Kwa ufupi
Vilevile, wamesema kuwa hawako tayari kukaa kimya
huku wakiona amani na utulivu nchini ikivurugika, badala yake
wataendelea kusema ili amani na utulivu viweze kurejea.
Kauli hiyo imekuja baada ya Rais Jakaya Kikwete,
kuwataka maaskofu hao na viongozi wengine wa dini nchini kuendelea
kuisaidia Serikali katika kuimarisha amani na upendo miongoni mwa
wananchi.
Akizungumza wakati wa kuadhimisha Jubilee ya miaka
25 ya uaskofu wake kwenye sherehe zilizofanyika jana katika Seminari ya
Mt Peter mjini Morogoro, Askofu wa Jimbo la Morogoro, Telesphor Mkude,
alisema meza ya mazungumzo ni lazima itumike katika kuimalisha amani na
upendo wa Watanzania badala ya kutumia jazba na nguvu.
Mkude alisema kwa hivi sasa kumeibuka mivutano ya
kidini na kisiasa na kutoa mfano wa vurugu zilizoibuka wilayani
Sengerema mkoani Mwanza juu ya nani ana haki ya kuchinja au kutokuchinja
kati ya waumini wa madhehebu ya Kikristo na Waislamu.
Pia vurugu za mikutano ya kisiasa, makanisa
kuchomwa, mapadri na watumishi wengine kuuawa na kuteswa, kutupwa kwa
mabomu katika mikusanyiko ya watu ikiwamo makanisa na kwamba yote hayo
yangeweza kumalizwa katika meza ya mazungumzo.
Vurugu kubwa zilitokea Jumamosi iliyopita mjini
Arusha baada ya mtu ambaye bado hajajulikana, kutupa bomu katika mkutano
wa Chadema wa kampeni ya uchaguzi mdogo wa udiwani uliofanyika katika
viwanja vya Soweto na kuua watu wawili na wengine zaidi ya 60
kujeruhiwa.
Mei 2, mwaka jana, Mwandishi wa Kituo cha
Televisheni cha Channel Ten, Daud Mwangosi aliuawa kwa kulipuliwa na
bomu na askari polisi katika vurugu zilizotokea katika eneo la Nyololo
mkoani Iringa.
Februaria 18, mwaka huu, Padri wa Kanisa Katoliki
Parokia ya Minara Miwili, Mji Mkongwe, Zanzibar aliuawa kwa kupigwa
risasi asubuhi wakati akienda kuendesha misa katika Kanisa la Mtakatifu
Theresia eneo la Mtoni. Mtuhumiwa wa tukio hilo, Omar Musa Makame,
anaendelea na kesi mahakamani kujibu tuhuma za mauaji.
Tukio lingine ni lile la watu wawili kuuawa na
polisi mjini Songea, Februari 22, mwaka jana, wakati wakizuia maandamano
ya wananchi wenye hasira kali waliokuwa wakipinga mauaji yanayohusishwa
na imani za kishirikiana.
Hivi karibuni maaskofu hao walitoa tamko la kuitahadharisha Serikali, kudhibiti vurugu za kidini na kisiasa nchini.
Walionya kuwa iwapo vurugu hizo hazitadhibitiwa huenda nchi ikaingia katika machafuko.
Awali, jana Rais Kikwete akizungumza katika hafla hiyo licha ya
kumpongeza Askofu Mkude kwa utumishi wake mwema wa miaka 25 ya uaskofu
wake, lakini pia alimpongeza kwa kuwa na mchango katika jitihada za
maendeleo zinazofanywa na Serikali.
Alisema Kanisa Katoliki Jimbo la Morogoro limekuwa
msaada katika kuimarisha huduma za jamii ikiwamo sekta ya elimu na afya
na kwamba baadhi ya zahanati na vituo vya afya vimejengwa na
kupandishwa hadhi kama Hospitali ya Mt Kizito na Turiani.
Rais Kikwete aliongeza kuwa mbali ya askofu huyo
kuisaidia Serikali katika nyanja hizo, pia amekuwa akiiunga mkono katika
jitihada zake za kujenga amani na upendo miongoni mwa wananchi ili
taifa liweze kuwa na raia wema.
Kwa upande wake Askofu wa Jimbo Kuu Katoliki la
Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, alimtaja Askofu Mkude
kuwa ni kuhani asiyekuwa na mwanzo wala mwisho, kwa vile anashiriki
katika ukuhani wa Yesu Kristo asiyekuwa na mwanzo wala mwisho.
Alisema mpaka kufikia umri huo katika utumishi
wake amekutana na mambo mengi magumu, lakini kutokana na kumtegemea
Mungu zaidi ameshinda na kwamba akawaomba waumini wa Kanisa Katoliki
kuendelea kumwombea na kumpa ushirikiano ikiwa ni zawadi yao pekee .
Askofu Mkude aliteuliwa kuliongoza Jimbo Katoliki
la Tanga mwaka 1988 na aliyekuwa Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani,
Papa Paulo II (kwa sasa ni marehemu), mwenye heri na miaka mitano
baadaye alihamishiwa katika Jimbo la Morogoro ambako amelitumikia kwa
miaka 20 mpaka sasa.
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !