HATIMAYE baada ya kelele za miaka mingi na waliozitoa kuitwa
wasaliti, si wenzetu, watu wenye nia mbaya na hawaitakii mema Tanzania
inaonekana kuelekea kule ambapo nchi nyingi zinazojenga utawala wa
kidemokrasia zimetangulia kuifanya safari hiyo.
Nayo ni kuwa na katiba mpya ambayo rasimu yake ilitolewa wiki hii na
sasa kuwa mada kuu ya mazungumzo kila pembe ya Jamhuri ya Muungano.
Kwa hapa Zanzibar rasimu hii imepokewa kwa mitazamo tofauti, wengine
kwa kuiona ni nzuri sana, wengine nzuri kiasi na wengine kuiona
haijakidhi haja na matarajio ya Wazanzibari.
Wapo pia wanaoisifu au kuiponda, lakini ukitafakari utaona hata
kilichokuwamo ndani hawakielewi isipokuwa wanajifanya wataalamu na
ukichunguza utaona wanasukumwa na utashi wa kisiasa badala ya masilahi
ya Zanzibar na Tanzania kwa jumla.
Ukweli ni kwamba mapokezi ya rasimu yameigawa Zanzibar kwa mapande,
makubwa na madogo. Lipo kundi linaloona maoni ya Wazanzibari hayakupewa
uzito unaostahiki, lakini wengine wanahisi waliokuwa wakipinga katiba ya
zamani na mfumo wake wa serikali mbili ‘wamepata zaidi’ kuliko wao
waliotaka serikali mbili au mbili kuelekea moja.
Maeneo yaliyotawala mjadala ni pamoja na kwa kiasi gani Zanzibar
itakuwa na mamlaka kamili juu ya masuala mbalimbali na hasa fedha na
biashara.
Hapa inafaa kukumbusha kwamba ukiachilia mbali wafanyabiashara,
Wazanzibari wengi, wakiwamo wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na wabunge,
wamekuwa wakitaka suala la fedha kama ilivyokuwa wakati wa muungano
ulipoundwa mwaka 1964 lisiwe la Muungano.
Kumbukumbu zinaonesha kuwapo kelele hata ndani ya Baraza la
Wawakilishi, kutaka Mamlaka ya Mapato Zanzibar (TRA) ifunge virago vyake
Visiwani kwa kile kinachoonekana na wengi hapa kuwa ni taasisi
isiyokuwa na masilahi na Zanzibar.
Mjadala unaosikika hapa ni kwamba kwa suala la fedha kuwa la Muungano
Zanzibar bado itakuwa haina uwezo wa kujitutumua kiuchumi, hasa kwa
vile mfumo wa kodi uliopo sasa wa Muungano unaonekana hauitendei haki
Zanzibar.
Kwa miaka mingi Wazanzibari wamekuwa na unafuu mkubwa wa ulipaji kodi
ukilinganisha na wenzao wa Bara, kwa hiyo wengine wanahisi kwamba
fedha kuwa chini ya Muungano, Zanzibar itaendelea kusononeka na kuumia
kiuchumi.
Eneo jingine ambalo watu wamekuwa na shauku nalo ni hili la Mambo ya
Nje, hasa kwa vile haijaelezwa wazi kama ushirikiano wa kimataifa nao
utakuwa katika kapu la Muungano.
Zanzibar imekuwa ikilalamika kuwa ushirikiano wa kimataifa uliingizwa
kinyemela katika orodha ya mambo ya Muungano ili Zanzibar isinufaike na
misaada kutoka nje. Eneo linalogusiwa sana ni kule kuzuiliwa kuijunga na
Jumuiya ya nchi za Kiislamu (OIC).
Kinachowaumiza Wazanzibari ni kile wanachokiona kama kudanganywa na
Serikali ya Muungano kwamba suala hili lingeshughulikiwa kwa Tanzania
kujiunga na OIC, badala ya Zanzibar peke yake. Lakini hili halijafanyika
kwa zaidi ya miaka 15 sasa na hazisikiki habari zozote za Tanzania
kujiunga na OIC.
Muundo wa kuwa na Bunge dogo badala ya utitiri uliopo sasa,
umewafurahisha wengi, lakini wapo wanaoona haki haikutendeka kwa Bara
kuwa na wabunge 50 na Zanzibar wabunge 20.
Wengi wanahisi mfumo huu hauoneshi kwamba Muungano ni wa nchi mbili,
sawa na wanaohisi angalau Bara ingelikuwa na Wabunge 45 na Zanzibar 25 .
Muda wa wabunge kuwa na kikomo cha vipindi vitatu umefurahiwa na
wengi, lakini wapo wanaohisi viwili vingelitosheleza kama alivyowekewa
rais.
Pendekezo la kulipa Bunge meno la kuidhinisha mawaziri na watendaji
wakuu linaungwa mkono na wengi. Lakini wapo wachache (wahafidhina)
wanaona rasimu haimtendei haki rais kwa vile mazoea yamewalemaza kuona
rais hakosei na anayo haki ya kufanya maamuzi bila ya kuhojiwa au
kukataliwa na yeyote yule katika nchi kwa kisingizio kwamba amechaguliwa
na wananchi.
Watu hawa hawa wanafumbia macho ukweli kwamba wabunge nao wanachaguliwa na wananchi.
Kwa suala la Baraza la Mawaziri kuwa na mawaziri 15 tu karibu kila mtu
ameipongeza Tume ya Katiba, kwani wanahisi Tanzania hivi sasa inalo
baraza kubwa kupita kiasi na hii inaigharimu nchi mabilioni ya shilingi.
Wapo wanaohisi Zanzibar nayo inafaa irekebishe sheria yake na iwe na
mawaziri wasiozidi 10 na iondokane na kuwa na mawaziri wasiokuwa na
wizara maalumu na utitiri wa manaibu mawaziri na washauri wa rais.
Kwa suala la kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi wengi wanasema tume imeona
mbali na kuipongeza, lakini wahafidhina wanahisi muundo wa sasa wa rais
kuchagua wajumbe ni sahihi.
Hoja ya watu hawa ni kwamba aliyekuwa mbele siku zote ndiye mshindi na si lazima apate zaidi ya asilimia 50 ya kura zote.
Lakini hapa baadhi ya wanasheria na watu ambao wanaona mbali wanasema
lazima pawepo tafsiri inayoeleweka ya maana ya zaidi ya asilimia 50 ya
kura zote. Je, hii ni ya kura zilizopigwa, zile zilizokuwa halali au ni
pamoja na zilizoharibika?
Vile vile kipengele cha mgombea kuhoji matokeo ya uchaguzi wa rais
mahakamani kimeleta furaha kubwa Zanzibar japokuwa watu wengi walikuwa
na shaka kama mahakama za Tanzania zitakuwa na ubavu na kujiamini kuwa
huru, hivyo kutenda haki na hasa kutokana na dhana iliyopo sasa kuwa
mahakimu wetu bado hawaamini kama wanaongozwa na sheria na si
mapendekezo ya viongozi.
Lililo muhumu, watu wengi wanasema ni kwa mahakama kuhakikisha sheria
zinaheshimiwa na anayezivunja anawajibishwa kisheria, bila ya kujali
nafasi yake katika jamii.
Kipengele cha rais kumpunguzia mamlaka ili asipande watu vichwani
kimefurahisha wengi, hasa wapinzani. Hata hivyo wapo wanaohisi na rais
naye aweze kushitakiwa kwa sababu akiwekewa kinga atakuwa na ubavu wa
kutowatendea wananchi haki kwa mujibu wa sheria.
“Kama rais atakuwa na kinga, basi na mawaziri nao wawe na kinga na
wananchi nao pia tuwe na kinga,” alisema kijana mmoja, Ali Mohamed wa
Michenzani.
Suala la umri wa kiongozi limeonekana kuleta mgawanyiko Zanzibar. Wapo
wanaohisi miaka 40 ni mingi kwa vile wapo vijana wa chini ya umri huo
wenye uwezo kuliko wakubwa wao kwa umri.
Katika hili wanatoa mfano wa Waziri Mkuu mstaafu na aliyekuwa Katibu
Mkuu wa Umoja wa Nchi za Kiafrika, Salim Ahmed Salim, ambaye
alichaguliwa balozi akiwa na miaka 21 na Nigeria ilipoongozwa na Yakubu
kutoka mwaka 1966 akiwa na miaka 32 hadi mwaka 1975.
Rais Joseph Kabila wa Congo ambaye alichukua uongozi mwaka 2001 akiwa
anakaribia umri wa miaka 30 na Muammar Gaddafi wa Libya aliyekuwa rais
akiwa na miaka 27.
Dada mmoja, Amina Suleiman wa Bububu alielezea suala hili kwa hasira
kwa kusema: “Tatizo lililopo katika nchi yetu ni wazee kuona wao tu ndio
wenye akili, uwezo na busara. Mwenendo huu umepitwa na wakati.”
Kwa ujumla mapendekezo ya katiba yametoa mwanga wa matumaini
palipokuwepo na giza. Lakini suala ni kwa kiasi gani mjadala wa hiyo
rasimu utakuwa na maana na kuboreshwa katika mabaraza ya katiba ambayo
hapa Visiwani yamelalamikiwa kuwa yameundwa kwa mizengwe na kudaiwa kuwa
chama tawala cha CCM kilicheza mchezo mbaya.
Watanzania sasa wanajua wapi walipo, lakini safari ya huko
wanakokwenda, hasa hapa Visiwani, bado ni ya milima na mabonde. Ni
uzalendo tu na si utashi wa kisiasa ndio utakaosaidia kupiga hatua
mbele.
Hongera Jaji Warioba na timu yako, lakini tume inapaswa kuwa makini na
hayo mabaraza ya katiba, kwani kazi nzuri ambayo imefanywa inaweza
kutiwa doa na kuchafuliwa na kunuka na kuwa sehemu mbaya ya historia ya
nchi hii.
CHANZO:TANZANIA DAIMA.
5-june-2013
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !