzee yule mwenye hekima. Muda aliotaka mzee yule
ulikuwa ni miaka minane (8) lakini kama Mussa atatimiza miaka kumi hiyo
ni kwa mapenzi yake. Lakini Nabii Mussa akaamua kufanya kazi ile kwa miaka
kumi, malipo yakiwa ni chakula na kuhifadhi utupu yake. Baada ya Mussa kumaliza
miaka minane alifungishwa ndoa. Hichi ndicho kisa cha Nabii Mussa na mabinti
wawili wa mzee Shu‘ayb kama Allah alivyokieleza katika Suratul Qaswas na
vilvile kimetajwa katika Taurati. Ndani ya Qur’ani Tukufu Allah anasema katika
aya ya 23 hadi 28 ya Suratul Qaswas:
{وَلَمَّا وَرَدَ مَاءَ مَدْيَنَ وَجَدَ
عَلَيْهِ أُمَّةً مِنَ النَّاسِ يَسْقُونَ وَوَجَدَ مِنْ دُونِهِمُ امْرَأَتَيْنِ
تَذُودَانِ قَالَ مَا خَطْبُكُمَا قَالَتَا لاَ نَسْقِي حَتَّى يُصْدِرَ
الرِّعَاءُ وَأَبُونَا شَيْخٌ كَبِيرٌ * فَسَقَى لَهُمَا ثُمَّ تَوَلَّى إِلَى
الظِّلِّ فَقَالَ رَبِّ إِنِّي لِمَا أَنْزَلْتَ إِلَيَّ مِنْ خَيْرٍ فَقِيرٌ *
فَجَاءَتْهُ إِحْدَاهُمَا تَمْشِي عَلَى اسْتِحْيَاءٍ قَالَتْ إِنَّ أَبِي
يَدْعُوكَ لِيَجْزِيَكَ أَجْرَ مَا سَقَيْتَ لَنَا فَلَمَّا جَاءَهُ وَقَصَّ
عَلَيْهِ الْقَصَصَ قَالَ لاَ تَخَفْ نَجَوْتَ مِنَ الْقَوْمِ الظَّالِمِينَ *
قَالَتْ إِحْدَاهُمَا يَا أَبَتِ اسْتَأْجِرْهُ إِنَّ خَيْرَ مَنِ اسْتَأْجَرْتَ
الْقَوِيُّ الْأَمِينُ * قَالَ إِنِّي أُرِيدُ أَنْ أُنْكِحَكَ إِحْدَى ابْنَتَيَّ
هَاتَيْنِ عَلَى أَنْ تَأْجُرَنِي ثَمَانِيَ حِجَجٍ فَإِنْ أَتْمَمْتَ عَشْرًا
فَمِنْ عِنْدِكَ وَمَا أُرِيدُ أَنْ أَشُقَّ عَلَيْكَ سَتَجِدُنِي إِنْ شَاءَ
اللَّهُ مِنَ الصَّالِحِينَ * قَالَ ذَلِكَ بَيْنِي وَبَيْنَكَ أَيَّمَا
الأَجَلَيْنِ قَضَيْتُ فَلاَ عُدْوَانَ عَلَيَّ وَاللَّهُ عَلَى مَا نَقُولُ وَكِيلٌ}
Aya hizi zina maana ya kuwa; “Na alipoyafikia maji ya Madyani (mahali wanapoteka maji watu
wa hapo), alikuta kundi la watu wananywesha (wanyama wao), na akakuta kando yao
wanawake wawili
wanazuia (wanyama wao wasiende kunywa maji pamoja na wale wanyama wengine).
Akasema (Mussa): “mna nini”? (Mbona hamteki na nyinyi na mkanywesha wanyama
wenu)? Wote wawili wakasema: “hatunyweshi mpaka wachungaji warudishe (wanyama
wao; hatuwezi kupigna nao vikumbo), na baba yetu ni mzee sana. Basi (Mussa)
akawanyweshea, kisha akarudi kivulini, na akasema: “Mola wangu! bila shaka mimi
ni mhitaji wa heri utakayoniteremshia”. Basi akamjia mmoja katika wale wawili,
anakwenda na huku anaona haya, akasema: “baba yangu anakuita ili akulipe ujira
wa kutunyweshea”. Basi alipomfikia na kumsimulia kisa chote, alisema: “usiogope
umekwisha kuokoka na watu madhalimu”. Akasema mmoja wa wale wawili: “ewe baba
yangu! mkodi huyu (awe anachunga wanyama wako badili yetu). Bila ya shaka mbora
uwezaye kumuajiri ni ambaye mwenye nguvu, mwaminifu (Na huyu ana sifa zote
hizi). Akasema: “Mimi nataka nikuoze mmojawapo katika binti zangu hawa wawili
kwa kunitumikia miaka minane; na kama ukitimiza kumi ni hiari yako, lakini mimi
sitaki kukutaabisha: utanikuta Inshaallah miongoni mwa watu wema”. Akasema
(Mussa): “mapatano hayo yamekwisha kuwa baina yangu na baina yako; muda
mmojawapo nitakaoumaliza basi nisidhulumiwe; na Mwenyezi Mungu ni mlinzi juu ya
haya tunayoyasema”. (Qaswas: 23-28)
Kalamu haiwezi kukiandika na kukimaliza kila kilichopo katika aya
hizi sita miongoni mwa Adabu, Mazingatio na Shari’ah zenye kumhakikishia
mtu mafanikio katika dunia na akhera. Si makusudio yangu kueleza mambo hayo
hapa lakini nitajitahidi kutohoa katika aya hizo mipaka ya wanawake kufanya
kazi nje ya nyumba zao na jukumu la kila upande katika kumchunga adabu na
nyajibu zinazotakikana kwa wote wanawake na wanaume. Aya zinawawekea wazi wenye
kutafakari mambo yafuatayo;
1.
Haifai kwa wanawake kutoka kwenda kufanya kazi nje ya nyumba zao
ila katika hali ya dharura kubwa. Na kubwa zaidi ya dharura hizo ni kukosekana kwa
wanaume katika maharimu zao wenye kufanya kazi. Mabinti wale wawili walimwambia
Nabii Mussa kuwa wao wamelazimika kufanya kazi ile kwa kuwa baba yao ni mzee
sana na hivyo hana uwezo wa kufanya kazi na hawakuwa na mwanamume mwingine
ambaye angeweza kufanya kazi ile. Hawakuwa na ndugu wa kiume kama kaka, mjomba,
baba mdogo, au baba mkubwa ambaye angefanya kazi ile badala yao. Hivyo
wamejikuta wanalazimika kutoka kwenda kuchunga na kuwanywesha wanyama wao ili wasije
wakafa kwa njaa na kiu.
2.
Wanawake wanapolazimika kutoka kwenda kufanya kazi basi iwe ni
kwa Heshima na Uchaji Mungu (Taq’wa) na wasijichanganye na wanaume wasiokuwa
maharimu zao. Kisa cha mabinti hao
kinatueleza kuwa Nabii Mussa aliwaona mabinti wale wawili wakiwazuia wanyama
wao wasiende kunywa maji pamoja na wale wanyama wa watu wengine mpaka wale wachungaji
wengine warudishe wanyama wao ndipo na wao waende kunywesha wanyama wao kwa
kuchelea kusongamana na kupigana vikumbo nao, jambo ambalo lingeweza kupelekea mathalani
mtu muovu kuwasogelea. Kwa kufanya vile walivyofanya wakawa wamefunga mlango wa
fitna za shetani na matamanio ya kuyaendea machafu ya Zinaa. Jingine ni kuwa
walikuwa hawasemi na yeyote. Na lau kama si Nabii Mussa kuwauliza kwa heshima
na adabu ili awasaidie basi wasingesema na yeyote. Unaona pia walimwachia
awafanyie kazi ile nzito ya kuteka maji kwa ajili ya wanyama.
3.
Wanawake kuzungumza na wanaume wa mbali ambao si maharimu zao ni
dharura tu tena mazungumzo hayo yawe katika kiwango cha lazima cha kusherehesha
hali hiyo ya dharura pasina kuzidisha zaidi ya hapo kama inavyoonyeshwa katika
kisa hicho ambacho zaidi ya hapo binti yule aliyekuja kumuita Nabii Mussa
alilazimiana na adabu, heshima, haya na aibu.
4.
Ni juu ya wenye madaraka au wenye uwezo katika jamii miongoni
mwa wanaume wafanye kila wawezalo katika kuwaondolea wanawake tabu na shida za
kufanya kwao kazi nje ya majumba yao. Kwa kufanya hivyo watawalinda na madhila
ya kuchanganyika na wanaume. Ndipo utaona kuwa Nabii Mussa alifanya haraka
katika kuwasaidia kuwanywesha wanyama wao. Lau kama tungekuwa tunafanya kama Nabii
Mussa alivyofanya basi tungeweza kuondoa katika jamii yetu shida na majanga
mengi yanayowasibu wanawake ambayo sote tunayajua vyema. Na ni juu ya wanawake
kumshukuru Allah pale wanapopata neema ya wanaume wanaosimama katika kufanya
kazi badala yao.
5.
Tunaona vile vile kuwa wanawake wale wawili walikubali hali ya
kuwa ni wenye kushukuru msaada wa Nabii Mussa na wakapupia katika kuitumia
fursa ile kumshauri na kumuomba baba yao amwajiri Nabii Mussa ili awe akifanya
kazi ile nao waweze kuondokana na tabu za kazi nje kama kazi ile ya kuchunga
wanyama na kuwanywesha. Wala hawakumwambia baba yao kuwa awape nafasi kama ile
ya “hawavumi lakini wamo” yaani wajitegemee, na kuhakiki kuwa wao
wanajiweza na kuwa hawana haja na kusaidiwa na wanaume kama wanavyodai wale
wanawake wa “khamsini kwa khamsini” katika lile tangazo maarufu la
jinsia na haki sawa hapa nchini Tanzania; ni kweli kuwa “mkono ubebao mwana
ndio uleao taifa”, lakini hilo ni “neno la haki ambalo ndani yake
itafutwao ni batili”. Au kama wale wanawake wasemao katika makongamano
yaliyoanzia kule Beijing China kuwa wanawake ni kama wanaume katika kila
kazi.
6.
Baba ambaye ni msimamizi wa mabinti wale wawili haraka haraka
aliamua kumuajiri Nabii Mussa ili awe akifanya kazi badala ya watoto wake ili
kuwahifadhi watoto wake na tabu, mitihani, na fitna kwa kufanya kwao kazi nje
ya nyumba. Bali kisa hiki kinatufundisha kuwa inafaa kwa mzazi kumwambia kijana
mcha Mungu kuwa amuoe binti wake, wala hapana aibu juu ya mzazi wa binti
kufanya hivyo kwa binti wake kwani kijana mwema na mchaji Mungu atamchunga
binti huyo na kumhifadhi na mambo ya haramu na mambo mabaya. Na tunaona vile
vile Hikma ya Mzee Shu‘ayb, katika kurahisisha ndoa ya mtoto wake. Nabii Mussa
alitoka Misri bila mali yoyote, wala asingeweza kulipa mahari lakini Mzee Shu‘ayb
akamfanyia Nabii Mussa utaratibu ambao Nabii Mussa kama mgeni katika mji ule
angeweza kuoa nao ni kumuajiri. Na hapa kuna dalili kuwa mahari yanafaa kuwa
huduma na si lazima yawe fedha au dhahabu tu. Katika kitambo cha Nabii Mussa
kufanya kazi kwa Mzee Shu‘ayb palipatikana manufaa kwa pande zote mbili,
matatizo ya wale mabinti wawili yaliondoka upesi baada ya baba yao kuafikishwa
na Allah kufanyia kazi ombi na ushauri wa mmoja wa binti zake wale wawili wa
kutaka Nabii Mussa aajiririwe ili awe akifanya kazi ile badala yao, na Allah
kumuwafikisha Mzee Shu‘ayb kumuozesha Nabii Mussa mmoja wa wale binti zake
wawili kwa mahari ambayo yalikuwa ni ujira wa kazi aliyokubaliana na Nabii Mussa
aifanye. Allah aliwatosheleza mabinti wale wawili kufanya kazi nje ya nyumba
yao na baba yao akapumua kutokana na wasiwasi wa kutoka kwao kila mara kwenda
kulisha na kunywesha wanyama wao. Vile vile Nabii Mussa alipata kazi tukufu,
makazi, na Allah akamruzuku mmoja wa
mabinti wawili kuwa mke.
Katika kisa hichi tunajifundisha pia kuwa inapasa kuepuka vitu
vinavyochochea Shaka na Shubha. Utaona kuwa mwananamke yule alimwambia Nabii Mussa
kuwa baba yake ndiye anayemuita na wala si yeye ndiye aliyekuwa anamuita. Vile
vile tunaona kuwa Nabii Mussa alikataa kutembea nyuma au pembeni ya msichana
yule kwa kuhofia isije ikatokea upepo ukamfunua au ukawa ndio sababu ya yeye
kuona umbile lake au uchi wake. Ni wazi kuwa Shari’ah ya nyumati zilizotangulia
ni Shari’ah yetu maadamu haijaja katika sheria yetu kinachopingana nayo au
kuifuta Shari’ah hiyo. Kwa mantiki hii basi mipaka hii ya kazi na kutoka nje
kwa wanawake iliyoonyeshwa katika kisa cha Nabii Mussa na Mzee Shu‘ayb
inawahusu Waislamu pia au Ummah huu hadi siku ya Qiyama kwani kila ujumbe wa
mbinguni sifa yake kuu ni moja ambayo ni Kumpwekesha Allah na kuwalea watu
katika Tabia njema.
Katika kukokoteza hilo Sunnah na Sira ya watoto na wake wa Mtume
Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama na tarjama za wanawake wa kiswahaba na
wakitaabiina vimeweka wazi mipaka ya mwanamke kufanya kazi. Hapa tutatosheka na
mifano michache.
Mfano wa
kwanza: Huu unaenda kwa Bi Khadija mke wa Mtume Swalla Llaahu ‘Alayhi
Wasallama. Tunakuta kuwa Bi Khadija alimwajiri Mtume Swalla Llaahu ‘Alayhi
Wasallama alipokuwa kijana kutokana na sifa ya ukweli na uaminfu wake ili
amfanyie biashara yake. Akamtuma kwenda katika mji wa Shamu katika msafara wa
kibiashara pamoja naye kijana wake aliyekuwa akiitwa Maysara kama
inavyojulikana katika Sira. Hapa kuna funzo kubwa kwa wanawake wanaofanya kazi
au biashara nalo ni kuwa hakuna ruksa ya kukaa faragha na wanaumme wanaomfanyia
kazi wala hairuhusiwi kusafiri nao kwa hoja ya kazi. Angalia Bi Khadija
alimtuma Mtume Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama pamoja na kijana wake Maysara
wala hakuchukua fursa ile ili asafiri naye na aweze kubadlishana mazungumzo kwa
hoja ya kuwa eti wanafanya biashara. Wala Mtume Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama
akiwa bado hajapewa Utume na akiwa bado hajamuoa Khadija hakuwahi kukaa naye
Faragha hata siku moja hadi pale rafiki yake wa kike wa Khadija alipomwambia
Mtume Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama kuwa amuoe Khadija naye Mtume Swalla Llaahu
‘Alayhi Wasallama akakkubali na uchumba ukafanyika ukifuatiwa na ndoa na hapo
ndipo Mtume Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama akakaa faragha na Khadija.
Mfano wa
pili: Mfano huu unaenda katika kile anachokisimulia Imamu Bukhaar Rahimahu Llaahu
katika mlango aliouita “Kufanya kazi
mwanamke katika nyumba ya mume wake”. Katika
mlango huo ameleta hadithi, Imamu ‘Aliy Radhiya Llaahu ‘Anhu anasimulia namna mkewe
Faatwimah Radhiya Llaahu ‘Anhaa alivyokuwa akipata tabu na kuchoshwa na kazi za
nyumbani kwake. Jiwe la kusagia nafaka lilikuwa likiiumiza mno mikono yake na
hadi mara nyingine kumchubua na kuvifanya kuwa vigumu vidole vyake. Hadi
ilifikia wakati akamuomba baba yake yaani Mtume Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama
amtafutie mfanyakazi au mtumishi wa kufanya kazi hiyo. Mtume Swalla Llaahu
‘Alayhi Wasallama akamwambia mwanawe Faatwimah: “Hivi nisikujulishe jambo lililobora zaidi ya huyo mfanyakazi
unayemtaka? Msabbihi Allah wakati wa kulala mara thelathini na tatu
(33), na Umuhimidi mara thelathini na tatu (33), na Umkabbir mara thelathini na
nne (34)”. Ushahidi hapa ni kuwa
Faatwimah alikuwa akifanya mwenyewe shughuli za nyumbani kwake. Imepokewa
katika vitabu vya Tarjama kuwa Imamu ‘Aliy Radhiya Llaahu ‘Anhu alikubaliana na
mke wake Bi Faatwimah Radhiya Llaahu ‘Anhaa kuwa mkewe Faatwimah awe akifanya
kazi za ndani ya nyumba na mumewe ‘Aliy Radhiya Llaahu ‘Anhu awe akitoka
kufanya kazi za nje. Na hii ndiyo asili na njia nzuri ya kudumisha maisha ya
ndoa na malezi bora kwa watoto. Kwa hakika kuwalea vijana mashababu wawili
ambao ni alama na nyota katika Ummah huu yaani Hassan na Hussayn ni zaidi ya
kutafuta chakula, mavazi na malazi.
Vile vile amepokea Imamu Bukhaar Rahimahu Llaahu hadithi muhimu
sana katika mlango wa “Wivu” ambayo
inakusanya mambo muhimu katika durusu au masomo na Hikma zikibaini mipaka ya
kutoka mwanamke kwenda kufanya kazi au kwa ajili ya dharura nyingine.
Anatusimulia Imamu Bukhaari Rahimahu Llaahu kisa kilichomtokea Asmaa Binti Abii
Bakr Allah Amuwie Radhi yeye na baba yake. Asmaa Radhiya Llaahu ‘Anhaa alikuwa
mke wa Zubayir Ibnul ‘Awaam Radhiya Llaahu ‘Anhu. Alihama kutoka Makkah ili
aishi na mume wake Madina. Hawakuwa na mali yoyote isipokuwa ngamia mmoja
ambaye walikuwa wakimtumia kubeba maji kutoka katika kisima kilichokuwa mbali
kidogo na kuyaleta nyumbani na farasi mmoja ambaye Zubayir Radhiya Llaahu ‘Anhu
alikuwa akimtumia kwa ajili ya kupigania vita na Mtume Llaahu ‘Alayhi Wasallama na kwa ajili
ya safari. Zubayir Radhiya Llaahu ‘Anhu alikuwa akienda kufanya kazi nje
kutafuta Rizki na Asmaa Radhiya Llaahu ‘Anhaa akibaki nyumbani kufanya kazi za
nyumbani ikiwemo kumlisha farasi. Kutokana na hali yao nguvu ya maisha Asmaa
Radhiya Llaahu ‘Anhaa alilazimika kutoka na kutembea takriban kilomita tatu
hivi kwenda katika kipande cha ardhi alichokuwa amepewa Zubayir Radhiya Llaahu
‘Anhu na Mtume Llaahu ‘Alayhi Wasallama. Asmaa Radhiya Llaahu ‘Anhaa alikuwa
akienda shambani huko ili kuokota kokwa za tende ili aje azisake na kumlisha
farasi wao. Siku moja Asmaa Radhiya Llaahu ‘Anhaa akiwa amebeba kokwa za tende
akirudi nyumbani alikutana na Mtume Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama akiwa
pamoja na baadhi ya Swahaba zake Radhiya Llaahu ‘Anhum. Hapo Mtume Swalla Llaahu
‘Alayhi Wasallama akamuinamisha chini ngamia wake ili Asmaa Radhiya Llaahu
‘Anhaa aweze kupanda nyuma yake. Mtume Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama alifanya
hivi kutokana na kumuonea huruma shemeji yake kutokana na uzito wa kokwa
alizokuwa amebeba. Lakini Asmaa Radhiya Llaahu ‘Anhaa aliona haya na akakumbuka
wivu wa mumewe Zubayir Radhiya Llaahu ‘Anhu. Kwa kwa maneno aya Asmaa Radhiya Llaahu
‘Anhaa ni kuwa mumewe Zubayir Radhiya Llaahu ‘Anhu alikuwa ni mtu mwenye wivu
sana. Mtume Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama kwa akili yake ya hali ya juu
alilijua hilo, akaondoka na kumuacha na jambo lake pasina kumsemesha
chochote. Na alipokuja Zubayir Radhiya Llaahu
‘Anhu Asmaa Radhiya Llaahu ‘Anhaa alimsimulia kilichotokea na kuwa alikataa
kupanda na Mtume Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama kutokana na kujiweka mbali na
vitu ambavyo vinaweza kuchochea wivu wa mumewe. Hapo Zubayir Radhiya Llaahu
‘Anhu akamwambia mkewe Asmaa Radhiya Llaahu ‘Anhaa: “Wallahi kubeba kwako kokwa za tende kulikuwa kuzito kwangu kuliko
kupanda kwako na Mtume Swalla Llaahu
‘Alayhi Wasallama” Asmaa aliongeza kuwa baba yake Abuu Bakr Radhiya Llaahu
‘Anhu alimtumia mfanyakazi kwa ajili ya kumchunga na kumlisha farasi yule na
hivyo kumpumzisha Asmaa Radhiya Llaahu ‘Anhaa na kazi ile. Asmaa Radhiya Llaahu
‘Anhaa anaelezea kuwa ni kama alikuwa ameachwa huru akimaanisha kuwa mfanya
kazi yule alimpumzisha na kazi nzito ambazo alijiona ni kama mtumwa nje ya
nyumba. Katika kisa hichi tunaweza kwa
ufupi tukabaini mipaka ya kazi ya mwanamke bali kutoka kwake nje ya nyumba yake
kwa dharura yoyote ile kama ifuatavyo:
1.
Asmaa Radhiya Llaahu ‘Anhaa hakutoka kwenda kutafuta kokwa za
tende katika ardhi ya mbali takribani kilometa tatu isipokuwa ni kwa kuwa Zubayir
Radhiya Llaahu ‘Anhu hakuwepo, wala hakukuwa na njia kwa Asmaa Radhiya Llaahu
‘Anhaa ya kuikwepa kazi ile ya kumlisha farasi kokwa zile ambazo alikuwa
anazileta kutoka mbali. Vile vile utaona kuwa Asmaa Radhiya Llaahu ‘Anhaa
hakutumia zaidi ya muda wa lazima kwa kazi ile. Jingine hapa ni kuwa Asmaa
Radhiya Llaahu ‘Anhaa kama mtoto wa Abuu Bakr Swiddiki Radhiya Llaahu ‘Anhu
alikuwa akitoka kuiendea kazi ile kwa heshima na adabu na katika hali ya kuwa
amevaa hijabu yake kamili na kujisitiri kama Shari’ah ya Kiislamu
inavyoamrisha.
2.
Asmaa Radhiya Llaahu ‘Anhaa hakuzungumza na mwanamume yeyote
miongoni mwa wale Maswahaba waliokuwa na Mtume Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama,
wala hakuna Swahaba yeyote aliyezungumza naye miongoni mwa wale Swahaba, bali
hakuzungumza hata na Mtume Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama ambaye ni Ma‘asuum
na yuko juu ya mstari wa Shubha, tena Mtume Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama ni
shemeji yake kwani ni mume wa dada yake
‘Aishah Radhiya Llaahu ‘Anhaa. Pamoja na haya yote aliona haya kama hadithi
inavyotuonyesha maana katika hadithi hiyo Asmaa anasema: “Nikajisikia haya kutembea nyuma ya wanaume”, kama alivyoheshimu
Asmaa hisia za mumewe, ambaye alikuwa hayuko kwa kuleta hisia za kuwepo kwake,
lau kama angekuwepo ingekuwaje. Zubayir Radhiya Llaahu ‘Anhu ni mtoto wa Swafiyya Radhiya Llaahu ‘Anhaa ambaye alikuwa
ni shangazi wa Mtume Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama na miongoni wa watu wa
mwanzo kabisa kuingia katika Uislamu, na mmoja kati aya watu kumi
waliobashiriwa pepo na Mtume Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama. Swahaba kama huyu
si rahisi hata mara moja awe na shaka na Mtume Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama,
Mtume ambaye Allah kamsifu kuwa ana tabia nzuri na iliyotukuka kabisa. Katika
hadithi iliyoko katika sahihul Bukhaar mlango wa “Wivu” ‘Umar Radhiya Llaahu
‘Anhu alimwambia Mtume Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama nitaonaje wivu juu yako
ewe Mtume hali ya kuwa wewe ni mchaji Mungu na mwanadamu uliyetwaharika na
mwanadamu uliye mkubwa sana?
3.
Japo Mtume Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama ni Ma‘asumu naye ni
kama baba kwa Ummah huu na hivyo kila mwanamke ni kama maharimu wake kwa
muktadha huu, lakini anatufundisha kuwaheshimu wanawake na hasa wale ambao
shida zimewalazimu kutoka na kwenda kufanya kazi au kutibiwa, na hilo si
kisingizio cha wao kuchanganyika na wanaume. Bali inayopasa ni kuwaacha
wanawake katika hali yao na wala si kama tunavyoona katika masiku haya ambayo
kuna matani mengi, kuzungumza sana kati ya wanawake na wanaume wasiokuwa maharimu
wanaofanya kazi. Ndipo utaona kuwa Mtume Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama
alimwacha Asmaa Radhiya Llaahu ‘Anhaa aendelee na jambo lake pasina kumsemesha
na kwa kuchunga wivu wa mume wake na akakiri kwa hilo kanuni ya udharura wa
wote kuheshimu hisia zake.
4.
Abuu Bakr Radhiya Llaahu ‘Anhu kwa nafasi yake anatufundisha
somo muhimu hapa nalo ni kuwa pindi aliposikia kilio cha binti wake alimpelekea
mfanya kazi kwa ajili ya kumchunga na kumpa chakula farasi. Na hili linaweka
wazi jukumu linalohitajika kwa kila mas’uulu wa mambo awe ni baba, mume au
hakimu, katika kuwalea wanawake na kuwaondelea kazi nzito zenye kuwataabisha
nje ya nyumba zao na kuwasaidia wafaniklishe lile ambalo ni muhimu zaidi kwao
nalo ni kulea na kuwakuza watoto malezi na makuzi bora na kuwashughulikia waume
zao vizuri, na kushughulikia mambo ya nyumba kwa ujumla. Ni kwa msingi wa Tabia
njema na Akhlaq kama hizi Asmaa Radhiya Llaahu ‘Anhaa aliwalea mafahali wawili
katika Uislamu nao ni Khalifa shujaa ‘Abdillah Ibn Zubayir na Musomi mkubwa ‘Uruwatu
Ibn Zubayir Radhiya Llaahu ‘Anhumaa.
5.
Asmaa Radhiya Llaahu ‘Anhaa anatufundisha kuwa pamoja na
kujiheshimu na kuepuka kuchanganyika na wanaume, wanawake wa Kiislamu wakubali
kufanya kazi za nyumbani pale inapotokea kuwa kuna wanaume wa kufanya kazi kwa
niaba yao. Kwa hiyo kufanya kwake kazi Asmaa Radhiya Llaahu ‘Anhaa nje ya
nyumba ni kutokana na dharura ya kukosekana wa kufanya kazi hiyo. Lakini pale
Allah alipoleta faraja hiyo ya Asmaa kuletewa mfanya kazi na baba yake
alifurahi sana hadi akakizingatia kitendo kile cha baba yake kumletea mfanya
kazi kama neema ya kuachwa huru.
Kwa ufupi tunaweza kusema baada ya yote hayo kuwa inafaa kwa
mwanamke kutoka na kwenda kufanya kazi nje ya nyumba yake katika hali ya
dharura na kulazimika kwake kufanya hivyo, lakini kwa sharti la kujiheshimu na
kusalimika na fitna na kuwa kazi yenyewe iwe ni ya halali Kishari’ah na
mwanamke huyo ajiweke mbali na kuchanganyika na wanaume wasiokuwa maharimu wake
na kuwa kazi hiyo isiathiri majukumu ya nyumba yake, watoto na haki za mume
wake.
DHARURA
ZA KIJAMII
Miongoni mwa sehemu ambazo inafaa wanawake kufanya kazi nje ya
nyumba zao ni pamoja na takhasusi au “specializations” maalumu na sehemu
za dharura kwao mfano Tiba ya Wanawake, Uzazi au Ukunga, Kutahiri, na Kufundisha
Wanawake katika hatua zote za elimu.
Katika historia tukufu ya Uislamu kuna mifano inayoonyesha maeneo ambayo
wanawake wanalazimika kufanya kazi hata kama ni nje ya nyumba zao.
1.
Eneo la kitabibu: katika eneo hili
wanawake walifanya kazi hata wakati wa Mtume Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama.
Hapa tunamkuta Ummu ‘Atiyyatul Answaariyyatu Radhiya Llaahu ‘Anhaa alikuwa
akifanya kazi ya kutahiri na pia kuzalisha wanawake. Kazi hii inaweza
ikafananishwa na kazi ya kutibu na kuuguza wanawake katika zama hizi. Rufaidah
Al aslamiyyat Radhiya Llaahu ‘Anhaa alikuwa akishughulika na kutibu majeraha na
huduma ya kwanza. Mtume Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama alimruhusu kutengeneza
hema ndani ya msikiti wa Mtume Madina. Akawa akipelekewa wagonjwa katika
nyakati za dharura mfano katika vita vya Ahzaabu au Khandaq na akiwapa huduma
ya kwanza. Jambo la wazi ni kuwa hakukuwa katika mji wa Madina na wanaume
waliokuwa wana takhasusi au ujuzi huu kwani lau kama wangekuwepo basi Mtume
angeliwataka wamtibu Saad Bin Mua’adh Radhiya Llaahu ‘Anhu alipojeruhiwa siku
ya Uhud, lakini tunakuta Mtume Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama katika hali ya
dharura aliamrisha Saad Radhiya Llaahu ‘Anhu apelekwe akatibiwe na bi Rufaida
Radhiya Llaahu ‘Anhaa katika hema lake. Lakini Qadar ya Allah ikashinda juhudi
za bi Rufaidah Radhiya Llaahu ‘Anhaa za kutaka kuokoa maisha ya Sa’ad Radhiya Llaahu
‘Anhu. Kwa hakuna ikhitilafu ya wanachuoni kuwa katika udharura wa hali ya
kitabibu na uuguzaji wa wanawake wenzao. Hakuna pia ikhitilafu vile vile kwa
wanawake kuwafundisha wanawake wenzao katika hatua zote za elimu. Imethibiti
kuwa Mtume Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama alimwamrisha Shaffaa bint ‘Abdillah
Radhiya Llaahu ‘Anhaa kumfundisha Ruq’ya kama alivyoeleza Ibn Sa’ad Rahimahu Llaahu
na kuboresha hati kama walivyotaja wengine. Hii ni dalili ya kuwa wanawake
wanatakiwa wawatibu wanawake wenzio. Hivyo katika hali ya kuwepo walimu wajuzi
wa kike wa kutosha katika kila hatua ya elimu haitakiwi kwa wanaume
kuwafundisha wanawake. Mtu ambaye hili halimfurahishi basi na arejee ripoti za
wataalamu wa elimu Ulaya na Marekani ambao wanataka wanawake na wanaume
watenganishwe na wanawake katika hatua zote za masomo kutokana na matatizo
mbalimbali yanayojitokeza kwa sababu ya wanawake kuchanganyika na wanaume.
Kisha swali ni kuwa; ni kwa nini watu wang’ang’anie wanawake lazima wafundishwe
na wanaume hata kama wako wanawake wajuzi na wa kutosha wa kuwafundisha
wanawake?
2.
Inawezekana kwa wanawake kutoa msaada wa chakula na dawa kwa
wanajeshi inapotokea kukosekana wanaume wanaofanya kazi hiyo au kuwa wachache.
Imamu Bukhaari Rahimahu Llaahu amepokea hadithi nyingi zikithibitisha kushiriki
kwa wanawake katika kazi ya kusaidia kuuguza wanajeshi vitani. Miongoni mwa
hadithi hizo ni kuwa ‘Umar Radhiya Llaahu ‘Anhu alimpa nguo ya thamani sana
Ummu Sulayt Radhiya Llaahu ‘Anhaa (mama yake na Abii Saidil Khudriy Allah Amuwie
radhi) na akakataa kumpa mke wake Ummu Kulthum Radhiya Llaahu ‘Anhaa (mtoto wa
Imamu ‘Alii Radhiya Llaahu ‘Anhu). Akasema Faaruq ‘Umar Radhiya Llaahu ‘Anhu
kuwa Ummu Sulayt Radhiya Llaahu ‘Anhaa anastahiki zaidi, na akatoa sababu ya
kufanya hivyo kuwa Ummu Sulayt Radhiya Llaahu ‘Anhaa ni miongoni mwa watu
waliombai Mtume Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama na alikuwa akitengeneza viroba
vya kunywea maji siku ya vita vya Uh’udi. Na amepokea Imamu Bukhaar Rahimahu Llaahu
kutoka kwa Rabiu binti Muhawadh Allah amuwie radhi amesema: “Tulikuwa pamoja na Mtume Swalla Llaahu
‘Alayhi Wasallama tukiwanywesha watu maji, na tukitibu majeruhi na
tukiwarejesha waliouwawa Madina”. Na amepokea Imamu Bukhaar Rahimahu Llaahu
kutoka kwa Anas Allah amuwie Radhi amesema: “Tulipokuwa Uhudi watu walimkimbia Mtume, na kwa hakika nilimuona
‘Aishah binti Abii Bakr na Ummu Sulaym Radhiya Llaahu ‘Anhumaa wakiwa
wananyanyua nguo zao, niliona vikuku katika nyayo zao, wakibeba viroba vya maji
mingoni mwao, kisha wakimimina maji midomoni mwa majeruhi, kisha wakirudi na
kwenda kuvijaza katika kisima kisha wakija navyo na kuwamiminia majeruhi
mdomoni”. Hadithi hizi na nyingine ni dalili kuwa mwanamke anaruhusiwa
kufanya kazi katika kutoa msaada wa chakula, maji na tiba panapokuwa na haja na
dharura ya kufanya hivyo, pindi wanaume wanaposhughulika na vita au katika
nyakati za majanga ya asili kama matetemeko ya ardhi, vimbunga, volkano,
mafuriko na kadhaalika.
3.
‘Umar Radhiya Llaahu ‘Anhu alimwachia usimamizi wa soko la
Madina na kudhibiti bei na kuwapiga wafanya biashara walaghai Sshaffaa Radhiya Llaahu
‘Anhaa ambaye alikuwa anaweza kusoma vizuri na kuandika na pia alikuwa anajua
vizuri hesabu na alikuwa mkali sana dhidi ya wafanya biashara wenye kuhadaa na
kudanganya Waislamu. Alifanikiwa sana kuzuia na kudhibiti kupanda kiholela kwa
bei na pia pia katika kufanikisha kupatikana bidhaa ghafi kwa waislamu.
4.
Uislamu umesisitiza na kuhimiza kuwalea wajane na masikini ili
kuwahifadhi na udhalili na madhila mbalimbali jambo ambalo linaweza kusababisha
wao kuingia katika njia mbaya wasipopata msaada katika jamii. Amepokea Imamu
Bukhaari na Abuu Dawuud kauli ya Mtume aliopsema: “Mwenye kuwaendea na kuwahudumia au kuwatunza wajane na masikini ni
kama mwenye kupigania jihadi katika dini ya Allah, au ni kama yule anayefunga
mchana na kusimama usiku akifanya ibada”. Ni ujira gani basi ulio mkubwa
kuliko Jihadi na mtu kufanya Ibada siku zote za uhai wake? Amepokea pia Imamu
Bukhar Rahimahu Llaahu katika mlango wa “Vita
vya Hudaybia” kuwa Umar Radhiya Llaahu ‘Anhu alitoka na mtumishi wake
kwenda sokoni njiani akakutana na mwanamke mmoja ambaye alikuwa bado kijana,
akamwambia Umar Radhiya Llaahu ‘Anhu ewe kiongozi wa Waislamu, mme wangu
kafariki, na kaacha watoto wadogo, Wallah sipati hata kwato za mbuzi au mifupa
ili niwapikie, wala hawana nafaka wala wala maziwa nami naogopa wasije wakaliwa
na fisi na mimi ni mtoto wa Khufaaf Ibn Iymaal Ghifaariy Radhiya Llaahu ‘Anhu
ambaye alishiriki vita vya Hudaybiya na Mtume Swalla Llaahu ‘Alayhi Wasallama.
Umar Radhiya Llaahu ‘Anhu kusikia hivyo akasimama na mwanamke yule pasina
kuondoka na akamwambia karibu nasaba ya karibu, kisha akaondoka kwenda kwenye
ngamia aliyekuwa na nguvu, akambebesha gunia mbili zilizokuwa zimejaa chakula
yaani unga na tende, na vyakula vingine, na akampelekea matumizi na nguo, kisha
akamwambia watumie bidhaa zile bila wasiwasi na kuwa Allah atawaletea kheri,
kwa maana ya kwamba yeye atawapa chakula na mahitaji mengine kabla chakula kile
hakijaisha. Pia kuna kisa kingine mashughuri kuwa ‘Umar Radhiya Llaahu ‘Anhu
alimkuta mwanamke mwanamke mmoja aiyekuwa akiweka maji pasina cha kupika ili
awatulize watoto wake waliokuwa na njaa. ‘Umar Radhiya Llaahu ‘Anhu aliamua
abebe chakula cha mwanamke yule mgongoni au kichwani mwake. Haya yote
yanaonyesha umuhimu na wajibu wa dola kusimamia wajane na Mayatima na Masikini
kwa kuwapa mahitaji muhimu ya maisha yao kutoka katika hazina ya Serikali au
mfuko maalumu wa Serikali unaohusika na shughuli hii. Basi la kama dola au
serikali ingesimamia jukumu hili pasingekuwa na haja ya wanawake hawa wajane na
watalikiwa kutoka na kwenda kufanya kazi nje ya nyumba zao. Na kama wana ndugu
wa kiume kama baba au kaka au mtoto anayefanya kazi basi anawatosha juu ya
suala hili la kutoka kwao kwenda kufanya kazi.
TOFAUTI
ZA KIMAUMBILE KATI YA MWANAMKE NA MWANAMUME.
Sio nususu tu peke yake ndizo zinazoonyesha kuwa kuna tofauti
kati ya Wanawake na Wanaume bali hata maumbile yaliyo salama, na fikra ya
kiakili, na kielimu iliyo salama na utafiti pia. Hebu jaribu kumuuliza kila mwanamke
mwenye akili timamu hivi; kipi kilicho bora zaidi kwake; kuwa awe na mtu mwenye
kumtunza na kumtimizia haja zake zote na haja za watoto wake, hivyo apate
kupumzika kutokana na tabu na shida za kutoka na kwenda kufanya kazi naye
ashughulike na kuwalinda, kuwakuza na kuwalea watoto wake ambacho ndiyo kitu
cha thamani kabisa anachomiliki au abaki peke yake akitoka na kwenda kupambana
kiwendawaziwendazimu katika kutafuta chakula, kinywaji, kivazi na dawa nk, katika
mahitaji ya maisha. Jambo ambalo pia litamuweka mbali na watoto wake kwa
kitambo kirefu cha mda wake wa siku nzima; jambo ambalo litawaweka watoto na
kuwaacha waking’aa ng’aa macho hadi mama yao huyo atakaporudi jioni au usiku,
akiwa amechoka sana kiasi kuwa hawezi kufanya kazi yoyote ya ndani na hata
kuwahudumia na kuwakumbusha watoto wake majukumu yao. Je hilo ni jambo jema
kwake au kukaa na watoto wake na kutatua matatizo mbalimbali yanayowakabili.
Hivi ni kweli mwanamke anathubutu kuwaacha watoto wake wachafuliwe na
mfanyakazi na vyombo vya habari kama Tv ambavyo vinaonyesha mara nyingine
habari ambazo zinaathiri tabia ya watoto. Atajibuje mwanamke huyo? Sidhani kama
jawabu la mwanamke mwenye akili litakuwa lingine zaidi ya kukataa yote hayo.
Bali atakataa hata kutoka tu nje ya nyumba yake na kuwaacha watoto pasina
sababu yoyote. Nadhani kuwa hisia zake kama mama haziwezi kutawaliwa na madai
ya Umagharibi ya kutaka kujitosheleza mwenyewe na kujihakikishia uhuru wa kila
kitu. Kwa kuwa hikma ni kuweka kila kinachostahiki katika pahala pake
kinapostahiki, kwa hiyo hikma hii katika sehemu ya kazi inatuambia waziwazi
kuwa kazi ya kuchunga, kulea na kuwafundisha watoto ni ya mama. Yeye anaweza
zaidi kulea watoto kuliko mwanamume. Na hilo ni kutokana na uwezo wake na sifa
za kimaumbile alizoumbiwa na Allah. Mwanamume kimsingi hana sifa hizo na hawezi
kufanya shughuli hizo kwa ukamilifu wake kwa kukosa sifa hizo kwani mwanamume
kwa kawaida yake ni mgumu na wala si mlaini kama mwanamke na hivyo kazi zake ni
za sulubu zenye tabu, zinazohitaji nguvu zaidi kiakili na kimwili. Ama mwanamke
yeye maumbile yake ni malaini, yenye sifa ya upole, ambayo ni muafaka kwa
watoto wadogo ili wapate kuwa karibu na joto lake na kulala kifuani kwake
wakicheza naye kwa utulivu bila wasiwasi wowote. Haya yote hayawezi kupatikana
kwa thamani yoyote iwe ni mali au kazi. Wala mtumishi au mfanya kazi hawaezi
kuchukua nafasi ya mama katika kulea watoto abdani. Anayestaajabishwa na haya
na atuambie basi ni kwa nini Allah amejaalia mimba, kuzaa na kunyonyesha ni
katika shughuli na sifa za mwanamke na si kwa mwanamume. Je hayo ni kwa bahati
mbaya? Hivi hii haitoshi kuwa ni dalili ya wazi kuwa Allah kamuumba mwanamke kwa
ajili ya wadhifa maalumu wenye kutofautiana na wadhifa wa mwanamume? Nataraji jawabu halitakuwa ni marekebisho ya kimwili na
upasuaji wa kumlazimisha mwanamume ili aweze kubeba mimba, kuzaa na kunyonyesha
ili kuhakiki usawa wa kindoto wa kimagharibi unaodaiwa kati ya mwanamke na mwanamume.
Ni kwa nini zaidi ya 70% ya wanawake wanaofanya kazi Marekani
wanalazimika kuacha kazi na kutafuta shughuli nyingine? Takwimu zinaonyesha
kuwa sababu kubwa kabisa ya wao kufanya hivyo ni kutokana na kubakwa na kudhalilishwa
kijinsia na wanaume makazini. Na hili linatokea hata kwa askari wa kike nao
hawajasalimika vile vile. Kwa hiyo linatosha kuonyesha wazi utukufu wa nidhamu
ya Kiislamu katika kulinda haki za mwanamke ndani ya nyumba na kuwa wanawake wasifanye
kazi nje ya nyumba isipokuwa kwa dharura kubwa. Watu wengi hawajui kuwa wasomi
wengi wa Kimagharibi sasa hivi wanaona kuwa iliyo bora kwa mwanamke ni kukaa
nyumbani akihudumia nyumba na watoto wake. Miongoni mwa wasomi hao ni
mwanafalsa mkubwa wa kifaransa August Comte aliyezaliwa January 17 mwaka
1798 na ambaye anadaiwa kuwa mwasisi wa Elimu ya Sosholojia na Saikolojia: “Inapasa maisha ya mwanamke yawe ndani ya
nyumba yake, wala asikalifishwe kufanya kazi za wanaume, kwani hilo linazuia kati yake
na kazi zake za kimaumbile, na linaharibu vipaji vyake vya kiasli. Inawapasa
wazazi watoe mali katika kuwahudumia wanawake pasina kungojea wao wafanye kazi
kama wanavyotoa kuwapa waandishi wa vitabu, washairi na wanafalsafa. Ikiwa watu
hawa wanahitaji muda mwingi ili kazi zao ziweze kuleta matunda ni hivyo hivyo
pia nao wanawake wanahitaji muda mwingi ili waweze kutekeleza majukumu yao ya
kijamii kama kubeba mimba, kuzaa, kunyonyesha na kulea watoto. Kwa upande
mwingine lau kama tungewaruhusu wanawake kwa unyonge wao wafanye kazi nje ya
nyumba utaona kuwa bila shaka watakutana na ushindani mkubwa sana na wanaume. Wataishia
kupata kazi za kinyonge kabisa ambazo wanaume wanazikimbia na hata malipo yao
yatakuwa chini sana. Hivyo watajikuta wakiingia katika umasikini. Na kazi
zenyewe hawatapata isipokuwa mabinti wadogo achilia mbali madhara
yatakayoikumba jamii yao kutokana na kutoka kwao kwenda kufanya kazi na
kughalifu kanuni sahihi za maisha”. Tunaona kuwa mwanafalsafa huyu mkubwa
akili na fikra yake ya kimantki imempelekea atafiti na kuona kuwa mfumo wa
kifamilia alioweka Allah ni sahihi sana na kuwa kazi ya mwanamke ni ile
aliyowekewa na Uislamu nayo ni kazi ya kulea watoto. Kayasema haya japo hakuwa
Mwislamu. Na huenda aliyasema haya kwa kuwa hakuwa anafahamu Uislamu unasemaje
kuhusiana na kazi za mwanamke. Na hii inatia nguvu zaidi hoja yangu dhidi ya
wasiokuwa Waislamu wanaohimiza mwanamke kutoka na kwenda kufanya kazi kwa kuwa
maneno hayo yamesemwa na mwanafikra mwenzao. Fikra yake imempeleka pasina yeye
kujua katika kukubaliana na Uislamu unavyosema kuhusiana na wanawake kukaa
majumbani mwao na wasitoke kwenda kufanya kazi ila ni kwa dharura kubwa sana na
kuwa wanaume wana jukumu la kuwatunza na kuwalinda wanawake na kuwahami na kazi
za tabu na fitna ya wao kufanya kazi nje ya nyumba zao. Lau msomi huyu angekuwa
Mwislamu basi Ulaya nzima ingezizima kwa makelele lakini kwa kuwa ni mtu wao
hakuna mbwa aliyeweza kunyanyua mkia achilia mbali mdomo wake ili kumbwekea!!!
Antony Lamalaf
mtafiti wa Kirusi katika utafiti wake wa tofauti za
kimaumbile kati ya mwanamume na mwanamke anakubaliana na dhana kuwa usawa kati
ya mwanamke na mwanamume ni jambo muhali. Anasema Antoni Lamalaf: “Inatupasa tusizidanganye nafsi zetu kuwa
tunaweza kusimamisha usawa kati ya mwanamke na mwanamue katika maisha ya
kivitendo. Sisi tulijitahidi sana kusawazisha kati ya mwanamke na mwanamme katika
Umoja wa Kisovieti kiasi hakuna watu duniani waliowahi kujitahidi juu ya jambo
hili mfano wetu, na tuliweka sheria ili kuhakikisha hili linafanikiwa lakini
kwa hakika hali ya mwanamke katika familia na katika jamii haikubalika sana”.
Na anasema Alex Crane kuwa: “kuna tofauti kati ya mwanamke na mwanamume katika fikra na maandalizi
ya kiakili katika kupokea elimu”
Anna Dyma ambaye alikuwa mwakilishi wa mambo ya kijamii Ulaya
anasema: “Kushiriki kwa mwanamke katika
shughuli za kijamii kunazidi lakini kwa pole pole sana, ulimwengu wa biashara
na kazi unadhihirisha tofauti kati ya jinsia hizi mbili kwa sura ya wazi sana,
kwani idadi ya wafanya kazi wa kiume katika mashirika inazidi sana idadi ya
wafanyakazi wa kike sehemu zote za ulaya”. Anaongeza kwa kusema: “Kuweka sawa kati ya kazi na maisha ya
familia inazingatiwa kuwa ni tatizo kubwa kwa wanawake wanaofanya kazi katika
mashirika na vile vile tatizo la kushuka kwa ujira wa mwanamke kwa takribani
16% kulinganisha na ujira wa mwanamme.”
La kushangaza sana ni kuwa wao walifanya sherehe kubwa
Swizilandi kuhusiana na siku ya mwanamke duniani. Miongoni mwa wageni mashuhuri
waalikwa katika sherehe hizi alikuwako
Baraanida Baarinisa ambaye
alitangaza kujiuzulu kazi yake nono katika shirika moja la kimataifa la
vinywaji. Ni kazi nono kwa sababu dada huyu alikuwa akipata kwa mwaka kiwango
cha dola milioni mbili za kimarekani. Katika kuelezea sababu ya
kujiuzulu kwake japo alikuwa anapata kiwango kikubwa kama hicho ambacho ni
takribani bilioni mbili na milioni mia sita na arobaini ukilinganisha na
shilingi za Tanzania alisema kuwa: “Nimegundua
kuwa starehe ya mume na watoto wangu ni bora zaidi kwangu kuliko kazi yangu na
kuliko mamilioni ya dola na kuwa katika nyumba yangu ndiyo sehemu pekee ninapopata
kupumzika na inarandana sawia na maumbile yangu”
Hali hii iliendelea Uingereza, ambapo tunakuta vile vile kuwa
mtoto wa Habii Niisi ambaye alikuwa mkuu wa tawi la shirika la maji ya
gesi duniani alijiuzulu ili azae na na apate nafasi nzuri ya kumlea mtoto wake.
La kushangaza zaidi ya hayo ni kuwa mhariri mkuu wa gazeti la Haa
ambaye alikuwa maarufu sana kuwatetea wanawake kutoka na kwenda kufanya kazi
alipeleka barua yake ya kujiuzulu ili akae nyumbani alee watoto wake.
Na akasema mkuu wa gazeti la Tahrirul Mustaqiili Lyda Kisler:
“Mimi
sijaacha kazi yangu kwa sababu ya watoto wangu kunihitajia mimi zaidi bali mimi
kuwahijajia wao zaidi. Nataka kuishi na watoto wangu katika nyumba yetu kwa
utulivu”.
Hivi ndivyo Allah alivyowafanya wanawake wa Magharibi waisemee
haki kwa vinywa vyao na wakawa wanautetea mfumo wa familia uliowekwa na Uislamu
bila wao kukusudia au kujua kuwa Uislamu unasemaje juu ya hilo au kuwa na elimu
ya Uislamu juu ya hilo.
Amesema Samwel Smith ambaye ni mwanafikra mashuhuri wa
Uingereza: “Mfumo wa kuwatumikisha
wanawake katika viwanda na maabara vyovyote utakavyoongeza katika uzalishaji,
kwa hakika madhara yake ni mengi sana na ni ya hatari zaidi kwa kuwa unavunja
nguzo ya mhimili wa nyumba na familia”
Gazeti la Thought la Uingereza linasema: “Balaa kubwa sana liko katika kutoka
mwanamke katika nyumba yake na kwenda kutafuta kazi za wanaume, jambo ambalo
linazidisha kuwepo wanawake mbali na familia zao na kukithiri kwa watoto wa nje
ya ndoa, kama aibu kubwa na mzigo kwa jamii, na hivyo hivyo kusongamana
wanawake na wanaume kutaleta maafa makubwa”
Mwisho anasema mwandishi mashuhuri Haa Mass Annaa Rudi
katika makala iliyoko ndani ya gazeti la Sittuuna Miil: “Kufanya kazi binti zetu nyumbani ni kheri
zaidi na hakuna balaa kama kufanya kwao kazi katika viwanda na maabara.
Natamani miji yetu iwe kama miji ya Kiislamu ambapo wanawake wananeemeka kwa
usafi, ucha Mungu na maisha ya utulivu wala hawafikwi na madhila kama sisi”
MANENO
HAYA NA HISIA HIZI ZA WANAWAKE WA ULAYA HAYATAJI UFAFANUZI MAANA YAKO WAZI
SANA. NI JUU YAKO KUCHAGUA PAURO AU PAPURO!
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !