Nyerere na fitina za Upemba na Uunguja
Na Ahmed Rajab
ALIPOFARIKI dunia Mwalimu Julius Nyerere Oktoba 14 mwaka 1999, gazeti
la Guardian la Uingereza liliniomba niandike makala maalumu ya
kuyatathmini maisha yake. Nilipokuwa naanza kuiandika tathmini hiyo
iliyochapishwa siku ya pili yake, niliyakumbuka aliyowahi kuyasema
Mwenyekiti Mao wa China kumhusu Josef Stalin, mtawala wa pili wa
Muungano wa Sovieti baada ya Vladimir Lenin.
Nami nikayatumia maneno hayohayo kuanzia makala yangu kwa kuandika:
Julius Nyerere was “a great leader who made great mistakes,” as one
ruler once famously said of another.(“Julius Nyerere alikuwa “kiongozi
mkubwa (adhimu) aliyefanya makosa makubwa,” chambilecho mtawala mmoja
aliyewahi kumuelezea hivyo mtawala mwenzake.)
Nyerere alifanya makosa ya kinadharia, ya kifikra na ya kiutendaji
katika utekelezaji wa sera zake. Sikulidhukuru jina la Stalin kwa sababu
sikutaka wasomaji wangu wafanye kosa la kudhania namfananisha Nyerere
na Stalin. Siamini kama Nyerere alikuwa na uovu wa Stalin. Na kama
ilivyokuwa kwa Stalin si yote ya Nyerere yaliyokuwa maovu. Alitenda mema
yanayostahiki sifa.
Watu wa kale wasema: “Kheri ya mja ni ulimi wake na shari ya mja ni
huohuo.” Kwa ulimi wake Nyerere aliwahi kutamka maneno ya maana na
mengine ya kibahaluli. Baadhi ya maneno yake yalikuwa kama lulu na
baadhi yalikuwa kama utumbo kama pale, kwa mfano, aliposema kuwa hakuna
watu waitwao Waswahili. Nilimsikia akiyasema hayo alipotoa hotuba katika
ukumbi wa London School of Economics alipokuwa ziarani London kabla ya
kuuacha urais.
Yote hayo yaonyesha kwamba Nyerere alikuwa mja, mtu kama watu
wengine. Hakuwa Mungu, hakuwa malaika. Wala hakuwa mtume na hata hakuwa
mpigaji ramli. Na si kila alichokitamka kilikuwa sahihi. Lakini binadamu
yule alikuwa na ulimi uliowalaza wengi na kuwafanya waache kufikiri
kwani alikuwa na kipaji cha kuwafanya waamini kwamba kila alilolisema
lilikuwa la kweli kabisa na hivyo hapakuwa na haja ya kumfanya mtu
mwengine alifikirie. Ilikuwa nadra kumpata mtu aliyethubutu kumpinga au
kumkosoa, hasa kadamnasi. Walikuwapo waliochelea kukiona cha mtema kuni
na wengine waliridhia kuwa vibarakalla vya kuitika tu ‘hewala bwana.’
Moja ya makosa makubwa aliyoyafanya Nyerere kwa kusudi au kwa sadfa,
ni hilo la kuwafanya wananchi wenzake waache kufikiri na wawe
wanayafuata tu aliyokuwa akiyasema bila ya kuyazingatia au kuyapima.
Miongoni mwa aliyowahi kuyasema Nyerere ni kuwa ati iwapo Zanzibar
itaachana na Tanganyika basi Tanganyika kutakuwa shuwari lakini
Wazanzibari wataanza kubaguana baina ya Wapemba na Waunguja na halafu
wataendelea kutafutana asili zao.
Tangu wiki iliyopita waandishi kadhaa wa Bara wamekuwa wakiyanukuu
haya kana kwamba ni maneno yenye ukweli usiopingika. Hii ni fitna tu; na
inatumiwa kuwatisha na kuwagawa Wazanzibari.
Wakoloni walipowaona wanaowatawala wanaungana kuwapinga, basi
walitumia mbinu ya kuwagawa wazidhoofishe nguvu zao ili waendelee
kuwatawala.
Mbinu kama hiyo inatumiwa siku hizi na baadhi ya viongozi wa CCM wa
Bara pamoja na baadhi ya waandishi wa huko huko Bara ‘walioshtushwa’ na
mwamko wa kisiasa uliowafanya Wazanzibari wawe na ujasiri wa kuujadili
kwa mapana na marefu Muungano wa Tanzania.
Ujasiri huo umewafanya wengi wao waseme kwamba ama wanaupinga muundo
wa sasa wa Muungano au hawautaki kabisa na wanataka Zanzibar iwe dola
huru yenye mamlaka yake kamili.
Huo si mwamko wa leo au wa jana; tumekuwa tukiugusia miaka nenda
miaka rudi lakini tukionekana kuwa ni wazushi na wazandiki. Sasa mambo
yanajidhihiri yenyewe. Matokeo yake ni kwamba waliokuwa wakijidanganya
sasa wamegutuka na hawajui jinsi ya kulizuia hilo wimbi la uzalendo
Wakizanzibari minghairi ya kutumia hoja finyu za kikabila na udini.
Mmoja amefika hadi ya kuandika kuhusu ‘Waarabu’ na ‘watu Weusi’ kana
kwamba hao wanaonasibishwa na uarabu ni wa rangi aina ya pekee iliyo
tofauti kabisa na ya Wazanzibari wasio na asili ya Kiarabu. Mwandishi
huyohuyo alitishwa na sura rahimu ya Sheikh Farid Hadi Ahmed, mmoja wa
viongozi wakuu wa Uamsho.
Aliandika kwamba baada ya kuiona picha ya Sheikh Farid yalimjia
mawazo kwamba Uamsho si jumuiya ya kidini na wala si ya Wazanzibari na
kwamba Sheikh Farid ametumwa (hakusema na nani) kuwafitinisha
Wazanzibari. Alichotaka kusema mwandishi huyo ni kwamba kwa vile Sheikh
Farid ana asili ya Kiarabu basi Uamsho inataka kuurejesha usultani.
Ni uchambuzi uchwara, tena wenye kutumia lugha ya kibri. Unashtua kwa
vile ni ‘uchambuzi’ wa hatari unaofanana na simulizi za Wahutu wa
Rwanda kabla ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini humo.
Hizi fitna za ‘Upemba’ na ‘Uunguja’, za ‘ubwana’ na ‘utwana’ na za
‘ugaidi’ wa Uamsho ni fitna zinazotiwa na watu walio maluuni. Lengo lao
kubwa ni kuwapotosha Wazanzibari wauzime mjadala wa Muungano. Hawajali
iwapo watalitimiza lengo hilo kwa kuyakiuka maadili ya uongozi au ya
uandishi.
Hila wanazotumia ni kwanza, kuwafitinisha Wazanzibari kwa kutia fitna
za kikabila na za kidini. Kwa mfano, wanawatisha wahafidhina wa
CCM/Zanzibar, wale wenye kusherehekea kaulimbiu ya ‘Mapinduzi Daima’,
kwa kuwaonya ya kuwa Uamsho ina “msukumo wa kiarabu” na kwamba kusudio
lake ni hatimaye kuyapinga Mapinduzi na kuirejesha Zanzibar katika
‘utumwa’. Maneno ya kijinga kabisa.
Hila yao ya pili ni kuwagonganisha vichwa Waunguja na Wapemba kwa
kutumia hoja zisizo na mshiko wowote wa kimantiki. Wanasema wamewapata
Wapemba wengi wenye kutaka Muungano uendelee kama ulivyo. Wamewahoji na
matamshi yao kusambazwa na magazeti fulani nchini. Huu ni mfano mzuri wa
propaganda ya kitoto.
Hila yao ya tatu ni kutumia lugha kuparaganya mambo. Ingawa Uamsho ni
jumuiya kamili wao badala yake wanasema kuwa hiki ni kikundi. Sio kundi
bali ‘kikundi.’ Na wanaishtumu jumuiya hiyo kuwa ‘inawatumia’ baadhi ya
vijana kufanya vitendo vya kihuni vya kuchoma moto makanisa. Hakuna
ushahidi wa hili.
Nne, wanajaribu kuwatisha Watanzania na hasa wakuu wa dunia hii kwa
kuifananisha Jumuiya ya Uamsho na mitandao ya kigaidi ya Al-Qa’eda, Boko
Haram na Al-Shabab. Bila ya shaka wenye kueneza fitna hii hawajui
walisemalo na wanajikashifu si mbele ya Watanzania wenzao tu bali hata
machoni mwa balozi za nchi za Magharibi.
Sijui kama wanaelewa ya kuwa maofisa wa baadhi ya balozi za Magharibi
wameshakutana na viongozi wa Uamsho katika juhudi zao za kuitathmini
Jumuiya hiyo na wanayaelewa makusudio halisi ya Uamsho.
Kwa hakika, kinyume na wanavyoandika baadhi ya waandishi wa Bara,
Jumuiya ya Uamsho haikuzuka juzi. Imekuwako kwa muda wa takriban miaka
10 sasa. Jumuiya hii ni kama mwavuli ambao chini yake kuna jumuiya
mbalimbali za Kiislamu, pamoja na ile ya maimamu.
Uamsho imekuwa ikiendesha harakati zake kwa msaada wa taasisi za nchi
za Magharibi. Ilikuwa miongoni mwa waangalizi rasmi wa Uchaguzi Mkuu
uliopita na ripoti yake kuhusu uchaguzi huo ni ya kupigiwa mfano kwa
maelezo yake ya kina.
Kati ya wafadhili wa Jumuiya hiyo katika harakati hizo za kuangalia
uchaguzi lilikuwa shirika la USAID la Marekani. Hata vizibao wanavovaa
baadhi ya viongozi wa Uamsho na vikuza sauti vyao walipewa na Wamarekani
wakati huo wa uchaguzi uliopita.
Wenye kujuwa mambo watakwambia kwamba kuna tofauti kubwa kama ya
mbingu na ardhi kati ya jumuiya ya Uamsho na mtandao wa Al-Qa’eda au
kundi la al-Shabab. Huwezi kabisa kuzifananisha falsafa zao au makusidio
yao. Hata Boko Haram nayo licha ya mbinu inazozitumia inatofautiana
sana na al-Qa’eda.
Huko Zanzibar mafatani hawa wana washirika wanaojulikana. Nao ni wale
wanaochomwa na kuwapo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK). Ndiyo
maana wakaruka harakaharaka kuwatupia lawama za machafuko ya hivi
karibuni viongozi wa CUF waliomo kwenye SUK na kutaka watimuliwe kutoka
serikalini. Na ni wao waliohusika na vipeperushi vilivyotolewa wiki
iliyopita kuwafitinisha Wapemba na Waunguja.
Na ni haohao wenye kujaribu kuwachimba waasisi wakuu wa Maridhiano
yaani Rais mstaafu Amani Abeid Karume na Maalim Seif Sharif Hamad.
Inasikitisha kuwaona baadhi ya Wabara wenye kujigamba kuwa ni wasomi
wakitaka mijadala ya kisiasa ipigwe marufuku katika majukwaa ya kidini.
Hawaelewi kwamba ni dhima ya dini za Ukristo na Uislamu kuzungumzia na
kuyatafutia ufumbuzi mambo yanayoyagusa maisha ya kila siku ya waumini
wa dini hizo. Na mambo hayo yawe yepi kama si ya kisiasa?
La kutisha ni kuwa ‘wasomi’ hao wanamtaka Rais Jakaya Kikwete
awachukulie hatua za kimabavu wakuu wenzake walio serikalini kwa
kisingizio kuwa ati wanaunga mkono harakati za Uamsho.
Ulimwengu haukufunga macho wala haukuziba masikio. Unawaona na
kuwasikia. La ajabu ni kwamba wanasiasa na waandishi wenye kuchochea
hisia kama hizo wamesahau ni nyakati gani tulizo nazo na ni ulimwengu
gani tulio nao. Katika ulimwengu wao wa leo Wazanzibari wanasema
hawakubali tena kugawanywa kwa propaganda za kikabila au za kidini.
Inatisha kwamba kuna wanasiasa na waandishi waliosahau kwamba siku
hizi kuna Mahakama ya Jinai ya Kimataifa (ICC) na mahakama nyingine
mahsusi za kimataifa, mithili ya ile Mahakama Maalumu ya Sierra Leone.
Mahakama kama ile ya Sierra Leone inaweza kuundwa mara moja na Umoja wa
Mataifa kuwatia adabu wenye kupalilia fitna zinazoweza kuzusha mauaji ya
kimbari.
Ni hiyo Mahakama Maalumu ya Sierra Leone iliyomhukumu Charles Taylor,
rais wa zamani wa Liberia, kifungo cha miaka 80 baada ya kupatikana na
hatia ya kuishushia nakama Sierra Leone.
Dhana waliyonayo baadhi ya wasomi na waandishi wa Bara ni kwamba
viongozi wa Uamsho ni mijitu isiyosoma. Kuna mmoja aliyepandwa na jeuri
na kuandika kwamba mbali na kujua kusoma Qur’an viongozi hao ni watu
wasiojuwa kuandika wala kusoma.
Ukweli ni kwamba viongozi wa Uamsho ni wasomi waliohitimu masomo ya
chuo kikuu na wana shahada za juu za uzamili katika fani mbalimbali kama
vile za uhandisi, sayansi na jiografia. Ni wasomi wa nyanja zote — za
dini na dunia.
Mfano mzuri ni Sheikh Msellem ambaye mbali na kuwa gwiji wa tafsiri ya Qur’an pia alisomea taaluma ya hali ya hewa.
Baadhi yao walisoma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako
walivutiwa na hotuba za kidini za Professor Malik, mtaalamu wa fani ya
hesabati, ambazo ziliwashajiisha na kuwafanya wawe na mwamko wa
Kiislamu. Wengine walisoma kwenye vyuo vikuu vya nje vikiwemo vile vya
Sudan, Saudi Arabia na Qatar.
Ni wazi kutokana na ripoti na taarifa zao kwamba baadhi ya wasomi na
waandishi wetu wa Bara wanawadharau Wazanzibari. Nadhani hizo dharau zao
ndizo zinazowafumba macho wasiweze kuona nani hasa aliyechochea fukuto
hili la upinzani dhidi ya makandamizo ya walioshika hatamu za utawala wa
Muungano.
Maandishi yao yamebainisha wazi kwamba hawaamini ya kuwa Unguja na
Pemba si majimbo wala koloni za Bara. Inakirihisha kuona namna wengi wao
wanavyozitapika hadharani chuki zao (na udini uliowapamba) bila ya hata
staha na uvumilivu wa kimaadili
Gazeti la Raia Mwema
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !