SERIKALI imewaomba viongozi wa dini kusisitiza amani kwa
waumini wao kutokana na viongozi hao kumiliki kundi kubwa la jamii ambalo
linawasikiliza, kuwaamini na kutekeleza maelekezo yao.
Kauli hiyo imetolewa jana jijini Dar es Salaam na Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda katika ibada ya misa ya kuwekwa wakfu Askofu msaidizi
wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Titus Mdoe.
Alisema kuwa kwa vile Kanisa Katoliki linaadhimisha Mwaka wa
Imani, ni vyema maaskofu wakatumia nafasi na kipindi hicho kuwaimarisha
waumini wao kiimani na hatimaye kuwa mfano kwa jamii.
Alisema kuwa Tanzania kwa sasa inapitia changamoto za
kisiasa, kijamii na utawala, hivyo ni vyema viongozi wakasimamia kwa karibu
maadili mema katika jamii yanayohitaji upendo, busara na hekima.
Pinda aliongeza kuwa changamoto nyingine ni vuguvugu la
ukosefu wa amani na utulivu katika baadhi ya maeneo nchini, hali
inayosababisha kuwepo na ishara ya uadui baina ya wananchi ikiwemo udini na
ukabila.
Balozi wa Vatican nchini, Askofu Mkuu Francisco Padilla,
alimtaka Askofu Mdoe kulilea kanisa, kufanya kazi kwa karibu na Mwadhama
Polycarp Kardinali Pengo, ambaye ni Askofu Mkuu wa jimbo hilo kutokana na
uzoefu alionao.
Pia alisema kuwa askofu huyo msaidizi amechaguliwa kutokana
na uwezo wake kiutawala na kumtaka kuwa karibu na Mungu na kuendelea
kuyatoa maisha yake kwa ajili ya kanisa.
Kardinali Pengo naye alimtaka askofu Mdoe aendeleze azimio
la kuhifadhi imani na kujenga mwili wa Kristo na kusimamia masuala ya
mawasiliano, uchungaji, litrujia, vijana, vyama vya kitume, katumene, afya
na majadilino ya kidini.
Askofu Titus Mdoe alizaliwa miaka 52 iliyopita, na alipata
daraja la ushemasi Desemba 3, 1985 na kupadrishwa Juni 24, 1986 na
anaungana na muhashamu Askofu Euzebius Nzigilwa kumsaidia Kardinali Pengo.
Mbali na Pinda pia walihudhuria marais wastaafu, Benjamini
Mkapa na Ali Hassan Mwinyi, mawaziri wakuu wastaafu, mawaziri, viongozi wa
dini mbalimbali na wanasiasa.
|
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !