Hali ilivyokuwa kwenye shule za Misheni
Ni kwa muda mrefu kumekuwa na maelezo na malumbano mengi kuhusu suala
la elimu na Waislamu wengi nchini mwetu kutopenda kutaka kusoma, pamoja
na kuwepo shule nyingi zilizojengwa na kuendeshwa na makanisa katika kipindi
cha ukoloni na mara baada ya uhuru (1961 - 1971).
Mwandishi PILI SALUM anaelezea hali ilivyokuwa wakati huo kwenye
shule hizo za Misheni katika makala hii. Endelea...
Kutokana na ukanushwaji na upotoshwaji unaoendelea kutolewa na watu
mbali mbali wa ngazi mbali mbali (rejea taarifa yya habari ya DTV ya tarehe
juni 2, 1998 ya saa moja usiku) kuhusu uzembe wa Waislamu wengi kutopenda
kusoma pamoja na mashirika mbali mbali ya kanisa kujenga na kuendesha shule
hizo kwa wananchi wote bila upendeleo au masharti yoyote.
Mimi nimeonelea leo nitumie fursa hii kutoa ushuhuda wangu kwa umma
wa Tanzania nikiwa kama mmoja wa Waislamu niliobahatika kusoma kwenye shule
hizo kuanzia darasa la pili hadi kidato cha nne (2-12) kati ya mwaka 1964-1973.
Nitatumia fursa hii kueleza mazingira ya shule, kanuni na sheria za
shule, taratibu za kila siku na mambo mengineyo yaliyokuwa yakijitokeza,
na nitatoa mifano hai iliyotokea. Nia na lengo ni kutaka kumfanya kila
msomaji aujue ukweli kuhusu shule hizo, kisha aweze yeye mwenyewe kupitisha
hukumu kama kweli Waislamu walikataa kusoma kkwa uzembe au ni mazingira
yaliwalazimisha kutokubali kwenda kusoma kwenye hizo shule.
Mazingira ya shule niliyosoma yalikuwa kwenye eneo la kanisa. Madarasa
yote, mabweni na chumba cha chakula yalikuwa yamepambwa kwa sananu za Yesu
akiwa msalabani. Picha hizi zilikuwa zimetundikwa juu ya ukuta mbele ya
chumba. Mabweni yalikuwa na sanamu za watakatifu mbali mbali. Tulikuwa
na Mt (St) Agnes, Mt Helen, Mt Mary, Mt Lucy, Mt Marietha. Hizi sanamu
zilikuwa na ukubwa kwa kimo cha mtoto wa miaka 3/4 na zilikuwa chini na
mbele ya chumba cha bweni.
Kulikuwa na bustani ndogo ambayo ilikuwa na pango dogo lenye sanamu
nyingi mbali mbali, ikiwemo ya Yesu, mama wa Yesu Maria, Mt Joseph, Malaika
na kondoo na mishumaa. Jirani ya shule kulikuwa na kijito kidogo kilichokuwa
kinatoa maji kwa ajili ya matumizi mbali mbali ya kila siku ya wanafunzi,
waalim, masista na mapadri.
Kanuni na sheria za shule zilikuwa ni sawa kwa wanafunzi wote, bila
kujali imani ya mwanafunzi. Kila siku asubuhi kabla ya masomo wanafunzi
hujipanga mstari saa 1.00 asubuhi na hapo kiranja wa zamu hhutakiwa kuanzisha
wimbo wa kwaya kufuatana na majilio (matukio ya kalenda ya kanisa) mathalani
wakati wa kipindi cha Pentekoste au kwaresma, muimbishaji hutakiwa kuimba
mwimbo unaohusiana na hali ya kipindi hicho. Kwa mfano wimbo huu "UJE ROHO
MUUMBAJI UTAKASE NYOYO ZETU...."
Hapo suala la dini ya mtu hakuna kuangaliwa, hivyo wanafunzi wote tuliitikia.
Baada ya hapo tuliingia darasani na huko kiranja wa darasa alianzisha sala
kabla ya kuanza kusoma kwa kusema kwa sauti kuwa "Kwa jina la Baba, na
la Mwana na la Roho Mtakatifu", kisha ikafuatia na Salam Maria na Baba
yetu Uliye Mbinguni. Haya tulisoma wote kwa sauti kubwa bila ya kujali
dini ya mtu. Saa nne tulikwenda chumba cha chakula na kiranja wa chakula
alianzisha sala ya BABA YETU kwa sauti na sote tuliitikia kisha tulikaa
chini na kunywa uji. Tulirejea madarasani na vipindi viliendelea mpaka
saa 6.30 kengele ya kanisa inalia ambayo tuliita ANJELUSI na ni lazima
kila mtu asimame na kutulia alipo mpaka itakaponyamaza, kisha hufuatiwa
na sala fupi na ndipo vipindi huendelea tena. Hii ni kila siku na hufanyika
hivyo mahali popote utakapokuwepo hata kama unakula inabidi uache kwanza
na kutekeleza ibada hiyo.Vipindi vikimalizika jioni tunafanya kazi za shamba,
mikono na usafi mpaka saa 11.30 ndipo kenglele ya shule hugongwa na kuamuriwa
wote kwenda pangoni kwa ibada. Hapo hakuna cha imani ya mtu. Tunapiga magoti
mbele ya pango na kusali.
Baada ya kujisomea usiku saa 3.00 wanafunzi tulienda mabwenini kwetu
na kabla ya kkulala tulipiga magoti mbele ya sanamu la bweni na kiranja
alianzisha sala kwa kusoma SALAAM MARIA na BABA YETU ULIYE MBINGUNI, KISHA
kisha tuliruhusiwa kulala. Hiyo ndiyo taratibu ya maisha ya kila siku unaingia
shule mpaka unapomaliza shule.Zaidi ya hapo kuna vipindi vya kusali ROZALI,
vipindi vya shida mbali mbali ambazo ibada hufanyika kwa pamoja bila kujali
imani ya mtu. Kutokana na hali hii kila mwanafunzi ni lazima afahamu vyema
sala na nyimbo hizo.
Siku za jumapili na siku za kanisa kama Pasaka, X-mas, kupaa Rabi mbinguni
na za watakatifu mbali mbali wakrisoto huenda Kanisani na ni siku ya neema
kwa wanafunzi kwani chai na mikate hun ywewa na wali kwa nyama huliwa.
Mwezi wa Ramadhan ni marufuku kwa mwanafunzi wa Kiislamu kufunga (kosa)
hivyo tulikuwa hatufungi wala hakuna cha sala ya Ijumaa au Idd. Siku za
Jumamosi tulifanya usafi hivyo wanafunzi walichaguliwa kumsaidia Sista
wa Kanisa kuandaa kwa ajili ya Misa ya Jumapili kama kuiandaa ARTARE, vikombe
vya divai, SAKRAMENTI. Yoyote alichaguliwa bila kujali imani yake.
Shuleni walikuwa wanafuga nguruwe ambao walihudumiwa na wafanyakazi.
Wakati wa kuchinja ukifika huchinjwa na utumbo huenda kuoshewa mtoni ambako
ndiko maji yake hutumika shuleni. Maji hayo huvutwa na pampu mpaka kwenye
tanki, pampu hiyo iko upande wa chini ya mto, na waoshaji nyama hizo upande
wa juu wa mto hivyo kufanya mafuta na vipande vya nyama kuingia kwenye
tanki la maji. Nyama hugawiwa nyingine kwa wanafunzi na kupelekwa jikoni
ambako hupikwa pamoja na nyama ya ng'ombe. Siku hiyo huwa ni ngumu kwa
wanafunzi wa Kiislamu kwani wengine hugomea kula chakula hicho. Lakini
maji, vyombo vyote tayari vinanajisi. Na hiyo ni ya kudumu kwani najisi
imeenea kote.Waalimu, wafanyakazi wote wa shule walikuwa ni Wakristo na
shule ilikuwa ni ya bweni iliyo mbali na kijiji hivyo malezi yote ya wanafunzi
yalikuwa kwa misingi ya Kanisa. Nakumbuka mara kadhaa kati ya mwaka 1964-1966
mwalimu mkuu alipokuwa anapenda kuwauliza wanafunzi mstarini asubuhi "ni
dini gani Waumini wake ni maskini?" Wanafunzi tuliambiwa kujibu "Waislamu".
Mwalimu huuliza tena "ni dini gani Waumini wake wanavaa viraka? Tunajibu
Waislamu. Kisha huuliza " ni dini gani waumini wake wanavaa Suti? Hujibiwa
WAKRISTO. Hapo hutuambia tumejibu vyema na kuturuhusu kuingia madarasani.
Ndugu msomaji hayo ndiyo baadhi ya mambo yaliyokuwa yakitendeka kwenye
mojawapo ya shule hizo tunazoambiwa Waislamu tulikataa kwenda kusoma kwa
uzembe wetu.
Tukirudi likizo ukithubutu kusimulia mikasa hiyo mzazi anahamaki na
kukutaka usirudi tena shuleni kutokana na mambo yanayotendeka kuwa kinyume
na Uislamu. Mimi binafsi nilimaliza kusoma baada ya baba yangu kuamua nisome
tu hivyo hivyo lakini nikimaliza nisilimishwe upya kwani aliamini kabisa
kwamba isikuwa tena Muislamu kutokana na tuliyokuwa tunayatenda hshuleni.
Hebu ndugu msomaji fikiria mtoto wa miaka kati ya 7-15 awe katika maisha
haya unategemea atakuwa muumini kweli wa Uislamu au Ukristo? Hivyo tulipata
kazi baada ya kumaliza shule, tuanze kufundishwa Uislamu pamoja na kubahatika
kuzaliwa kwenye familia za Kiislamu.
Katika kipindi hicho baadhi wanafunzi waliamua kubatizwa baada ya kuvutiwa
na mambo ya kanisani kutokana na nyimbo na sherehe mbalimbali za kanisa.
Pia baadhi ya walio na umri mkubwa kiasi waliacha shule kati ya darasa
la 3-4 kutokana na kuelewa nini kinachotendeka na kuchoka kusikia Uislamu
ukitukanwa kila siku hapo shuleni.Kwa muhtasari huo wa mambo yaliyokuwa
yakitendeka kwenye shule ambayo mimi mwenyewe nimezisoma kati ya mwaka
1964-1973, ndugu msomaji utawahukumu ivipi Waislamu. Walikuwa wazembe hawakutaka
kusoma, au wenye shule walikuwa wanawatoa Waislamu wasisome kwenye shule
zao?"Akukataae hakuambii toka ila utaona mamboye yanavyokwenda": Hii ni
methali ya kiswahili yenye maana, usisubiri kauli ya kufukuzwa ila utumie
hekima zako na busara kuondoka kutokana na vitendo unavyotendewa.
Suala la imani ni zito, hivyo kutuambia tulikataa shule wakati mazingira
yote yalikuwa yanamkataa Muislamu, ni kuudanganya umma na kuukataa ukweli
wa kihistoria ambao uko wazi kabisa. Hii ni sawa na kisa cha Adili na Nduguze
katika kitabu cha marehemu Shaaban Robert, kilichoelezea kisa cha Adili
cha kuwatandika bakora nduguze mpaka wazimie, wakisha zinduka anawaandalia
chakula kizuri na kula nao mezani. Lakini, kwa kuwa Adili alifanya hivyo
kwa kulazimishwa, na pia alijua kufanya hivyo ni kuwatesa (manyani) hao
nduguze, ndiyo maana kila ulipowadia wakati huo alilia sana kwa uchungu
kuonyesha kuwa si haki na wala si halali kumtandika mtu kisha umpe chakula.
Ni bora usimpe kabisa kuliko kudanganya unampenda na kumpa chakula kizuri
wakaiti unamtesa. Ndiyo maana mgeni wa Adili alishangaa na kushindwa kumuelewa
na hivyo kuchukuwa hatuwa ya kuitoa hiyo siri kwa kiongozi wa nchi. Pia
hali kadhalika haikuwa halali kutoa elimu hizo kwa misingi hiyo iliyokuwa
natendeka. Imani ya mwanafunzi ilipasa kuheshimiwa na kuthaminiwa.
|
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !