UPANDE wa Jamhuri katika kesi ya uchochezi na wizi wa malighafi ya sh milioni
59 inayomkabili Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Ponda Issa
Ponda na wenzake 49 umeiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam
iwaone wana hatia kwa mujibu wa kesi inayowakabili na iwahukumu kwa mujibu wa
sheria.
Katika kesi hiyo, Jamhuri inawakilishwa na wakili mwandamizi wa serikali,
Tumaini Kweka na Jessy Peter ambao waliwasilisha ombi hilo kwa njia ya maandishi
mahakamani hapo jana kama walivyoamriwa na hakimu mkazi Victoria Nongwa Machi 21
mwaka huu.
Hakimu Nongwa alizitaka pande zote katika kesi hiyo ziwasilishe majumuisho
yao ya mwisho yanayoomba mahakama iwaone washitakiwa wana hatia au la.
Wakili Kweka aliikumbusha mahakama kuwa washtakiwa wanakabiliwa na kosa la
kula njama kutenda kosa, kuingia kwa jinai, kujimilikisha ardhi ya kiwanja cha
Chang’ombe Markas kinyume na sheria, wizi wa malighafi zenye thamani ya sh
milioni 59 na kosa la uchochezi linalomkabili Ponda na mshitakiwa wa tano
Mkadamu Swallehe.
Alidai katika kuthibitisha kesi yao waliweza kuleta jumla ya mashahidi 16
ambapo shahidi wa kwanza, tatu na nne waliieleza mahakama kuwa wao wanafanya
kazi katika Baraza Kuu la Waislamu (Bakwata).
Kwamba waliieleza mahakama kuwa eneo la Markas lilikuwa ni mali ya Bakwata,
lakini ikaamua kulibadilisha na Kampuni ya Agritanza Ltd ambaye ndiye mmiliki
halali wa eneo hilo na si mali ya Waislamu.
“Jamhuri imeweza kuleta ushahidi madhubuti ambao unatosha kuishawishi
mahakama hii iwaone washitakiwa wote wana hatia katika makosa yanayowakabili,”
alidai Kweka.
Aliongeza kuwa hakuna ubishi kwamba washtakiwa wote walikamatwa eneo la tukio
(Markas), na Ponda wakati akitoa utetezi wake alidai kuwa kuna mgogoro wa
umiliki wa eneo hilo na yeye kama kiongozi wa taasisi hiyo, alitoa agizo kwa
viongozi wa misikiti kuwatangazia Waislamu wote kuwa kutakuwa na ujenzi wa
msikiti wa muda katika eneo hilo lililoibwa ili waweze kulirejesha mikononi
mwao.
“Kwa utetezi huo wa Ponda, sisi upande wa Jamhuri tunaona kisheria kuwa
makosa yote yanayowakabili washitakiwa waliyatenda kwa makusudi na walikuwa
wakijua wanavunja sheria za nchi, hivyo tunaiomba mahakama hii iwaone
washitakiwa wote wana hatia,” aliadai Kweka.
Hakimu Nongwa alisema atatoa hukumu Aprili 14 mwaka huu.
Oktoba 18 mwaka huu, kesi hiyo ilifunguliwa mahakamani hapo kwa mara ya
kwanza na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Dk. Eliezer Feleshi aliwasilisha hati
ya kuwafungia dhamana Ponda na Mkadamu. {Chanzo: Tanzania Daima-Alkhamis 04-04-2013}
|
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !