Kardinali Pengo akoleza msako.
20 Feb 2013
Sheikh alonga nchi za nje zimetia
mkono
Kanisa jingine lachomwa Zanzibar
KAULI ya Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu
Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, kwamba serikali
imezembea kutekeleza wajibu wake, uzembe ambao moja ya matokeo yake ni kuuawa
kwa risasi kwa Padri wa kanisa hilo, Evaristus Mushi, imezua mgongano wa
kimjadala miongoni mwa maofisa waandamizi serikalini, Raia Mwema, limeelezwa.
Kwa mujibu wa vyanzo kadhaa vya
habari, baadhi ya maofisa waandamizi wamelazimika kujadili kauli hiyo, sambamba
na kupima athari au faida zake katika operesheni inayoendelea ya kuwasaka
wahusika wa tukio hilo.
Hatua ya maofisa hao imetokea saa
kadhaa baada ya Pengo kuzungumza na vyombo vya habari na Raia Mwema ikielezwa
ya kwamba, mabishano yamejitokeza miongoni mwa maofisa hao.
“Imebainika kuna baadhi ya
taarifa ambazo hazikuwa zinafikishwa katika eneo husika, wakubwa (maofisa
waandamizi wa masuala ya usalama) wamelumbana. Wengine inadaiwa walikuwa
wakifikishiwa taarifa za dalili mbaya lakini hawakuwa wepesi kuchukua hatua, ni
kama vile wamelewa kuendelea kufanya kazi katika nchi iliyojaa amani kila
siku,” kilieleza chanzo chetu cha habari.
Katika mazungumzo yake na
waandishi wa habari kuhusu tukio la kuuawa kwa Padri Evaristus Mushi wa Parokia
ya Mtakatifu Joseph ya Mjini Magharibi, Unguja, Zanzibar, Pengo alitoa maelezo
yanayotilia shaka kwamba mauaji hayo yana mkono wa baadhi ya watu wanaojitambulisha
kwa jina la Kundi la Kidini la Uamsho.
Kwenye mazungumzo hayo
yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, Pengo alisema; “Tunahitaji rehema (za
Mwenyezi Mungu) ili tuendelee kuwapo. Tunahitaji utulivu na kuelezana ukweli.
Na endapo mmoja wetu atazembea, ni jukumu kuambiana kwamba hapo umezembea na
utalifikisha Taifa pabaya.”
Kwa mujibu wa maelezo hayo ya
Pengo, wauaji hao walipanga na kutekeleza unyama wao huo kutokana na uzembe na
udhaifu wa vyombo vya dola kwa kushindwa kusoma alama za nyakati, kwa kuwa tayari
wauaji hao walikwishasambaza vipeperushi vilivyoashiria dhamira hiyo mapema.
“Watu wanasema kikundi cha Uamsho
kule Zanzibar ni kikundi cha kidini, lakini kinatoa vipeperushi kama hiki
(alikionyesha kwa waandishi) ambacho kimenifikia mkononi. Kwa hiyo, ni wazi
kuwa hadi kinifikie mimi, Watanzania wengi watakuwa wamefikiwa na kipeperushi
hicho…inathibitisha kwamba vipeperushi hivi ni vya Uamsho, lakini si kazi yangu
kuhakikisha (kuthibitisha) tamko la Uamsho ni la Uislamu, siamini kwamba vyombo
vya usalama vya taifa letu vinaweza kusema havina habari,” alieleza Pengo.
Maziko ya Padri Mushi
Padiri Mushi aliyeuawa kwa
kupigwa risasi Jumapili iliyopita asubuhi wakati akishuka kutoka kwenye gari
lake ili kwenda kuongoza ibada katika Kanisa la Betras, lililopo Minara Miwili,
Mji Mkongwe, Unguja, anazikwa Jumatano wiki hii Visiwani humo.
Mazishi hayo yanafanyika jioni ya
Jumatano hii katika Kijiji cha Kitope, Kaskazini B, Unguja yakiongozwa na
Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Eusebius Nzingilwa.
Lakini kabla ya muda wa ibada
hiyo ya mazishi, Kardinali Pengo ataongoza misa ya kumwombea marehemu pamoja na
kuliombea Taifa itakayofanyika katika Kanisa Kuu Katoliki la Mtakatifu Joseph,
jijini Dar es Salaam.
Masikitiko ya Rais Kikwete
Tayari Rais Jakaya Kikwete
kupitia kwa Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu jijini Dar es Salaam, ameeleza
kusikitishwa na tukio hilo na kuahidi serikali yake kuwasaka wote wanaohusika
na kuwachukulia hatua za kisheria.
Hata hivyo, kauli hiyo ya Kikwete
kupitia kwa Kurugenzi hiyo inatajwa na duru za baadhi ya viongozi wa dini
nchini kuwa ni ya kawaida na imeanza kuzoeleka. Viongozi hao wanarejea ahadi
yake aliyoitoa wakati Padri Ambrose Mkenda aliponusurika kuuawa huko Zanzibar,
wakati wa Sikukuu ya Krismasi mwaka jana, na kuishia kujeruhiwa.
Lakini si padri huyo pekee
aliyenusurika kuuawa bali vitendo vya kudhuru baadhi ya viongozi wa dini nchini
pia vimemfika Sheikh Fadhil Suleiman Soraga, ambaye ni Katibu wa Mufti
Zanzibar, ambaye alimwagiwa tindikali.
Hata hivyo, katika hatua nyingine
tayari Serikali ya Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, nayo kama ilivyo
kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, imeahidi kuwasaka wahusika na kuwachukulia
hatua.
Makanisa zaidi yacharuka
Hali imezidi kuwa tete ikiibua
kauli na matamko mbalimbali ya viongozi wa dini nchini.
Jukwaa la Wakristo mkoani Mbeya
ambalo linaundwa na mabaraza makuu matatu ya madhehebu ya kikristo; Tanzania
Episcopal Council (TEC), Christian Council of Tanzania (CCT) na Pentecostal
Council of Tanzania (PCT), limeitahadharisha serikali juu ya kile walichokiita
undumilakuwili na tabia yake kulichukulia suala la mauaji ya viongozi wa dini
ya Kikristo kama jambo la mazoea.
Jukwaa hilo, limesema katika
tamko lake la wiki hii kwamba ili Serikali ya Rais Kikwete iweze kuaminika
mbele ya macho ya waamini wa dini hiyo, lazima ionyeshe usawa katika sakata la
mauaji ya Mchungaji Mathayo Kachila wa Buseresere, mkoani Geita na Padri Mushi
wa Zanzibar.
“Miongoni mwa harakati hatarishi zinazosambazwa
kwa njia ya CD na DVD ni za Sheikh (Hussein) Ilunga kuhusu kuuawa wachungaji,
mapadri na maaskofu. CD na DVD zimeanza kuwa na matokeo mabaya kwani Padri
(Ambrose) kule Zanzibar alipigwa risasi na watu walioitwa na Serikali wahuni,
na sasa vifo vimetokea.
“Mchungaji Mathayo Kachila kule
Buseresere mkoani Geita ameuawa na kikundi kinachodhaniwa ni wanaharakati wa
kidini wenye jazba na ghadhabu kali inayotokana na mvutano uliopo kuhusu nani
mwenye haki ya kuchinja wanyama, na juzi Padri Mushi wa Kanisa Katoliki kule
Zanzibar,” alisema Askofu Damianus Kongoro wakati akisoma tamko la Jukwaa hilo
mbele ya wandishi wa habari jijini Mbeya.
Mauaji kwingineko duniani
Mauaji ya mapdri yamewahi kutokea
katika maeneo tofauti duniani na kati ya nchi ambako mauaji hayo yamepata
kutokea ni Colombia.
Katika Jiji la Bogotá, Colombia,
Kardinali Ruben Salazar aliwahi kuja juu dhidi ya mauaji ya Padri Luis Alfredo
Suarez Salazar (50), akisema aliyeuawa hakuwa na hatia yoyote na wajibu wake
ulikuwa ni mwema kwa jamii iliyokuwa ikimzunguka..
Padri huyo aliauwa kwa kupigwa
risasi na watu wawili ambao baada ya tukio hilo walitoroka kwa kutumia
pikipiki. Aliuawa wakati akimsaidia dada yake kupakia mizigo katika gari.
Dereva wa padri huyo, Hernan Torres Ramos, naye alijeruhiwa vibaya.
Kutokana na tukio hilo, familia
ya Padri Suarez ilieleza ya kwamba padri huyo hakuwa na kisasi na mtu yeyote na
walishangazwa na mauji hayo, hali ambayo pia inafanana na maelezo ya
wanafamilia wa Padri Mushi ambao kupitia kwa Aloyce Mushi aliyezungumza na
mwandishi wetu anaeleza padri huyo naye hakuwa na kisasi na mtu au kundi
lolote.
Mwanza balaa tupu
Kutoka mkoani Mwanza na Geita,
Mwandishi Wetu anaripoti ya kwanza sakata la nani mwenye haki ya kuchinja
wanyama katika Kijiji cha Buseresere-Geita, ambako Waziri Mkuu Mizengo Pinda
alikwenda kutafuta suluhu, bado halijapata suluhisho.
Moja ya mambo yaliyoshuhudiwa na
Waziri Mkuu Pinda katika ziara yake hiyo ni kuibuka kwa madai mapya ya
kusambazwa biblia feki ambazo inadaiwa zinatumiwa na baadhi ya kundi lililoko
kwenye mvutano huo kuthibitisha madai ya nani hasa mwenye mamlaka ya kuchinja
kwa mujibu wa vitabu vyote vitakatifu vya Quraan na Biblia.
Katika kikao cha usuluhishi na
Waziri Mkuu jijini Mwanza, inadaiwa ya kwamba Sheikh Issa Kalenga akiwa mmoja
wa wajumbe wa mkutano huo alikuwa na biblia ambayo kwenye tafsiri ya maneno
magumu imelieleza eneo kibudu kuwa ni mnyama aliyejifia mwenyewe au ambaye
hakuchinjwa kwa mujibu wa taratibu za dini ya Kiislamu.
Taarifa zinaeleza kuwa biblia
hiyo iliibua mjadala mzito kwa wachungaji kutoitambua na kumpelekea biblia
nyingine tatu (Pinda) ili kuwaonyesha tafsiri hiyo lakini zikawa
zimetofautiana.
Baada ya mkutano huo Shekh
Kalenga waliowanyesha waandishi wa habari kipengele cha ufafanuzi huo na kusisitiza
kuwa mkristu haruhusiwi kula kibudu na hivyo ni halali kula vilivyochinjwa na
Waislamu.
Hata hivyo hoja hiyo ilipingwa na
Askofu Augustine Mpemba wa Kanisa la TFE kwa Neema, ambaye alisema kuwa kuna
watu wenye pesa ambao wamekuwa wakichapisha biblia zisizoendana na mafundisho
ya Kikristo ili kuchakachua imani yao.
Alieleza kuwa katika ulimwengu wa
leo kuna biblia nyingi sana wasizokubaliana nazo Wakristo, akitoka mfano wa
Biblia ya John Hagee ambaye ni mwanzilishi wa Cornerstone Church, ambayo
haikubaliki na Wakristu wengine kwa kuwa watu wanachapisha biblia hizo kwa
maslahi, na kuwatahadharisha waumini wao kutonunua bila mitaani kwa kuwa ziko
nyingi zilizochakachuliwa.
Lakini akizungumzia hali ya
vurugu za kidini, mmoja wa wanazuoni wa Kiislamu alisema kwa jinsi matukio
yalivyotokea (vurugu za uchinjaji na mauaji ya padri Zanzibar) inaashiria kuwa
kuna watu mahali fulani ambao dhamira yao ni kuona Tanzania inaingia kwenye
machafuko ili wao watimize malengo yao.
" Hii haiwezi kuwa imetokea
kwa nasibu tu, kwamba Waziri Mkuu ana ratiba ya kukutana na viongozi wa dini
zote halafu mtu anakwenda kumpiga risasi padri hadharani akijua wako waumini
wanamsubiri kuwasuluhisha, huyu alidhamiria kutengeneza mshindo ambao utafanya
mazungumzo yawe magumu," alieleza.
Alipoulizwa anadhani kuwa watu
hao wanaweza kuwa nani na wanafanya hayo kwa manufaa gani alijibu; "Kwanza
karibu asilimia kubwa ya biashara sasa zimeshikwa na bidhaa kutoka China, na
hii ni kwa dunia nzima, mataifa makubwa ya Magharibi yamebakiza biashara ya
maana ni silaha tu, wanaweza kuwa wanatafuta hilo soko Tanzania ambako kila
kona imejaa dhahabu, gesi au mafuta na hivi vyote ni vivutio vya mataifa
makubwa na China ndiyo wanaongeza ushawishi wao kwetu, mataifa makubwa
yangependa kuona tunafarakana ili wapate fursa ya kunufaika kirahisi."
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !