Written By Msamaa on Thursday, June 27, 2013 | 12:21 PM
Tanzania imekuwa ikijulikana kama kisiwa cha amani na hivyo kuwa kimbilio la wakimbizi kutoka nchi jirani. Hata hivyo kwa takribani miaka mitatu tumeshuhudia amani hiyo ikitoweka kwa kuwepo matukio mbalimbali yanayohusiana na itikadi za kidini yanayojenga mazingira ya kutokea kwa mauaji ya halaiki (mass killings) au ya kimbari (genocide). Kwa muda mrefu, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimekuwa kikifuatilia hali ya kuendelea kupungua kwa uvumilivu (tolerance) baina ya vikundi vyenye misimamo tofauti ya kisiasa au vile vinavyotofautiana kwa imani za dini. Kupungua kwa uvumilivu wa kisiasa kulianza mwishoni mwa miaka ya 1990 na kwa wakati huo hali ilikuwa tete zaidi kwa upande wa Tanzania Zanzibar. Kwa upande wa Tanzania bara hali hiyo ilikuwa ikijitokeza zaidi wakati wa chaguzi ndogo. Kwa ujumla uvumilivu wa kidini haukutetereka sana kama ulivyokuwa uvumilivu wa kisiasa. Hata hivyo, hali ya kupungua kwa uvumilivu wa kidini ilianza kujitokeza kwa kasi zaidi kwenye kampeni za uchaguzi wa mwaka 2010 wakati ambapo baadhi ya wanasiasa walitumia dini kama kiungo cha kupata madaraka na kuweka mambo mbalimbali yanayohusiana na dini kwenye ilani za uchaguzi. Aidha wakati huohuo viongozi tofauti wa kidini walitoa matamko kadha wa kadha kuhusiana na mustakabali wa taifa.
Labels:
taswira
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !