Dk. Shein: Siitambui Kamati ya Maridhiano Zanzibar
Rais wa
Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein amesema haitambui kamati ya maridhiano
inayotetea Zanzibar kuwa na mamlaka kamili kama taifa linalojitegemea na
kuwa na kiti katika Umoja wa Mataifa.
Dk. Shein alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari
baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani
Karume baada ya kukamilisha ziara ya kikazi nchini China juzi.
Alisema kwamba haitambui kamati hiyo lakini alikiri kukutana nayo
mara tatu baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, ilikwenda kumpongeza
Ikulu baada ya kuibuka na ushindi, mara ya pili walifika kumpa mkono wa
pole kufuatia ajali ya meli ya Spice Islanders kabla ya kukutana nao kwa
mara ya mwisho.
Alisema shughuli zinazofanywa na kamati hiyo hazina baraka zake na
wala hatambui mtu aliyeunda au kuteua kamati hiyo ambayo imekuwa
ikifanya kampeni kubwa za Zanzibar kuwa na mamlaka yake kamili na
kuwahusisha viongozi wastaafu akiwemo Rais wa Awamu ya Tano, Dk. Salmin
Amour Juma ‘Komandoo’ na Rais wa Awamu ya Sita, Dk. Amani Abeid Karume.
“Waulizeni nani aliyeunda kamati hiyo na nani aliyeteua kama
wakishindwa nitawaeleza mimi katika mkutano nitakaouitisha kuzungumza na
waandishi wa habari, na walipokuja kwangu wanajua nini nilichowaeleza
waseme,” alisema Dk. Shein.
Kamati hiyo ambayo ilikuwa ikitetea sera ya Muungano wa mkataba
inaundwa na wanachama watatu kutoka CCM na watatu kutoka CUF, ikiongozwa
na waziri wa kwanza wa Katiba na Sheria wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Hassan Nassor Moyo(CCM), Makamu Mwenyekiti Waziri wa Katiba na
Sheria wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Abubakar Khamis Bakari(CUF),
Katibu wake ni Mwakilishi wa jimbo la Mji Mkongwe Ismail Jussa
Ladhu(CUF) na wajumbe ni pamoja na Waziri wa zamani wa SMZ na Mwakilishi
wa jimbo la Kiembesamaki, Mansour Yusuph Himid(CCM) na Mkurugenzi wa
Uenezi na Mahusiano na Umma Salim Bimani(CUF).
Hivi karibuni, kamati hiyo iliandaa mkutano wa hadhara na kutangaza
mambo 10 yanayopaswa kuondolewa katika orodha ya mambo ya Muungano,
ikiwa ni siku chache kabla ya Mwenyekiti wa tume ya katiba Jaji Joseph
Warioba kuzindua rasimu ya katiba ya awali.
Kutokana na hali hiyo joto la kisiasa na vuguvugu la mabadiliko ya
katiba mpya limechukua sura na mitizamo mbalimbali kutoka kwa wanasiasa,
wanaharakati na wasomi ambao baadhi yao wamewanyooshea vidole wanasiasa
wakiwataka kutoingilia mchakato wa katiba na kuipa nafasi tume ya
mabadiliko ya katiba ambayo imepewa mamlaka ya kusimamia jambo hilo kwa
mujibu wa sheria.
CHANZO: NIPASHE
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !