Waziri Dossa Azizi: Shujaa aliyesahaulika
Na. Mohammed Said
Baada ya vita kuu ya pili (1938-1945) nchi nyingi zilizokuwa chini ya
ukoloni hasa barani Afrika zilianzisha harakati za kudai uhuru.
Uongozi uliokuwepo Tanganyika wa chama cha Waafrika kilichojulikana
kama African Association wakati ule ulishindwa kabisa kubuni mbinu mpya
za kupambana na utawala wa kigeni.
Ili Tanganyika iende mbele ilikuwa ni lazima uongozi ule uondolewe madarakani.
Sababu kuu za kuung’oa madarakani uongozi ni kule kushindwa kwake kupambana
na mabadiliko ya siasa yaliyokuwa yakitokea dunia nzima.
Harakati za Waziri Dossa Aziz na kuweka wazi mali yake ili kupambana
na dhuluma za Serikali ya Kiingereza katika Tanganyika zinaanza wakati
huu. Dossa wakati ule alikuwa kijana mdogo wa miaka 25.
Ili aweze kupata picha halisi ya siasa katika mji wa Dar es Salaam ni
lazima msomaji afahamishwe hali iliyokuwepo Dar es Salaam katika miaka
ya 1950.
Katika mji wa Dar es Salaam ya miaka 1950 kulikuwa na koo mbili maarufu.
Ukoo wa Azizi Ali baba yake Dossa, Ramadhani na Hamza Azizi na ukoo wa
Kleist Sykes baba yao Abdul-wahid (1924-1968), Ally na Abbas Sykes.
Wazee hawa wawili walikuwa marafiki na urafiki huu ulienea hadi kwa
watoto wao. Watoto wao wakafanya mengi pamoja katika harakati za kudai
uhuru wa Tanganyika; na ndiyo maana haiwezekani ikaelezwa habari za Dossa
bila kugusa habari za akina Sykes.
Halikadhalika haiwezekani yakaandikwa maisha ya Nyerere au historia
ya uhuru wa Tanganyika na mwandishi akapuuza mchango wa watu hawa. Watoto
wa koo mbili hizi, Dossa akiwakilisha ukoo wa Azizi Ally na Abdulwahid
na Ally Sykes wakiwakilisha ukoo wa Sykes ndiyo mwaka 1950 waliohusika
na mapinduzi ya kuung’oa madarakani uongozi wa African Association wa wazee
uliodumu kuanzia mwaka 1929 hadi 1950 rais wake wa mwisho akiwa Mwalimu
Thomas Sauti Plantan.
Muhimu katika mazingira ya siasa za wakati ule ni kuwa hakuna chochote
ambacho kingeliweza kufanyika Dar es Salaam katika jitihada ya kupambana
na Serikali ya kikoloni bila ya msaada wa Dossa na watoto wa Kleist Sykes
kwa sababu hawa walikuwa kwanza na elimu ya kutosha na pili walikuwa na
hazina ya kuendesha harakati za siasa.
Kleist Sykes (1894-1949) alikuwa mwajiriwa wa Tanganyika Railway kama
mhasibu. Kleist alikuwa mwanasiasa muasisi wa African Association (1929)
na Al Jamiatul Islamiyya (Muslim Association) (1933) katika miaka ya mwisho
ya uhai wake Kleist akawa mfanyabiashara maarufu.
Azizi Ally alikuwa mkandarasi wa kujenga majumba. Lakini kwa kuwa Azizi
Ali alikuwa Mwafrika wakoloni walimbagua wakakataa kumpa leseni ya ukandarasi
wa daraja la juu ambayo ingelimwezesha kujenga majumba makubwa ya ghorofa.
Leseni hizo walipewa Wahindi na Wazungu. Juu ya ubaguzi huu wote baba yake
Dossa alifanya kazi ya ujenzi na akatajirika katika biashara kama alivyotajirika
rafiki yake Kleist. Mali hii ndiyo iliyokuja kuwa mtaji wa kwanza waliotumia
Waafrika wa Tanganyika katika miaka ya mwanzo kuanzia harakati za kudai
uhuru.
Wakati ule mtu hakujiingiza katika siasa ili anufaike binafsi. Nafasi
hiyo haikuwepo kwa kuwa hakukuwa na fedha katika siasa. Kila aliyeingia
katika harakati aliingia kwa uchungu na mapenzi ya nchi. Kama alikuwa na
mali basi aliingia ili atoe mali yake kuikomboa nchi. Kama hana mali basi
alijitolea chochote katika vipawa alivyojaaliwa.
Dossa aliingia katika harakati za siasa mwaka 1950 siasa ikiwa katika
hali hii. Aliingia katika African Association na uongozi mpya wa vijana
miongoni mwao akiwa Abdulwahid na Ally Sykes, Hamza Mwapachu (1918-1962),
Tewa Said Tewa (1924-1998), Dk. Vedast Kyaruzi, Dk. William Mwanjisi, Dk.
Luciano Tsere, na vijana wengine ambao ingawa hawakuwa Watanganyika walishiriki
kikamilifu katika harakati za kudai uhuru. Hawa walikuwa Dennis Phombeah
kijana wa Kinyasa kutoka Nyasaland (Malawi), Patrick Aoko na Dome Budohi
kutoka Kenya na vijana wengine wengi.
Dossa aliguswa na madhila ya ukoloni kwa dhahiri yake mwaka 1947. Dossa
pamoja na mtoto mmoja wa Mwarabu tajiri aliyekuwa akiishi Dar es Salaam,
Ali Mmanga walichaguliwa kuhudhuria mahojiano Nairobi kwa ajili ya kozi
ya urubani wa ndege. Walipowasili Nairobi wakoloni walikataa kumfanyia
usaili Dossa kwa sababu alikuwa Mwafrika. Dossa alifahamishwa kuwa yeye
kama Mwafrika hastahili kupewa ujuzi wa kurusha ndege. Dossa alifadhahika
sana na alimweleza mwandishi wa makala hii kuwa alipiga simu kwa baba yake
na akawa analia machozi kwa uchungu. Kwa kumuonea huruma baba yake alimtumia
fedha ili anunue gari pale Nairobi kama zawadi ya kumfajiri. Hii ndiyo
ilikuwa gari ya kwanza kuwa nayo Dossa na aliitumia hadi 1955 alipoitoa
kwa TANU ili itumike kwa ajili ya kudai uhuru.
Lakini Dossa alipokwenda Nairobi alimkuta Ally Sykes yupo mjini hapo
na tayari alikuwa akifahamiana na wanaharakati wa Kenya kama Jomo Kenyatta,
W.W. Awori, Tom Mboya na wengineo. Ally alikuwa akihudhuria mikutano ya
siasa ya Wakikuyu iliyokuwa ikifanyika kwa siri Limuru.
Ally Sykes alimchukua Dossa katika moja ya mikutano ya hadhara ambao
Kenyatta alikuwa anahutubia katikati ya Nairobi sehemu moja ijulikanyo
kama River Road. Aliyoyaona pale yalimtosheleza kabisa Dossa kujua kuwa
Tanganyika ilikuwa imechelewa katika harakati za kudai haki yake. Waafrika
wa Kenya walikuwa wamefikia hali ya kuzungumza siasa kwenye majukwaa wakati
Waafrika wa Tanganyika walikuwa bado wakifanya mikutano yao ndani ya kiofisi
kile kidogo cha African Association chini ya uongozi dhaifu wa Thomas Plantan
akiwa kama Rais na Clemet Mtamila kama Katibu. Dossa alifikisha yote aliyoyaona
Kenya kwa wenzake.
Mzee Dossa alimfahamisha mwandishi wa makala hii kuwa ni katika kipindi
hiki kati ya mwaka 1947-1950 ndipo njama za kupindua uongozi wa Africa
Association zilipoanza washiriki wakuu wakiwa yeye mwenyewe Dossa, Abdulwahid
na mdogo wake Ally na rafiki yao Hamza Kibwana Mwapachu. Huku akicheka
Mzee Dossa alimfahamisha mwandishi kuwa:
"Ilikuwa kutokea Tanga Club, Club mahsusi ya vijana wasomi Waafrika
iliyokuwepo New Street (hivi sasa Lumumba Str.) si mbali sana na ofisi
ya African Association ndipo Abdulwahid na Hamza Mwapachu walipoivamia
kwa nguvu ofisi ya African Association na kufanya mapigano ambayo yalimfanya
Katibu Mzee Mtamila apigwe na kutupwa nje ya ofisi".
Dossa anasema yeye ingawa alikuwa anauchukia ule uongozi wa wazee hakuwa
na moyo wa kuwatoa wazee wale kwa nguvu na kwa taadhira, kwa ajili hii
basi alibaki nje akawa anaangalia sakata ile kwa mbali. Uchaguzi ulifanyika
na wazee wakang’olewa madarakani. Dk. Kyaruzi akachaguliwa Rais na Abdulwahid
akiwa Katibu wake.
Kuanzia wakati huu mikutano ya siasa ikaanza kufanyika Ilala Commuity
Centre ambako Hamza Mwapachu alikuwa akifanya kazi kama Assistant Welfare
Officer. Nyakati za jioni mijadala hii ikawa inahamia nyumbani kwa Dossa
Mtaa wa Mbaruku Gerezani au Tanga Club, Agenda kuu ikiwa namna ya kuwaunganisha
Watanganyika chini ya chama cha siasa ili kudai uhuru.
Mwaka wa 1950 Gavana Edward Twining alipoteua Kamati ya Katiba (Consitutional
Development Committee) ili kukusanya mapendekezo ya Waafrika ni vipi wangependa
katiba ya nchi iwe, Dossa alisema kuwa hapo ndipo Waingereza walipopata
kwa mara ya kwanza kuhisi kuwa uongozi mpya wa vijana katika African Association
ulikuwa umepania kuleta mabadiliko katika nchi. Uongozi wa akina Dossa
uliihimiza Serikali ya kikoloni kuhusu umuhimu wa kuwa na uwakilishi wa
Waafrika katika Baraza la Kutunga Sheria, uwakilishi wa kuchaguliwa na
wananchi wenyewe badala ya ule uwakilishi wa kuchaguliwa na Gavana rangi
ya mtu zaidi kuliko sifa nyingine yoyote.
Kipindi hiki cha mwaka 1950-1954 kilikuwa kipindi kigumu sana kwa kuwa
kwanza chama kilikuwa hakina fedha kikitegemea sana msaada wa Dossa. Wakati
ule chama kilitegemea sana fedha za Dossa katika shughuli za kuendesha
ofisi na gari yake katika kutimiza majukumu yake ya kila siku.
Kwa kipindi kirefu wakati wa uongozi wa wazee kulikuwa hakuna mawasiliano
yoyote kati ya Waafrika wa Tanganyika kupitia African Association na Baraza
la Udhamini la Umoja wa Mataifa ambalo ndilo lililokabidhi Tanganyika kwa
Waingereza wailee nchi hadi hapo Waafrika watakapokuwa tayari kujitawala.
Kwa bahati mbaya Waingereza hawakutoa umuhimu wowote katika kuwafahamisha
Waafrika mapatano hayo kati yake na Umoja wa Mataifa. Vijana walichukua
nukta hii kama kazi ya kwanza kwa umuhimu katika chama na walipeleka barua
nyingi sana katika matawi ili kuyaamsha kwa kuwa yalikuwa yamelala kwa
muda mrefu.
Kati ya mwaka 1950-1952 Dossa alishiriki katika mikutano kati ya TAA
na Earle Seatonn mwanasheria kutoka Bermuda aliyekuwa akikishauri chama
katika masuala mbali mbali ya Katiba na sheria, kutayarisha mapendekezo
kwa Constitutional Developmet Committee na katika mgogoro wa ardhi ya Wameru.
Vile vile Dossa alishiriki katika kutuma ujumbe wa TAA ulioongozwa na
Abdulwahidi kwenda Kenya ambao ulikutana na uongozi wa KANU wa Jomo Kenyatta,
Fred Kubai, Bildad Kaggia na Kungu Karumba mwaka 1951.
Halikadhalika Dossa alikuwa mjumbe wa TAA uliokuwa ukutane tena na Kenyatta
kwa mazungumzo ya siri Arusha mazugumzo yaliyoombwa na KANU. Wajumbe wengine
wakiwa Abdulwahid na Stephen Mhando.
Katika salaam alizoleta Kenyatta kwa TAA alihimiza kuwa kila mjumbe
wa TAA asije mkutanoni ila awe amebeba silaha. Ujumbe huu ulikuwa uondoke
kwa siri mmoja mmoja ili kukwepa makachero.
Dossa alikuwa wa kwanza kuondoka kuelekea Arusha akiwa na bunduki. Wakati
ule ili kwenda Arusha njia ilipita Dodoma. Mkutano huu haukufanyika kwa
kuwa Kenyatta na wenzake walikamatwa kwa makosa ya kuwa wafuasi wa Mau
Mau.
Akiwa Dodoma Dossa alifahamishwa na Ali Juma Ponda katibu wa TAA Dodoma
kuwa mkutano hautakuwepo kwa kuwa viongozi wa KANU wote wametiwa mbaroni.
Akiwa njiani kwenda Arusha palitokea mapigano kati ya Mau Mau na askari
wa kikoloni.
Tarehe 20 Oktoba, 1952 serikali ya kikoloni Kenya ilikuwa imeshindwa
kabisa kupambana na Mau Mau, kwa sababu hii basi serikali ilitangaza hali
ya hatari, Kenyata na Uongozi mzima wa KANU ukatiwa kizuizini ( tarehe
8 Aprili 1953)wakahukumiwa kifungo cha miaka saba kazi ngumu). Dossa aliamua
kwenda Mwanza ambako alipokewa na Dk. Joseph Mutahangarwa, Makamo wa Rais
wa TAA Lake Province. Dk. Mutahangarwa aliulaumu uongozi wa Makao Makuu
kwa kuunganisha harakati za TAA na KANU kwa hofu ya kusababisha kamata
kamata kama ile iliyokuwa ikiendelea Kenya.
Dossa Azizi alikwenda Bukoba ambako alipokelewa na Chief Rutinwa na
viongozi wengine wa TAA kama Ali Migeyo na Suedi Kagasheki.
Mwaka 1953 Dossa alihusika na uamuzi wa kuupeleka ujumbe wa TAA wa Saadan
Abdu Kandoro, Japhet Kirilo na Abbas Sykes utembee nchi nzima kuwaeleza
wananchi kile kilichopitika Umoja wa Mataifa kuhusu kesi ya ardhi ya Wameru.
Vile vile katika mwaka huo huo Dossa alihusika katika uamuzi wa kuupeleka
ujumbe wa TAA Southen Rhodesia (Zambia) kuhudhuria mkutano uliojulikana
kama Pan African Congress uliotayarishwa na mwanasiasa mmoja aliyeitwa
David Keneth Kaunda aliyekuwa Katibu wa African National Congress. Wajumbe
waliochaguliwa kuiwakilisha TAA katika mkutano huu walikuwa Ally Sykes
na Denis Phombeah. Katika harakati hizi zote zilipotakikana fedha kwa ajili
ya kufanikisha hili au lile jukumu lilimwangukia Dossa. Dossa alitoa fedha
zake kwa ukarimu na bila kinyongo.
Mwaka wa 1951 wakati Dossa na wenzake wako katika juhudi za kuipa uhai
mpya TAA Dossa aliandikiwa barua na V.M. Nazerali aliyekuwa mjumbe wa Baraza
la Kutunga Sheria akimuomba aunge mkono juhudi zake na za Ivor Bayldon
na Brig. Scupham za kutaka kuunda chama cha siasa kitachowashirikisha watu
wa rangi zote. Bayldon na Birg. Scupham walikuwa kama alivyokuwa Nazerali,
wajumbe wa Baraza la kutunga sheria.
Wanasiasa wengine walioombwa kuunga mkono juhudi hizi walikuwa Chifu
Kidaha Makwaia. Liwali Yastio Mponda wa Newala. Dk. Joseph Mutahangarwa,
Chifu Abdieli Shangali wa Machame, Chifu Thomas Marealle wa Marangu, Chifu
Adamu Sapi Mkwawa, Chifu Haru Msabila Lugusha, Dk. Wiliam Mwanjisi, Abdulkarim
Karimjee, Dk. Vedast Kyaruzi, Liwali Juma Mwindadi, H.K. Viran, Stephen
Mhando, Ally Sykes na Abdulwahid Sykes.
Dossa na wenzake waliikataa ghilba hii kwa kuwa lengo lao lilikuwa ni
kuanzisha chama cha siasa cha Waafrika wa Tanganyika kwa minajili ya kudai
uhuru.
Itaendelea toleo lijalo
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !