Posted
MWANANCHI: Jumatano,Juni26
2013
saa
12:57 PM
Kwa ufupi
Akifafanua hoja yake, Profesa Shivji
anabainisha kuwa rasimu hiyo imekosa maelezo ya wazi na thabiti kuhusu
ukuu wa Katiba ya Muungano, juu ya Katiba nyingine za washirika wa
Muungano.
Rasimu ya Katiba Mpya inaendelea kuibua mambo na hisia mpya.
Safari hii aliyevunja ukimya ni Mhadhiri mstaafu na mwanasheria maarufu
nchini, Profesa Isaa Shivji.
Profesa Shivji anazungumzia sehemu muhimu ambazo
zimegusa makundi mbalimbali katika rasimu hiyo, kama vile muundo wa
Muungano, ambapo anasema ule wa Serikali tatu unaopendekezwa ni tegemezi
na dhaifu.
Anasema mfumo huo, haujawekewa nguvu ya kikatiba ya kuulinda na kuupa mamlaka thabiti.
Shivji ambaye alikuwa anaagwa kama Mwenyekiti wa
Kigoda cha Mwalimu Nyerere, anasema muundo huo mpya unaweza kusababisha
kuzuka kwa migogoro mingi na mikubwa itakayovunja Muungano.
“Huu muundo ingekuwa sahihi zaidi kama mtu
atauita kuwa muundo wa dola tatu badala ya Serikali tatu kama rasimu
inavyoeleza, kwa sababu tunaona Serikali zote tatu zina mihimili mikuu
mitatu ya dola – Bunge, Mahakama na Serikali,” anasema.
Anaonya kuwa iwapo Rasimu hiyo itakubaliwa bila mabadiliko makubwa, itasababisha kuvunjika kwa Muungano.
Angalizo la Prof. Shivji, limekwishatolewa na
Chama cha Mapinduzi ambacho kinaendelea kushikilia sera yake ya Serikali
mbili na makundi mengine mbalimbali. Hata hivyo, yapo makundi mengine,
kikiwamo Chama cha Demokrasia na Maendelo ambayo yamefurahishwa na
muundo unaopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Akifafanua hoja yake, Profesa Shivji anabainisha
kuwa rasimu hiyo imekosa maelezo ya wazi na thabiti kuhusu ukuu wa
Katiba ya Muungano, juu ya Katiba nyingine za washirika wa Muungano.
“Hali hii itasababisha migongano na kutoelewana kati ya mamlaka za washirika wa Muungano na mamlaka ya Jamhuri ya Muungano.
Anasema Ibara 8, ya rasimu hiyo inayozungumzia
ukuu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano inaeleza kuwa “ukuu wa Katiba ya
Jamhuri ya Muungano utakuwa katika mambo ya Muungano tu na si
vinginevyo”.
“Ukisoma rasimu hii ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano katika Ibara ya 8(1) inasema na hapa nitanukuu: “Bila ya
kuathiri masharti ya Katiba za washirika wa Muungano kwa mambo yasiyo ya
Muungano, Katiba hii itakuwa sheria kuu katika Jamhuri ya Muungano”.
Kwa hiyo Ibara hii inaeleza kuwa Katiba
inayopendekezwa haitakuwa na nguvu za kisheria juu ya Katiba za
washirika wa Muungano,” alisema Shivji.
Anasema Katiba zote za nchi zinazofuata muundo wa shirikisho
kama unaopendekezwa na Tume, zikiwemo za Marekani na Australia, zina
vipengele vinavyoeleza wazi kuwa katiba ya shirikisho ni sheria kuu juu
ya katiba za washirika ambayo inaondoa mianya ya kuibuka kwa migongano
kati ya mamlaka za shirikisho na washirika wao.
“Nadhani masharti mengi ya Rasimu na muundo wake mzima ni matokeo ya mivutano mikali katika Tume,” anasema na kuongeza:
“Bahati mbaya hatuna mwenendo wa majadiliano ya
Tume wala taarifa yao rasmi, … lakini usomaji wangu wa awali unaniambia
kwamba Rasimu hii ni maelewano (compromise), na sio mapatano, au
mwafaka, kwa maana ya consensus.”
Anasema katika maelewano pande zinazokinzana
hatimaye hukubali kwa shingo upande ili kutokukwamisha uamuzi ambapo
pande zote zinapata kidogo na kupoteza kidogo, na kila upande huwa na
mkakati wake wa kupata zaidi katika duru ya pili.
Anaongeza kuwa vile vile, maelewano hayo ya pande mbili kamwe hayawezi kuwa kwa moyo safi.
“Maelewano au compromise, yanazaa uamuzi legelege,
mapatano au consensus, kwa upande mwingine, ni maafikiano yanayofikiwa
baada ya mjadala mrefu, kila mmoja akilenga kuthibitisha hoja yake na
kwa njia hii kusadikisha wenzake kwamba hoja yake ni sahihi. Baada ya
kufikia uamuzi wa mwafaka, kila mmoja anatoka akiwa ameridhika na
amefurahi. Katika compromise, kila mmoja anatoka amenuna,” anasema.
Profesa Shivji anasema Rasimu ya Katiba inasema
hati ya Makubaliano ya Muungano iliyorejewa katika ibara ndogo ya (1),
ndio msingi mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba kwa kadri
itakavyorekebishwa, itakuwa ni mwendelezo wa makubaliano hayo.
“Ukiangalia kwa jicho la kisheria, ukisema hati
ndio msingi, maana yake ni kwamba hati bado inaendelea kuwa na nguvu ya
kisheria na ndio sheria kuu inayotawala Katiba…. Lakini hati iliweka
Serikali mbili; sasa iweje rasimu inayozungumzia Serikali tatu iwe na
msingi ambao ulijengeka kwenye Serikali mbili?” anahoji.
Anaongeza kuwa huenda Tume hiyo iliyosheheni
wanasheria wazoefu na waliobobea, walijua na kuelewa walichokuwa
wanaandika na haiwezekani walikosea au kuteleza, isipokuwa
walichokifanya ilikuwa ni ‘kusalimu amri’ na ‘kuelewana’ ili mambo
yaendelee.
“Ndivyo tulivyopata ibara legelege ambayo kisheria
haina kichwa wala mkia, ibara kama hii isiyoeleweka inashusha hadhi ya
Katiba. Inawezekana kabisa kwamba ibara hii isiwe na madhara makubwa kwa
sababu majaji wenye busara hawatatia maanani sharti kama hili. Lakini
unaweza kupata jaji ambaye anaegemea zaidi kwenye ufundi na kuitafsiri
ibara hii kama ilivyo, na madhara yake yanaweza kuwa makubwa.
Eneo la washirika
Katika mfano mwingine aliouita mzito zaidi,
alisema ni kuhusu mipaka ya madaraka ambapo eneo la utawala wa Serikali
ya Shirikisho limetajwa kuwa ‘eneo lote la Tanzania Bara ikijumuisha
sehemu yake ya bahari na eneo lote la Zanzibar ikijumuisha sehemu yake
ya bahari, wakati eneo la utawala wa Serikali ya Bara na Serikali ya
Zanzibar halikutajwa.
Anasema pande mbili za Muungano zimewahi kutofautiana kuhusu
eneo lao la bahari, hasa kwa sababu inadhaniwa kwamba bahari inayopakana
na maeneo ya Tanganyika na Zanzibar ina mafuta na rasilimali nyingine.
Anasema ukimya wa Rasimu juu ya kueleza kwa uwazi
mipaka ya utawala wa Washirika ni wa ajabu kwa sababu huwezi kuzungumzia
utawala wa mamlaka yoyote yale bila kubaini mipaka yake, anabainisha
kuwa ukimya huo unaweza kuzaa migogoro.
Profesa Shivji anasema magwiji wa Katiba wanaafiki
kwamba mfumo wa shirikisho una angalau sifa kadhaa –mwananchi
anatawaliwa na serikali mbili, yaani serikali ya shirikisho na serikali
ya mshirika; na kuna mgawanyo wa madaraka miongoni mwa serikali, na
katiba/sheria zao zina hadhi sawa; na kuwa Katiba ya Shirikisho ni
Sheria Kuu (supreme law).
Je, Rasimu inakidhi sifa hizi? Kwa maoni yangu,
kwa kiasi kikubwa kila mwananchi wa pande zote mbili atatawaliwa na
Serikali mbili; Wabara watatawaliwa na Serikali ya Shirikisho na
Serikali ya Bara, Wazanzibari watatawaliwa na Serikali ya Shirikisho na
serikali ya Zanzibar. Pia kuna mgawanyo wa madaraka kati ya serikali
tatu,” anasema.
Anasema kwa msingi huo, washirika, yaani Bara na
Zanzibar watakuwa na hadhi sawa lakini akasema sifa inayotatanisha ni
ya mwisho, ile inayosema Katiba ya Shirikisho ni Sheria Kuu.
Akielezea dhana ya Ukuu wa Katiba Shivji anasema
ni sheria zote, madaraka, majukumu na mamlaka yanatokana na Katiba, na
Katiba ndio chanzo cha uhalali wa utawala.
Anaongeza kuwa Katiba yenyewe inapata mamlaka yake
kutoka kwa wananchi katika ujumla wao. Ndiyo maana, katika msamiati wa
kawaida, tunasema katiba ni sheria mama.
“Nikitumia msamiati huo kwa katiba ya shirikisho,
naweza nikasema kwamba katiba ya shirikisho ndio mama na baba wa
shirikisho. Katiba na sheria za washirika, ingawa zina mamlaka kamili
katika maeneo yao, zinatokana na katiba ya shirikisho na zinapata uhai
wao wa kisheria kwa mujibu wa katiba ya shirikisho.
Anasema kwa kawaida ukitaka shirikisho liwe imara
na liwe na nguvu, basi hakuna budi Washirika wakubali kutambua na kutii
masharti ya Katiba ya Shirikisho vinginevyo shirikisho litayumba na
kutakuwa na migogoro kutokana na vipengele vya katiba na sheria na
vitendo vya vyombo vya washirika kukinzana na kugongana kila mara.
Ukuu wa Katiba
Akisisitiza juu ya ukuu wa katiba, Shivji anasema
Ibara ya 61(4) inasema ‘Washirika wa Muungano watatekeleza majukumu yao
kwa kuzingatia masharti ya Katiba hii na Katiba zao”.
“Wanasema ‘Kuzingatia’ sio kubanwa; Kiingereza
chake ni ‘to take account of’, ‘to bear in mind’. Hii ina maana unaweza
ukazingatia masharti ya Katiba ya Shirikisho, na baada ya hapo ukatenda
kinyume chake, lakini hata hivyo utakuwa hujavunja Katiba” anasema.
Anasema hii inaeleweka zaidi ukisoma ibara ndogo inayofuata
inayotaka Washirika kutekeleza majukumu yao kwa masuala yasiyo ya
Muungano ‘kwa mujibu’ wa masharti ya katiba zao.
“‘Kwa mujibu inaleta maana ya kubanwa, huwezi
ukakiuka. Kwa hivyo, masharti ya Katiba ya Shirikisho yanakushawishi;
masharti ya Katiba ya Mshirika yanakushurutisha.”
Anaielezea Ibara 109 (5) kuwa inasema ‘bila ya
kuathiri’ kutumika kwa Katiba ya Tanzania Bara na Katiba ya Zanzibar,
Katiba hii itakuwa na nguvu ya sheria katika Jamhuri ya Muungano kwa
mambo yanayohusu Muungano na endapo sheria nyingine yoyote itakiuka
masharti yaliyomo katika Katiba hii, basi sheria hiyo nyingine, kwa
kiasi kinachokiuka Katiba hii, itakuwa batili.
“Kuna dhana mbili zilizotumika katika kipengele
hiki: ‘mambo yanayohusu’ (Muungano) na ‘sheria’. Bila shaka ‘mambo
yanayohusu Muungano’ ni dhana pana zaidi kuliko ‘mambo ya Muungano’.
Mambo ya Muungano ni yale saba yaliyotajwa katika nyongeza…Mambo
yanayohusu Muungano ni hayo saba pamoja na yale yote yaliyozungumziwa
katika Katiba ya Shirikisho,” anasema
Anaongeza kuwa kwa mantiki hiyo hiyo, neno
‘sheria’ haliwezi likawa na maana pana zaidi ya sheria inayohusu mambo
ya Muungano inayotungwa na Bunge la Shirikisho kwa mujibu wa ibara 109.
Kwa hivyo, ukuu wa Katiba ya Shirikisho
unaozungumziwa katika ibara hii ni juu ya shughuli za Muungano tu, na
kuwa sheria yoyote juu ya mambo yanayohusu Muungano ikikiuka masharti ya
Katiba ya Shirikisho, sheria hiyo ni batili. Lakini hii haihusu katiba
na sheria za Washirika.
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !