- Kitoloho
Headlines News :
Home » »

Written By Msamaa on Wednesday, June 19, 2013 | 9:56 AM



Utajiri mkubwa wa wachungaji, ‘kutoa ni moyo’ kwa waumini!
SOURCE_RAI: Alhamisi, Octoba 04, 2012 06:20 administrator .


ETI wajinga ndio waliwao! Hivi ni kweli wanaliwa kupitia utumwa wa imani? Si kuna msemo usemao kuwa utumwa wa imani ni mbaya zaidi kuliko utumwa wa mwili? Wazungu wanasema “slavery of the mind is far harsher than physical slavery!” Upo hapo, kama Kingereza chako kinapanda?

Habari kwamba baadhi ya viongozi wa dini, hususan wachungaji na maaskofu wa makanisa ya kiroho, wana utajiri mkubwa si ngeni.

Gazeti moja la wiki, wiki iliyopita lilichokonoa na kubainisha mali za wachungaji hao na vyanzo vya mapato yao.

Eti wachungaji na maaskofu, baadhi yao wanadaiwa kumiliki majumba ya kifahari, magari ya thamani kubwa, mashamba, vituo vya redio na televisheni pamoja na mali nyingine nyingi! Watu wa Mungu hawa nao wamo bwana!

Eti utajiri wa wachungaji na maaskofu hawa unatokana na misaada ya waumini na watu wengine pamoja na zawadi mbalimbali ambazo hupewa kutokana na huduma nzuri wanayotoa! Jamani mpo hapo?

Duh, eti baadhi ya wachungaji hawa wamekuwa tishio hata barabarani wanapokatiza, wakiendesha magari yenye thamani kubwa kama Hammer, Range Rover Sport na mengineyo!

Eti waheshimiwa hawa wana mbwembwe bwana, baadhi yao kwa kutembea kwa misafara inayounga magari ya kifahari, hasa wanapoalikwa kufanya ziara zao za kutoa huduma ya kanisa!

Gazeti hili tajwa hapo juu halina mchezo,  linachokonoa kweli sehemu mbalimbali! Linachokonoa Kanisa la Ufufuo na Uzima, na kudai kuwa kiongozi wake, Josephat Gwajima, anasema kuwa magari waliyonayo viongozi waandamizi wa kanisa hilo yametokana na misaada ya watu!

Eti kiongozi huyu anamiliki gari la kifahari aina ya Hammer, na kwamba gari hili halijatokana na sadaka za waumini, bali ni zawadi aliyopewa! Wee, usibishe na kumung’unya maneno kuwa hata nyumba anayoishi amepangiwa na kanisa. Si waumini wanawapenda sana wachungaji wao?

Eti naye kiongozi wa Kanisa la Living Water, Mtume Onesmo Ndegi, mbali na kuendesha gari la kifahari na kuishi kwenye nyumba ya kisasa, anadaiwa kumiliki mashamba Bagamoyo, mkoani Pwani. Lakini eti yeye anasema kwamba maisha yake binafsi hayategemei kanisa, kwani ana biashara zake ambazo haziweki wazi.

Na mchungaji Lusekelo je, yule wa Kanisa la Maombezi (GRC), maarufu kwa jina la Mzee wa Upako? Eti yeye anakiri kwamba uwezo wake kifedha unaridhisha na anajitosheleza, na kwamba hana tamaa ya kukwapua sadaka za waumini, akidai kuwa ana biashara zake ambazo pia haziweki wazi.

Eti ya Getrude Rwakatare wa Kanisa la Mikocheni “B” Assembles of God, hivi karibuni nyumba yake inayodaiwa kuwa na thamani ya Sh bilioni 1.5 iliingia kwenye mzozo!

Mbali na jumba hilo, mchungaji Rwakatare ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu, anamiliki shule kadhaa, redio pamoja na vitega uchumi mbalimbali.

Eti gazeti hilo lililomchokonoa linaandika kuwa baadhi ya waumini wa kanisa lake wanamtetea kwamba baadhi ya mali si zake binafsi, ila zinamilikiwa na kanisa, ikiwamo redio, Praise Power.

Lakini mchungaji Rwakatare si ni Mbunge bwana, si pia ana biashara mbalimbali ambazo yeye mwenyewe hazitaji? Sasa kwa nini anachokonolewa? 

Na Josephat Mwingira ambaye hupenda zaidi aitwe Mtume na Nabii, akiwa ni kiongozi wa Kanisa la Efatha, eti mmoja wa viongozi wa kanisa lake ambaye hakutaka kutaja jina lake, anasema mali anazomiliki mchungaji wake zinatokana na huduma inayotolewa na mchungaji huyo, hivyo kila muumini kwa wakati wake analeta kile alichonacho kama shukrani.

Eti Mwingira anadaiwa kumiliki majengo yenye thamani kubwa, benki inayoitwa Benki ya Efatha, pamoja na viwanja mbalimbali.

Eti hivi karibuni Mwingira aliingia kwenye mzozo wa umiliki wa jumba lake la kifahari lenye thamani ya shilingi bilioni moja.

Ebo, sasa tatizo ni nini?  Mwingira si anatajwa kuwa mkombozi wa waumini wake, kwani Benki ya Efatha, inadaiwa kuwasaidia kujikwamua kiuchumi. Isitoshe eti benki hiyo ni mali ya Kanisa na ilianzishwa na Mwingira kwa dhumuni la kuwasaidia waumini wake.

Vile vile, Mwingira, anadaiwa kumiliki Kituo cha Televisheni the Trinity, kilichopo Dar es Salaam. Sasa kosa liko wapi?

Na ‘Mtanganyika’ wetu Christopher Mtikila wa Kanisa la Full Salvation, pamoja na kwamba anamiliki jumba la ghorofa mbili lililopo Mikocheni, Dar es Salaam, lakini eti anajitambulisha kwamba ni masikini.

Eti yeye alimwonyesha mwandishi wa gazeti tajwa akisema “hata wewe ndugu yangu si unaona mimi ni mchungaji lakini nyumba yangu haijaisha!” Na hiyo ni kweli.

Kuthibitisha kile alichokisema Mtikila, jengo hilo ni la miaka mingi na ni uwekezaji wa muda mrefu alioufanya mchungaji huyo.

Kwa mujibu wa gazeti hilo chokonozi, eti na Askofu Mkuu wa Kanisa la International Evangelism, Eliud Isangya, anasema kuwa kiongozi wa dini kuwa na mali si vibaya, na kutolea mfano kwamba Nabii Suleiman na Abraham walikuwa na mali nyingi, ikiwamo dhahabu kutokana na kazi zao.

Anakuwa mwepesi kuongeza kuwa yeye hatangulizi mali, bali anaangalia huduma ya Mungu pamoja na kulea yatima. Haya, maneno safi hayo.

Mchungaji Isangya anadaiwa kumiliki ndege na uwanja wa ndege uliopo karibu na kanisa lake eneo la Sakina, mkoani Arusha.

Lakini Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Methodius Kilaini, eti anasema kuwa ni aibu kwa kiongozi kuanzisha kanisa na kuanza kujinufaisha yeye binafsi.

Askofu Mkuu wa Anglikana, Valentino Mokiwa, kwa mujibu wa gazeti hilo, anakiri kwamba kiuchumi yupo vizuri, lakini akaweka wazi kwamba anategemea biashara zake nyingine ambazo hazitaji, si kanisa peke yake.

Mokiwa anasema eti tatizo la wachungaji wengine ni kujinufaisha kupitia kanisa, na kusisitiza kuwa kiongozi wa dini si lazima awe masikini.

Hilo ni darasa na elimu tosha. Sasa kazi kwenu, ni kipi kingine mnataka?

Share this article :

0 comments:

Speak up your mind

Tell us what you're thinking... !

ZILIZOSOMWA SANA.

Followers

Blog Archive

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Proudly powered by Blogger
Copyright © 2011. Kitoloho - All Rights Reserved
Template Design by Creating Website Published by Mas Template