|
IMEANDIKWA NA: Mohamed Said
BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM
Imebidi kuandika makala hii kutokana na makala iliyoandikwa na Kaanaeli
Kaale yenye kichwa cha habari 'Kusigana kwa matokeo baina ya shule za
Kikatoliki na Kiislamu' (Mwananchi 17 Oktoba 2006). Makala ilikuwa inaeleza
yaliyojadiliwa katika mkutano ulioandaliwa na Shirika la Elimu ya Sheria
Tanzania (TANLET) katika moja ya harakati za kumuenzi hayati Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere.
Katika mkutano huo, ilielezwa kuwa shule za Kikatoliki ndiyo shule bora
zinazoshika nafasi 'kumi bora' kwa kutoa matokeo mazuri ya mitihani na shule
za Kiislam ndiyo 'zinazoshika mkia' katika kutoa matokeo mabaya. Ama taarifa
hizo za shule za Wakatoliki kufanya vyema katika mitihani si habari mpya ni
jambo linalotangazwa na vyombo vya habari kila mwaka kwa hiyo linafahamika.
Ila kitu cha kushangaza ni kuwa kimezidi nini hii leo hadi ikawa ni muhimu
kujadili ufanisi wa shule za Waislam hadharani kisha tukapewa ushauri kuwa
Waislamu tujifunze kutoka kwa Wakatoliki ili nasi shule zetu zifanye vyema
kama zao ili huu upogo wa elimu kati ya Waislam na Wakristo utoweke?
Ushauri huu umenitia simanzi kubwa na ndiyo hasa sababu ya kuandika makala
hii. Bubu alizungumza kwa uchungu wa mwanaWe ni msemo mashuri. Leo hii sisi
Waislam tumekuwa watu wa kusaidiwa na Wakatoliki tuelimike! Waswahili tuna
msemo 'Akutukanae hakuchagulii tusi.'
Laiti hao wanaotushauri wengeijua tarikh (historia) yetu wasingetamka hayo.
Wamishionari wameingia nchi hii wamewakuta babu zetu pwani yote ya Afrika
Mashariki na bara kulikokuwa na Uislam wakijua kusoma, kuandika na kuhesabu.
Lakini haya tuyaache yanahitaji muda kueleza.Turudi kwenye mada husika.
Awali ya yote ni kumkejeli hayati Mwalimu Julius Nyerere kwa kuadhimisha kifo
chake kwa mkutano wa kuzungumza kubaki nyuma kwa Waislam katika elimu kwa
kuwa, kwa kauli yake mwenyewe alisema kuwa upogo katika elimu baina ya
Waislam na Wakristo uliorithiwa na serikali yake kutoka kwa Waingereza yeye
ameuondosha katika kipindi cha utawala wake. Kauli hii aliitoa Novemba 5,
1985 katika hotuba aliyoitoa Ukumbi wa Diamond Jubille akiwaaga Wazee wa Dar
es Salaam. Kabla hajastaafu urais, Mwalimu Nyerere alikuwa na haya ya kueleza
kuhusu suala la elimu ya Waislam:
"Waislam wametupa nafasi kupitia sera yetu ya elimu, kurekebisha upogo.
Sasa nipo katika hali ya kufurahia kwa kuwa wakati mwingine sielewi kama
mbunge mpya, waziri, au katibu mkuu katika wizara zetu za serikali, ni
mwislam au mkristo au hana dini labda pale jina lake la kwanza linapotoa
utambulisho. Na hata hivyo hiyo siyo njia ya kuaminika kutoa utambulisho wa
dini kwa kuwa tuna wakristo wenye majina ya Kiislam, na waislam wenye majina
ya Kikristo. Kuvumiliana huku ndiyo sababu; nilichofanya mimi ni kuzungumzia
maadili haya kwa niaba yenu." Sasa ikiwa Baba wa Taifa keshawanyanyua
Waislam katika elimu na kafurahishwa na kazi yake nzuri, hawa wanaokuja leo
na kusema kuwa Waislam wako nyuma wanataka kumshika uongo Mwalimu Nyerere?
Wanataka hii leo kumsimamisha Baba wa Taifa kizimbani ajibu tuhuma za
kuwakandamiza Waislam katika elimu?
Kwa hakika si adabu wala ustaarabu kupinga kauli ya Mwalimu Nyerere kuwa
hakusema kweli katika tatizo la elimu ya Waislam. Je, hawa waliokuja na hoja
hii nyeti wanatambua uzito wa kauli zao hasa katika kipindi hiki ambapo
Kanisa Katoliki lipo katika mchakato wa kumfanya Mwalimu Nyerere kuwa
mtakatifu? Hivi hawasikii nchi nzima inavyomtukuza Mwalimu Nyerere kwa sifa
za uadilifu? Majibu wanayo wenyewe. Hili la kwanza.
Waswahili tuna msemo mwingine "Asiekujua hakuthamini.' Historia ya
kupigania uhuru wa Tanganyika ni ushahidi wa juhudi za Waislam katika
kujitafutia elimu. Wakati wa kupigania uhuru wa Tanganyika tatizo la elimu ya
Waislam ndiyo chanzo cha kuanzishwa chama cha upinzani Tanganyika All Muslim
National Union (AMNUT) pale akina Ramadhani Mashado Plantan na wenzake
walipotoka TANU mwaka 1958, sababu kuu wakihofu Wakristo waliokuwa na elimu
kuja kushika madaraka peke yao katika Tanganyika huru na kuwaweka Waislam
pembeni.
Suala hili lilileta mjadala mkubwa katika TANU. Ukipenda unaweza ukarejesha
msuguano huu ndani ya TANU nyuma kidogo mwaka huo huo wa 1958 pale Sheikh
Suleiman Takadir (aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa TANU Dar es
Salaam) alipomkabili Nyerere uso kwa uso na kumtuhumu kwa udini. Haya
yalitokea baada ya Uchaguzi wa Kura Tatu pale TANU ilipoteua Wakristo
kusimama kugombea nafasi za Legislative Council na kuwaweka Waislam wana TANU
pembeni. Lakini katika hili palikuwa na sababu maalum za msingi. Hapa si
mahali pake kuzieleza. Kipande hiki cha historia kinaogopwa sana na kwa ajili
hiyo nami sitokiendeleza.
Baada ya uhuru kupatikana mwaka 1961 Waislam kwa pumzi ile ile waliyopigania
uhuru wakaingia katika harakati za kutafuta elimu. Hawakusubiri wajengewe
shule na serikali. Wazee wetu waliitisha mkutano chini ya taasisi zao -
Daawat Islamiyya (Mwito kwa Waislam), Jamiatul Islamiya fi Tanganyika (Umoja
wa Waislam wa Tanganyika na Muslim Education Union kujadili nini kifanyike
ili Waislam wapate elimu waliyodhulumiwa na wakoloni. Mipango ikatayarishwa
ya kujenga shule Tanganyika nzima na mwishowe kujenga Chuo Kikuu cha kwanza
kwa Waislam katika Afrika ya Mashariki. Huu ndiyo ukweli wa historia ya
Waislam. Waislam hatuna sifa ya uvivu wala kusubiri misaada kutoka Ulaya.
Ufupi wa maneno ni kuwa shule sabini zilijengwa na EAMWS na jiwe la msingi la
Chuo Kikuu liliwekwa na Mwalimu Nyerere mwenyewe kwa mkono wake. Sasa la
kujiuliza ni kuwa juhudi hizi zote za kutafuta elimu ziliishia wapi na nini
sababu yake
Ufupi wa mambo ni kuwa Mwalimu Nyerere alipiga marufuku jumuia zote za
Kiislam mwaka 1968 na akwaundia Waislam Baraza Kuu la Waislam Tanzania
(Bakwata). Historia ya TANU na uhusiano wa Mwalimu Nyerere na Waislam ina
majibu ya swali hili. Mzee Rashid Mfaume Kawawa yu hai na ni shahidi wa yote
yaliyopita katika kipindi kile. Mzee Kawawa anaweza kutoa majibu ya
kitendawili hiki.Hili la pili.
Waswahili tuna msemo mwingine 'Chokochoko mchokonoe pweza binadamu
hutamuweza.' Imekuwa vyema leo hii, hili tatizo la elimu ya Waislam limesemwa
na wasiokuwa Waislam maana laiti tungelisema Waislam tungeambiwa 'siasa kali'
tunataka kuvuruga 'amani na utulivu' kama alivyosakamwa marehemu Profesa
Kighoma Abdallah Ali Malima alipoionya serikali kuhusu hujuma dhidi ya
Waislam kama alivyoikuta ndani ya Wizara ya Elimu. Mwaka 1987 Profesa Malima
aliteuliwa kuwa Waziri wa Elimu akiwa Muislam wa kwanza kushika nafasi hiyo.
Mawaziri wanane waliopita walikuwa Wakristo. Kulikuwa na malalamiko kutoka
kwa Waislam kuwa wizara hiyo imegeuzwa jimbo la Wakristo hasa Wakatoliki,
maana ilifika hadi padri (Simon Chiwanga) kuteuliwa na Mwalimu Julius Nyerere
kuongoza wizara hiyo.
Profesa Malima aliposhika wizara hiyo aliona upo umuhimu wa kufanya
marekebisho kadhaa ili kurejesha imani ya Waislam katika wizara hiyo.
Kulikuwa na tuhuma kuwa Wizara ya Elimu ilikuwa ikiwabagua vijana wa Kiislam
kupata nafasi katika vyuo vya elimu ya juu na ilikuwa ikizuia kupanda vyeo
kwa Waislam. Tatizo hili liliwekwa wazi kwa mara ya kwanza mwaka 1981 na
wanafunzi wa Sheikh Malik na ndiyo ikawa sababu ya yeye kufukuzwa
nchini.Profesa Malima alipoona dhulma ile iliyokuwapo katika wizara ile dhidi
ya Waislam, aliwateua Waislam wanne kushika nafasi katika kurugenzi
mbalimbali. Hali kadhalika Profesa Malima alibadili mtindo uliokuwapo wa
kutumia majina badala ya namba katika mitihani. Baada ya mabadiliko yale
mwaka ule idadi ya wanafunzi Waislam walifaulu kuingia sekondari ilipanda kwa
asilimia 40. Profesa Malima akaandika taarifa ya siri kwa Rais Ali Hassan
Mwinyi kumtaarifu udini ulioota mizizi Wizara ya Elimu.
Katika taarifa ile kwa rais Mwinyi, Profesa Malima alieleza kuhusu kudumazwa
kwa Waislam kwa makusudi katika mgawo wa elimu. Taarifa hii ilivujishwa kwa
vyombo vya habari na kwa Wakristo wengine.
Katika watu walioipata taarifa hii ni Mwalimu Nyerere akiwa mstaafu lakini
akiwa Mwenyekiti wa CCM. Hiki kisa ni kirefu inatosha tu kusema kuwa
yaliyomkuta Profesa Malima kwa kutaka kutenda haki hakuna asiyeyajua.
Alisimamishwa kizimbani mbele ya Kamati Kuu ya CCM kwa udini na akatolewa
Wizara ya Elimu.
Lakini kabla hatujatoka katika nukta hii ningependa kueleza kuwa katika moja
ya sababu kuu iliyofanya serikali ikifungie kitabu kilichoandikwa na Profesa
Hamza Mustafa Njozi Mwembechai Killings and the Political Future of Tanzania
ni kule kuanika hadharani mbinu zinazotumika nchini kuwanyima Waislam elimu.
Profesa Njozi's aliandika:
"…Arabia (May, 1985) wrote under the heading "A Closed Door to the
Corridors of Power": 'The majority of pupils in Tanzanian primary
schools are Muslim (80 percent), a percentage which dwindles to 15-20 percent
in secondary schools, sinking to a mere five percent at University level'.
Almost fifteen years later, on 2 February, 1999 the Member of Parliament for
Kigamboni Hon. Kitwana Kondo told the parliament that out of every 100 students
who sat for the standard seven examination in Dar es Salaam in the year 1998,
71 were Muslim and 29 Christian. But out of every 100 students selected to
join government secondary schools only 21 were Muslim while 79 were
Christian. The MP wanted to know whether Muslim children were inherently dull
(An-Nuur, February 5-11, 1999).
Yaliyomfika Mzee Kondo nayo yanafahamika. Yapo mengine mengi yaliyofichuliwa
katika kitabu hicho yanayohusu mbinu zinazotumiwa katika kuhakikisha Waislam
wanabaki nyuma lakini hapa hii leo si mahali pake. Hili la tatu. Sasa leo
Waislam tunaambiwa tukajifunze mbinu za Wakatoliki ili tuboreshe shule
zetu…tukajifunze mbinu gani? Kuhodhi madaraka na nafasi katika Wizara ya
Elimu na kujipendelea kwa kuwanyima Wakristo nafasi za elimu ya juu? Hili ni
muhali kwa Waislam.
Hata kama tungekuwa na uwezo nalo Uislam unakataza vyote kudhulumu na
halikadhalika kukubali kudhulumiwa. Kwa Waislam elimu ni fardh jambo ambalo
ni lazima litekelezwa na kwa kushindwa kufanya hivyo mja huandikiwa dhambi.
Hatuhitaji kujifunza kwa yeyote yule kuhusu umuhimu wa elimu. Historia ya
Waislam wa Tanganyika inapingana na dhana hiyo. Sasa tuzungumze kuhusu
matokeo mabaya ya shule za Waislam. Kwangu mimi kwa uzoefu wangu na yale
ambayo nayaelewa kuhusu historia ya Waislam wa Tanganyika hili linahitaji
uchunguzi zaidi ili tudhihirishe kuwa kweli shule za Waislam zinashika mkia
na za Wakatoliki ndiyo zinazotawala 'kumi bora' miaka nenda miaka rudi kwa
haki au ndiyo hizo hizo mbinu alizotahadharisha marehemu Profesa Malima na
Mzee Kondo akahoji katika Bunge na zilizosababisha kitabu cha Profesa Njozi
kifungiwe na serikali ya Rais Benjamin William Mkapa?
Katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia, Wajerumani walikuwa wakiwakamata Wayahudi
Poland na kwingineko Ulaya wakawatoa katika nyumba zao nzuri na kuwarundika
katika ghetto. Umati mkubwa wa watu waliokuwa na nafasi na heshima zao katika
jamii wakajikuta wanaishi katika sehemu finyu, chafu isiyo na mifereji ya
maji taka wala maji safi. Wajerumani wakawa wanatuhumu na kuwakashifu
Wayahudi kwa uchafu. Katika hali kama hiyo vipi utategemea mtu awe msafi? Huu
ndiyo mfano wetu Waislam hii leo. Hatuna fursa sawa kama walizonazo Wakristo,
shule zetu duni na juu ya hayo bado tunahujumiwa kisha tunalaumiwa kwa
kutotoa matokeo mazuri.
Hili la nne ambalo ningependa lizingatiwe.
Kwa taarifa kwa wale wasiojua ni kuwa Organisation of Islamic Conference
(OIC) walitaka kujenga Chuo Kikuu Dar es Salaam. Watendaji Wakristo katika
Wizara ya Elimu walipiga vita mradi huo na mwisho chuo hicho kikajengwa
Mbale, Uganda. Darul Iman ya Saud Arabia ilitaka kujenga shule ya ufundi
Kibaha na yale yaliyoikuta OIC na wao yaliwafika sawia. Huu ndiyo ukweli wa
nchi yetu. Waswahili tunapokabiliwa na mtu mwingi wa mbinu na ghilba tuna
msemo maarufu tunautumia kumweleza mtu huyo. Tunasema 'Kwa nyakanga hakwishi
nyimbo.'
Kichwa kinaniuma kutaka kujua hii agenda ya kudumazwa kwa Waislam katika
elimu iliyozuka ghafla bin vuu ni ya nani hasa, yao wenyewe TANLET au
wametumwa na mtu? Kama wametumwa, nani huyu kawatuma na kwa maslahi ya nani?
Agenda hii si ndiyo iliyomfanya Profesa Malima aandamwe na hatimaye kufukuzwa
Wizara ya Elimu? Agenda hii si ndiyo iliyomfanya Mwalimu Nyerere amfukuze
Tanzania Bara Mufti Sheikh Hassan bin Ameir na kumrejesha Zanzibar chini ya ulinzi
mkali na kuwaweka kizuizini wafuasi wake?
Agenda hii si ndiyo iliyomfanya Sheikh Hussein Malik afukuzwe nchini na
serikali ya Mwalimu Nyerere baada ya wanafunzi wake kupitia taasisi yao ya
Waandishi wa Kiislam (Warsha) kuzungumza kuhusu tatizo la elimu ya Waislam?
Hii leo kimebadilika nini? Wakati una majibu kwa kila jambo, Waislam
tusubiri.
MWISHO
|
|
|
|
|
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !