Posted Jumatatu,Juni24 2013 saa 9:50 AM
Kwa ufupi
Alisema hali imekuwa mbaya kiasi kwamba hata
nafasi za uongozi hivi sasa zinapatikana pasi na kuzingatia uwezo
kiutendaji na uadilifu wa mhusika na badala yake kinachoangaliwa ni
mhusika anayeomba uongozi ametoa fedha kiasi gani za kuwahonga wapiga
kura.Arusha.
Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye amewataka viongozi wa dini na Watanzania kwa jumla kuwa makini na watu wanaojipitisha na kutoa fedha kutaka uongozi akisema hiyo imezaa matabaka kwa wanyonge kukosa haki za msingi kwa kuwa hawana fedha.
Sumaye alisema hayo jana kwenye sherehe za
maadhimisho ya miaka 50 ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania
(KKKT), zilizofanyika Chuo Kikuu cha Makumira, Arumeru.
Mbele ya Maaskofu wote 20 wa Dayosisi zote za KKKT
nchini na wageni waalikwa kutoka ndani na nje ya nchi, Sumaye alisema
jeuri ya fedha na mamlaka imesababisha mambo mengi machafu katika jamii
ikiwamo wanyonge kukosa haki zao za msingi, huku wenye uwezo kifedha
wakipata haki kwa kutoa hongo au rushwa.
Alisema hali imekuwa mbaya kiasi kwamba hata
nafasi za uongozi hivi sasa zinapatikana pasi na kuzingatia uwezo
kiutendaji na uadilifu wa mhusika na badala yake kinachoangaliwa ni
mhusika anayeomba uongozi ametoa fedha kiasi gani za kuwahonga wapiga
kura.
“Hata katika baadhi ya dayosisi na sharika zetu
watu wamekuwa wakipewa sifa za ajabu si kwa sababu ya uadilifu wao au
wema wao, bali kwa sababu tu wamechangia fedha kwa shughuli zetu za
kanisa au hata binafsi,” alisema.
Aliwataka viongozi wa kidini kutojielekeza kwenye
huduma za kiroho pekee, bali washughulike na mambo yote yanayoikwaza
jamii wanayoiongoza ikiwamo kukemea vitendo viovu vinavyohatarisha
usalama, amani na misingi ya Taifa.
Akizungumzia amani ya nchi, Sumaye aliwataka
Watanzania kukemea vitendo viovu vinavyolikumba taifa bila kujali kama
kukemea huko kutawaudhi wenye mamlaka na nguvu za fedha.
Alisema taifa litaangamia iwapo hali ya uhasama wa
kiimani, kiitikadi na maeneo mabomu kutupwa kwenye mikusanyiko ya watu
kwa nia ya kuua, itaachwa iendelee.
“Taifa linakabiliwa na matatizo mengi. Watu
wamefikia hatua ya kuchukiana kwa sababu ya imani zao. Mabomu
yanalipuliwa katika mikusanyiko ya jamii na kuteketeza watu wasio na
hatia,” alisema Sumaye na kuongeza:
“Je, tumekuwa na ujasiri wa kukemea mabaya hata
kama kukemea huko kunawaudhi au kuwakera wenye mamlaka au na wenye nguvu
za fedha?”
Sumaye alihoji kilichotokea hadi leo Watanzania
waanze kubaguana kwa maeneo wanakotoka, viongozi wa dini kuuawa,
makanisa kuchomwa moto na Wakristo na Waislamu kupigana kugombea nani
achinje mnyama.
“Haya yote ni mambo mageni nchini mwetu, tuendelee
kuiombea nchi yetu amani lakini wakati maombi yakiendelea, Watanzania
tujue tunajichimbia kaburi letu wenyewe kama hatutapiga vita maovu
haya,” alisema.
Sumaye aliyekuwa Waziri Mkuu kwa miaka 10 ya Serikali ya Awamu
ya Tatu chini ya Rais mstaafu Benjamin Mkapa, alihoji uadilifu na
dhamira ya Watanzania, wakiwamo viongozi wa dini ambao hivi sasa
wanawasifia na kuwakumbatia watu wanaotoa michango mikubwa ya fedha
madhabahuni bila kujali uadilifu wao na jinsi walivyochuma fedha hizo.
Mkuu wa KKKT, Askofu Alex Malasusa alisema Kanisa
halitaogopa kusema ukweli pale panapobidi huku akiahidi kuwa litaendelea
kujenga marafiki wema bila kujali itikadi zao kisiasa wala ukwasi.
Sherehe hizo zilihudhuriwa pia na viongozi wa
Kiislamu kitendo ambacho Askofu Malasusa alisema ni ishara ya
ushirikiano na uhusiano mwema kati ya dini na madhehebu yote nchini
tofauti na chuki inayojaribu kupandikizwa na wasiolitakiwa mema taifa.
MWANANCHI:
MWANANCHI:
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !