‘Madeni yameielemea Serikali’
MWANANCHI.
Zikiwa zimesalia siku mbili kabla ya Bajeti Kuu ya Serikali kusomwa, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti na Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge amesema Serikali imeelemewa na mzigo wa madeni.
Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa anatarajia kuwasilisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2013/14 keshokutwa.
Chenge alisema hayo juzi Mjini Dodoma baada wa
mkutano wa majadiliano ya namna bora ya utendaji kazi baina ya Kamati ya
Bunge ya Bajeti na kamati za Miundombinu, Ulinzi na Usalama, Mambo ya
Nje, Hesabu za Serikali (PAC) na Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).
Alisema Serikali imeelemewa na madeni huku kila
wizara ikitaka kukamilishiwa mafungu yake ya fedha jambo ambalo
linashindikana kwa kuwa hazipo.
Kwa mujibu wa hotuba ya Kambi ya Upinzani ya
Wizara ya Fedha, mpaka sasa deni la taifa limefikia Sh21.028 trilioni
bila dhamana ya Serikali kwa mashirika ya umma na binafsi hadi kufikia
Desemba 2012 na kati ya fedha hizo, asilimia 75.97 ni deni la nje.
Hata hivyo, katika majibu ya Serikali, Waziri
Mgimwa alisema Serikali imeanza kulipa na kuanzia Julai 2012 hadi Aprili
2013, malipo ya madeni yamefikia Sh1,666.77 bilioni na kati ya hizo,
deni la nje lililolipwa ni Sh213.57 bilioni.
“Unapoamua kuminya eneo moja kwa ajili ya kupeleka
fedha eneo jingine, hapa panapominywa wanahangaika na wao wanahitaji
fedha, inatakiwa kutafuta njia nyingine ya kupata fedha kwa ajili ya
eneo hilo,” alisema Chenge.
Mwenyekiti huyo alisema wizara zote 32 zinahitaji
fedha kulingana na bajeti wanazowasilisha bungeni wakati wizara nyingine
zikihitaji fedha zaidi ili kukamilisha mipango kwa matumizi ya kawaida
na maendeleo.
“Katika vikao vyetu vya ndani, tumezungumza na
kila wizara. Zina matatizo mengi kweli... wanatutaka tuwaongezee kasma,
sasa sisi siyo Serikali, tunachokifanya kamati ni kuishauri Serikali
kuelekeza fedha eneo moja lenye mahitaji ya fedha nyingi kwa masilahi ya
taifa.
“Tumeishauri Serikali kuondoa fedha maeneo kadhaa
na kuitaka kutenga fedha kwa ajili ya mipango ya maendeleo, lakini
wakati mwingine, hata hizo fedha zenyewe hakuna kwa kuwa
tunachokitegemea zaidi hapa ni pato la ndani. “Sasa watu walipe kodi.
Tabia ya ukwepaji kodi inasababisha Serikali kushindwa kukusanya mapato
yake. Watu wanalalamika hakuna hiki na hiki, lakini wananchi na taasisi
mbalimbali wenyewe ndiyo hao wanaokwepa kodi, sasa utapata wapi fedha za
maendeleo?
Meghji: Bajeti ina presha.
Waziri wa zamani wa Fedha, Zakhia Meghji amesema kipindi cha
kuelekea kwenye bajeti, kinakuwa cha ‘presha’ hasa ikiwa waziri
hakujiandaa kisaikolojia.
Akizungumza kwenye Viwanja vya Bunge, Dodoma jana,
Meghji ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Kuteuliwa, alisema: “Ninajivunia,
katika kipindi changu kuanzia 2005-7 nikiwa Waziri wa kwanza wa Fedha
mwanamke, nilikuwa naona fahari, ni heshima kubwa kwangu kusimama mbele
ya wabunge kuwasilisha Bajeti.
“Nilikuwa nina hofu sana mwanzoni. Nilikuwa
ninawaza jinsi ya kuwasilisha Bajeti, wabunge wananisikiliza, Watanzania
wote wananisikiliza lakini nilichokuwa ninakifanya ni kurudia-rudia
kuisoma.
“Kitu kilichokuwa kinanikwaza ni kutaja zile
namba... ma-trilioni sasa nilichokuwa ninakifanya ni kuandika pembeni na
kusoma moja kwa moja bila matatizo,” alisema huku akicheka.
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !